Nani anasema ukweli kuhusu hali ya chakula?

TATIZO la upungufu wa chakula sio la Tanzania peke yake. Wakati mamilioni wanaendelea kulala usiku bila ya kula chakula duniani, kwa upande mwingine, mamilioni wengine wanakula na kusaza.

Uhaba huo unatokana na sababu nyingi  zikiwemo kupungua kwa uzalishaji wa mazao ya chakula, kupanda holela kwa bei za vyakula, kutokea kwa majanga ya asili yakiwemo mafuriko na ukame na vipato duni.

Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Chakula Duniani, tatizo la uhaba ama ukosefu wa chakula duniani limeonekana kwenye upande wa ugawaji kwani iwapo kungekuwepo na utaratibu mzuri, basi tatizo la ukosefu wa chakula lisingekuwepo.

Kutokana na hali hii, taharuki kubwa inaendelea mingoni mwa watanzania kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Wapo wanaosema kwamba kuna tatizo la uhaba wa chakula miongoni mwa watanzania, lakini kwa upande serikali mwingine, serikali inasema kwamba suala hili halipo na hali ya usalama wa chakula ni nzuri.

Wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu hali ya chakula nchini, mtandao wa mfumo wa utoaji wa tahadhari kuhusu hali ya upungufu wa chakula(FEWS) ulitoa tahadhari kuwa Tanzania ni kati ya nchi zinakazokabiliwa na uhaba wa chakula.

Mtandao huo ambao pia unatoa tathmini ya hali ya chakula duniani umetahadharisha kwamba takribani asilimia mpaka tano ya watanzania (takriban milioni 2) wanakabiliwa na upungufu wa chakula.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, FEWS imebainisha kwamba mtanzania mmoja kati ya watano sasa wanakabiliwa na upungufu wa upatikanaji wa chakula kwani vipato vyao haviwawezeshi kupata chakula cha kutosha.

FEWS imebainisha kwamba tatizo la upatikanaji wa chakula hapa nchini litaendelea hadi mwezi Julai mwaka huu, hali itakayotishia kuongezeka kwa matatizo ya kiafya yanayosababishwa na kushindwa kupata milo kamili.

Kwa mujibu wa mtandao huo, upungufu wa chakula hapa nchini imetokana na kupungua kwa mvua za vuli ambazo zilitarajiwa kuanza Septemba hadi Desemba mwaka jana, hasa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Pwani na Tanga.

Kukosekana na mvua katika maeneo hayo, imetishaia usalama wa chakula, kuathiri ajira hasa sekta ya kilimo, kupunguza uwezo wa wananchi wa maeneo hayo kununua vyakula na kupanda kwa bei za vyakula.

“Kuna uwezekano mkubwa kwa familia maskini  kushindwa kupata chakula cha kutosha katika kipindi kilichofanyiwa tathmini,” FEWS imeseme kwenye taarifa iliyopo kwenye tovuti yake.

Pia, familia maskini kwenye mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mwanza na Shinyanga nao wanakabiliwa na matatizo ya upatikanaji wa chakula kutokana na kuchelewa kwa mvua za msimu.

“Kupungua kwa shughuli za mashambani kumeathiri vipato vya familia na wengi wao wameshindwa kupanda tena mazao mengine mashambani,” imesema taarifa hiyo.

“Mazao yatakayopatikana katika msimu ujao wa mavuno kwenye miezi ya Machi na Aprili yatakuwa kidogo na hali hii itawaondolea familia nyingi uwezo wa kupata chakula na kuongeza utegemezi wao kwenye masoko.”

Kwa mujibu wa mapitio ya uchumi kwa mwezi Novemba mwaka huu ya benki kuu ya Tanzania, bei za mazao yote ya chakula isipokuwa mpunga  zilipanda kwa mwezi Oktoba ikilinganishwa na Oktoba mwaka juzi.

Bei ya jumla ya mahindi kwa mwezi Oktoba mwaka jana ilifikia shilingi 64,054 kwa kilo mia moja kutoka shilingi 58,000 za mwezi Oktoba mwaka jana, ambayo ni ongezeko la asilimia 10.4.

Kwa mujibu wa BOT bei ya jumla ya kilo mia moja ya maharage nayo ilipanda hadi kufikia shilingi 185,466 Oktoba mwaka jana kutoka shilingi 164,536 za Oktoba mwaka juzi na vilevile bei ya mtama nayo ilipanda kwa asilimia 26.4 katika kipindi hicho.

Hata hivyo, bei ya jumla ya mchele, ambao ni moja ya vyakula vikuu kwa watanzania, ilishuka katika kipindi hicho hadi kufikia shilingi 145,466 mwezi Oktoba mwaka jana kutoka shilingi 170,588 za Oktoba mwaka juzi.

Tathmini ya awali ya uzaliahaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2015/2016 na upatikanaji wa chakula mwaka 2016/2017 inaonyesha kuwa kitaifa uzalishaji wa chakula utafikia tani 16,172,841 za chakula kwa mlinganisho wa nafaka.

Kwa mujibu wa wizara wa kilimo, mifugo na uvuvi nchi ina hali ya chakula kwa kiwango cha utoshelevu ambapo kuna ziada ya asilimia 23.

Hata hivyo, wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wameiomba serikali kufanya tathimini ya uhaba wa chakula kote nchini ili iwe na majibu sahihi ya hali iliyopo.

Walisema hivi karibuni kuwa kuna baadhi ya mikoa kuna hali mbaya sana ya ukame na inatishia uhaba wa chakula na kinachotakiwa kufanywa na serikali kufanya tathimini ya kina na kuja na majibu sahihi na nini cha kufanya kutokana na tathimini hiyo.

Makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara ya kilimo mifugo na uvuvi kwa mwaka 2016/17 yaliyosomwa Juni mwaka jana yalionyesha kwamba hali ya chakula mwaka 2015/2016 iliendelea kuimarika kutokana na mavuno mazuri na ya ziada yaliyopatikana msimu wa kilimo wa 2013/2014 na 2014/2015.

Vilevile, tathmini ya uzalishaji iliyofanyika mwezi Agosti 2015 nchini ilibaini kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa 2014/2015 ulikuwa tani 15,528,820 zikiwemo tani 8,918,999 za nafaka na tani 6,609,821 za mazao yasiyo ya nafaka.

Kiasi hicho cha chakula kikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 ya tani 12,946,103 (8,190,573 nafaka na 4,755,530 si nafaka) kinaonyesha kuwepo kwa ziada ya tani 2,582,717 za chakula.

Kutokana na hali hiyo, taifa limejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120 ambapo katika Mikoa 25 ya Tanzania Bara mikoa tisa ilibainika kuwa na ziada, sita utoshelevu na sita uhaba.

Hata hivyo kiwango hicho cha utoshelevu (asilimia 120) ni pungufu kwa kile cha mwaka 2014/2015 (asilimia 125) kwa asilimia tano.

Pamoja na utoshelevu huo, tathmini ilionesha uwepo wa Mikoa 18 yenye maeneo tete katika Halmashauri 69.

Ili kukabiliana na upungufu wa chakula nchini, katika mwa 2016/2017 Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI ilielekeza kila kaya iwe na mazao yanayostahimili ukame kwa ajili ya akiba.

Mwishoni mwa wiki jana, waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba alisema nchi ina chakula cha kutosha wala siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi. 

Dk Tizeba alisema Wakala wa Hifadhi ya Akiba ya Chakula (NFRA) ina na akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani milioni 16 ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula hivyo wakala haukununua chakula kingi. 

Pamoja na majibu mazuri ya waziri, hali inaonyesha kwamba suala la uhaba wa chakula bado halijafanyiwa tathmini ya kutosha ili kuweza kuja na majibu yenye uhakika.

Tathimini hii ingeweza kujikita kufanya mapitio ya kuangalia je tatizo hili limesababishwa na kushuka kwa uzalishaji, kuisha kwa akiba ya chakula, uhaba wa mvua, kupanda kwa bei ya chakula ama kupungua kwa uwezo wa watanzania kununua chakula.

2 thoughts on “Nani anasema ukweli kuhusu hali ya chakula?”

  1. Eliazari Machumu serengeti , mara says:

    Hiv serikali hii inaogopa mini kusema Tanzania kuna upungufu wa chakula na tishio la baa la njaa? Watu huku hatuoni mvua, mazao yameshakauka siku nyingi, tumekata tamaa na tunaishi kwa matumaini, hela hakuna, vyakul vimepanda being tunayasubiri mauti yatokanayo na njaa lkn wenye serikali wanakanusha hili? Hii inasikitisha sana

  2. SIRAM says:

    Duh !!

    Tutubie tu,

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *