KATIKA sehemu ya kwanza na ya pili ya makala haya, nilieleza chimbuko na udhaifu wa “Katiba ya Uhuru” ya mwaka 1961 na sababu za kufutwa kwa Katiba hiyo na kuandikwa “Katiba ya Jamhuri” ya mwaka 1962, ambayo nayo hata hivyo, kwa udhaifu kama ule wa Katiba ya Uhuru na pengine kuzidi huo, ilisababisha migomo mingi nchini, yakiwamo maasi ya Jeshi ya Januari, 1964.
Na ili kutibu udhaifu wa Katiba ya Jamhuri, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na TANU, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alielekeza na kuagiza kutekelezwa haraka kwa Azimio la TANU kwa Tanganyika kuingia kwenye mfumo wa chama kimoja kuwezesha chama kushika hatamu za nyanja zote za uongozi wa nchi na maisha ya Watanganyika.
Mpaka hapo, ni bayana kwamba si Katiba ya Uhuru wala Katiba ya Jamhuri, na hata hii ya chama kimoja iliyozaliwa baadaye; iliyotokana na mjadala wala ridhaa ya wananchi; ila kwamba, tabaka la “vibwenyenye uchwara” [petty bourgeoisie] nchini ndilo lililoelekeza/lililoamua kwa kuhodhi hoja, mabadiliko ya Katiba kwa kulazimishwa na mazingira, migongano ya kitabaka na mitafaruku ya ndani isiyozuilika, ili liweze kujiponya dhidi ya nguvu/ghadhabu ya umoja na kulinda maslahi binafsi.
Je, Katiba ya chama kimoja ililetwaje? Kupata jibu endelea na sehemu hii ya tatu ya makala hii.
Udikteta wa Chama na Muungano.
Wakati uamuzi wa kuingia mfumo wa chama kimoja tayari ukiwa umefikiwa na mchakato wa kuandaa Katiba mpya ukiendelea, kulitokea tukio moja kubwa na la aina yake nchini ambalo halikutarajiwa; nalo ni kuzaliwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Tunasema halikutarajiwa kwa sababu, si Rais wa Tanganyika [Nyerere] na Watanganyika wala Rais wa Zanzibar [Karume] na Wazanzibari, waliotarajia Muungano huo kwa sababu haukukusudiwa; ulitokea tu kwa kasi ya radi na ngurumo, na kufumba na kufumbua Muungano ukazaliwa.
Katika kipindi hiki, harakati za kisiasa na siasa kwa nchi zote huru barani Afrika zilijikita zaidi katika kuunda Umoja wa Afrika kwa kuanza na miungano ya kikanda kabla ya kufikia Muungano wa Afrika, na si kwa namna ya nchi moja moja kama zilivyofanya Tanganyika na Zanzibar.
Kwa hiyo, kwa kanda ya Afrika Mashariki agenda kuu ilikuwa ni kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki [EAF] likijumuisha nchi za Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar iliyotarajiwa kupata uhuru Desemba 1963.
Ukweli ni kwamba, wakati mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 yakifanyika, Nyerere alikuwa mjini Nairobi akikutana na Viongozi wenzake wa Kenya na Uganda kukamilisha mchakato wa shirikisho hilo.
Ni pale tu wenzake (Kenyatta na Obote) “walipomsaliti” kwa kutupilia mbali hoja ya shirikisho dakika za mwisho, ndipo Mwalimu alipoamua kukamata ‘kifaranga’ [Zanzibar] kwa shinikizo la mataifa makubwa, katikati ya vita baridi ya kimataifa na kuunda Muungano mdogo usiotarajiwa, ili angalau kulegeza koo baada ya Shirikisho la Afrika Mashariki kuota mbawa, ambalo nalo hata hivyo, lilikuwa likisimamiwa na kuratibiwa na mataifa makubwa kama ambavyo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulivyosimamiwa na kuratibiwa na mataifa hayo kukidhi sababu na matakwa yake ya kibeberu.
Tukio hili la Muungano lilisimamisha, kwa muda, mchakato wa Katiba ya chama kimoja kwa Tanganyika iliyobuniwa mwaka 1963 ili kuweza kushughulikia kwanza Katiba ya Muungano, ambayo kwa madhumuni ya makala haya, ni sehemu ya “Constitutionalism” nchini.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifikiwa kwa kutiwa sahihi Mkataba [Treaty] wa kimataifa uitwao “Hati ya Muungano” [Articles of Union] na wakuu wa nchi hizo – Julius Nyerere [Tanganyika] na Abeid Amani Karume [Zanzibar], na kuridhiwa na mamlaka za kutunga Sheria za nchi hizo [Bunge/Baraza la Mapinduzi] na kuwa sehemu ya Sheria za nchi hizo kwa ajili ya utekelezaji.
Maudhui ya Sheria ya Muungano yanatawala mambo mengi kwa nchi hizi, lakini hapa itoshe tu kutaja makuu machache yafuatayo: Kwanza, Sheria ya Muungano ni hati ya Kikatiba inayodhibiti Katiba ya Muungano na Katiba ya Zanzibar.
Pili, Sheria ya Muungano ndiyo iliyoanzisha Muungano tata wenye Serikali mbili ndani ya Muungano ambapo mambo kumi na moja [11] tu yaliwekwa chini ya usimamizi wa Bunge na Rais wa Muungano; na mambo mengine yote yalibakia na kuachwa kusimamiwa na Serikali za nchi husika, yaani Tanganyika na Zanzibar ambazo hazikuuawa na Muungano.
Kwa upande wa Tanganyika, mambo yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano yaliwekwa [kinyemela, kinyume na matakwa ya Mkataba wa Muungano] chini ya, na kusimamiwa na Serikali ya Muungano; wakati Zanzibar iliendelea kusimamia mambo yake yote yasiyo ya Muungano.
Aina hii ya Muungano imedumu na kubakia kwa njia ya kimbindembinde tu na kwa kubahatisha. Mabadiliko yote ya Katiba ya nyuma yaliendelea kuwa msingi mkuu wa “Constitutionalism” na yameingizwa katika Katiba ya sasa, ya mwaka 1977.
Tatu, Sheria ya Muungano ilibainisha utaratibu wa kufuata katika kupata Katiba mpya ya kudumu ya Muungano kwa kuteua Tume ya kupendekeza Katiba, na hatimaye kuitishwa kwa Bunge la Katiba [ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku ya Muungano] kupitisha Katiba hiyo.
Madhumuni ya utaratibu huo yalikuwa ni kuruhusu ushiriki wa watu wa nchi hizi mbili katika kujadili na kutengeneza Katiba ya Muungano wao. Hata hivyo, si Tume iliyoundwa, wala Bunge la Katiba kuitishwa katika muda uliowekwa na Sheria ya Muungano, kwani mchakato huo uliahirishwa kwa muda usiojulikana hadi leo hii. [Angalia Sheria ya Bunge ya kuahirisha, Na. 18 ya 1965].
Kwa kipindi cha kuanzia siku ya Muungano, Aprili 26, 1964, hadi Julai 1965 ilipopitishwa Katiba ya Muda chini ya mfumo wa chama kimoja, Serikali ya Muungano iliongozwa kwa Katiba ile ile ya Jamhuri ya Tanganyika iliyofanyiwa marekebisho kwa njia ya AMRI ya Rais [Decree] kuingiza mambo yote ya Muungano, na kujulikana kama “KATIBA YA MUDA”, hadi hapo Muungano utakapopata Katiba yake.
Sehemu ya Amri hiyo ya Rais iliyofanya Katiba ya Tanganyika kuwa ndiyo pia Katiba ya Muungano, ilisomeka hivi:
Ibara 1: “This Decree may be cited as the Interim Constitution Decree 1964, and shall come into operation on Union day”
Ibara 2: “Subject to the provisions of this Decree, the Constitution of Tanganyika shall have effect from the Commencement of the Interim Constitution…..”.
Katiba hii ya Tatu, kama zilivyokuwa Katiba zilizoitangulia, na kama pia jinsi Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ulivyofikiwa kinyemela, haikupitishwa na Bunge la Katiba, wala Bunge la kawaida kwa kujigeuza kuwa Bunge la Katiba; bali ni Katiba ile ile ya Jamhuri iliyorekebishwa na kubatizwa jina jipya kwa AMRI ya Rais – beberu na asiyeambilika, kama tulivyoeleza katika sehemu ya pili ya makala haya.
Nimekwishaelezea katika sehemu ya pili ya makala haya, jinsi uamuzi wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja ulivyofikiwa na TANU mwaka 1963; na jinsi ambavyo tume iliyoteuliwa na Rais kuona juu ya uwezekano huo ilivyonyimwa uwezo wa kubadili au kujadili uamuzi huo wa kiimla, ila kusema tu jinsi mfumo huo utakavyotekelezwa. Kwa nini Tume haikupewa uwezo huo?
Lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo, nionavyo mimi, lilikuwa na madhumuni makuu mawili: Kwanza, ni kuvuruga upinzani wa kisiasa ndani ya jamii iliyokabiliwa na mitafaruku, mikanganyiko na changamoto kufuatia tabaka la vibwenyenye uchwara kushindwa kuwasilisha matunda ya uhuru kwa wananchi wenye kiu ya maendeleo.
Pili, kumwongezea nguvu za kiimla, za kuzima hoja na changamoto, Rais asiyeambilika; si kwa njia ya vyombo vya dola pekee, bali [sasa] pia kwa njia ya Chama cha siasa [TANU] ambacho kilipewa ukuu juu ya Bunge la wananchi.
Tume iliyoteuliwa na Rais ilikamilisha Ripoti yake haraka na kuwasilisha kwenye kikao cha pamoja cha Halmashauri za TANU na ASP Mei 3, 1965, na uamuzi wa kikao hiki ndio uliozaa Katiba ya Muda ya 1965 [Sheria Na. 43 ya 1965] kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja!
Kufuatia uamuzi huo, vyama vingine vya sasa, vingi vikiwa vile vilivyoanzishwa baada ya 1962, vilipigwa marufuku. Kwa kutaja vichache, hivi vilikuwa ni pamoja na Chama cha People’s Democratic Party [PDP] cha Kasanga Tumbo, “The Nationalist Enterprise Party” [NEP] cha Yahya Hussein ambacho baadaye kiliungana na Chama cha “The People’s Convention Party” [PCP] cha Samson Mshalla, kuunda chama kipya cha “African Independence Movement” [AIM].
Vingine ni vyama vikongwe vya “African National Congress” [ANC] cha Zuberi Mtemvu, “United Tanganyika Party” [UTP]; huku Chama cha Kiislamu cha “All Muslim Nationalist Union of Tanganyika” [AMNUT] nacho hakikuweza kukwepa panga hilo.
Kana kwamba udhibiti huu haukutosha, miaka 10 baadaye, TANU, kwa kukabiliwa na migogoro, mitafaruku na ukinzani wa kitabaka wa ndani kwa ndani, mbali na uamuzi iliochukuliwa wa kufanya nchi kuwa ya chama kimoja, ililazimika pia kupiga nyundo ya mwisho kwa uhuru wa wananchi wa kujieleza kwa kutangaza ukuu mpya wa “Chama kushika hatamu” za nyanja zote za maisha ya Mtanzania, likiwemo Bunge ambalo sasa lilifanywa kuwa Kamati ya Chama, lenye kuwajibika kwa Chama na Serikali, badala ya kuwajibika kwa wananchi.
Hilo lilifanyika kwa njia ya Marekebisho ya Katiba kufuatia maamuzi ya Kikao cha Halmashauri Kuu [NEC] ya TANU, iliyokutana mjini Shinyanga, Machi 10 – 12, 1975, na marekebisho hayo kupitishwa na Bunge Juni 3, 1975.
Kwa heshima zote, nadiriki kusema kwamba, utaratibu uliotumika kutunga Katiba hii ya Tano haukuwa sahihi, na kwa TANU kujipa jukumu la kuitangaza Tanzania kuwa nchi ya chama kimoja. Chama hakikuwa na mamlaka hayo kwa sababu si kila Mtanzania alikuwa mwanachama wa TANU; wala vibwanyenye uchwara nchini havikuwa na haki wala mamlaka ya kuwakilisha tabaka la wajanja wenye kulinda maslahi yao, wala uwezo wa kuwachagulia mamilioni ya Watanzania hatima yao. Ilitakiwa kura ya maoni kuwakilisha matakwa ya wengi.
Nawasilisha pia hoja kwamba, kwa kuwa jambo la vyama vya siasa halikuwa la Muungano [Angalia ibara ya 4, Mkataba wa Muungano; na ibara ya 5, Sheria ya Muungano] Rais wa Tanzania, NEC ya TANU, Bunge la Tanzania, mtu au taasisi yoyote, haikuwa na mamlaka wala uwezo wa kuingiza katika Katiba ya Muungano, jambo [kama hilo] lisilo la Muungano!
Mbaya zaidi, Katiba hiyo ilipitishwa na Bunge la kawaida, badala ya Bunge la Katiba, na zaidi kwamba liligusa mhimili [structure] wa Muungano ambapo hata Bunge la kawaida lisingekuwa na mamlaka ya kutenda.
Kwa miaka 13 mfululizo tangu mwaka 1964, Jamhuri ya Muungano iliendeshwa kwa kutumia Katiba ya muda hadi ilipotungwa Katiba ya kudumu, mwaka 1977, ambayo nayo hata hivyo, kutungwa kwake, na jinsi ilivyosimikwa, kuna walakini unaokera.
Nimeeleza mwanzo kwamba, ilitakiwa Tume ya kupendekeza Katiba ya kudumu ya Jamhuri ya Muungano, mapendekezo ambayo yangewasilishwa na kupitishwa na Bunge la Katiba kabla ya Machi 26, 1965, jambo ambalo halikufanyika kutokana na mchakato huo kuahirishwa kwa muda usiojulikana kwa Sheria ya Bunge kutokana na kero za Muungano zilizokuwa zimeanza kujitokeza.
Hapa maswali mengi yanazuka; mfano: Kwa kuwa Tume ya Katiba na kuitishwa kwa Bunge la Katiba lilikuwa sharti kuu kwenye Mkataba wa Muungano [ibara ya 8] na Sheria ya Muungano [ibara ya 9] katika kuupatia Muungano Katiba yake; Je, Bunge la kawaida lilikuwa na mamlaka gani kukiuka Mkataba wa Muungano kwa kuahirisha mchakato huo kama lilivyofanya?
Sehemu ya sheria hiyo iliyoahirisha mchakato wa Katiba inasomeka hivi:
Notwithstanding the provisions of the Acts of Union of Tanganyika and Zanzibar or the Articles of Union …., the President of the United Republic shall not be required to appoint a Commission to make proposals for a Constitution for the United Republic, or to summon a meeting of a Constituent Assembly….”.
Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano haimpi Rais hiari ya kuteua, kuahirisha, kuitisha Bunge la Katiba au kubadili tarehe na muda uliowekwa. Maneno yaliyotumika ni: “The President shall appoint a Commission …… Summon a Constituent Assembly…..” [Ibara ya 8 mkataba wa Muungano].
Hapa, ni dhahiri tena kwamba, Tanzania na Watanzania waliporwa kwa mara nyingine na Bunge [kwa kutumiwa na Rais asiyeambilika] haki yao ya kushiriki katika kutunga Katiba wanayoitaka; hali iliyosababisha Muungano kuendeshwa kwa mitulinga, minyukano na mitafaruku isiyoisha.
Katiba ya sasa ina mapungufu
Mchakato wa Katiba ya sasa [ya 1977] ulitanguliwa na kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP, kuunda Chama cha Mapinduzi [CCM], kwa ridhaa ya Halmashauri Kuu NEC] za vyama hivyo kutokana na mapendekezo ya Kamati ya Wana CCM 20 iliyoteuliwa kwa ajili hiyo.
Kinachoshangaza hapa ni kwa NEC ya CCM kuiteua kamati hiyo ya watu 20 baada ya zoezi la kuunganisha vyama, kuwa ndiyo Kamati [Tume] ya kupendekeza Katiba ya Jamhuri ya Muungano, kinyume kabisa na matakwa ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano, juu ya uteuzi wa Tume ya kupendekeza Katiba; lakini yote hayo mbali na kwamba muda kwa jambo hilo ulikuwa umepita kwa miaka 13.
Ni kwamba, chini ya Mkataba wa Muungano, Tume ya Katiba iliyotakiwa ilipashwa kuwa ya kiserikali badala ya Kamati ya Kichama iliyotumika!
“Tume” hiyo, kwa muda mfupi kabisa iliwasilisha mapendekezo yake kwenye NEC, nayo ikayapitisha siku hiyo hiyo kwenye Kikao cha siri [in camera] cha kujifungia, kwa maelekezo kwamba, kwa kuwa Kamati Kuu ya CCM ilikwishayapitisha, NEC haikupashwa kuhoji wala kuyajadili, isipokuwa kupitisha tu.
Lile linalodaiwa kuwa Bunge la Katiba, nalo liliteuliwa siku hiyo hiyo, na Muswada wa Katiba mpya ukachapishwa siku saba tu kabla ya Bunge hilo kukutana, kinyume kabisa na Kanuni za Bunge kuhusu “wasiwasi” wa miswada ya Sheria Bungeni.
Na hata Bunge lilipokutana, lilikumbushwa kwamba, kwa kuwa NEC ya CCM ilikwishayapitisha mapendekezo hayo, Bunge hilo halikupaswa kujadili wala kupinga chochote, na hivyo muswada huo ukapitishwa katika muda usiozidi saa 3 za mazungumzo, na si kwa njia ya mjadala.
Katiba ya 1977 si matokeo ya mjadala au ushiriki wa wananchi katika, ama kuanzishwa kwake au kuridhiwa. Kwa sababu hii, kwa mara nyingine, wananchi waliporwa haki yao ya kuyajadili kikamilifu na kuweza kuamua juu ya muundo na mgawanyo wa madaraka ndani ya Muungano kwa kuzingatia misingi ya Mkataba wa Muungano na Sheria ya Muungano. Je, Katiba ya sasa itahimili “wakati ukuta”?
Kwa muhtasari kufikia hapo, tunaona kwamba nchi yetu haikuwahi kuwa na Katiba iliyotokana na wananchi wenyewe kwa ajili ya wananchi. Tukianzia na Katiba ya Uhuru [1961] iliyototolewa kwenye Ofisi ya Makoloni ya Uingereza, na kurithishwa kwetu, Katiba hiyo haikuwa na ibara kuhusu haki za binadamu na haki za raia na iliwekwa kuendeleza mfumo wa kikoloni.
Na pale Katiba hiyo ilipofanyiwa marekebisho, pamoja na Katiba zilizofuata zilizoibuka juu ya majivu ya Katiba hiyo, zilifanya hivyo kuimarisha udhalimu uliojengwa na msingi wa Katiba hiyo ya Kikoloni kufanya uhuru wetu kuwa wa bendera.
Kwa mfano, Katiba zote zilizopita hadi hii ya sasa, hazikumpa uhuru na madaraka kila mwananchi, zilimfanya Rais [na baadaye Chama] kuwa juu ya Sheria na mwenye madaraka kupita kiasi.
Zaidi ya hayo, Katiba yetu sasa haikuwa wazi juu ya maadili ambayo viongozi wanapaswa kuzingatia na kuyaheshimu kama vile uzalendo, uadilifu, uwezo na sifa za kufaa kushika nafasi za uongozi, demokrasia na imani katika utawala bora na utawala wa Sheria.
Haya yote yanawakilisha ukoloni chini ya Gavana/Malkia na ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais beberu/asiyeambilika na kufifisha kabisa ndoto ya uhuru.
Zaidi ya hivyo, marekebisho ya Katiba ambayo yamekuwa yakifanyika hayakuwa kwa hiari, ila kwa njia ya ukinzani na mitafaruku ya ndani itokanayo na watawala kutelekeza wajibu wao kushindwa kukidhi matarajio ya wananchi.
Mabadiliko hayo hayakuwa kuboresha au kukidhi matarajio hayo; bali kuepusha shari na kufanya tabaka la “vibwanyenye uchwara” kuendelea kula matunda ya uhuru, japo kwa muda, hadi mtafaruku mwingine unapotokea kushinikiza mabadiliko mengine.
Kwa msingi huu, kila Katiba inayotumika ilijengeka na kusimama juu ya mhimili au mihimili isiyokidhi ya Katiba zilizotangulia, hadi kufikia Katiba ya sasa. Je, Katiba hii itahimili kishindo cha “wakati ukuta”?, ndilo swali letu.
Katiba ya sasa ilitungwa na kusimama [hadi sasa] juu ya mihimili mitatu mikuu: Kwanza, ni Rais beberu [Imperial Presidency] au Rais asiyeambilika, kuanzia na Katiba ya Jamhuri ya 1962, kama tulivyoona.
Pili, Katiba hii inasimama kwa mguu wa pili wa Muungano wenye Serikali mbili uliopotoshwa katika utekelezaji, na ambao umezaa kero za Muungano zinazoyumbisha Serikali ya Muungano mpaka sasa.
Wengi tunakumbuka jinsi Rais wa awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe Mwinyi alivyovuliwa uongozi wa Chama na Serikali mwaka 1984, kwa sababu tu ya kutumia haki yake ya kikatiba kutaka kujua muundo sahihi wa Muungano.
Ilikuwa dhambi kuu enzi hizo kuuliza na kuzungumzia Muungano; lakini leo si dhambi tena kwa sababu “wakati ukuta”.
Tatu, sambamba na madaraka makubwa ya Rais asiyeambilika, Katiba hii bado ina harufu ya chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi. Ndiyo maana CCM na baadhi ya viongozi wa CCM na Serikali wanashindwa kutofautisha ni wakati gani wapo, kwa mambo ya Chama, wakati gani wanatakiwa kutenda kwa kuheshimu Katiba ya nchi. Ni ubatili kudai kuna kitu kiitwacho “chama dola”, kwani nchi haiongozwi na hisia za vyama au Katiba za vyama vya siasa; bali kwa Katiba ya nchi ambayo iko juu ya Katiba za vyama vya siasa na Viongozi wa vyama.
Kwa hiyo, kufuatia kufutika kwa mfumo wa Chama kimoja na Chama kushika hatamu; siasa ya Ujamaa [Azimio la Arusha] kupigwa ngwara na sera za soko huria na ubinafsishaji mambo ambayo ndiyo yalikuwa Mhimili Mkuu wa Katiba ya sasa, ni dhahiri kwamba Katiba hii haiwezi kuhimili “minyukano” ya sasa na hivyo haina budi kuanguka. Wala upachikaji wa bendeji [viraka] kwa majeraha inayopata kwa jina la “Marekebisho ya Katiba”, hauwezi kuiokoa.
Suala la Muungano ndani ya mazingira mapya na huru wa kujieleza nayo ni mkuki wa kupasua matumbo. Hapo kale, ilikuwa ni dhambi kuu kujadili Muungano; leo si hivyo tena – Zanzibar ina bendera yake, ina ngao yake ya Taifa, ina Wimbo wake wa Taifa; na sasa imejitangaza kuwa “nchi”, kwa usahihi kabisa na kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano.
Zaidi ya hayo, vita baridi kati ya mataifa makubwa ya Magharibi [Ubepari] na ya Magharibi [Ukomunisti] ambayo ilikuwa chimbuko na kichocheo cha Muungano huu, sasa haipo tena kuweza kuupa Muungano uhai kwa mazingira ya sasa.
Na kwa kuwa pamoja na hayo, Katiba ya sasa imejengeka juu ya dhana ya Muungano usiohojika wala kujadilika, matukio haya ni ya kusitua, na hapana shaka kwamba lazima yafuatiwe na mabadiliko ya Kikatiba ili, kama ulivyo utamaduni wa kubadili Katiba tangu kale, kuepusha shari.
Pamoja na kuvunjika kwa mihimili ya Katiba hii, suala la [kuheshimiwa kwa] Haki za Binadamu na haki za raia kwa mujibu wa Tamko la Umoja wa Mataifa la 1948, ambalo nchi yetu iliridhia shingo upande tangu mwaka 1984 [Sheria Na. 15 ya 1964] na kuwa sehemu ya Katiba, haliruhusu tena kuendelea kwa mfumo wa Rais beberu/asiyeambilika au Chama dola, kama zilivyokuwa Katiba zilizotangulia.
Ninasema tuliridhia shingo upande kwa sababu marekebisho ya Katiba yaliyofuatia hayaonyeshi kwamba tulifanya hivyo kwa hiari wala utashi kwa mazoea ya ubeberu. Ndiyo maana, ibara zote za Katiba zenye kutoa na kulinda haki za Binadamu na haki za raia zilianza na maneno: “Bila kuathiri Sheria za nchi zinazohusika …..”, kumaanisha kwamba, Katiba inatoa haki hizo kwa mkono wa kulia na kuzinyakua hima kwa mkono wa kulia na kuzinyakua hima kwa mkono wa kushoto.
Kuwekewa mipaka kwa haki hizo kwa njia ya “saving clauses”, kwa lugha ya kisheria; kuliwezesha Bunge kutumia ubabe kutunga “Sheria za nchi zinazohusika kubana haki hizo, kiasi kwamba zilibakia bila kuwa na maana iliyokusudiwa, na kufanya mhimili wa utawala kubakiwa na madaraka makubwa kupita kiasi. Kwa mazingira ya leo mhimili huu hauwezi kujificha ndani ya kichaka hiki tena.
Kwa kuzingatia yote haya, sambamba na kujengeka kwa jamii ya kiraia yenye uelewa mkubwa juu ya haki za wananchi na wajibu wa watawala kwa umma, hii ni baruti tosha kushinikiza Katiba mpya itakayoashiria kuzaliwa upya kwa Jamhuri ya pili. Yanayotokea sasa ni dalili tu kuashiria mvua kubwa ya mafuriko.
Toa maoni yako