MASLAHI bora ya wafanyakazi nchini hayawezi kupatikana kwa kutegemea utashi wa wanasiasa.
Kama alivyowahi kuzungumza Rais wa 35 wa Marekani, aliyeuawa kwa risasi, John Kennedy: Things do not happen. Things are made to happen; (kwa tafsiri inayokidhi mjadala wa leo tunaweza kusema; mambo hayajinyooshi, bali hunyooshwa.
Maslahi ya wafanyakazi yanapatikana kwa kuzingatia hesabu mahsusi za kiuchumi, zikihusu uvunaji wa rasimali za nchi na mgawanyo katika matumizi yake.
Wanasiasa hawana hakimiliki ya Taifa wala rasilimali zilizopo. Tatizo ni kwamba wakati mwingine wafanyakazi kupitia vyama vyao wamewaachia wanasiasa kuamua hatima yao katika wigo usio na mantiki uliopewa jina la “utashi wa kisiasa.”
Haiwezekani uwezo wa mfanyakazi wa kima cha chini kujinunulia chakula cha mwenzi mzima utegemee utashi wa wanasiasa.
Haiwezekani mfanyakazi wa kima cha chini aendelee kukosa fedha za kuhudumia afya ya familia zake kwa sababu tu hakuna utashi wa kisiasa.
Huu ni unyonge mbaya zaidi ya unyonge wa kutawaliwa na wakoloni. Lugha ya utashi wa siasa haiwezi kuendelea kuachwa ikinyanyasa wafanyakazi wa kima cha chini, unyanyasi wenye kiwango sawa na ule uliojitokeza wakati wa biashara ya watumwa.
Takriban miaka mitatu iliyopita, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) lilipendekeza kima cha chini cha mishahara kuwa Sh. 315,000, sababu ikiwa ni kupanda kwa gharama za maisha.
Katika utekelezaji, Serikali iliongeza kima hicho kwa asilimia nne tu, kutoka Sh 80,000 hadi 84,000.
Lakini malalamiko yamezidi miongoni mwa wafanyakazi na kutokana na hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholaus Mgaya, wiki iliyopita ametangaza nia ya kufanya mgomo wa wafanyakazi wakati wowote mwezi huu.
Mgomo unalenga kushinikiza mapendekezo ya nyongeza ya kima cha chini cha mishahara yatekelezwe.
Mbali na hilo, TUCTA pia wanaitaka kupunguza kiwango kikubwa cha kodi ya mshahara kinachotozwa kwa wafanyakazi pamoja na kurekebisha utaratibu mbovu wa malipo ya Mfuko wa Hifadhi za Jamii.
Kubwa zaidi, kama Serikali itatia mizengwe mgomo usifanyike, TUCTA wamedai kuhamasisha wafanyakazi kususia upigaji kura.
Lakini wakati wafanyakazi wakiwa na madai hayo, na kwa kiasi kikubwa wakitegemea utashi wa kisiasa, wanasiasa wamezembea na serikali imepoteza Sh. bilioni saba, kwa malipo hewa ya mishahara.
Serikali imejikuta ikilipa mishahara hewa ya Sh. bilioni saba katika kipindi ambacho mapendekezo ya wafanyakazi yametolewa bila utekelezaji; yaani kati ya mwaka 2006 hadi 2009.
Upotevu huo wa shilingi bilioni saba umethibitishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, bungeni Januari 29, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri Ghasia, tatizo lilibainika baada ya kufanyika uhakiki wa raslimali watu katika sekta ya elimu na afya pekee. Sekta za ulinzi na nyinginezo hazikuhakikiwa.
Uhakiki ulihusisha sekondari, vyuo vya elimu, hospitali za serikali, vituo vya afya, zahanati, vyuo vya afya, hospitali binafsi na za mashirika ya umma.
Kubwa zaidi, wizara mbili zilibainika kung’ara kwa malipo hewa. Hizi ni Wizara za Elimu na Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Serikali iliyotarajiwa kutoa nyongeza muafaka ya kima cha chini haikufanya hivyo na badala yake ilikuwa ikilipa mishahara hewa kwa wastaafu, marehemu na waliofukuzwa au kuacha kazi.
Marehemu hao waliendelea kuwamo kwenye orodha ya watumishi wa umma na hatimaye kitita cha Sh. bilioni saba kikatimia.
Ingawa Waziri hakutaja majina ya waliofanikisha hasara hiyo ya Sh. bilioni saba, lakini naamini ni mtandao mpana wa maofisa waandamizi, wanasiasa vigogo na hata waganga njaa.
Ndiyo, wamo wanasiasa vigogo wenye ukwasi usio na maelezo kiasi cha kuwawia vigumu kutaja mali wanazomiliki hadharani kama alivyofanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Masuala mawili yanajitokeza hapa. Mosi, madai ya maslahi bora na ya muda mrefu ya wafanyakazi, hasa wa kima cha chini.
Pili, serikali kuzembea na hivyo kujipunguzia uwezo wa kifedha kukidhi madai ya wafanyakazi kutokana na kupoteza Sh. bilioni saba katika sekta mbili tu za afya na elimu.
Katika hayo masuala mawili, uhakika unajitokeza kwamba; bila shaka yoyote uwezo wa kutimiza madai ya wafanyakazi upo.
Wafanyakazi sasa lazima wapate haki zao bila kusubiri tabasamu la wanasiasa ndani ya wigo wa utashi wa kisiasa.
Ni dhahiri, kutotekeleza mapendekezo ya wafanyakazi hakutokani na uwezo mdogo wa kifedha serikalini bali ni kutokuwapo kwa utashi wa kisiasa.
Viongozi wanashindwa kuelewa ustawi wa wafanyakazi ni suala la kipaumbele kwa sababu kadhaa.
Sababu hizo ni mosi, mfanyakazi anayelipwa vizuri ni mlipaji kodi wa uhakika wa serikali (kwa kutozwa kodi nafuu).
Pili, mfanyakazi anayelipwa kwa kiwango cha kumudu mahitaji yake ya msingi ni mjenzi imara wa Taifa, katika nyanja za kibiashara, kitaifa na kati ya nchi moja na nyingine.
Tatu, mfanyakazi anayelipwa kwa kiwango cha kumudu mahitaji yake ya msingi ni mdau muhimu katika kudhibiti usalama wa taifa.
Nisisitize, usalama wa uhakika wa taifa msingi wake si kukamata ovyo watu au kuwa na silaha kali bali ni wafanyakazi wenye ujira wa kuwawezesha angalau kumudu mahitaji yao ya msingi ya kila siku.
Usalama wa Taifa, hauwezi kuwapo kama kuna viongozi wanaonufaika kwa malipo hewa ya Sh. bilioni saba, ilhali wafanyakazi wa kima cha chini wakisubiri utashi wa kisiasa kupata nyongeza.
Nne, nchi yenye wafanyakazi wa kima cha chini wenye ujira wa wastani inakuwa katika nafasi nzuri ya uchochezi wa kimaendeleo na uwajibikaji.
Tano, ingawa takwimu nchini zinabainisha asilimia 80 ya Watanzania wako vijijini (wakulima), ukweli unabaki pale pale kwamba mfanyakazi asiye na mgogoro wa maslahi na mwajiri, wakulima pia watafikiwa na athari chanya za mfanyakazi wa aina hiyo.
Nimnukuu mpigania haki maarufu nchini Marekani, Martin Luther King Jr alisema: “History is a great teacher. Now everyone knows that the labor movement did not diminish the strength of the nation but enlarged it.. Those who attack labor forget these simple truths, but history remembers them."
Tafsiri isiyo rasmi kwamba: “Historia ni mwalimu bora zaidi. Sasa kila mmoja anafahamu kwamba harakati za wafanyakazi hazidhoofishi taifa bali zinaimarisha. Wanaopinga wamesahau ukweli huu lakini historia inawakumbusha.”
Naam, historia ya ulimwengu inaweza kuchukua mkondo wake hata hapa nchini. Nasisitiza serikali inaweza kulipa wafanyakazi kima cha chini kinachopendekezwa.
Uwezo upo kama gharama zisizo za msingi za uendeshaji serikali zitafutwa. Kipaumbele cha serikali hakiwezi kuwa matumizi makubwa yasiyo ya lazima.
Bajeti inayoelekea kuhitimishwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilioongoza kwa kumegewa bajeti nono takriban asilimia 18. Leo, tunaambiwa wizara hiyo inahusika na malipo hewa ya mishahara.
Je, kuna ulazima gani wa gharama kubwa zinazotokana na serikali kuwa na magari ya kifahari mengi? Kwa nini hata watumishi wasiosafiri vijijini kikazi wapewe magari ya kifahari wakati serikali hiyo hiyo ikizidi kujigamba imeboresha barabara?
Bado nasisitiza, uwezo wa kulipa wafanyakazi kima cha chini cha mshahara wa Sh 315,000. Ni haki yao kudai na si kusubiri utashi wa kisiasa ambao hawajui lini utajitokeza.
Nakubaliana na hoja za Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, isipokuwa hoja inayohusu tishio la kususa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu.
Sikubaliani naye kutokana na ukweli kuwa, njia pekee ya kuwang’oa viongozi wasiojali maslahi ya Wafanyakazi ni upigaji kura.
Kama tunaridhika kuwa mawaziri fulani hawakuwa msaada kwa wafanyakazi, basi wafanyakazi kupitia TUCTA wawaanike hadharani kama kikwazo cha maslahi ya wafanyakazi na hatimaye wahukumiwe kwa kura.
Kura ya kila mfanyakazi itumike kama kichocheo cha kutafuta au kuchagua viongozi watakaotanguliza maslahi ya Wafanyakazi, wakulima na Taifa kwa ujumla.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Simu:
0787-643151