KATIKA sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala hizi, tuliangalia kwa karibu ni jinsi gani Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad, alifanya jaribio la kuandika upya historia ya Zanzibar huku akiyang’arisha yaliyo mazuri na kuyakana yaliyo na machungu.
Katika makala ya pili nilijenga hoja kuwa mambo ya Zanzibar yanawagusa Watanzania wote, na hakuna mtu mwenye uwezo wa kuzuia Watanzania wasijadili mambo ya Zanzibar kwa sababu wao si Wazanzibari.
Lakini vile vile nilidokeza kuwa ni rahisi zaidi kutafuta kuridhishana kuliko kupatana. Nasikitikia kuona kuwa viongozi wa CCM na CUF (Bara na Visiwani) wamechagua kuridhiana kuliko kupatana.
Ninatambua ugumu wa kupatana; kwani katika kupatana ni lazima kwanza mkubali kuelewana tofauti zenu, mitazamo yenu na maono yenu ya kila mnachokitaka. Katika mazungumzo ya mapatano kila mmoja anakuja na hasira zake, uchungu wake, furaha zake, matamanio yake, n.k na kuviweka mezani.
Katika kufanya hivyo, kila mmoja anamuelewa mwenzake na anajifunua hata yale ambayo angependa yasitambulike. Mazungumzo ya mapatano ni magumu zaidi kuliko kupiga kura za maoni!
Vikorombwezo vya msingi katika mapatano
Ili kuweza kuwa na mazungumzo ya mapatano mambo makubwa matatu yanahitajika. Kwanza kabisa ni usawa. Wanaokuja katika kuzungumza ni lazima waje wakiwa sawa; yaani asiwepo kati yake anayejiona yuko juu ya mwingine au mwingine anayekuja akiwa anajiona duni.
Bila kuwa na usawa ni rahisi sana kuendeleza kutuhumiana. Pili, ni ukweli. Mazungumzo yote ya mapatano ni lazima yajikite katika ukweli. Huwezi kuwa na mapatano ambayo msingi wake ni ulaghai, uongo au ukanaji wa ukweli. Tatu, mapatano ya kweli yana msingi katika utayari wa kukubali kubadilika au kubadilisha msimamo. Anayekwenda kwenye mazungumzo tayari akiwa ameshaamua anachotaka na chochote nje ya hicho, hafai.
Nitatoa mfano ambao unaeleweka vizuri sana. Mojawapo ya mambo yanayokwaza upatanisho wa Waisraeli na Wapalestina ni hadhi ya mji wa Yerusalemu. Waisraeli wanasema Yerusalemu ni mji mkuu usiogawanyika wa taifa la Waisraeli. Wapalestina wanasema Yerusalemu Mashariki uwe mji mkuu wa Taifa la Wapalestina. Hakuna aliye tayari kubadilika au kubadilisha msimamo! Je, ni kitu gani kinaweza kuwafanya wakubaliane? Hakuna.
Mgongano wa Zanzibar haukuanza 1964.
Naomba nirudi nyuma kidogo tena kwenye historia. Kuna baadhi ya watu ambao wanajitahidi sana, tena sana, kuwabambikizia watu wa Bara mzigo wa matatizo ya Zanzibar. Wapo ambao kwa kutokujua historia wamefikia mahali pa kulaumu tofauti za Zanzibar kuwa zinatokana na watu wa Bara.
Na wapo ambao wanaamini kabisa kuwa Zanzibar imegawanyika sababu ya Muungano. Mwanahistoria yeyote (awe Mzanzibari au mtu mwingine) anajua ukweli (kikorombwezo cha pili).
Tofauti za Zanzibar hazikupandwa na Muungano wala na Mapinduzi. Hivyo vyaweza kuwa vimechangia kwa kiasi kikubwa tofauti ambayo tayari ilikuwepo. Na wanafanya makosa wanaodhania kuwa ati Muungano ukivunjika basi tofauti zao nazo zitatoweka kama ukungu wa alfajiri.
Kanuni za mapatano
Ni lazima kutambua tofauti;
hivyo mapatano ni lazima tayambue Kanuni ya kwanza: Tutambue tofauti zetu. Je vyama vya ASP, ZPPP, na ZNP vilisimamia misingi gani wakati vinaundwa? Je ajenda zao za uchaguzi ziliwakilisha maslahi gani.
Je masalia ya wafuasi wake leo wanaamini nini? Je tunaweza kuona mwelekeo wa sera za vyama vilivyopo sasa kama vimebeba itikadi na sera za vyama hivyo vya zamani?
Bila kujua tofauti zetu za msingi ni rahisi sana kuendeleza utawala wa woga na wa kutokuaminiana. Tofauti hizi za kimtazamo, kiitikadi na kimwelekeo ndizo zilisababisha kuwe na mgongano Zanzibar na kuendeleza mgawanyiko katika chaguzi zote za 1957, 1961 (mara zote mbili) na hata 1963. Kujaribu kutafuta maridhiano bila kutambua kiini cha tofauti hizo ni kujaribu kukana historia.
Zipo tofauti za msingi zinazowagawa watu wa Zanzibar na tofauti hizo hazitafutika kwa sababu wanasiasa wameamua kuitisha kura ya maoni kuhusu serikali ya Mseto! Anayefikiria kuwa serikali ya Mseto itafuta matatizo yote ya Zanzibar na tofauti za wananchi wake ni mkanaji wa historia.
Kutambua yale yanayounganisha
Haitoshi peke yake kutambua tofauti za watu mbalimbali na makundi mbalimbali lakini ni muhimu zaidi kutambua kile kinachowaunganisha. Leo hii kitu kibaya kinawaunganisha Zanzibar na ninaamini wao wenyewe wanaamini ni kitu kizuri.
Kitu hicho ni chuki ya baadhi ya watu dhidi ya Tanzania Bara. Ukweli huu ni lazima usemwe. Tangu nimeanza kuandika juu ya somo hili wiki chache zilizopita nimepokea maneno ambayo hata nikiamua kuyaandika hapa kuwa ni mawazo ya watu ambao ninaamini ni Watanzania wenzangu (sikuzaliwa Tanganyika!) huwezi kuamini.
Chuki hii kwa upande mmoja inachangiwa na ukweli kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 yasingefanikiwa na kusimama kama Tanganyika isingejiunga na Zanzibar miezi michache baadaye.
Kwamba Muungano wa Tanzania ulizuia kwa kiasi cha kushangaza umwagikaji damu mkubwa zaidi katika visiwa hivyo endapo serikali ya Sultani wa Oman aliyeng’olewa ingeweza kujiandaa kurudi madarakani. Naogopa kukisikia kile ambacho kingetokea endapo mashabiki na wafuasi wa Sultani wangepata muda wa kujiandaa kuiangusha Serikali ya Mapinduzi.
“Kosa” hili la Muungano halijasamehewa na baadhi ya watu, na ni kutokana na hilo wapo ambao wana kisirani na kinyongo na Bara kwa sababu hiyo tu.
Lakini hata hivyo, kipo kizazi kipya ambacho kimezaliwa katika Tanzania (siyo Jamhuri ya Zanzibar) ambao leo nao wanaamini kabisa kuwa Muungano ni kitu kibaya na kuwa watu wa Bra hawataki maendeleo ya Zanzibar. Mtu mmoja ameniandikia hivi:
“Ni kweli kuwa kura ya maoni tunayotaka isiishie maridhiano, tu lakini hata Muungano kwa vile hili pia ni jambo zito na watu hawakuwahi kuulizwa wakati Watanganyika walipovimeza visiwa hivi. Ni bahati tu kuwa havimezeki. Kashindwa Mreno na Mwarabu atakuwa Mtanganyika mjukuu wa watumwa zetu?” – Mkombe
Binafsi, naamini Wazanzibari wanapaswa kuunganishwa na mambo makubwa zaidi kama tulivyoshuhudia siku za karibuni. La kwanza ni suala la matumizi ya raslimali zake na uhuru wake kujiendeshea mambo yake ya kisiasa.
Mimi ni mmoja wa watu ambao tunaamini kabisa kuwa suala la mafuta yanayopatikana Zanzibar lisimamiwe na Zanzibar yenyewe. Zanzibar kama kisiwa ina vikwazo vingi vya nafasi ya kujiendeleza kiuchumi na kama mafuta yatapatikana, basi, itakuwa heri.
Na ninaamini kabisa kuwa mafuta yakichimbwa Zanzibar hakutadhuru Bara wala kusababisha matatizo makubwa ya kiuchumi. Haya ndiyo mambo ya kuunganisha.
Lakini wale wanaofikiria kuwa udugu wa watu wa bara na Zanzibar utakoma kwa sababu watu walichukizwa na Muungano, hawa wanaota. Udugu na damu ya watu wa Zanzibar na Bara vimechanganyika katika miili ya Wazanzibari kiasi kwamba usishangae watu wakipimwa vinasaba (DNA) wakajikuta wana damu zaidi ya watu wa Bara kuliko ya Uarabuni; japo wao wenyewe wanajiita Waarabu, Washirazi nk.
Tume ya Ukweli na Mapatano (Truth and Reconciliation Commission)
Lakini kuna mambo ambayo kwa kadri ya vizazi vya watu vinaishi yataendelea kuwa sumu katika maisha yao na kuwatofautisha Wazanzibari. Lakini ninaamini ili kuweza kufikia mapatano ya kweli, naamini ipo haja ya kuundwa kwa tume huru ya Ukweli na Mapatano.
Ni tume ya ukweli kwa sababu jukumu lake la kwanza lapaswa kukusanya ukweli wote kwa watu wote bila ya kuogopa matokeo ya ukweli huo. Tume iwe tayari kutoa msamaha kwa wote watakaokubali kusimama na kutoa ushahidi wa ukweli.
Tume hiyo iongozwe na mtu mwenye kaliba ya kimataifa, anayejulikana kwa weledi wake katika mambo ya sheria na haki za binadamu na ambaye yeye mwenyewe hatokuwa mtu wa kugawanya.
Tume hiyo ipewe jukumu la kufuatailia, kukusanya na hatimaye kuweka hadharani mambo yafuatayo.
- Ikusanye historia kabla na baada ya ujio wa Sultani. Historia hii inajulikana na imeandikwa kwa kiasi kikubwa na imepokelewa vya kutosha. Jukumu ni kuhakikisha historia hii inaandikwa kwa ukweli na kwa uwazi tena ikijibu maswali muhimu ya maisha ya watu wa Zanzibar.
- Pasipo kuogopa kuwaudhi watu au kuwakera tume ipewe nafasi ya kuchambua hali ya maisha ya matabaka mbalimbali wakati wa utawala wa Sultani na kutolea maoni kama hali hiyo ingeweza kuendelea na kukubaliwa kizazi na kizazi.
- Iangalie hali ya kisiasa Zanzibar chini ya Usimamizi wa Uingereza hadi kuelekea harakati za Uhuru.
- Iangalie historia ya kisiasa na kimaisha ya wakati wa Uhuru na kuchambua kwanini tayari kulitokea migongano ya kisiasa 1957, 1961, na 1963.
Hii ni katika kuelewa kiini cha tofauti za kisiasa za Zanzibar bila kuona haya. Historia ya vyama vya ZNP, ZPPP, ASP na Umma na makundi mengine yaliyokuwa na mirengo ya kisiasa yaangaliwe kwa uwazi na ukweli. Kwa vile baadhi ya watu waliokuwepo wakati huo bado wa hai ni vizuri kukusanya historia hiyo kutoka kwao vile vile.
- Tume iangalie matukio yaliyofuatia uchaguzi wa 1963 ulioingiza Serikali ya Mseto ya Shamte na hatimaye matukio yaliyosababisha mapinduzi ya 1964. Katika hili ni lazima kuangalia gharama kubwa ya maisha na vitu ambayo visiwa hivyo vililipia katika mapinduzi hayo.
- Tume iangalie nafasi ya Sultani katika Zanzibar huru na kama kwa namna yoyote uzao wa Sultani wa sasa wapaswa kushirikishwa katika kuleta mapatano ya kweli. Ni wazi kuwa Sultani wa Zanzibar hajakana kiti chake cha Usultani wala watoto wake kukana haki yao ya kurithi kiti hicho. Kwa kadri ya kwamba bado wanadai haki hiyo, ni wazi kuwa mapatano ya kweli hayawezi kufikiwa.
- Tume iangalie mtiririko wa uamuzi wa Zanzibar kuungana na Tanganyika na kuangalia kama makubaliano yale ya Muungano yalifuatwa ipasavyo.
- Tume iangalie vile vile mauaji ya Mzee Karume na matukio yaliyochangia hilo.
- Tume ichunguze mambo yote ambayo ni muhimu katika kuleta maridhiano na mapatano ya kweli.
Tume ikishamaliza kazi yake ni LAZIMA itoe Mapendekezo ya mambo gani yafanyike kwa upande wa Zanzibar na kwa upande wa Serikali ya Muungano katika kuleta umoja na mshikamano ndani ya tofauti za kisiasa visiwani humo na vile vile kudumisha Muungano.
Aidha, ripoti yake yote ITOLEWE hadharani ili kila Mzanzibari na kila Mtanzania apate nafasi ya kuangalia ripoti hiyo. Na ni kutoka hapo ndipo mazungumzo ya kutekeleza mapendekezo hayo yafanyike.
Na ni kutoka hapo ndio kwa mara ya kwanza Zanzibar na Tanzania, kwa ujumla, tutakuwa tumepiga hatua ya kwanza ya mapatano ya kweli.

Barua-pepe: