NITANGULIE tu kusema kuwa mimi si mwanasiasa; japo hainizuii kufuatilia siasa kwa karibu. Hiyo ni kwa sababu tumewakabidhi wanasiasa hatima ya maisha yetu. Wao ndio wanaopanga sera za maendeleo yetu, wao ndio wanaopanga mipango ya uchumi wetu, na zaidi ya hapo ndio wanaotunga sheria zetu.
Siasa ni kazi ya maneno. Lakini chama cha siasa ni watu na sera, si maneno matupu. Hata wanasiasa wangekuwa na maneno mengi kiasi gani bila kuwa na watu na sera nzuri, ni kazi bure.
Ndio maana Tanzania kuna vyama zaidi ya kumi na tano, lakini kuna vyama ni kama havipo; maana havina watu japo viongozi wao ni wasemaji kweli kweli lakini havina sera!
Huwa nashangaa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa anasubiri nini kuviondoa katika daftari lake la vyama vya siasa nchini?. Maana sera za vyama hivyo hazijulikani, havina wafuasi na wala havijulikani vinafanya shughuli gani katika siasa za nchi hii.
Viongozi wake wanapoona wamesahauliwa kabisa na umma, wanaamua kwenda kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam na kuitisha press conference za kusifia vyama vya wenzao bila kuonyesha wao wanafanya nini hasa.
Si vibaya chama cha siasa kukisifia chama kingine cha siasa kama kinafanya vizuri, lakini ni ujinga kiongozi wa chama cha siasa kusifia kiongozi wa chama kingine cha siasa bila kuonyesha yeye anafanya nini hasa katika chama chake au chama anachokiongoza kinafanya nini hasa.
Kiongozi wa chama cha siasa hana budi kuonyesha na kutetea sera za chama chako, na si kusifia sera za vyama vingine. Kama huna zako, ni vyema ukavunja chama na kujiunga na hao wanaofanya vizuri.
Kilichonichochea kuandika makala hii, ni taarifa za kuundwa chama kipya cha siasa kinachojulikana kama Chama Cha Jamii (CCJ). Hiki kimekuwa ni chama cha maneno.
Nasema hivyo kwa sababu hata sera zake hatuzisikii zikitangazwa sana; bali kila mara tunaaminishwa (kupitia vyombo vya habari) kuwa kuna vigogo watajiunga nacho. Vigogo wenyewe hawatajwi ni akina nani.
Inaonekana kama vile sera ya CCJ ni vigogo! Sijui kama ni kwa makusudi au kwa kutojua, lakini hata chama tawala cha CCM kimeingia mtegoni kwa kuanza kulumbana na chama hiki ambacho bado hata kusajiliwa.

John Chiligati
Katibu Mwenezi wa CCM, John Chiligati na viongozi wengine wa CCM wametoa maelezo, mara kadhaa, kuwa hawatishwi na ujio wa CCJ! Inashangaza kwa nini wasishughulikie sera zao na matatizo ndani ya chama chao na badala yake wapoteze muda wao kuzungumzia chama ambacho hata hakijasajiliwa, chama ambacho hata makao yake makuu hayajulikani yako wapi, chama ambacho wanachama hawajulikani zaidi ya viongozi wawili waliokipeleka kwa msajili kuomba usajili wa muda.
Mimi naona ni bora viongozi wa CCM au hata wa vyama vingine makini washughulike zaidi na kujibu hoja za zinazowakabili kuliko kupoteza muda na chama ambacho, angalau mpaka sasa, bado ni chama hewa.
Wakati nikitafakari ujio wa CCJ, kama nilivyokuwa nikihabarishwa na vyombo vya habari, nilikumbuka baadhi ya vitu vinavyoweza kukifanya chama tawala chochote, popote pale duniani, kiendelee kuwa madarakani. Kwanza, ni kuwa na sera nzuri na kuzitekeleza ipasavyo kwa maendeleo ya wananchi. Kutimiza ahadi zote kama walivyozitoa.
Pili, chama tawala kikianza kufilisika kisera mara nyingi kitatumia nguvu za dola kuendelea kutawala. Tunayo mifano mingi kama ya Zimbabwe, Kenya na kwingineko.
Lakini ipo njia ya tatu ambayo ndio lengo la makala hii. Hii ni matumizi ya ghiliba; yaani kuwaghilibu wananchi ili waache kufikiria mambo ya msingi na badala yake wananchi waanze kupoteza muda na nguvu katika mambo ya hovyo, tena ya msimu.
Mbinu hii ni maarufu sana katika nchi za Kikomunisti. Mwanafalsafa wa Kiitaliano aitwaye Antonio Gramsci aliiita Hegemony. Kwa maneno yake: “Hegemony denotes the predominance of one social class over other. This represents not only political and economic control, but the ability of the dominant class to project its own way of seeing the world (things) so that those who are subordinated by it accept it as a “common sense and natural.”
Utawala ulio madarakani (kama CCM) unapokabiliwa na matatizo ya kiutawala, unapokosa majibu kwa ufisadi unaotokea, unaposhindwa kutimiza ahadi zake, basi, unawaghilibu wananchi wakati wakiangalia upepo unakwenda vipi.
Tukichukulia mfano wa hali ya kisiasa katika Tanzania wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, kuna mambo mengi yanayohitaji majibu lakini kwa makusudi au kwa kukosa umakini, mambo hayo yamekuwa wimbo usiokwisha.
Mfano, sakata la Richmond limekuwa wimbo bungeni kwa karibu miaka mitatu sasa. Aidha, masuala ya ufisadi wa Kagoda Agriculture, Meremeta na kadhalika, ni mambo yanayohitaji majibu ya haraka kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Lakini inawezekana majibu yake si mazuri kwa watawala (CCM), na hivyo wanaweza kufanya kila liwezekanalo kuwasahaulisha wananchi. Na hapo ndipo CCJ inapoingia katika hegemony. Badala ya wananchi kushinikiza kupata majibu ya msingi kwa maswali nyeti kama hayo ya Richmond, nyumba ya gavana yenye thamani ya mabilioni na kadhalika, tunakaa kuwaza habari za CCJ! Kuwaza vigogo watakaojiunga nacho; kama vile vigogo ndio sera.
Sisemi moja kwa moja kuwa CCJ ni mbinu ya chama tawala, lakini inawezekana kabisa ikawa hivyo.
Kwa kutambua nguvu ya vyombo vya habari, watawala wanaweza kabisa kupandikiza ajenda yao isiyokuwa na maslahi kwa taifa kwa lengo la kuzipoteza ajenda zenye maslahi zisiwafikie wananchi kupitia vyombo vya habari.
Na hilo kama ni kweli, basi, nafikiri watawala wetu watakuwa wamefuzu mafunzo ya propaganda; maana propaganda ni silaha mojawapo katika vita.
Ukitazama kwa makini unauona mushkeli katika ‘ajenda’ ya CCJ kwamba vigogo wa CCM watajiunga nacho muda ukiwadia. Ni muda gani wanaouhitaji?
Hatuna haja na sura za vigogo hao; kwani sera hazina uhusiano wowote na sura ya mtu. Sura ya mtu ingelikuwa ndio sera, basi, kina Miss Tanzania wangekuwa viongozi.
Nawashauri Watanzania wenzangu tupime kwa makini mtego huu wa watawala tunaoungia, na vyombo vya habari navyo visitumike kuondoa hoja muhimu mezani na kuleta porojo katika mambo yanayoamua hatma yetu.
Kwanza siamini kwamba Tanzania tuna uhaba wa vyama vya siasa mpaka tuletewe vyama vipya. Nasema hivyo kwani hivyo vilivyopo ni vingi mno. Wingi wa vyama unaondoa hata ushindani wa maana. Wingi wa wagombea unawatatiza hata wapiga kura wakati wa kupiga kura.
Mfano mzuri ni mikanganyiko iliyotokea wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa hivi karibuni. Wananchi wengi wa vijijini walishindwa kujua wachague yupi; maana karatasi ya kura iligeuka ‘kitabu’ badala ya karatasi kwa jinsi ilivyojaa majina ya wagombea.
Demokrasia yetu inaturuhusu kuwa na uamuzi wa kupendelea chama chochote mtu akipendacho, lakini sioni tija yoyote katika kuwa na utitiri wa vyama. Uwepo wa vyama mamuluki ni mojawapo ya mbinu za watawala kugawa kura na kujihalalishia kuendelea kuwa madarakani. Hiyo ndiyo hegemony!
