KWA mtu asiye makini au mwenye kasumba zake, ziwe za kisomi, kidini, kibepari au kiutandawizi, atachora picha inayoonyesha kuwa Watanzania wengi ni fukara na mbumbumbu kama mzungu wa reli.
Kwa vigezo vinavyopima ufukara kwa kutumia pesa au mali-dunia, pengine ni kweli Watanzania walio wengi wamefukarishwa, ama kwa uvivu wao, lakini wengi ni matokeo ya sera fukarishi, sera zinazototoa watu fukara na kuwatamia wakiwa mayai viza.
Lakini nakataa kwamba Watanzania ni mbumbumbu; kwa maana kwamba hawana wanalolijua, na kwamba ni watu wakupelekwa tu kama ng’ombe!
Kwa wale ambao wanafanya kazi au kukutana na Watanzania hawa waliofukarishwa, hawa wadogowadogo na akachukua muda kuwasikiliza na kuwaelewa, iwe kijijini au maofisini, atabaini kwamba Tanzania ina watu ambao wanaweza kutatua matatizo yetu.
Tatizo ni kwamba watu hawa ambao ni wengi kuliko watunga sera na watoa maamuzi , wamepuuzwa kwa muda mrefu mpaka wakapoteza uwezo wa kujiamini kwamba nao wanaweza. Mifumo ya maendeleo tuliyorithi kutoka nchi za Ughaibuni ambayo ni kandamizi na ina bagua walio wengi imezidi kutufanya tufarakane.
Kwa mfano, demokrasia ya vyama na hasa ya vyama vingi, imetujengea matabaka na kutulazimisha tujiunge huku au kule. Ni dhana nzuri lakini je ni kwa nini wengi hawajiungi na kujitoa mhanga na kujenga vyama vyao kama enzi ya vita vya ukombozi?
Je, chama cha siasa katika zama hizi za ‘utandawizi’ kina kazi gani ya ziada ukiacha kushika dola na mihimili yake Bunge na Mahakama?
Ukweli ni kwamba kwa mfumo tulionao, na kitawale chama chochote, na aje mtawala mwingine ye yote, hakuna jipya kwa Watanzania.
Kwa maoni yangu, kazi kubwa ya chama cha siasa ni kuwaunganisha wananchi kifikra na kimoyo ili wajitambue wao ni nani na kuwajengea matumaini kuwa wanaheshimiwa, wanapendwa, wanafursa za kuendesha maisha yao leo, kesho na keshokutwa bila hofu.
Chama cha siasa kina wajibu wa kujenga taswira na haiba ya watu wake ili popote watakapokuwa kila mtu anauliza; “nadhani wewe ni m-Tanzania?”.
Na kama nchi zote za ki-Afrika zitakua na mwelekeo wa namna hiyo, basi, inaleta heshima kubwa zaidi unapoingia popote hata kama huna ngozi nyeusi, watu wanajua wewe ni mwana wa Afrika. Jinsi ulivyovaa, unavyozungumza, unavyohusiana na watu, ulivyo tayari wakati wowote kutetea maslahi ya nduguzo kwa akili na uwezo wako wote! Lazima watakebehi “hebu toka hapa na U-Afrika wako, ni ushamba tu”. Wanakebehi kwa kuwa wanajua umeokoka na unajitambua wewe ni nani!
Mfano mwingine ni vyombo vya habari ambavyo haviwafikii wengi kwa wakati, labda afadhali kidogo Redio na magazeti; hata kama utalipata baada ya mwezi na kwenye umeme labda nao wanaangalia luninga. Lakini suala hapa ni je wanapata na kutafuta habari gani?
Je vyombo vya habari kwa mfumo huu wa kileo vinajenga vipi umoja wa kitaifa? Vinatumiaje dhamana waliyopewa ya kutoa huduma iwe leseni au masafa ya redio na luninga kwa maslahi ya Watanzania?
Mwenye leseni ya kuuza mchele au madawa akiuza vyakula vilivyooza au madawa yaliyopitwa muda wake wa kutumia anashughulikiwa lakini kwa vyombo vya habari nini ukomo wa uhuru wao? Wanachangia vipi katika kutoa mijadala inayojenga fikra na kutekenya ari za ubunifu wa kisayansi, teknolojia na sanaa ili tupate kuwekeza kwenye shughuli zitakazotufanya tujiletee maendeleo?
Kwa wale tuliolelewa na kukua katika miaka ya 1950, 60 hata 70, tulikua tunasikia baadhi ya viongozi katika vita vya ukombozi walisalitiwa na wenzao na hivyo kupoteza maisha yao.
Enzi hizo mashirika makubwa ya kijasusi yalikua yakihusishwa na kashfa hizi. Kwa mfano FBI na CIA, KGB, MOSSAD walikua na mipango kabambe ya kuwavuruga, kuwavunjia heshima na kuwaangamiza baadhi ya viongozi weusi na vyama vyao huko Marekani na Afrika.
Baadhi ya mbinu walizotumia ni kuwagombanisha wenyewe kwa wenyewe, kuweka majasusi wao ndani ya vyama. Inasemekana lengo kubwa lilikua kuhakikisha kuwa hata siku moja hapatatokea kiongozi mweusi atakayewaunganisha watu weusi ili wawe na umoja wenye nguvu na kuwaleta vijana wengi katika vuguvugu hilo la kimapinduzi.
Tanzania tulishuhudia wanamapinduzi wasanii kama Mzee Makongoro akiimba kuhusu wasaliti wa enzi hizo ”eti walinunuliwa pombe, na mikate ya siagi na nyama za mishikaki, wako wapi?” Au wasaliti wa FRELIMO chini ya Komredi Samora Machel.
Nahisi hii ilikua ni juhudi ya viongozi kuwakumbusha wananchi kuwa macho wakati wote; maana adui hana rangi na kikulacho kinguoni mwako.
Haijalishi wewe ni mtendaji mkuu katika taasisi au kiongozi wa dini, mbunge, waziri au mkuu wa wilaya, unaweza bado ukawa msaliti! Unaweza ukatumiwa kuvuruga nchi isitawalike kwa kupewa mikate ya siagi - siku hizi vijisenti.
Naamini mbinu za kuangamiza mapinduzi ya kweli bado zipo isipokua hizi za sasa “zimeenda shule” kwa hiyo si rahisi kuziona; hasa kwa sisi ambao ni waathirika.
Hivi karibuni tu tumeshuhudia Rais Barack Hussein Obama wa Marekani akiandamwa wakati anatimiza mwaka mmoja wa uongozi. Wabaya wake wanasema kashindwa kutimiza ahadi alizotoa kwa hiyo kashindwa kazi. Kama wangeweza kumtoa urais, wangefanya hivyo.
Kwa watu ambao ni wanafiki walifurahia tathmini iliyofanywa juu ya Obama bila kuangalia ukweli kwamba kwa karne zaidi ya mbili Marekani imetawaliwa na Wamarekani wenye asili ya Ulaya.
Mifumo ya kibepari imeota mizizi kwa muda wote huo. Leo hii, kwa mara ya kwanza, amepatikana Rais mwenye asili ya Afrika umma wa Marekani unataka apindue sera za karne na karne katika mwaka mmoja!
Hawakumbuki kuwa mwaka mmoja tu kabla ya Obama kuingia Ikulu, Marekani ilikua inanuka na kuchukiwa dunia nzima. H ata Wamarekani wenyewe walikua wanaona haya kujitambulisha kama wazawa wa huko!
Kwa hiyo, kazi ya kwanza ilikua kufagia uchafu ulioachwa na kurudisha hadhi ya nchi, kazi ambayo amejitahidi; hata kama sio mia kwa mia.
Hawaangalii kuwa watendaji na watoa maamuzi katika ngazi na vitengo mbalimbali wamesheheni kila aina ya watu ambao japo hajui kama kweli wako upande wake, lakini inabidi awaamini!
Nchi inapoonekana haitawaliki, au kazi hazifanyiki ni kwamba kuna wasaliti wachache ambao kwa makusudi wanahujumu juhudi za Obama ili aonekane kazi imemshinda.
Katika mwaka wa kwanza, Rais Obama, pamoja na vikwazo vyote, anawabana mabepari hasa kwenye mabenki warudishe fedha walizokopeshwa na serikali wakati wa sekeseke la uchumi kudorora ambazo ni kodi za watu. Kaamua achukiwe na wakubwa hao ambao wananeemeka kwa ajili ya kuwanyonya jasho na damu ya watu fukara.
Sasa tatizo ni kwamba ukilishwa taarifa kama hizo mchana na usiku, ambazo labda huzielewi vizuri na hujui nani yuko nyuma ya pazia, basi nawe utaanza kuamini Obama na kusema ‘Obama bwana, bomu tu, bora wazungu’ kumbe tatizo la Marekani ni kubwa kuliko Obama. Watauana bure!
Watanzania tumepitia mitihani mingi. Amini usiamini, athari za biashara ya utumwa bado zipo, athari za ukoloni na ukoloni mambo leo bado zipo. Cheki majina yetu, cheki tunavyoikataa lugha yetu wakati hata Wa-fini wanazungumza Kifini ndani ya Bunge lao la Ulaya, na huwaelezi kitu.
Ni kwa sababu bado wanakumbuka walivyotawaliwa na wa-Swidi na kisha Wa-Rusi na walivyonyang’anywa lugha yao.
Awamu ya Kwanza, chini ya Mwalimu Nyerere, ilifanya jitihada ya kujenga taifa jipya lenye kufuata misingi ya haki sawa kwa wote; angalau kwa kuanzia zile za msingi; na kujenga uwezo wa vijana kupitia elimu ili waweze kujenga taifa linalojitegemea.
Awamu ya Pili ilijitahidi kwa kusaidiwa na wakubwa kututoa katika ‘utumwa’ wa Awamu ya Kwanza na kutulambisha utamu wa ubepari kwa kuwa ‘mateja’ wa bidhaa zilizozalishwa kutoka nje na anasa bila kufanya kazi.
Awamu ya Tatu ikajitahidi kuweka sera, sheria na taratibu ili tusiende kiholela katika juhudi za kuwa dampo la bidhaa za nje, na tuwe wanakijiji wa utandawazi watiifu.
Awamu ya Nne imeachiwa itekeleza yaliyoachwa na awamu ya tatu kwa kutembea katika kamba nyembamba ili kwa upande mmoja, kukidhi matarajio yetu na upande wa wapili kukabiliana na wakubwa wa nje ambao tulishawakubali watuendeshee nchi kwa rimoti kontroli.
Watanzania tuko njia panda. Suala hili silakufanyia mzaha wala kuleta ushabiki. Viongozi na wananchi tujiulize tunataka taifa la namna gani katika miaka 50 ijayo. Tunataka serikali ifanye nini, iwe ya CCM, CUF au CHADEMA au hata kama kutakuwa hakuna chama ili tuwe na uhuru wa kuamua kwa dhati mambo yetu bila vitisho vya kuangamizwa na machifu wa kijiji cha ‘utandawizi’?
Wakati wanasiasa wanazunguka kutafuta kupigiwa kura, inabidi wajiulize kwa nini wanadhani wanastahili?
Hatutaki wasaliti wala wanafiki ambao wanataka tuwapigie kura ili wazidi kutuchoma moto, wazidi kuharibu rasilimali na maadili kwa ajili ya vizazi vyetu vijavyo.
Hatutaki viongozi ambao wanafanya maamuzi ili kukidhi mahitaji ya leo tu. Matatizo yetu yanahitaji miongo mingi kuyatatua.
Je serikali ya Awamu ya Nne, kimkakati, ianzie wapi kubandua gogo ili awamu itakayofuata ipokee na iendelee wapi?
Kama ni kuanzia kwenye tuhuma za ufisadi, Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kuwajibika kwa kosa ambalo hakulitenda wakati akiwa waziri, na bado akaja kuwa Rais wa Jamhuri yetu. Kwa nini katika zama hizi tunaona muhali kuwajibika kwa hiyari mpaka Rais atulazimishe?
Tunawaomba wenzetu msicheze na roho za Mwenyezi Mungu zisizo na hatia kwa kutaka madaraka au sifa!
Mwisho hatutaki viongozi waliochoka kifikra, viongozi ambao hawajakomaa kifikra, viongozi ambao ni akina “ndiyo mzee” au kina “pondamali kufa kwaja”.
Tunataka uongozi ulio na uwiano kati ya wazee na vijana; kwani vijana wana mbio na wazee ndio wanaojua njia. Uwiano kati ya wanawake na wanaume; kwani wanaume ni mabingwa wa kuongea na kuagiza na wanawake ndio wanaojua namna ya kutekeleza, kusimamia, kufuatilia na kuleta mabadiliko.
