NIANZE kwa kuwapa pole walimu waliotandikwa viboko wilayani Bukoba, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uzembe. Poleni sana walimu, inawezekana mlikuwa na makosa fulani ya kiutendaji lakini hamkustahili kuchapwa viboko.
Hamkustahili kwa kuwa kama nchi itaanza utaratibu wa kuwatandika viboko wazembe, basi wanasiasa wengi itabidi wacharazwe bakora na hasa waliomo katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Lakini kwa bahati nzuri au mbaya, nchi yetu haijaingia katika ulimwengu huo, ingawa pia naamini tukio hili linafungua fikra zetu kutambua kuwa nchi ina tatizo la mfumo madhubuti wa kudhibiti uwajibikaji wenye kutii matakwa ya maadili ya uongozi.
Mfumo wetu kiutawala katika kudhibiti uwajibikaji umekuwa ukizingatia zaidi utashi wa kiongozi wa eneo husika, na si taratibu rasmi za kisheria. Na wakati mwingine, sheria husika zimekuwa zikitafsiriwa kwa kuzingatia matakwa ya viongozi wa eneo husika au hata viongozi wakuu kitaifa.
Kitendo cha walimu kuchapwa kwa madai ya uzembe kinathibitisha udhaifu katika mfumo wa kusimamia uwajibikaji, lakini pia kitendo cha Mkuu wa Wilaya kuamuru walimu wachapwe kinathibitisha kuwapo kwa viongozi walioteuliwa kwa makosa kushika nyadhifa zao. Hili nitajadili siku zijazo.
Leo nitajadili taswira ya nchi yetu ndani ya ukumbi wa Bunge, ambalo wiki iliyopita lilihitimisha mkutano wake wa 14, mjini Dodoma.
Ukweli ni kwamba, zaidi ya tukio la kuahirishwa kwa kikao cha Bunge kutokana na Serikali (mawaziri) kutokuwapo katika ukumbi wa Bunge, yapo mengine ya kujadili.
Tujadili mambo hayo kwa kuweka taswira ya nchi yetu ndani ya ukumbi wa Bunge. Ukumbi unaokutanisha wawakilishi wa wananchi na Serikali. Yapo maeneo manne ya kujadili. Mosi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda.
Pili, mawaziri na naibu mawaziri. Tatu, viongozi wa Bunge na hasa Spika, Samuel Sitta. Lakini nne ni wabunge wenyewe, na kisha Watanzania nje ya Bunge na Serikali.
Tuanze na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Bungeni anaonekana ni kati ya viongozi wachache wasio wanafiki kutetea maslahi ya wengi. Unaweza kumwelezea kama kiongozi anayesimamia kile anachoamini kina manufaa kwa Watanzania, bila kujali nguvu za kundi linalopinga msimamo huo au athari dhidi yake mbele ya safari yake ya kisiasa.
Sitashangaa siku moja kusikia Waziri Mkuu Pinda anajiuzulu baada ya kubaini msimamo wake wa kutetea maslahi ya Watanzania wengi unapuuzwa au kudhalilishwa na viongozi wenzake serikalini au katika CCM.
Nadiriki kusema hivyo kwa kuwa naamini ndani ya fikra za Mizengo Pinda, uwaziri mkuu wake si jambo la kipaumbele. Naamini kipaumbele kwake ni matokeo ya uwaziri mkuu huo kwa Watanzania na Tanzania yao. Nadhubutu kusema, Mizengo Pinda, anatofautiana kwa sehemu kubwa na baadhi ya mawaziri wakuu waliomtangulia.
Pinda ndani ya Bunge anaonekana muungwana, asiyetayari kuwabeba mawaziri wanaoyumba bila sababu za msingi.
Si ajabu kwa Pinda kuinuka na kutoa majibu yanayobeba tafsiri kuwa Waziri au viongozi wa taasisi fulani ni wababaishaji wanaohitaji ama kujirekebisha au kuenguliwa.
Na ukweli ni kwamba, baadhi ya mawaziri au naibu mawaziri ndani ya Bunge wanaonekana kubaini mwenendo huo wa Waziri Mkuu Pinda. Kigezo hiki cha uungwana wa namna hiyo ndicho kinawafanya hata wanasiasa wanaotaka kumshambulia kwa hoja, wakiwamo baadhi ya wabunge wa upinzani, kukwama.
Kati ya wabunge walioonekana kukwama kutokana na uungwana wa Pinda ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed. Katika moja ya vikao vya mkutano wa 14 wa Bunge, Hamad alijiandaa kumshambulia kwa hoja Pinda, akitaka ajiuzulu kutokana na kauli yake ya kutaka wauaji wa albino wauawe.
Lakini pia, uungwana wa Pinda kwa Taifa unabainika katika suala la nyongeza ya muda wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, muda ambao unakwisha mwaka huu, lakini Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, alionyesha jitihada dhahiri akitaka uongezwe.
Jaribio hilo la Waziri Mwangunga na timu yake kwa kuwahusisha baadhi ya wabunge wachache, lilizaa hoja binafsi. Hoja ya kuingiliwa kwa haki na madaraka ya Bunge, iliyowasilishwa na Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya.
Pengine kwa kutambua kuwa Pinda ni muungwana na mwepesi katika kupima maslahi ya taifa na maslahi ya kikundi kidogo cha watu, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, alimtaka ahitimishe utata huo, naye akafanya hivyo akasema muda hauongezwi.
Ingawa hakuwahi kueleza hadharani mbinu anazotumia kumudu madaraka yake, ni wazi kuwa uungwana ni nguzo ya msingi kwa Pinda kufanikiwa zaidi kiutendaji.
Uungwana wake huo unamsaidia kufikisha ujumbe wa wazi kwa mitandao ya rushwa serikalini, na katika taasisi nyingine za umma kwamba “Mimi Waziri Mkuu siko pamoja nanyi.” Lakini pia uungwana huo, unawafanya Watanzania masikini kuona kuwa wanaye kiongozi wa juu serikalini anayefanana nao.
Ndani ya ukumbi wa Bunge, Pinda ni kiongozi asiyesita kukiri kuwa Serikali imeteleza, na akaomba radhi ili mambo yaishe.
Hapa nakumbuka maneno ya Mwalimu Julius Nyerere, alipokuwa akizungumzia sifa za mtu anayepaswa kuwa “Rais wetu.”
Pamoja na mambo mengine mengi, Nyerere alisema awe ni mtu mwenye uwezo wa kuwaambia rafiki zake Ikulu siyo pango la walanguzi, na hao rafiki zake wakaelewa hivyo.
Pinda anaonekana kuishi katika sifa hiyo. Uungwana wake umekuwa silaha hata kwa wale wenye tabia ya kufanikisha mambo yao kwa kutoa rushwa kwa viongozi wakubwa. Hao wanatambua kuwa Pinda haingiliki, na kwa maana hiyo inawezekana mipango yao ya rushwa huishia kwa viongozi wa ngazi nyingine.
Unaweza kujiuliza, ni kwa nini tuwe na uhakika kuwa haingiliki kwa rushwa wakati rushwa ni siri kati ya mtoaji na mpokeaji.
Ni kweli, rushwa ni suala la siri. Hata hivyo, uhakika wa suala hili tunaubaini ndani ya nguvu za uungwana wa Waziri Mkuu Pinda.
Kama utachunguza au kufuatilia zaidi uamuzi na kauli za Waziri Mkuu Pinda, unaweza kubaini uzito wa nguvu zilizopo ndani ya uungwana wake, utaridhika kuwa ni muungwana wa dhati na si muungwana wa bandia au kubabaisha.
Kubwa zaidi hapa ni ukweli kuwa kwa muda mrefu sasa Tanzania ilikosa Waziri Mkuu mwenye sifa hizo. Katika mazingira haya, sasa tuwatazame mawaziri na naibu mawaziri. Katika kundi hili kuna sifa mchanganyiko.
Wapo mawaziri ambao wamedhihirisha kuwa viatu vya uwaziri au unaibu waziri vimepwaya. Lakini pia miongoni mwa mawaziri na naibu mawaziri hao, wamo ambao kitabia ni wepesi katika kubadilika na kufuata mwelekeo wa bosi wao (Waziri Mkuu).
Katika kundi hilo, wamo wanaobadilika kwa dhati lakini pia wengine hubadilika hadharani tu, huku fikra zao zikiendelea kuishi katika ulimwengu wa zamani. Tunaweza kuwagawa mawaziri na naibu mawaziri katika makundi mawili.
Kwanza ni wale wenye jitihada za wazi katika kuwatumikia Watanzania. Mfano hai, ni Waziri wa Maendeleo ya Mifungo, John Magufuli.
Lakini pili, ni mawaziri na naibu mawaziri ambao mbele ya macho ya Watanzania wameteuliwa kujaza nafasi tu, pengine kwa malengo maalumu yasiyowasaidia moja kwa moja Watanzania.
Katika kundi hili la pili, baadhi ya viongozi hao hutumia muda na madaraka yao kufanikisha mipango binafsi ya kisiasa au kibiashara.
Hutumia ofisi zao kufanikisha mipango yenye kukumbatia maslahi ya kundi au mtu anayeaminika kuwa chanzo cha waziri husika kupata madaraka hayo.
Viongozi wa aina hii utawabaini wakati wanapokabiliwa na misukosuko ya kikazi, yenye mwelekeo wa kuwatumbukiza katika kashfa.
Kikubwa unachoweza kubaini katika mazingira hayo ni kuibuka kwa kundi alilokuwa akilitumikia au kulinda maslahi yake kwa siri, chini ya kivuli cha uongozi wa umma.
Waziri au naibu waziri wa aina hii utendaji wake hulenga kutumikia wananchi kwa kuhakikisha kuwa kila mpango atakaotekeleza unanufaisha kwa asilimia fulani kundi lake la kisiasa au kibiashara.
Baraza la mawaziri wa sasa limejidhihirisha kuwa na watu wa namna hiyo katika mkutano uliokwisha wa Bunge. Ni haki kusema kuwa wapo mawaziri wasiofanana kimalengo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na walio nje ya wigo wa matarajio ya Watanzania.
Wapo mawaziri na naibu mawaziri ambao si waaminifu kwa nchi na si waungwana kwa Watanzania, bali ni waaminifu kwa makundi yao ya kisiasa au mitandao binafsi ya kibiashara.
Wamedhihirika kutowekeza vya kutosha nguvu na maarifa yao katika majukumu yao wizarani. Si viongozi elekezi, hawana ufahamu wa kutosha kumudu changamoto zinazowakabili Watanzania, ambazo zinapaswa kutatuliwa na wizara wanazoongoza.
Wengi wao wamejigeuza kuwa matawi ya makundi yao ya kisiasa na mitandao ya ufisadi yenye taswira ya mitandao ya kibiashara. Hivyo ndivyo ninavyoweza kuelezea kuhusu Serikali, ndani ya ukumbi wa Bunge.
Sasa vipi kuhusu Spika wa Bunge, Samuel Sitta na wabunge wake. Spika anaonekana kuhangaika kutaka kutoka katika ulimwengu wa zamani. Ulimwengu wa kutafsiriwa na wananchi kuwa kazi ya msingi ya Spika ni kuchagua wauliza maswali bungeni na kuendesha vikao.
Anahangaika kutaka kuchomoza mbele ya jamii ya Watanzania akiwa kama Spika, akilenga kupandikiza hisia au nguvu za Bunge katika mihimili mingine ya taifa au taasisi nyingine za umma.
Hali hii inaweza kuonekana kama kutuma ujumbe kwa taasisi au mihimili hiyo kwamba, utendaji wenu wa kazi uzingatie kulinda maslahi ya Taifa, vinginevyo uwezo wenu utahojiwa ndani ya Bunge.
Lakini juhudi zake hizo tayari zimemwingiza katika matatizo. Wapo wanaomtafsiri kuwa anavuka mpaka wake kama kiongozi na kwamba anataka kujipa umaarufu kuwa kiongozi bora zaidi ya wenzake.
Ni vigumu kuwa na uhakika juu ya namna mtazamo huo unavyoweza kumwathiri Spika mbele ya umma. Athari dhidi yake itategemea zaidi na mwitikio wa jamii na si viongozi wa taasisi au mihimili mingine.
Hapa vile vile si ajabu kwa wanajamii wengine kumuunga mkono Spika. Wanaweza kumuunga mkono kwa kumwona kama kiongozi anayegusa matatizo yao ya muda mrefu kwa lengo la kutia shinikizo yapatiwe ufumbuzi wa haraka.
Matatizo kama ya rushwa katika mfumo wa mahakamani, urasimu katika idara za serikalini. Urasimu ambao umekwishalalamikiwa si tu na wananchi bali hata wawekezaji wa kigeni kiasi cha kumlazimu Rais Jakaya Kikwete kuunda chombo cha kusikiliza malalamiko ya wawekezaji, chini ya Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.
Lakini wakati Spika akionekana hivyo hali ni ya mkanganyiko miongoni mwa wabunge. Wakati mwingine unaweza kujiuliza ni kwa nini wabunge wanajikuta wakigawanyika katika masuala yanayohusu kutetea maslahi ya Taifa?
Kwa mfano, jiulize ni kwa nini wabunge wengine wawe mstari wa mbele kupinga ufisadi na wengine wasifurahishwe na hali hiyo? Je, wanaopinga wananufaika na mitandao ya vitendo vya ufisadi nchini?
Kwa ujumla, hivi ndivyo ninavyoweza kuielezea kwa muhtasari nchi yetu ndani ya ukumbi wa Bunge. Na ukweli ni kwamba, si ajabu katika mazingira haya, Watanzania kujikuta njia panda. Ndiyo! Watanzania wapo njia panda, lakini wakiwa tayari kuwaunga mkono viongozi wanaotetea maslahi yao.
Na katika kubaki njia panda, watabaki wakitazama ni kiongozi gani hasa anayeonekana kutetea maslahi yao huku wakipuuza mipaka ya kiutawala kati ya kiongozi na kiongozi, au muhimili na muhimili.
Kikubwa hapa watajikuta wakipuuza hoja ya mipaka ya uongozi kutokana na kuzongwa zaidi na matatizo yasiyostahili, ambayo msingi wake ni uzembe ndani ya mihimili au taasisi husika.
Lakini ni hatari kwa raia kufikia hatua ya kuamini kuwa mipaka muhimu kwao ya kuheshimiwa ni mipaka ya nchi yao na nchi nyingine na si mipaka ya uongozi au mihimili.
Ni hatari kwa kuwa hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa Watanzania wengi wanaanza kupoteza imani na uongozi wa baadhi ya vyombo vyenye wajibu wa kuwatumikia.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Toa maoni yako