Natamani Kiba na Diamond wasipatane

KAMA wewe ni shabiki wa muziki wa kizazi kipya, ni lazima utakuwa unafahamu kuhusu miamba miwili inayotamba hapa nchini hivi sasa; Diamond na Ali Kiba.

Kwa sasa, hawa ndiyo mabalozi wakubwa zaidi wa muziki wa Tanzania. Bila wao, pengine leo tungekuwa tunazungumza mengine kuhusu muziki huo.

Kwa bahati nzuri, miamba hawa wawili wametengeneza aina ya ushindani unaoelekea kuwa kama uadui. Ni ushindani wa nani zaidi baina yao. Ni ushindani ambao unahitajika kwenye muziki.

Mara ya mwisho kwa wasanii wa Tanzania kuwa na ushindani wa namna hii ilikuwa yapata miaka saba iliyopita. Kulikuwa na waigizaji wawili maarufu wa filamu hapa Tanzania. Mmoja akiitwa Vincent Kigosi (Ray) na mwingine akiitwa Steven Kanumba (Mungu amrehemu).

Wasanii hawa walikuwa na upinzani mkali katika wakati ambao naweza kusema ulikuwa wa dhahabu katika tasnia ya filamu hapa nchini. Kila baada ya miezi mitatu kulikuwa na filamu mpya kutoka kwa mmoja wa hao.

Kukaibuka kada ya watu walioitwa wasanii. Kukaibuka vibanda vingi vya kuuza filamu za Kitanzania. Wakati wote huo, Ray na Kanumba walikuwa wakiishi kama maadui. Huyu akisema hili, huyu anasema lile.

Tofauti ya ushindani wa Ray na Kanumba na huu wa Kiba na Diamond ni mitandao ya kijamii pekee. Wakati ule, ushindani wao ulichagizwa zaidi na magazeti ya udaku lakini sasa mitandao ndiyo inakoleza na kwa bahati nzuri inafika mbali zaidi kuliko magazeti.

Kwa bahati mbaya kwa tasnia, ingawa imani za kidini zinasema Mwenyezi Mungu huwa hakosei, Kanumba akatangulia mbele ya haki. Leo hii, takribani miaka minne baada ya kifo hicho, tasnia ya filamu imetetereka.

Ray anaendelea kutoa filamu kama kawaida lakini bila mshindani wake, kuna ladha inapotea. Na kwa sababu mtu aliyekuwa akimsukuma kufanya vizuri zaidi hayupo, hata kazi zake za siku hizi zinaonekana hazikui. Zina kiwango kilekile kilichokuwapo wakati Kanumba akiwa hai.

Ushindani wa Diamond na Kiba unakuza thamani ya muziki wetu. Kabla hajatoa wimbo wowote mpya, ni lazima mmoja wa hawa akune kichwa kujua utapokewaje na wapinzani wake. Matokeo yake ni kuwa ubora unaongezeka.

Ubora huo unapoongezeka, maana yake ni kuwa wanasababisha hata wasanii walio chini yao nao waongeze ubora wao. Hivyo kinachoonekana kuwa ugomvi wa watu wawili walio juu, kinasababisha makubwa katika mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya muziki hapa nchini.

Kwanini tunataka Diamond na Kiba wasiwe washindani wakati siku zote hatuombi Simba na Yanga zipatane na kuwa kitu kimoja. Kuna mtu amewahi kutoa hoja ya kupatana kwa Barcelona na Real Madrid au kwa Al Ahly na Zamalek?

Kinachofanya ushindani ukue, popote pale duniani, ni kuwapo kwa kani mbili zinazofutana. Kama hakuna kani mbili zinazoshindana, maana yake ni kuwa watu watakosa kitu cha kuamka na kuzungumzia.

Na ushindani huu wa Kiba na Diamond haupo hapa Tanzania pekee. Karibu katika michezo yote, sekta zote, kunakuwa na watu au taasisi zinazoleta changamoto inayosababisha kukua kwa tasnia husika.

Nakumbuka kwenye mchezo wa mbio za magari mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kulikuwa na upinzani mkali kati ya magwiji wawili, Alain Prost wa Ufaransa na Ayrton Sena wa Brazil.

Hawa walifikia hatua ya kutosalimiana wakiwa mashindanoni. Prost alikuwa mjivuni na Sena alikuwa mtu wa kujichanganya na watu. Ushindani wao ulikuwa kiboko.

Kwa bahati mbaya, Sena akafariki kwa ajali ya gari. Mashindano ya Formula One yalipoteza umaarufu hadi alipokuja kuibuka Michael Schumacher baadaye. Tatizo la Mjerumani huyu ni kwamba yeye alitamba peke yake. Hakuwa na mtu wa kumsukuma.

Nyakati za dhahabu za mchezo wa ngumi zilikuwa wakati Muhammad Ali alipokuwa akitukana wenzake ulingoni na majumbani kwao. Kuna tukio moja mashuhuri la Ali kwenda nyumbani kwa Sony Liston na kutoa maneno ya kashfa akidai kwamba mshindani wake huyo amefanana na nyani.

Ni wakati huo ambao pia Ali alikuja kutengeneza ushindani mkali na mwamba George Foreman. Hawa watu hawakuwahi kuwa marafiki. Ushindani ulikuwa mkali kiasi kwamba washabiki waligawanyika katika kambi mbili.

Faida ya ushindani wa namna hii ni kwamba mchezo wa ndondi ulikuja kukua katika kiwango ambacho kimesaidia leo akina Floyd Mayweather wanalipwa fedha za ajabu kwa kupigana kwa sekunde chache tu.

Huko Marekani ambako biashara ya muziki imekua kubwa kuliko kwingine kote duniani, hali hii ya nyota kutopatana ni ya kawaida. Kuna mifano inatolewa kuhusu kilichotokea kwa Tupac Shakur na Notorius BIG lakini ukweli ni kuwa upinzani wa jadi hitimisho lake si hili mara zote.

Wakati mwingine, wafanyabiashara wa sekta ya burudani hutengeneza uhasama miongoni mwa wasanii au wachezaji kwa sababu za kibiashara kabisa. Hii ni kwa sababu, binadamu, kwa asili, ni kiumbe anayependa mapambano.

Kama mwanadamu angekuwa muungwana, watu wasingekuwa wanajaa kwenye kumbi za Warumi kuangalia watumwa wakigombana na kuuana na wanyama wakali au wakiuana wenyewe kwa wenyewe.

Watu wasingekuwa wanajaa uwanjani kutazama wanaume wakicheza soka ambako ndani yake watu wanapigana viwiko, mateke, matusi na rafu mbaya za kila aina.

Binadamu, kwa asili, ni mtu anayependa kuona mateso kwa wengine. Na ndiyo sababu, kwenye baadhi ya vitabu vya sayansi, binadamu huwekwa katika kundi la wanyama. Tofauti kubwa ya wao na sisi ni kwamba sisi tunaweza kuchati kwenye simu zetu na wao hawawezi.

Mwenyezi Mungu ametupa ubongo wenye maarifa. Lakini, moyo wetu na miili yetu bado haijaondokana na chembe chembe za utesi wa kinyama.

Na ndiyo sababu, hata Diamond mwenyewe hivi sasa anajulikana pia kwa jina la Simba.

Nadhani wakati mwingine tunaogopa mambo yanayoleta faida. Uzuri wa ushindani wa aina hii ya Diamond na Kiba ni kwamba huwa haudumu milele.

Kama alivyopata kusema Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, mzee Ali Hassan Mwinyi, kila zama zina kitabu chake. Kwa vyovyote vile, hizi ni zama za Diamond na Kiba.

Zama zao zitapita na zitakuja zama nyingine mpya za watu wapya. Nina uhakika kwamba miaka mingi kutoka sasa, wale watakaokuwa hai wakati huo, watakuwa wanakumbushana kwamba kuna nyakati walishuhudia ‘bifu’ kati ya wasanii hawa wawili.

Wakati huo, huenda kutakuwa na vijana wengine wawili wanaosumbua katika anga ya muziki au filamu. Na nina uhakika kwamba wakati huo pia watakuwepo watu watakaosema kwamba ni vigumu mahasimu hao wakapatana na kuondoa uhasama.

Washauri hao pia watakuwa wamekosea wakati huo. Watakachokuwa wanakifanya ni sawa na kupambana kuzuia maji yasipite katika njia yake iliyozoea na hilo si jambo rahisi.

Natamani kwamba upinzani huu mkali kati ya Diamond na Kiba uendelee kama ulivyo na pengine uzidi. Kwa maana kama utaongezeka, wote watapata mafanikio zaidi na walio chini yao pia watafanikiwa.

Na nasema hivi kwa sababu najua kuwa ipo siku uhasama huu utamalizika kwa asili. Ataingia Simba mwingine sokoni na wale waliokuwepo watapotezwa.

Hivi ndivyo dunia ilivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *