Nani aangalie usalama watoto wetu shuleni?

HIVI msomaji unaonaje kama shule zetu na hasa zile zilizopo maeneo ya mijini zingeajiri mabaunsa ili kudhibiti tabia chafu miongoni mwa wanafunzi wakorofi, na hasa wale wenye tabia mbaya zilizoshindikana?

Nauliza swali hili baada ya kufanya uchunguzi katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Dar es Salaam ambapo nimegundua kuwa kuna vitendo vichafu vinavyofanyika ambavyo kwa sasa vinahitaji kutafutiwa suluhisho la haraka kwa manufaa ya watoto wetu wanaosoma huko.

Nitaeleza taratibu uelewe msomaji wangu, ili jamii yetu ianze kuweka mikakati ambayo hatimaye itasaidia watoto katika shule hizi kuwa na nidhamu nzuri na baadaye wawe raia wema wanaolitumikia taifa lao kwa uadilifu.

Hivi majuzi sikuweza kuamini macho yangu, baada ya kuwaona wanafunzi wa kike wa shule moja ya binafsi maeneo ya Sinza wakivuta sigara mchana baada ya kutoka shuleni tena bila kuogopa. Wangekuwa wavulana nisingeshangaa sana, lakini wasichana mhh!!! Inafikirisha kidogo.

Wakiwa kama wanne hivi, wasichana hawa wadogo waliingia katika baa moja (sio hoteli) wakaagiza chips-kuku na soda, na baada ya kula na kunywa walitoka nje ya eneo hilo na kuanza kuvuta sigara kwa ule mtindo wa kupokezana, yaani mmoja anapiga pafu, kisha anampasia mwenzake.

Kwa mbali nilifuatilia mazungumzo ya wanafunzi wale, na nilipata shida kidogo kuamini walichokuwa wanakijadili, kwani sehemu kubwa ya mazungumzo yao ilijikita katika uhusiano na wanaume watu wazima, huku ‘wakikandia’ sana wenzao walio na marafiki wa kiume ambao ni wanafunzi wenzao.

Bado sikuridhika na kile nilichokuwa nimekiona, nikaamua kuwafuata waendesha bodaboda wanaoegesha karibu na eneo lile na kuwaambia mbona wale wasichana wadogo vile walikuwa wanavuta sigara na mmoja wao akanijibu hivi: “Mzee ulichokiona hapo ni cha mtoto. Wote wale huwa wanavuta bangi na leo wamevuta sigara kwa vile yule mshikaji wao ambaye huwa anawaletea bangi kafiwa na yupo kwao Mbagala.” Sikuwa na jambo la ziada bali kuondoka kimya kimya.

Baada ya kuona nidhamu ‘mbovu’ ya wale mabinti, nilirudi nyuma na kutafakari nilichokiona miaka 14 iliyopita kule Uingereza, wakati nilipokuwa nafundisha elimu ya kikristo (Christian instructions) kwa shule moja ya msingi katika Jimbo Katoliki la Westminister jijini London.

Nilipata nafasi hiyo adimu baada ya kuhitimu masomo yangu katika Chuo Kikuu cha Gregorian kule Roma nchini Italia, lakini bahati mbaya sikuweza kuendelea kufundisha pale kwa sababu nilipaswa kuwa na kibali cha ajira kutoka nchini kwangu na sio Italia, na kukipata ilikuwa mchakato mrefu kweli, hivyo nikaamua vinginevyo.

Nilipoingia darasani kufundisha dini Grade Four pale Uingereza nilipumbazwa kidogo, kwani niliwakuta vijana wawili wa kike na kiume, mmoja akisimama nyuma ya darasa na mwingine mbele ya darasa, na nikaelezwa kuwa kazi yao ni ku-monitor (kufuatilia) mienendo ya wanafunzi ili kuwasaidia.

Kazi ya mabaunsa wale ilikuwa ni kuhakikisha kuwa mwalimu anapofundisha, basi kila mwanafunzi anahakikisha kuwa anamsikiliza mwalimu na kuacha kusinzia au kufanya mambo ya ajabu ambayo itamfanya mwalimu ashindwe kutimiza wajibu wake awapo darasani.

Kazi ya waangalizi wale haikuishia darasani tu bali hata wakati wa mapumziko, kwenye chai na chakula, maktaba, maabara, kwenye paredi na hata kwenye mabasi yanayowapeleka na kuwachukua wanafunzi kutoka kwenye makazi yao.

Mama mmoja mwalimu kutoka Zimbabwe ambaye nilionana naye pale Uingereza alinieleza jinsi mabaunsa wale walivyokuwa wanasaidia kuimarisha nidhamu miongoni mwa wanafunzi, na hivyo kurahisisha kazi ya kufundisha.

Ni katika muktadha huu naona umuhimu wa kuwa na waajiriwa zaidi ya walimu katika shule zetu, na hasa zile zilizopo maeneo ya mijini, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wetu wanalelewa katika mazingira mazuri na hivyo kuwafanya kuepukana na tabia mbaya.

 Ukiangalia baadhi ya shule zetu za msingi leo utakuta zinakabiliwa na matatizo lukuki na walimu nao kwa uchache wao hawawezi kufuatilia maisha ya kila mwanafunzi kuhakikisha hapotei njia.

Nijuavyo, shule mbalimbali za msingi zina ‘Kamati ya Shule’ na wengine huziita ‘Bodi ya Shule’ ambayo pamoja na mambo mengine inaangalia namna ya kuboresha huduma katika shule husika na hasa mambo ya maadili.

Kwa shule za mijini ambapo wazazi wana muda kidogo sana wa kukaa na watoto hao kutokana na ratiba za kikazi na zile za shule, kuna haja sasa kuwahusisha wazazi katika malezi ya watoto wao shuleni, ili washauri mbinu bora za kuimarisha nidhamu  miongoni mwa watoto wao.

Nimejaribu kuzungumza na baadhi ya walimu wa shule za msingi kujua ukweli wa tabia mbaya kama ngono za mapema katika shule wanazofundisha, na wengi wao wamekiri kuwa vitendo hivyo vipo, na inabidi jamii ianze kuviangalia kwa makini na kuweka mikakati ya kuvitokomeza kabisa.

Wanasema kuwa baadhi ya wahusika katika uovu huo ni baadhi ya vijana wanaoishi maeneo karibu na shule wanazofundisha na mara nyingine huko majumbani kwao ndugu na jamaa zao ndio wanawaharibu watoto, ambao baadhi huacha shule na kujiingiza katika mambo ya ajabu huko mitaani.

Kuna mfano wa taasisi moja inayofanya kazi pale Moshi kutoka Uingereza iitwayo Mkombozi, ambayo miaka kadhaa iliyopita iliwahi kufanya uchunguzi wa vitendo vya ulawiti katika baadhi ya shule za msingi mjini humo, na wao waligundua madudu ya kutisha kuhusiana na tabia hiyo chafu katika baadhi ya shule zilizopo mjini Moshi.

Kwa shule zote ambazo walifanyia kazi, iligundulika kuwa taasisi hizo za awali za elimu baadhi ya watoto wamewahi kulawitiwa, huku wakiathirika kwa matendo hayo maovu.

Nini kifanyike sasa? Kwa kweli inasikitisha kuwa mpaka sasa vyombo husika vinashindwa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa vitendo viovu katika shule zetu vinakomeshwa na kuifanya jamii kwa pamoja kuanza juhudi za kupiga vita jambo hilo.

Nionavyo mimi kuna haja sasa kwa wakurugenzi wa miji, meya, madiwani, wenyeviti wa mitaa, walimu wakuu wa shule zote zilizopo mijini, baadhi ya wazazi, viongozi wa dini, vyama vya siasa, na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuungana kwa pamoja, kuhakikisha kuwa wanaweka mikakati thabiti ya kumaliza kabisa vitendo vya ulawiti na tabia nyinginezo mbaya katika shule zote zilizopo katika maeneo hayo.

Nina uhakika kuwa mashirika mengi yanayoangalia haki za watoto yapo tayari kusaidia juhudi hizi, kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinaendelea kulindwa katika jamii.

Mashirika kama UNICEF yamekuwa yakijikita katika kuangalia usalama wa mtoto tangu kuzaliwa mpaka anapoingia katika ujana, na ndio maana limekuwa linafanya uchunguzi katika maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha kuwa afya ya mtoto na makuzi yake vinatiwa maanani.

Ni matumaini yangu kuwa kama kutakuwa na juhudi za pamoja, baadhi ya mashirika ya kiserikali na yale yasiyokuwa ya kiserikali yapo tayari kutoa msaada wa hali na mali ili kusaidia juhudi hizi za pamoja.

Kinachowezekana leo kisingoje kesho, hivyo jamii ianze juhudi za pamoja za kukomesha tabia chafu katika shule kwani kama sio mwanangu au mjukuu wangu kupatwa na hali hii, kesho inawezakana akawa mwanao au mjukuu wako. TAFAKARI.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *