IKIWA imesalia miezi michache kabla ya mchakato wa uteuzi wa wagombea ubunge, katika vyama vya siasa, hali imezidi kuwa tete kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkanganyiko ukijitokeza katika Umoja wa Wanawake (UWT)na mikakati zaidi ikiwekwa dhidi ya wagombea wenye tuhuma za ufisadi kukatwa majina.
Uchunguzi wa Raia Mwema kwa wiki kadhaa ukihusisha mazungumzo ya ana kwa ana na baadhi ya makada waandamizi wa chama hicho na baadhi ya viongozi umebaini kuwapo kwa mikakati ya kukiandaa chama hicho kutopata wakati mgumu majukwaani.
Imebainika, baadhi ya makada waandamizi wa chama hicho wameshtushwa na wimbi kubwa la baadhi ya viongozi watuhumiwa katika baadhi ya halmashauri na taasisi za serikali kunyemelea kuwania ubunge kwa tiketi ya chama hicho, hali inayokilazimu chama hicho kujiandaa kukabili wimbi hilo .
“Wapo watu walioonyesha nia ya kutaka kuwania ubunge na wameanza kampeni lakini zipo taarifa za uhakika baadhi yao wamegubikwa kwa kashfa nzito za ufisadi na utapeli.
“Tumeanza kuwashtukia na uzoefu unaonyesha wakiachiwa wapenye katika nafasi za ubunge uwajibikaji utazidi kuwa ndoto, itakuwa ni mwendelezo wa kashfa.
“Unajua mawaziri wanapatikana kutoka miongoni mwa wabunge kwa hiyo ukiwa na watu wanaoanza safari ya ubunge wakizongwa na kashfa ni wazi utakuwa na Bunge la ovyo na serikali yenye kashfa. Sasa chama ni lazima kijiandae kuzuia hatari hiyo,” alisema kiongozi mwandamizi wa CCM, ambaye ni mbunge na mjumbe wa kamati kuu akitaka kutoandikwa gazetini kwa sababu maalumu.
Aliongeza kuwa kuna uwezekano wa mambo mawili kutolewa tamko. Kwanza, ni onyo kwa wanaotaka kuwania ubunge kuhakikisha hawana kashfa na pili, kama wataingia kwenye kinyang’anyiro basi mchujo wa majina yao kwa kigezo hicho utapewa nafasi kubwa.
Kwa kawaida, CCM kupitia vikao vyake vya vya juu imekuwa ikijadili na hata kuchuja majina ya wagombea ubunge kwa kuzingatia taarifa mbalimbali zinazowahusu wahusika.

Yusuf Manji
Kati ya wana-CCM waliowahi kuchujwa majina yao katika kinyang’anyiro cha ubunge uchaguzi uliopita licha ya kushinda kura za maoni ni pamoja na mfanyabiashara wa Dar es Salaam , Yusuf Manji na mfanyabiashara wa Morogoro mjini, Abood. Sababu za kukatwa majina hazikuwahi kuwekwa wazi.
Lakini wakati hayo yakijitokeza kama sehemu ya maandalizi ya kujipanga kwa chama hicho, kumeibuka mgogoro wa chini kwa chini kati ya wabunge wengi wa vitimaalumu na uongozi wa UWT, hususan Mwenyekiti wa umoja huo, Sofia Simba.
Chanzo cha mgogoro huo ambao kama utashindwa kuhitimishwa utafikishwa kwenye vikao vya Halmashauri (NEC) ya CCM, ni uamuzi unaopigiwa debe na Sofia Simba wa kutowaruhusu wabunge wa vitimaalumu waliodumu bungeni kwa mihula miwili au zaidi kutopewa tena fursa hiyo.
Uamuzi huo unatajwa kupitishwa na Baraza la UWT lakini ikielezwa kuwa ulifikiwa bila kufuata utaratibu kwa Kamati ya Utekelezaji kutopewa fursa ya kujadili suala hilo . Kwa kawaida, kamati hiyo ndiyo inayojadili masuala ya aina hiyo na kuyafikisha kwenye baraza.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Raia Mwema kuna uwezekano mkubwa wa kukwamishwa kwa mpango huo kwa kuzingatia hoja zilizotumika katika kupinga hoja inayoungwa mkono na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya kuweka ukomo wa mihula ya ubunge.
Baadhi ya wabunge wa vitimaalumu ambao wengine ni mawaziri na naibu mawaziri wameungana kupinga mapendekezo hayo na kama watashindwa, shinikizo la kutaka hata ubunge wa majimbo uwe na ukomo litaibuliwa kwa nguvu na mlipuko mkubwa.
“Wabunge wa vitimaalumu ni tofauti na wale anaowateua Rais. Wabunge wa vitimaalumu hupigiwa kura na wajumbe husika mikoani. Wanapigiwa kura kama ilivyo wabunge wa majimbo pengine tofauti iliyopo ni idadi ya wapiga kura na majimbo.
“Kimsingi ni haki ya Katiba ya kuchagua na kuchaguliwa, kwa hiyo ni kama mbunge wa jimbo anachaguliwa kwa kura na vitimaalumu hivyo hivyo, hawa ni raia wanachama wenye haki zao,” alisema mbunge mmoja wa vitimaalumu ambaye ni waziri na kuongeza kuwa;
Baadhi ya viongozi wameonyesha tatizo la uelewa wa masuala ya siasa nchini kwa kulinganisha na matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .

Mwenyekiti wa UWT, Sofia Simba
Lakini Mwenyekiti wa UWT, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora Sofia Simba alizungumza na Raia Mwema na kusisitiza kubaki katika uamuzi huo wa kutoruhusu wabunge wa vitimaalumu waliokaa zaidi ya mihula miwili kurejea bungeni kwa tiketi hiyo.
“Kama kwa mtazamo wao wanaamini tatizo ni uamuzi kufikiwa bila kufuata utaratibu, vikao vingine vinaweza kuitishwa ili suala hilo lifuate mchakato wanaoamini umekosewa. Lakini hoja ya msingi iko pale pale, vitimaalumu vimewekwa ili kutoa nafasi kwa wanawake kupata uzoefu na si kudumu katika nafasi hiyo.
“Wapate uzoefu waende majimbo. Leo hii mbunge wa vitimaalumu aliyekaa muda mrefu hawezi kushindana na mgombea mpya wa nafasi hiyo kwa haki. Kwanza , atakuwa na uzoefu mkubwa wa kisiasa na kiuchumi..ndiyo maana tunataka waende majimboni,” alisema na kuongeza kuwa;
“Wote wanaopinga kama wataendelea na msimamo wao huo wanaweza kuingia kwenye mchakato lakini wakumbuke kuwa majina yao yatapitia mikononi mwake kwa ajili ya mchujo na kwamba, anachofanya ni kusimamia matakwa ya Baraza Kuu na si matakwa yake binafsi.”
Kwa sasa, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina wabunge wanawake 99, kati ya hao ni wabunge 18 tu wa majimbo, na wabunge wa vitimaalumu ni 58 wakijumuisha vyama vyote vya siasa bungeni.
CCM inaingia katika hali hiyo ya mgogoro mpya wakati wakisubiri matokeo ya Kamati Teule ya Halmashauri Kuu (NEC) inayoongozwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi iliyoundwa kudadisi na kupendekeza ufumbuzi wa kile kilichotajwa kuwa ni mpasuko miongoni mwa wabunge wa chama hicho kwa upande mmoja, na malumbano yaliyojitokeza kati ya baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Muungano.
Taarifa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwenye kikao cha NEC kinachotarajiwa kufanyika Februari 10, mwaka huu, baada ya kuahirishwa kwa takriban mara mbili.
Kikao hicho kitafanyika kikiwa tayari kimetanguliwa na kikao cha ghafla cha Kamati Mahsusi ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM- Zanzibar, ambayo pia ilijadili hali tete iliyojitokeza Zanzibar ikihusu suala la serikali ya mseto na Rais wa Zanzibar , Aman Abeid Karume kuongeza muda.
Baada ya kikao hicho, Rais Karume aliweka wazi kuwa hayuko tayari kuongezewa muda. Hoja ya Karume kuongeza muda madarakani ilipigiwa debe na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad.
