Makala
Nani kasema nini, kasimamia nini katika mkutano uliopita wa Bunge?
Mwandishi Wetu
Toleo la 226
15 Feb 2012
Mbunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe
  • Tamko la Ikulu lawakinga wapinga posho akina Zitto, Januari
  • Waondoka Dodoma wakiwa mashujaa wa kupinga posho
  • Anne Kilango atibua mambo Katiba mpya, Mbowe atuliza joto
  • Ni Bunge lililochochea madaktari kudai posho zaidi

Mwandishi Wetu aliyehudhuria mkutano wa sita wa Bunge uliokwisha wiki iliyopita mjini Dodoma. Katika makala hii, anasimulia kwa kifupi kilichojitokeza, ili kufahamu mengi endelea kusoma.

SAA 11 jioni, Februari 10, mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa sita wa Bunge la Tanzania, ikiwa ni ishara ya kuhitimisha siku takribani tisa za majadiliano bungeni.

Zilikuwa siku chache lakini zilizoliweka Bunge katika mwelekeo mpya. Siku ambazo, ziliibua wabunge mashujaa wa kupinga ongezeko la posho kwa wabunge wenzao, huku tamko la Ikulu kwamba Rais Jakaya Kikwete hakuwa ameidhinisha posho hizo likiwaongezea ujasiri, sambamba na nguvu za umma, lakini pia, madai ya nyongeza hiyo ya posho yakizidi kuwapa nguvu madaktari kudai posho zaidi na maslahi mazuri ya kazi.

Mambo matatu makubwa yalijitokeza. Kwanza, ni lile linaloweza kutajwa kama mabishano kuhusu nyongeza ya posho, kuanzia kwenye duru za uongozi wa Bunge na wabunge, wananchi na Ikulu.

Pili, ni suala la mgomo wa madaktari ambalo lilikuwa likizidi kutanuka kwa kadiri siku za mkutano wa Bunge zilivyokuwa zinapungua. Lakini tatu, ni muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011.

Katika masuala hayo matatu, wananchi, kama walivyokuwa wabunge, nao walikuwa na maoni yao na makundi hayo yote yalitegemea vyombo vya habari katika mawasiliano yao kupitia maoni. Turejee kilichojiri kama ifuatavyo. 0Nyongeza ya posho kwa wabunge.

Vuguvugu la kupinga nyongeza ya posho mpya za wabunge lilianza kufukuta tangu mkutano wa tano wa Bunge, uliokwisha Novemba, mwaka jana.

Ni wakati huo ambao, vyombo vya habari vilinasa taarifa hizo na kuzifikisha kwa umma. Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, alijitokeza na kueleza hakuna posho mpya zilizolipwa kwa wabunge.

Lakini bila kuzingatia kuwa Dk. Kashilila ndiye mlipaji wa posho hizo (accounting officer), Spika Anne Makinda, ambaye hata hivyo, ndiye msemaji wa Bunge kama mhimili, aliutangazia umma kuwa wabunge wameanza kulipwa posho hizo.

Mkanganyiko ukajitokeza. Ofisi moja, mtendaji mkuu na msemaji mkuu wa mhimili wakawa na kauli tofauti. Lakini baada ya uchunguzi, ukiwamo wa gazeti hili, ilibainika kuwa posho ni lazima ziidhinishwe na Rais ndiyo zianze kulipwa na kwa hiyo, Rais alikuwa bado hajaidhinisha.

Lakini wiki moja kabla ya kuanza mkutano huu wa Bunge, Waziri Mkuu, Pinda, alikutana na wahariri wa vyombo vya habari ofisini kwake Dar es Salaam . Hapo aliulizwa kuhusu nyongeza hiyo na kilichotokea Ikulu, akiwa kama kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni.

Akajibu ya kuwa suala hilo limeshatoka Ikulu na liko mikononi mwake naye atalifikisha kwa wabunge, lakini akitetea hakuna tatizo wabunge kulipwa posho hizo, pengine tofauti na malalamiko ya wananchi kupitia makundi yao maalumu.

Lakini wakati wote, bila shaka, wabunge wengi, pengine ukiondoa wawili, Zitto Kabwe na Januari Makamba, mioyo yao ilikuwa ikiwalaani wote waliokuwa wakipinga ongezeko hilo , ambalo kwao lingezidi kuongeza pengo kati ya wabunge na wapiga kura wao.0Hali hiyo ya mioyo ya wabunge hao kulaaini (kimya kimya) wanaopinga posho inatajwa kujitokeza wakati wa kikao cha wabunge wote, siku moja kabla ya kuanza mkutano wao mjini Dodoma . Kilikuwa kikao cha kupeana mihtasari kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa.

Zitto, Januari mashujaa dhidi ya nyongeza

Katika kikao hicho, kinyume cha hali ya kawaida, mjadala wa posho ulifunika karibu kila kitu. Na bila shaka, wito wa ‘laana’ dhidi ya wapinzani wa posho mpya ulishika kasi.

Lakini hata hivyo, ‘laana’ hiyo haikuwa na nguvu. Ndani ya kikao hicho, Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) na Januari Makamba, Mbunge wa Bumbuli- Tanga (CCM), waligeuka ngome ya wananchi wengi dhidi ya mashambulizi hayo.

Kwa lugha rahisi, ni kama vile wananchi wengi wapinga ongezeko hilo walitanguliza kikosi chao hicho kidogo mbele ya jeshi kubwa lenye njaa ya posho mpya. Ni kama vile ndani ya kikao hicho, Januari na Zitto walishindwa ingawa pia, hawakuwa mateka wa kikao hicho, waliendelea na msimamo wao.

Lakini tofauti na Zitto, taarifa za kina zinaeleza kuwa Januari aliweza kuungwa mkono na kijana mwenzake ndani ya sekretariati ya CCM, Nape Nnauye.

Hawa walikuwa katika mawasiliano ya karibu ‘kukabiliana’ na nguvu kubwa ya wabunge wa chama chao. Lakini mbali na ‘mtandao’ huo wa Zitto, Januari na Nnape kwa upande mmoja, Ikulu ni kama ilikuwa nyuma yao .

Ilibidi Ikulu kujitokeza mbele kusaidia ‘mtandao’ huo mdogo lakini wenye kuungwa mkono na wananchi. Baada ya Spika kutaka kuuaminisha umma kuwa Rais ameidhinisha posho mpya, Ikulu ilitoa taarifa fupi, ikieleza Rais hakufanya hivyo, isipokuwa amewataka wabunge kutumia busara katika suala hilo la posho.

Na hatimaye, Naibu Spika, Job Ndugai, akajitokeza na kusema, hakuna nyongeza ya posho mpya. Lakini wakati wote, mjadala mwingine uliokuwapo ni wapi fedha hizi za ziada za kulipana posho zitapatikana.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini, mpango wa kuchukua fedha hizo kutoka katika mradi wa ujenzi wa nyumba za wabunge ( Bunge Village ) ambao ulipangwa kufanywa kwa kushirikisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Hii haikuwa safari rahisi kwa Januari na Zitto, ambao muda wote ilibidi, hata hivyo, wafanye kazi nyingine za kitaifa na wabunge wenzao wenye uchu wa posho mpya.

Inaelezwa, posho ziliwaunganisha wabunge wa kambi zote, upinzani na chama tawala, kasoro hao wabunge wachache, ingawa wengine walichagua kukaa kimya, lakini angali mioyo yao ikitamani posho mpya.

Katika hali ya kipekee, Zitto na Januari wamefanya kazi kubwa kwa niaba ya sehemu kubwa ya wananchi, angalau kuna fedha fulani zitafanya kazi ya maendeleo tofauti na ambavyo uamuzi wa posho mpya ungeidhinishwa, ingawa pia ni vigumu kupima namna matumizi hayo ya fedha iliyookolewa yatakavyokuwa.

Bunge na mgomo wa madaktari 0Wakati wabunge wakiwa katika mvutano wa kung’ang’ania posho mpya, madaktari nao walikuwa wakidai nyongeza ya posho, mazingira bora ya kazi na kuthaminiwa kama watalaamu muhimu kwa Taifa.

Ni kweli, kwa muda mrefu, kama ilivyo kwa walimu, madaktari hawakuthaminiwa kama ilivyotarajiwa. Umuhimu wao ulitambuliwa na kiongozi au raia mmoja mmoja, tena baada ya kutibiwa na kunusurika kifo.0Mengi ya madai yao yalikuwa ya msingi. Lakini nao walidai katika njia isiyomuadhibu aliyepaswa kuwa mfano wa kwanza kuwathamini, yaani Serikali. Wenzetu hawa waliwaadhibu waliovunjika viungo kwa ajali au wanaohitaji upasuaji. Kwa ujumla, waliwaadhibu wagonjwa wenye maumivu makali, na hasa wale masikini ambao husaka tonge juani kila kukicha.

Wakati madaktari wakiwa katika “malumbano ya hoja” dhidi ya maofisa waandamizi wa Serikali, wagonjwa walikuwa wakijigeuza vitandani wodini kubahatisha kama kwa kufanya hivyo, wangepunguza maumivu makali ya ugonjwa unaowasumbua.

Kwa hiyo, wakati madaktari wakirejea kwenye makazi yao kuungana na familia zao baada ya kutwa nzima kulumbana na Serikali, wagonjwa wenyewe waliendelea kufuta machozi ya maumivu makali na ndugu zao, wakiomba Mungu mgonjwa wao apate uhai wenye maumivu kidogo kidogo hadi mgomo uishe.

Masikini, macho ya wagonjwa yalizidi kumwagika, wakaanza hospitali ikiwamo ya Rufaa Muhimbili. Sehemu kubwa ya vitanda wodini vikabaki wazi, wagonjwa wengine waliitwa na Mwenyezi Mungu kwenye pumziko la milele, wakiwa na alama za ugonjwa ambao ungeweza kutibiwa na madaktari waliogoma. Wengine ambao hawakuitwa na Mwenyezi Mungu, kwa uchungu waliondolewa na ndugu zao kwenda kutibiwa wanakokujua.

Kwa ujumla, mawasiliano ya kitabibu kati ya mgonjwa na tabibu yalikatika, yakabaki mawasiliano kati ya viongozi wa Serikali wenye afya na madaktari wenye afya tele.

Katika wakati wote huo wa wagonjwa kulowesha magodoro ya hospitali kwa machozi ya maumivu, wabunge ambao ni majeruhi wa posho mpya, wakaanza kupata uchungu, wakikumbuka wanaoteseka ni wapiga kura wao, ingawa Uchaguzi Mkuu ni mwaka 2015, lakini lazima kutambua uchaguzi mdogo unaweza kutokea kabla popote nchini.

Wabunge sita tofauti, walijaribu kutaka muhimili huo wa dola ujadili suala hilo , hao ni pamoja na John Mnyika wa Ubungo (CHADEMA), Godfrey Zambi wa Mbozi Mashariki (CCM) na Peter Serukamba-Kigoma Mjini (CCM). Dhamira ya wabunge hawa haikutimia.

Bunge likaamua kumpa nafasi kushughulikia kadhia hiyo, Waziri Mkuu Pinda, ambaye mwanzo wa mgumu alitoa tamko madaktari warudi kazini, wasipofanya hivyo watakuwa wamejifukuzisha kazi. Pinda alitoa kauli hiyo, wakati Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, Naibu Waziri, Dk. Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa Wizara, Blandina Nyoni, wakiwa katika mvutano mkubwa na madaktari, ikiaminika wao ni chanzo cha tatizo.

Kwa hiyo, mawasiliano yalikatika kati ya uongozi wa wizara na madaktari. Madaktari walitii agizo la Waziri Mkuu, wakaripoti kazini lakini bila kufanya kazi, wagonjwa wakizidi kulia kwa maumivu.

Joto la Bunge kutaka kujadili suala hilo likazidi kiasi cha uongozi wa Bunge, chini ya Spika Makinda, ukakabidhi jukumu hilo kwa Kamati ya Huduma za Jamii inayoongozwa na Margreth Sitta. Waziri Mkuu akarudi Dar es Salaam kutoka Dodoma ili kukutana na madaktari Jumatano wiki ya mwisho kabla Bunge kukamilisha mkutano wake wa sita.

Katika kikao hicho, Katibu Mkuu, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu, Dk. Deo Mutasiwa, wakasimamishwa kazi na Rais Kikwete akaachiwa kibarua cha kuamua hatua ya waziri na naibu wake. Madai ya ongezeko la posho na mazingira mazuri kwa madaktari yakasilizwa na kutolewa uamuzi wa kuridhiwa na Waziri Mkuu.

Madaktari wakachukua sindano, mikasi ya upasuaji kurejea wodini lakini loo, wagonjwa wengine walikwishaitwa na Mwenyezi Mungu kwenye pumziko la milele kwa kukosa matibabu wakati wengine wakiwa wameamua kwenda kujiuguza nyumbani, yaani, idadi ya madaktari ikawa kubwa kuliko wagonjwa pale Muhimbili kwa mfano. Hapa, tunajifunza kuchukua hatua za haraka kabla maafa, hasa maafa yanayogusa uhai wa Watanzania.

Shukurani kwa madaktari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliofika Muhimbili kusaidia kazi wakati wa mgomo, inawezekana wameokoa maisha ya baadhi ya Watanzania wenzetu, Mungu awajaalie.

Itaendelea toleo lijalo

 

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.