Nani mwenye jeuri ya kununua Simba na Yanga?

VUGUVUGU la kutaka mabadiliko katika uendeshaji wa klabu za soka nchini; hasa klabu za Simba na Yanga, zimeonesha kuna tatizo kubwa la uongozi katika kalbu hizo kuliko inavyodhaniwa.

Tatizo kubwa kabisa walilonalo viongozi wa timu hizi mbili kubwa ni kutokufahamu kabisa thamani halisi ya taasisi wanazoziongoza kiasi kwamba hamu yao ya kubadilishana almasi na goroli haimithiliki.

Viongozi wa klabu hizi mbili kubwa wameshindwa walau kujiuliza swali moja tu la msingi ‘Kwa nini Simba na Yanga tu?’ Viongozi wa klabu hizi mbili walau wangepata muda wa kujiuliza swali hili, hakika wasingeweza hata kufikiria kuisogolea mikataba hiyo ambayo haina tofauti na mkataba wa Chifu Mangungo wa Msowelo na Karl Peters enzi hizo.

Kuwepo tu kwa majadiliano ya uuzwaji au ukodishwaji wa klabu hizi mbili , kunaonesha kuwa viongozi wa klabu hizi mbili hawafahamu thamani halisi ya klabu wanazoziongoza. Ukifahamu thamani ya klabu hizi mbili ni lazima utajiuliza nani mwenye hiyo jeuri ya kununua Simba au Yanga?

Inawezekana pia si viongozi tu wa Simba na Yanga wasiojua thamani halisi ya klabu hizi mbili kumbe pengine hata wanachama na washabiki hawafahamu thamani ya klabu hizi mbili.

Kama ambavyo watoto wengi wasivyo fahamu thamani ya mali za urithi kutoka kwa wazazi wao, inawezekana hali ndivyo ilivyo pia kwa wanachama na washabiki wa Simba na Yanga. Hawafahamu thamani ya mali waliyoihangaikia wazazi wao sasa wao wanataka kuitoa kwa bei ya kutupa kuwanufaisha wengine wenye kufahamu thamani ya ‘almasi’ hiyo.

Thamani halisi ya Simba na Yanga ni ipi basi?

Wengi wetu wanafikiri thamani ya Simba na Yanga ipo tu kwenye uchumi na kwenye kushinda vikombe vya mpira. Thamani ya Simba na Yanga ni kubwa zaidi ya thamani ya kiuchumi na thamani hizo zikiwekwa katika mizani ya fedha, basi ni muhimu tujiulize kama kweli yupo mwenye kuweza kukodisha au kununua Simba au Yanga?

Thamani ya Malengo.

Timu hizi mbili zenye chimbuko la kihistoria kuwa timu moja ya New Young zilianzishwa kwa lengo la kudumisha udugu, mshikamano, kufahamiana, kushirikiana katika mambo ya kijamii kubwa likiwa kuzikana.

Timu hizi ziligawanyika kutokana na upendeleo wa upangaji timu timu ya New Young uliposhiriki ligi katika serikali ya kikoloni. Baada ya kuona vijana wanaotokea mitaa ya Jangwani na Twiga ndio wanaopangwa kila mechi huku timu ikifanya vibaya, wazee wa mitaa ya Msimbazi na Gerezani wao wakaamua kujitoa na kuanzisha timu yao.

Muhtasari wa historia ya timu hizi unaonesha thamani ya malengo waliyojiwekea, kuunganisha watu, watu kuwa wamoja. Lengo hili limefanikiwa kwani mpaka leo nchi imeunganishwa kiasi kwamba sehemu kubwa ya Watanzania ni washabiki wa mojawapo ya timu hizo mbili.

Watu wanafahamiana, wanajenga urafiki kwa usimba na uyanga. Watoto wanazaliwa wanakuwa Simba au Yanga. Nani asingependa lengo hili libaki? Lengo hili thamani yake kifedha ni shilingi ngapi?

Tumewahi kujiuliza kwa nini lengo hili linafanikiwa?Jibu ni rahis sana, lengo hili linafanikiwa kwa kuwa Simba na Yanga ni mali ya Watanzania wote, mali ya umma, si mali ya mtu binafsi. Kila Mtanzania anajisikia huru kujiunga kwani hawi chini ya mtu yeyote, hamtumikii yeyote, anajitumika mwenyewe.

Simba na Yanga zimekuwa alama ya uhuru wa Mtanzania. Simba na Yanga zimedhihirisha nguvu waliyonayo Watanzania pasipo kuwa na fedha, Simba na Yanga zimedhihirisha Umoja na Mshikamano una nguvu kuliko fedha.

Zilikuwapo timu zilizoundwa na serikali ya kikoloni kabla ya uhuru lakini timu hizo leo ziko wapi? Ziko wapi timu zilizochukuliwa na kununuliwa kwa mbwembwe na matajiri na watu wenye kudhaniwa kuwa na maarifa ya uongozi?

Mifano ya timu za matajiri zilizoshindwa kufikia malengo na hatimae kufa ipo mingi.Hii inatudhihirishia uendeshaji wa hizi klabu hauhitaji fedha tu bali kuna mambo mengine pia.

Thamani ya kihistoria.

Simba na Yana zina thamani ya kihistoria kwani zimeanzishwa kabla ya nchi kupata Uhuru.Timu hizi zilianzisha na wazee wetu ambao tunawaona hawakuwa na elimu ya kutosha ya darasani. Klabu hizi katika vuguvugu la uhuru zilitumika kama sehemu za kukutania wanaharakati pasipo kushukiwa na serikali ya kikoloni katika mwavuli wa michezo.

Hivyo historia ya Simba na Yanga inabeba historia ya nchi. Historia hii ina thamani gani ikipimwa katika mizani ya kifedha? Nani mwenye uwezo wa kuinunua historia hii? Tunafahamu historia hii haimpendezi kila mtu. Kuna watu inawasuta na inaonesha ujanja na maarifa waliyokuwa nao wazee wetu.

Kuna watu hawapendi kabisa kuona maarifa yaliyotokana na Waafrika Weusi nyakati za kikoloni kuenziwa kwani Waafrika tulionekana hatuwezi kufikiri.

Kweli leo tunataka kuuza na kukodisha historia hii? Hii pia ni alama ya kuonesha maarifa tuliyokuwa nayo yalikuwa yanafaa kwa mazingira yetu kwani miaka kadhaa baadaye, watu wenye elimu nzuri na pesa nyingi wameshindwa kabisa kutengeneza klabu kama Simba na Yanga na badala yake wanataka kutumia nguvu kupora ‘intellectual property’ ya makabwela wasio na shule, ajabu!

Elimu zao za Harvard na pesa zao zimeshindwa kabisa!

Thamani ya Utani wa Jadi

Utani wa jadi wa Simba na Yanga unaweza kuuthaminisha kwa fedha kiasi gani? Tumeona hapa timu zimeanzishwa kwa kiasi kikubwa cha fedha lakini je hizo fedha zinaweza zikanunua utani wa jadi na timu nyingine? Fedha inawezaje kufanya hilo?

Tukiamua kuupa thamani ya fedha utani wa jadi wa Simba na Yanga tuupe shilingi ngapi? Utani wa Simba na Yanga ambao siku ya mechi unafanya zaidi ya nusu ya Watanzania wote kufuatilia una thamani gani?

Taasisi gani hapa Tanzania inayoweza kukusanya watu wengi kiasi hicho katika kitu kimoja kama utani wa Simba na Yanga? Je tunafahamu thamani ya hiyo kitu?

Thamani ya Idadi ya Mashabiki.

Ukweli usiopingika ni kuwa ushabiki wa Simba na Yanga umegawa taifa katikakti. Mwenyekiti wa klabu moja nchini akimwandikia barua Rais John Magufuli alijinadi kuwa yeye ni kiongozi wa taasisi yenye wafuasi zaidi ya milioni ishirini. Kama klabu moja ina wafuasi milioni ishirini basi tufanye na klabu nyingine pia ina wafuasi milioni ishirini.

Je, tukiamua kumpa thamani kila mshabiki mmoja wa klabu tutampa thamani ya fedha kiasi gani? Kila mtu afikirie thamani ya mshabiki mmoja halafu azidishe mara milioni ishirini kupata angalau thamani ya ushabiki tu wa kila timu.

Hivi washabiki wakihamasishwa ipasavyo kama walivyohamasishwa kuchangia madawati kwa hiyo thamani ya kila mshabiki kuna haja kweli ya kuuza au kukodisha hizi klabu?

Thamani ya Majina.

Hivi tumeshawahikufikiria thamani ya majina ya hizi timu zetu ndani na nje ya nchi? Tunaweza kufanya nini na thamani ya majina ya timu hizi? Simba na Yanga kwa majina yake na uwepo wake tu haziwezi kuwa amana benki? Kama zikiamua kwenda benki kukopa zinaweza kukopeshwa shilingi ngapi?

Hivi hizi timu zikiamua kujitambulisha na Benki mfano Yanga ijitambulishe na CRDB na Simba ijitambulishe na NBM na kuwahamasihsa wanachama wao wawe wateja wa mabenki hayo na kuanda programu za kuwatangazia masoko, haya mabenki ya wazawa na hizi klabu kwa kutumia majina yao tu watapata kiasi gani cha fedha kwa mwaka?

Hizi taasisi au watu binafsi wanaotaka kununua au kukodishwa vilabu vya Simba na Yanga zina ukubwa gani? Utajiri wake una thamani ipi ya kifedha? Maana vinginevyo, ninachokuja kukiona mimi ni kitendo cha taasisi ndogo kuja kununua taasisi kubwa.

Thamani ya Wanachama Maarufu

Ndani ya klabu hizi kuna wanachama maarufu ambao wana heshimakubwa na wafuasi ndani na nje ya nchi. Hivi watu kama hawa, mfano Rais Mstaafu Jakaya Kikwete thamani yake ni ipi unapoamua kuinunua timu ambaye yeye ni mwanachama. Inawezekana tukaamini kila mwanachama ana thamani sawa lakini je hii ni kweli?

Rais mstaafu wa nchi anakuwa mwanachama katika klabu inayomilikiwa na mtu au Waziri Mkuu aliye madarakani anakuwa mwanachama katika klabu ya mtu binafsi?

Kuwa na wanachama wenye nyadhifa na umaarufu kama hawa katika klabu ambayo haimilikiwi na mtu yeyote kunaonesha mchangamano wa Watanzania wa kada mbalimbali katika masuala ya jamii. Klabu ikiuzwa mwenye mali anaweza akaamua kuweka mashrti mapya ambayo yatawaengua na kuwatenga wengine.

Thamani ya Waasisi

Hizi klabu mbili zimeasisiwa na watu wanaotajwa kuwa makabwela hasa kwa Yanga  na ndio maana ya ile alama yake maarufu ya kandambili. Vivyo, hivyo kwa wasomi na watu wa kada ya kati kuhusishwa na Simba.  Thamani ya hawa majirani, marafiki na watani wa Kariakoo ni ipi?

Thamani ambayo imekua na kubaki mpaka hii leo ikiendelea kukua? Dhahiri kuwa kama hakuna klabu nyingine iliyoanzishwa kuzifikia klabu hizi mbili, basi thamani yao ni kubwa sana. Je kuienzi thamani hiyo ndio kwa jinsi ya kuamua kuiuza au kuikodisha?

Kwa nini thamani yao isiachwe kwa kadri ya maono yao ili ije kuwa simulizi na chanzo cha kutolea maarifa kwa vizazi vijavyo? Kama wazo lao limedumu kwa zaidi ya miaka sabini pasipo kuhitaji fedha za matajiri, iweje leo tupate hamu ya kusambaratisha na kupondaponda juhuhudi na kujitoa kwa wazee wetu hawa?

Thamani ya Ulinzi na Usalama

Tumeona kuwa Simba na Yanga zimegawa taifa katika makundi mawili ya wafuasi. Kwa sasa, Simba na Yanga ni utani, udugu, urafiki, majigambo na hatimaye mshikamano. Lakini Simba na Yanga zinaweza kutumika kukuza uadui, uhasama, visasi, vurugu na vita.

Washabiki wanaoingia uwanjani wakitaniana kwa furaha huenda wakaishia kupigana na kuumizana kama upande mmoja unaona hautendewi haki. Simba na Yanga kuwekwa mikononi mwa wafanyabiashara ni jambo la hatari sana. Wafanyabiashara hawaachi kuhasimiana na hawachagui silaha wakihasimiana.

Tumeona katika Tanzania hii, mfanyabiashara mmoja akiwakosesha mamilioni ya washabiki wa mpira kuangalia mpira katika runinga timu yake ikicheza kwa vile tu amehasimiana na mdhamini anayerusha matangazo hayo mubashara.

Mfanyabiashara yule hakujali maslahi ya wanachama na washabiki wa timu yake na Watanzania wapenda soka kiujumla. Hakuna kitu chochote kinachotuhakikishia kama tabia ile hatokuwa nayo tena.

Hatuna uhakika kama hao wanaotaka kukodisha na kununua hizi klabu hawatahasimiana. Hivi hawa wafanyabiashara wakihasimiana na wakaamua kutumia Simba na Yanga kama silaha ya kupigania tutapona?

Simba na Yanga zinatusaidia kuimarisha ulinzi na usalama nchini mwetu. Watu wanafahamiana, wanaingiliana, wanatambuana, wanataniana kwa kutumia Simba na Yanga.

Kwa kufanya hivyo kunaongeza udugu, upendo na urafiki miongoni mwetu. Thamani ya hili ni kubwa kuliko makombe ya Ubingwa Afrika. Tukikosa ubingwa wa Afrika tutaendelea kubaki kama taifa. Tukikosa amani na mshikamano hatutobaki kama taifa.

 Kuna vitu vya thamani katika Simba na Yanga kuliko ubingwa. Viongozi wa klabu hizi yawapasa kutambua thamani halisi ya klabu zao. Hapa zimeanishwa thamani chache sana ili kutufanya tufikiri, kuna wengi mnazozifahamu thamani nyingine nyingi za klabu hizi kuliko zilizoandikwa kwenye makala hii.

Tafadhali tuziibue na kwa pamoja tuwaambie hawa wenye kujinasibu kuwa na  nia ya kuendeleza soka la nchi hii waanzishe klabu zao zikiwa na malengo mwafaka na matakwa yao.

Watuachie Simba na Yanga zetu kwani zinabakia na malengo yake na  tukizipa thamani halisi hakutakuwa na mwenye jeuri ya kuweza kununua wala kukodi klabu yeyote kati ya hizi klabu mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *