Nenda ATC anga zimefunguka

WIKI iliyopita nilisafiri kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (Air Tanzania) kwenda Mbeya tukitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, kwangu ikiwa mara ya kwanza.

Nilipata kusafiri na ndege za Shirika hilo huko nyuma, na hasa, katika kipindi lilipokuwa limejiingiza/limeingizwa katika ubia tata na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).

Nimebahatika pia kusafiri ndani na nje ya nchi kwa ndege za mashirika mbalimbali. Lakini tangu miaka ile ya katikati ya 2000 sikuwahi kupanda ndege ya Air Tanzania.

Hivyo niliitamani sana safari ya wiki iliyopita ya Bombardier Dash 8 Q400 yenye uwezo wa kupakia abiria zaidi ya 70 kwenda Uwanja wa Songwe.

Utajiuliza kwa nini nilikuwa na hamu kubwa na safari hiyo ya Mbeya, ilihali si mgeni wa safari za ndege, tena nyingine za madege makubwa, yenye uwezo wa kukaa angani kwa saa zaidi ya 12?

Ni udadisi tu. Mara ya mwisho nilisafiri na ndege ya Shirika letu kutoka Johannesburg, Afrika Kusini kuja Dar es Salaam. Wakati tukikaribia kuruka yalitangazwa majina ya marubani na wahudumu. Nikiri kwamba siyakumbuki majina ya wahudumu wengi. Lakini kubwa nikiri pia sikumbuki majina ya marubani wa siku hiyo.

Yalitajwa majina ya marubani yaliyoashiria hawakuwa Watanzania. Wakati ule kulikuwa na habari za chinichini kuwa SAA haikuwa ikiwapa nafasi sana marubani wa Kitanzania.

Wakati najiandaa na safari ya Songwe suala la marubani wale wageni lilirejea akilini. Shirika lenyewe hili ni kama ni jipya baada ya misukosuko mingi; ndege zenyewe nazo ni mpya, nilitaka kujua nani angeturusha?

“ Karibuni katika ndege yetu aina ya… yenye namba ya safari 106 itokayo Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe Mbeya…ndege yetu itaruka futi 27 elfu juu ya usawa wa bahari…

“Pamoja nawe angani, watakuwa ni marubani Budodi ( Kapteni Budodi N. Budodi) na Mrisho (F/O Maneno S. Mrisho) na wanaanga wenzao Jamilah (F/P Jamilah Bablia), Latifah (SCC Latifah Bakari) na Anna (CC Anna Mgaya), alitangaza kwa sauti laini dada Jamilah.

Orodha ya wanaanga hao wa Air Tanzania siku hiyo, ndiyo sababu ya kwanza ya kuandika hiki ukisomacho. Nilikuwa nakerwa sana kupanda ndege za Air Tanzania zilizokuwa zinarushwa na watu wa nje, wengine ambao dakika tano tu baada ya kutua usingekumbuka majina yao!

Nilikuwa nakerwa sana na taarifa za chinichini kuwa SAA haikuwa ikiwapa nafasi marubani wazawa huku nikijua kuwa kwamba katika nchi nyingi za kusini mwa Afrika marubani wa Kitanzania walikuwa mali, wengine kufikia kuwa marubani wakuu (Botswana).

Nilifarijika sana kwamba safari hii tulikuwa tunarushwa angani na wenzetu na wanetu Budodi na Mrisho na kina dada Jamilah, Latifah na Anna. Hakika kwa mfumo huu ATC imerudi kwao.

Si mashirika yote ya ndege nchini hutoa huduma za bure za viburudisho kwa abiria wake. Najua ATC imekuwa na utaratibu huu wakati wote, lakini tofauti na nyakati hizi, wakati ule viburudisho karibu vyote, kama si vyote, vilitoka nje, vikitengeneza ajira huko.

Tulikunywa maji ya nje; chai, kahawa na sukari vya nje; juisi za nje na bia za nje, wakichanganya kidogo na za ndani (Safari na Kilimanjaro) kwa sababu ya umaarufu wa bia hizo.

Na hiyo ni sababu ya pili ya kuandika makala haya mafupi. Maji tuliyokunywa wiki iliyopita ni Cool Blue ya kampuni ya ndani; juisi tulizokunywa ni za kampuni ya Bakhresa, wote tunamfahamu; Korosho ni za kampuni ya NatureRipe Kilimanjaro yenye anuani ya Dar es Salaam; kahawa sukari na chai, vya ndani, na, kubwa zaidi mvinyo waliotugawia, Image, unatoka Dodoma, kwenye kampuni ya Alko Vintages, pale karibu na ofisi za Bunge, ulioandaliwa kwa ajili ya abiria wa ATC. Si Capetown wala Durban.

Mimi si mchumi, lakini akili ya kawaida inaniambia kwamba ATC inapokua, wanakua pia kina Bakhresa (zaidi), Cool Blue, Alko Vintages na NatureRipe kwa maana ya mnyororo na mtawanyiko wa uchumi na ajira.

Najua ATC haijakaa sawa, na katika hali halisi ndege mbili tu haziwezi kuhudumia ndani na nje zikaingiza faida, lakini ukizingatia idadi ya abiria inayokua kila mara, na ikaendelea kuthamini wazawa kazini na katika biashara, ni ATC yenyewe itakayojiharibia soko au kujihumu.

Nimalize kwa swali dogo kwa wasimamizi wa Uwanja wa Songwe. Hivi ile mitambo inayochakaa mbele ya uso wa Uwanja, inayoharibu mandhari katika eneo hilo, inamsubiri nani arudi kuihamisha?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *