Pamoja na kuwakamua wananchi wa daraja la tatu kiasi hicho, uchumi wa nchi ulizidi kudidimia; sababu kubwa ikiwa ni matumizi mabaya, makubwa na ya anasa ya ikulu pamoja na ya jeshi yaliyochukua robo ya bajeti ya taifa, kwa upande wa jeshi pia bila kutaja ununuzi wa vifaa na ukarabati wa majengo na miundo mbinu usiozidingatia gharama halisi.
Nayo riba kwa mikopo ya zamani ilichukua zaidi ya asilimia 50 ya Bajeti ya Serikali mwaka 1788 pekee. Serikali ya Ufaransa, kama ilivyokuwa Serikali yetu miaka ya karibuni, ilikuwa haikopesheki.
Hatua ya serikali ya kuongeza idadi ya kodi kwa walala hoi, badala ya kusaidia uchumi wa nchi, ilizua malalmiko na kuchochea hasira ya wakulima na wananchi wa tabaka la chini na wasomi.
Katika kipindi hiki, nafasi na ushawishi wa waandishi na wasomi waliojitambua na tabaka la wanyonge, kama walivyo akina Jenerali Ulimwengu, Ndimara Tegabwage, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Shivji na wengine hapa kwetu, katika kuchochea mabadiliko haikuwa ndogo wala kudharaulika.
Francois – Marie Arouet, maarufu kwa jina la “Voltaire” (1694 – 1788), aliandika kushambulia ukiritimba wa Kanisa kwa kushikilia ukale na kwa kuhodhi ardhi na utawala wa msonge kwa mateso ya wanyonge .
Baron Montesquie (1689 – 1755) alishambulia madaraka makubwa ya watawala. Katika kitabu chake “The Spirit of the Laws”, alitaka kuona mipaka ya utendaji kwa njia ya mgawanyo wa madaraka, kati ya Watawala, Bunge na Mahakama.
Naye Jean Jacques Rousseu (1712 – 1778), katika Kitabu chake “The Social Contract”, alisisitiza kwamba, watawala wanashika madaraka kwa ridhaa (matakwa) ya wananchi, chini ya mkataba maalum wa kutawala; na kwamba, mtawala anayekiuka mkataba huo hupoteza ridhaa hiyo na anapaswa kuondolewa mara moja; na hata kwa matumizi ya nguvu ya umma, kama hatataka kuachia ngazi kwa hiari.
Kero za wananchi zingeweza kutatuliwa ndani ya Bunge huru na makini; lakini kwa mfumo wa utawala wa wakati huo, ambapo Bunge lilikuwa kama chombo au taasisi ya Serikali, na kwamba lilikuwa halijakutana tangu mwaka 1614, nafasi hiyo ilipotea.
Ni sawa na hapa kwetu hivi leo, kwamba Bunge letu lipo kutetea maslahi ya vyama vya siasa na wanasiasa, kiasi kwamba kazi pekee iliyobaki ni kuendeleza harakati za (Chama na Watawala) kubakia au kuingia madarakani, badala ya kutoa ufumbuzi wa matatizo ya wananchi. Kwamba madaraka sasa ni jambo la kufa na kupona; na wanapoyapata, wanataka kutumikiwa badala ya kutumikia, kama alivyokuwa Mfalme Louis wa XVI na serikali yake.
Inapokuwa hivyo, chama tawala na serikali hujiweka mbali na wananchi kutokana na ama kukosa muda wa kuchanganyika nao ili kupanga mipango ya maendeleo kwa pamoja kwa njia shirikishi; au kutokana na kutekwa nyara na tabaka la wenye nguvu ya fedha katika siasa, na wenye mawazo yasiyoshabihiana na matarajio ya wananchi walio wengi.
Hapo, viongozi huanza kuogopa changamoto kutoka kwa umma, kiasi cha kuwaita wanaohoji “wakorofi”, “wahuni” au “wehu”; na hivyo hali huzidi kuwa tete zaidi, pasipo ushauri wa kutatua kero, wala maono kwa kugubikwa na uchu wa madaraka, majigambo na majivuno.
Kadri hali ilivyozidi kuwa tete kwa Mfalme Louis, hatimaye Bunge la Wawakilishi liliitishwa, Mei 1789 mjini Versailles; likijumuisha Wabunge 308 wa Tabaka la kwanza, (the Clergy), Wabunge 285 wawakilishi wa tabaka la Pili, na wabunge 621 wa tabaka la walala hoi.
Uliwasilishwa muswada bungeni, kutaka kuongeza kodi mpya ambazo zingewagusa pia viongozi wa tabaka mbili za kwanza, kwa madhumuni ya kuongeza pato la serikali ili iweze kukopesheka kwa wadai wa nje.
Muswada huu uliotokana na pendekezo la Waziri wa Fedha, Lomenie De Brien, ulifurahiwa na wabunge wa tabaka la walala hoi; lakini ulipingwa vikali na wabunge wa tabaka mbili za juu kiasi kwamba mkutano wa Bunge ulivunjika bila maelewano.
Kufuatia hali hiyo, wabunge hao wa makabwela walikusanyika kwenye kiwanja cha mpira (tennis court), na kujitangaza kama Bunge halali la Taifa, lenye kauli ya mwisho katika utawala wa nchi. Kwa maana nyingine ni kwamba, Bunge lilichukua nafasi yake halali ya kuwa juu ya Serikali kwa kusimamia shughuli zote za Serikali.
Mfalme Louis, kwa ushauri wa mkewe, Marie Antoinette, aliita jeshi kuvunja kusanyiko la Wabunge hao, lakini alishangaa na kufadhaika askari wake walipotupa silaha na kujiunga na Wabunge hao, na hata kuongoza maandamano mjini kupinga Serikali madarakani.
Kwa siku mbili mfululizo, maandamano ya wanyonge yalitikisa mitaa ya Jiji la Paris na kusambaa hadi vijijini; magereza yalivunjwa na wafungwa kufunguliwa; serikali ya Louis haikuwa na nguvu tena mbele ya walala hoi hao na hivyo ikawa imepinduliwa, Oktoba 1789.
Ndipo Wabunge hao walipotangaza Azimio juu ya Haki za Binadamu na za raia, na kuweka misingi ya Serikali inayokubalika, hususan, juu ya usawa wa binadamu na uhuru wa kumiliki mali, haki ya kulindwa na serikali na ya kutonyanyaswa.
Haki nyingine zilizotangazwa na Wabunge hao ni haki ya kushiriki katika kutunga sheria za nchi moja kwa moja au kwa njia ya uwakilishi kupitia wabunge; utawala wa sheria, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kujieleza. Kufuatia Mapinduzi hayo, Louis na mkewe walijaribu kutoroka nchini, lakini walikamatwa mpakani na kurejeshwa Paris, wakanyongwa kwa kosa la uhaini.
Hatimaye, Septemba 1791, Katiba ya nchi iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wapenda demokrasia wote ilizaliwa, ikibainisha haki asilia za binadamu na za raia, mgawanyo wa madaraka kati ya utawala, bunge na mahakama.
Kwa kuzingatia hali yetu ya kisiasa nchini, tuna mengi ya kujifunza kutokana na mapinduzi ya Ufaransa ya mwaka 1789.
La kwanza “kwamba, kile kinachoanza kama kero za kweli na za kawaida kwa umma; zikaungwa mkono kwa hoja za wabunge makini, wasomi na maoni ya waandishi, lakini zikiachwa bila kushughulikiwa, au kuonekana kama mawazo ya wahuni na wehu, kwa lugha ya Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba; hatimaye huzaa machafuko yanayoweza kusababisha mapinduzi. Serikali makini haiwezi, wala haipashwi kupuuza kero za wananchi kwa kujivika tabia ya mbuni; labda kama serikali hiyo ni ya wehu na wahuni; au ile iliyowekwa mfukoni na Mibaka – Uchumi. Je, haikusemwa kwamba ukidharau mwiba mguu huota tende?
Pili ni kwamba, Bunge ndilo taasisi pekee inayowakilisha matakwa ya wanyonge, na ni ishara ya nguvu ya umma.
Kiongozi anayepingana na Bunge anapingana na nguvu ya umma, na hivyo atarajie matata daima – kwa sababu atakuwa anapingana na wananchi ambao ndio waliompa mkataba wa kuongoza au kutawala.
Na hapa lazima niseme kidogo: Bunge letu, kwa sehemu kubwa ni la wabunge watoto wa wakulima na wafanyakazi, si la wafanyabiashara na matajiri (wachache) waliovamia na kuteka siasa nchini.
Na kwa sababu hii, wabunge wanapaswa kujitambulisha na umma wa Kitanzania (kama walivyofanya wenzao 621 wa Ufaransa mwaka 1789), badala ya kukubali kuendeshwa na wabunge wachache wa tabaka la kimamluki, aina ya lile la tabaka la kwanza na la pili nchini Ufaransa ya kale.
Kwa mbunge kutetea ufisadi na mafisadi, au sera za uchumi zinazomdidimiza mwananchi wa kawaida, ni kujitambua na tabaka la kimamluki bungeni.
Kwa kufanya hivyo haisaidii serikali, rais wa nchi wala chama chake; badala yake anawachonganisha na wananchi, ili nchi iyumbe, na mwisho isambaratike au kuparanganyika!
Tatu, ni kwamba, kunapotokea mtafaruku wa kijamii kama ule wa Ufaransa ya kale; na hasa inapoonekana mawazo kinzani yanaanza kuchipuka hima na kwa nguvu kwa misingi ya kitabaka, mithili ya magugu katika shamba lenye rutuba lililotelekezwa, kama inavyotokea sasa hapa nchini, ni heri viongozi, Bunge na Rais mwenyewe wasimame upande wa wanyonge, badala ya kujitambulisha na tabaka la wachache wenye nguvu; vinginevyo, hawatakwepa kufagiliwa na mafuriko ya ghadhabu ya umma.

Simu:
0713-526972
Barua-pepe: