MIONGONI mwa hadithi za kale tulizosoma enzi hizo ilikuwepo ile inayohusu binti wa masikini aliyepata nafasi adimu ya kukutana na mfalme na akamuambia kuwa alikuwa na uwezo wa kufuma nyasi zikageuka dhahabu.
Inasimuliwa kuwa baada ya mfalme kusikia habari hiyo aliwatuma watumishi wake kukusanya nyasi na kuziweka ndani ya chumba, na kisha kumfungia binti huyo na kumtaka hadi ifikapo asubuhi awe amegeuza nyasi hizo kuwa dhahabu; la sivyo kichwa chake kingekatwa.
Inasimuliwa kuwa binti yule aliishia tu kulia na kuomboleza asijue cha kufanya na rundo lile la nyasi hadi kijitu cha ajabu kilipomuonea huruma na kujitokeza na kuamua kumsaidia kwa mapatano kuwa binti yule aliyeponzwa na ulimi wake mwenyewe angekapa kale kajitu mtoto wake wa kwanza atakayemzaa.
Jina la kale kajitu ambalo pia lilikuwa ndio la hadithi yenyewe lilikuwa ni lile linaloweza kufanya uteguke ulimi ukilitamka. Jina hilo ni Rumpelstiltskin.
Hadithi inaeleza kuwa kila asubuhi mfalme akakuta nyasi zimegeuzwa dhahabu na hali hiyo ikaendelea hivyo hadi akaamua kumuoa kabisa yule binti bila angalau hata siku moja kutaka kujua tu binti wa kimasikini anawezaje kugeuza nyasi kuwa dhahabu lakini amemkuta akiwa masikini!
Tunaambiwa kuwa mfalme aliishia kumuoa binti yule ambaye alipojifungua mtoto wa kwanza akakataa kuheshimu mkataba wake na kale kajitu kalikomsaidia wa kukapa mtoto wake wa kwanza. Kajitu kakapasuka kwa hasira na hadithi ikaishia hapo!
Ni baadaye sana tulipopata ufahamu ndipo tulipoanza kuitafakari upya hadithi ile. Kwamba iweje mtu unapata nafasi ya kipekee ya kukutana na sultani halafu badala ya kumuambia jambo la maana unamdanganya kuwa una uwezo wa kugeuza nyasi kuwa dhahabu wakati unajua kabisa kuwa huna?
Lakini la ajabu zaidi ni yule sultani, ambaye pamoja na busara zote anazotegemewa kuwa nazo, si tu kwamba anaamini moja kwa moja mwananchi wake - binti wa kimasikini, ana uwezo wa kufuma nyasi zikawa dhahabu; bali pia hajisumbui hata angalau tu kukesha na binti yule ili kuona anageuzaje nyasi kuwa dhahabu!
Nilikumbuka sana tafakuri hizi, hasa ile ya mtu kupata nafasi ya nyota ya jaha ya kukutana na sultani wake na kuongea naye mambo ambayo hayana faida kwake, Alhamisi iliyopita wakati nikiangalia kipindi cha Bunge cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambacho kinarushwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vyetu vya televisheni.
Hiki ni kipindi cha nusu saa ambacho wabunge hupata nafasi ya kumuuliza maswali kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kupata majibu ya papo kwa papo kutoka kwake.
Kwa kanuni za kawaida kabisa, mpiga kura wa Tanzania anategemea kumsikia mbunge wake akimuuliza swali Waziri Mkuu linalomhusu yeye mpiga kura moja kwa moja na pia kusikia jibu la swali hilo kutoka mdomoni mwa Waziri Mkuu moja kwa moja (from the horse’s mouth), na sio kutoka kwa watendaji wake.
Katika kipindi cha Alhamisi iliyopita, moja ya maswali yaliyoulizwa na mmoja wa wabunge wetu ni lile la kumtaka Waziri Mkuu kueleza ni kwa nini, pamoja na kuwa tumeuondoa ukoloni barani Afrika, bado Wafaransa wanaendelea kuvikalia visiwa vya Komoro.
Hata kabla swali hilo halijamalizika kuulizwa, tayari mimi kama mpiga kura wa nchi hii nilikuwa nimeshaanza kujiuliza moyoni iwapo maswali yote yanayohusu changamoto zinazonikabili kama mwananchi wa kawaida wa Tanzania yalikuwa yamekwisha kiasi cha mbunge wangu kuuliza swali linalohusu Komoro. Yale yale ya Rumpelstiltskin!
Ni kweli kwamba hata wimbo wetu wa taifa unaanza kwa kumtaka (hakuna neno kuomba!) Mungu aibariki Afrika na viongozi wake kwanza ndipo kwenye ubeti wa pili aibariki Tanzania na kudumisha uhuru na umoja wake (bila kumtaka pia abariki na viongozi wake labda kama Wabunge wetu, Mawaziri wetu, Wakuu wetu wa Mikoa na hata viongozi wetu wa serikali za mitaa nk wanaingia katika lile kundi la viongozi wa Afrika!)
Lakini pia ni kanuni ya kawaida kabisa kwamba ni lazima hisani ianzie nyumbani (charity begins at home). Huwezi kuuliza kwa nini mtoto wa jirani yako anakwenda shule na shati lililochanika mgongoni wakati wa kwako anakwenda na kaptura iliyoraruka makalioni!
Kwa kanuni ya kawaida kabisa mpiga kura wa Tanzania anaamini kwamba kipindi cha nusu saa cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, ni chake kwa ajili ya kusikiliza majibu ya serikali kupitia kwa Waziri Mkuu kuhusiana na masuala mbalimbali yanayomhusu.
Lakini pia hata inapotokea swali kama tunalohoji hapa, mpiga kura kama mimi ningependa kuona ni swali ambalo ni gumu mno kiasi cha majibu yake kustahili kutolewa na Waziri Mkuu tu.
Majibu ya Waziri Mkuu kwa swali la Mheshimiwa mbunge kuhusu Komoro yalikuwa ya wazi na rahisi mno kiasi kwamba mbunge aliyeliuliza alipaswa kuwa anayafahamu, na hivyo kutolazimika kutumia nusu saa ya maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kuuliza alichouliza.
Kwamba Komoro ni mjumuiko wa visiwa vinne ambavyo vyote vilipewa uhuru wa kupiga kura kuamua kama vinataka kuwa huru kujiendeshea mambo yake ama kuendelea kuwa chini ya himaya ya Wafaransa, na kwamba visiwa vitatu viliamua kuwa huru na kimoja tu ndicho wananchi wake waliamua kuendelea kubaki chini ya himaya ya Wafaransa, ni mambo ambayo wengi (nina hakika na mbunge mwenyewe) tunayafahamu.
Inawezekana kuna maelezo mengine ya ndani zaidi kuhusu visiwa vya Komoro, lakini majibu haya ya Waziri Mkuu kwa swali la Mheshimiwa yalikuwa ni short and clear mno kiasi kwamba nilitegemea mheshimiwa mbunge awe pia anayafahamu na hivyo kutolazimika kumsubiri Waziri Mkuu kumfahamisha.
Lingine lililonishangaza ni kipindi hicho cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kuchukua muda mchache sana kutokana na kukosekana kwa maswali kutoka kwa waheshimiwa wabunge, na hivyo kumlazimu Spika wa Bunge Mh. Samwel Sitta kukikatisha na kuendelea na ratiba nyingine za bunge.
Kipindi cha Alhamisi iliyopita kilitumia dakika 15 tu badala ya 30 zilizopangwa kutokana na kukosekana kwa maswali kutoka kwa waheshimiwa wabunge wetu.
Kwa vile hakuna maelezo ya kuwepo kwa hali yoyote isiyokuwa ya kawaida iliyosababisha hali hiyo tunabaki kuelewa tu kuwa wabunge wetu hawakuwa na maswali ya kumuuliza Waziri Mkuu.
Nimejiuliza maswali kadhaa kuhusu hili. Hivi kweli waheshimiwa wabunge wetu zaidi ya 300 wanaotuwakilisha walikuwa hawana maswali ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kiasi cha kipindi hicho kulazimika kukatishwa na kuendelea na ratiba nyingine za Bunge kwa kukosa maswali?
Ni kweli kwamba waheshimiwa wetu wabunge walikuwa wameshindwa kujaza kipindi cha nusu saa tu cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kwa kumuuliza maswali kemkem ambayo yangemlazimisha Mheshimiwa Spika kukatisha kipindi kwa vile muda umekwisha na sio kwa kuwa maswali yamekwisha?
Kwa hali kama hii waheshimiwa wabunge wetu watakuwa na haki ya kutaka kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu kiongezwe muda wakati wanashindwa kujaza hata nusu saa tu ya kipindi hicho kwa maswali magumu yanayohusu ‘mtoto wetu kuvaa shati lililochanika mgongoni hata kabla hatujajiuliza ya mtoto wa jirani kuvaa kaptura iliyoraruka kwenye makalio?
Tumalizie kwa kuwataka waheshimiwa wabunge wetu kumuuliza Waziri Mkuu wetu maswali magumu ambayo sio tu yatamtoa jasho; bali pia yatadhibitisha pasi na shaka kuwa nusu saa iliyotengwa kwa ajili ya kipindi hicho haitoshi.

Blogu: