NATUMANI kwamba nimeeleweka kwamba napendekeza kwamba viongozi wote wa wilaya wachaguliwe moja kwa moja na wananchi watakaowaongoza. (Mantiki ya kweli ya neno ‘kiongozi’ wa kisiasa ni mtu aliyechaguliwa, vinginevyo anakuwa ni ofisa tu).
Napendekeza kwamba katika uchaguzi mkuu unaofanyika kila baada ya miaka mitano, wananchi katika wilaya zao wachague viongozi wao wa kiwilaya kwa kura ya moja kwa moja. Hili linaweza kufanyika katika ngazi zote, ndiyo kusema wananchi wanaweza kuchagua wajumbe wa halmashauri ya wilaya na wakati huo huo wakamchagua mwenyekiti ambaye ndiye atakuwa mkuu wa wilaya, au wakiisha kuichagua halmashauri wanaiachia halmashauri hilo jukumu la kuchagua mwenyekiti wake na wasaididizi wake katika idara mbali mbali.
Baina ya mifumo hii miwli, binafsi ningependelea zaidi kuwa na mkuu wa wilaya anayechaguliwa moja kwa moja na wananchi, kwa sababu utaratibu huo unamfanya kila mwananchi ajihisi kwamba anao mchango wa moja kwa moja katika kumweka kiongozi wake madarakani, na hivyo kujihisi anayo haki ya kumtaraji awajibike kwake.
Ndani ya halmashauri ya wilaya wajumbe wanaweza kuwachagua wakuu wa idara mbali mbali za serikali ya wilaya ambao wataongoza vitengo mbali mbali, kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, maji, ardhi, mazingira, afya na kadhalika, nao hao watakuwa na watendaji wanaoajiriwa kufuatana na sifa za ujuzi na uwezo.
Maofisa watendaji wanaweza kuajiriwa kutoka ko kote nchini bila kujali kama ni wazaliwa wa wilaya hiyo, alimradi wanazo sifa za kiutendaji, na wamepitia utaratibu wa ushindani ulio wazi kwa maana ya nafasi kutangazwa hadharani, na usaili unafanyika kwa utaratibu unaoeleweka.
(Yumkin, ziko idara ambazo kwa silika yake hazina budi kubakia mikononi mwa serikali kuu, kwa mfano Polisi, Jeshi la Ulinzi, Usalama wa Taifa, Mahakama, Sheria, n.k).
Mantiki ya kupendekeza utaratibu wa wakuu wa wilaya wanaochaguliwa na watu wao ni kuwapa wanancui mamlaka juu ya ngazi muhimu sana katika maisha yao, ngazi ambayo ndiyo inayosimamia masuala yote muhimu ya uchumi na uhai wa wananchi wa wilaya, kiasi kwamba si haki kuendelea na utaratibu wa wakuu wa ngazi hii wateuliwe kutoka Dar es Salaam bila kuwapo vigezo vya kuwapima.
Ukosekanaji huu wa vigezo wakati mwingine unatisha. Kulikuwa na wakati baadhi ya wakuu wa wilaya walipewa nafasi hizo kwa sababu awali walikuwa madereva wazuri wa chama cha TANU enzi za harakati za kudai Uhuru, jambo ambalo labda lilikuwa na mantiki wakati ule kwani ni uungwana kumzawadia mtu aliyetoa mchango muhimu katika harakati kama hiyo.
Hata hivyo, kadri tulivyopiga hatua ndivyo tulivyogundua kwamba haifai tena kuzitumia nafasi hizi kama zawadi kwa huduma zilizopita, hata kama zilikuwa muhimu, bali kuwaweka watu ambao watafanya kazi ya kusaidia kusukuma maendeleo.
Tatizo limekuwa kwamba nafasi ya mkuu wa wilaya imebakia kuwa ofisi ya kujazwa na serikali kuu, hususan na rais, waziri mkuu au waziri mhusika na utawala wa mikoa. Hakuna vigezo vinavyotumika kumpata mkuu wa wilaya, kwa hiyo ye yote yule anaweza kuteuliwa.
Hakuna ukomo wa kipindi cha ajira, kwa hiyo wapo wakuu wa wilaya waliokaa ofisini miaka ishirini na haieleweki wanafanya nini. Baadhi yao hupata bahati ya kupandishwa na kuwa wakuu wa mikoa, lakini wengi huishia huko huko wilayani, wakafifia, wakajitowekea kimya kimya wakiwa wamechoka ‘ile mbaya.’
Wala hawafanani. Imewahi kutokea kwamba katika orodha ya wakuu wa wilaya yumo mwenye shahada ya udkatari wa falsafa, lakini pia yumo mwingine anapata shida kuandika jina lake. Pia akawamo brigedia-jenerali mstaafu na papo hapo yumo koplo mstaafu.
Wakati fulani brigedia-jenerali alikuwa chini ya mkuu wa mkoa aliyekuwa ni kapteni - kichekesho hasa katika mazingira yetu ambamo watu hupenda sana kubeba vyeo vya kijeshi wakati wanafanya kazi za kisiasa.
Hii imekuwa na maana kwamba sifa zinazotafutwa kwa mkuu wa wilaya zinajulikana kwa anayemteua, basi; wengine wanabaki kujiuliza ni kitu gani kinamfanya mtu ateuliwe na mwingine asiteuliwe.
Hivyo, haishangazi kwamba wengi wanaamini kwamba baadhi ya walioteuliwa wana uhusiano wa kimapenzi na waliowateua. Kama hivyo ndivyo, hakuna matumaini kwamba hata siku moja watu kama hao wataweza kusimamia maendeleo katika wilaya walikopelekwa ili “wawapokee’ mabosi wanapokuwa ziarani.
Rai yangu ni kwamba sasa tunalazimika kuondokana na utaratibu huu usiofaa na tufanye mapinduzi ya kiutawala na kiuongozi kwa nia ya kuleta maendeleo ya kweli na ya haraka kidogo, kwa sababu tumechelewa sana kimaendeleo na ipo hatari ya kushindwa kuelewana baada ya muda si mrefu.
Wananchi wapewe uwezo wa kuamua mustakabali wao kwa kuwachagua watu wanaoamini watawaongoza wajitafutie maendeleo yao. Mkuu wa wilaya na timu yake watafanya kazi wakijua kwamba wanatathminiwa na wapiga kura wao, na kwamba wakishidnwa kufanya walichoahidi watatimuliwa katika uchaguzi ujao. Hivi sasa hofu hiyo haipo, na ndiyo maana mambo hayaendi.
Mkuu wa nchi anayesema kwamba katika kipindi chote cha miaka kumi aliyokuwa madarakani “alisahau kilimo”, ni kielelezo cha tatizo ninalolijadili hapa. Mkuu wa nchi “anaposahau kilimo” ina maana kwamba anasahau kuwaelekeza wakuu wa wilaya wasimamie kilimo, na wao pia “wanasahau kilimo.”
Kwa sababu mwenye mamlaka ya kuwaadhibu ndiye yule yule aliyesahau kilimo kitaifa, wakuu wa wilaya waliosahau kilimo hawana la kuhofu; ajira zao zi salama.
Lakini atakuwa ni mkuu wa wilaya mwendawazimu au asiyetaka kazi atakayesahau kilimo wakati kachaguliwa na jamii ya wakulima na anajua kwamba muhula wake unapoisha inabidi arudi kwa wananchi wake kuomba wamchague tena.
Isitoshe, kila jamii ina shughuli zake. Katika maeneo ya wafugaji hakuna mkuu wa wilaya aliyechaguliwa na watu atathubutu ‘kusahau’ ufugaji. Hali kadhalika katika jamii ya wavuvi na shughuli nyingine za maendeleo.
Hatuna budi kujiuliza maswali muhimu na tujipe uhuru wa kusaili kila kitu kwani hakuna kisichosailika:
Hivi, kama ni haki kwa Watanzania kumchagua mkuu wa nchi yao, ni kwa nini hawana haki ya kuchagua mkuu wa wilaya yao?
Je, si kweli kwamba mwana wa eneo fulani, aliyekulia katika mazingira ya eneo hilo, ana ujuzi mkubwa zaidi, na uchungu mkubwa zaidi kuhusu eneo lake hilo kuliko mtu anayeletwa kutoka Magogoni?
Hivi, wote hawa wanaobanana na kupigana vikumbo Dar es Salaam na Dodoma wasingetulia katika wilaya zao na wakaridhika na udiwani na madaraka ya serikali za mitaa na kupunguza misongamano isiyokuwa na maana?
Je, hatuwezi kupata ‘fomula’ ya kugawana mapato kati ya serikali kuu na serikali za wilaya ili kila mmoja apate haki yake, na walio wanyonge wapigwe jeki?
Hivi, (kwa sababu imesemwa mara nyingi) tunaamini kwamba kuwanyima wananchi haki ya kuchagua watawala wao ndiyo njia mwafaka ya kuzuia ‘ukabila’?
Je, mfumo uliodumu kwa nusu karne bila kuzaa matunda tunaamini utakuwa na tija kubwa zaidi katika nusu karne ijayo? Au hatujagundua kwamba hauzai?
Itaendelea
