Leo naomba nirejee katika makala niliyowahi kuandika yenye kichwa cha habari: "Suala la Ngassa limedhihirisha ushamba wetu katika soka ya kulipwa" iliyochapishwa kwenye gazeti hili toleo namba 068 la Februari 11-Februari 17,2009.
Nikimzungumzia Mrisho Ngassa wa Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, niliandika: "...kwa sasa kijana huyo ni mchezaji wa kipekee mno nchini. Umpende au umchukie, ukweli utabaki kama ulivyo kwamba Mrisho Ngassa ana vitu vingi vya kumfanya awe juu ya wachezaji wengi, Watanzania na wageni,wanaocheza soka kwenye ligi zetu za Tanzania."

Mrisho Ngassa
Nukuu yangu ya makala hiyo inaendelea ifuatavyo: "Hata hivyo, licha ya kiwango chake kikubwa na mchango wake mkubwa wa mafanikio ya timu anazochezea mchezaji huyo, kwa mshangao wa wengi, hajawahi hadi sasa kushinda tuzo mojawapo ya mchezaji bora wa mwezi, jambo ambalo halionekani kumkera bali siku zote anaendelea kupigana kwa nguvu zake zote uwanjani, zaidi, kwa mafanikio ya timu na wala si kwa sifa binafsi."
Namalizia nukuu hiyo ifuatavyo: "Kwa maneno mengine, ushindi wa timu yake ni jambo kubwa kuliko sifa za kuwa mfungaji hodari na mchezaji bora wa mwezi.
“Hajali sifa ya ufungaji zaidi ya ushindi wa timu yake ingawa mara nyingi anakuwa katika nafasi za kumuwezesha kufunga mwenyewe mipira anayohangaika nayo tangu mbali ya goli la wapinzani. Matukio ya namna hiyo yamekuwa mengi kwake..." Huu ndiyo mwisho wa nukuu yangu ya makala yangu iliyochapishwa gazetini humu mwaka mmoja uliopita kasoro siku nane.
Sababu kubwa ya kufanya nukuu hiyo ni kuepuka kurudiarudia kama kitu kipya kitu kilichoongelewa tayari na gazeti hili hili kuhusu suala linalomhusu mtu yule yule.
Nimefanya nukuu hii katika kushangaa imekuwaje TASWA wasimpe Mrisho Ngassa haki aliyostahili ya kuwa mwanamichezo bora wa Tanzania wa Desemba 2009?
Atakayesema mchezaji huyo hakustahili tuzo hiyo kwa mwezi huo lazima atakuwa anachuki binafsi kwake au haipendi klabu yake ya Yanga ama yule aliyeshinda tuzo hiyo kwa mwezi huo ana marafiki, ndugu na jamaa zake.
Nje ya hapo, hakuna mtenda haki atakayesema kwa dhati kabisa kwamba Ngassa hakustahili uanamichezo bora kwa Desemba 2009.
Chama cha Waandishi wa habari za Michezo (TASWA) hakika wanatuangusha katika hili la uteuzi wa wanamichezo bora wa mwezi.
Shaka yangu ni kwamba kitu kinachotokea ni hiki: Waandishi wa michezo ambao wanaongozwa na ushabiki wakati wa uteuzi huwa wanajisemea hivi: “Hata kama Mussa Hassan Mgosi ameteuliwa kuwa mmoja wa wachezaji wa CHAN wa Afrika, sisi mashabiki wa Yanga ndani ya TASWA tutahakikisha hapati tuzo ya uchezaji bora wa mwezi husika kwa sababu ni mchezaji wa Simba!
“Hata kama mwezi Desemba 2009 Ngassa kafanya makubwa kwenye michuano ya Chalenji na Tusker, sisi mashabiki wa Simba ndani ya TASWA lazima tumpe uanamichezo bora wa mwezi huo mtunisha misuli kwa sababu Ngassa ni mchezaji wa Yanga!”
Katika hali hiyo ni lazima kura zisitoshe kwa mchezaji wa Yanga au Simba aliyestahili uanamichezo bora kwa mwezi husika.
Hii si ajabu kwa sababu miongoni mwa wanachama wa TASWA ni hawa hawa wanaoingia uwanja wa Taifa kuandika mechi ya Yanga na Simba wakiwa wametinga jezi za timu wanazoshabikia, Yanga au Simba, huku wakizishangilia timu zao kuliko hata baadhi ya mashabiki wasio waandishi wa habari, wasiokuwa na majukumu ya uandishi wa mechi hizo!
Baadhi ya wanachama hao wa TASWA ni hao hao wanaoandika leo makala kali ya kulaani kitendo fulani cha mchezaji wa timu pinzani, Yanga au Simba, na kushauri aadhibiwe vikali lakini kesho wataandika makala kali yenye utetezi wa nguvu wa mchezaji wa klabu yao, Yanga au Simba aliyetenda tendo lile lile huku wakitafuta mtu wa kumbebesha lawama za mchezaji huyo kusababishwa atende tendo hilo!
Hapa, naomba nichekeshe kidogo. Kufuatia makala niliyoandika yenye kichwa cha habari "Kwa nini Haruna Moshi anaogopwa hivi?" (Raia Mwema, Desemba 30,2009-Januari 5,2010) kuna mwandishi mmoja kijana ambaye navutiwa sana na hoja zake za uchambuzi alinitaka niache kazi ya uandishi na nitafute kazi nyingine kwani siiwezi kazi hiyo.
Lakini mwandishi mwingine kijana pia ninayemkubali sana pia kwa kazi yake nzuri akinitaka nikaze uzi kwa kuzungumza vitu kwa uwazi bila uoga na kunitaja kuwa mmoja wa waandishi wazuri wa makala za michezo nchini wa nyakati hizi!
Kichekesho ni kwamba, niache uchambuzi wa michezo gazetini kwa sababu siiwezi kazi hii, au nikaze uzi kwa sababu naiweza sana kazi hii?!
Ni wazi yule wa kwanza ni Yanga na wa pili ni Simba, na wote wanaweza kuwa wanachama wa TASWA! Inasikitisha kwamba hata waandishi walihusisha hoja zangu kuhusu Boban kwenye makala hiyo na Uyanga na Usimba kama walivyofanya mashabiki wengi wengine wa klabu hizo waliowasiliana nami kuhusu makala hiyo.
TASWA inapaswa ijue kuwa mwanamichezo bora wa kipindi fulani hujulikana wazi na kinachosubiriwa ni yeye kutangazwa tu. Dunia nzima ilijua kuwa Cristiano Ronaldo wa Manchester United wakati huo (sasa yuko Real Madrid) alistahili uchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2008 kabla hajatangazwa na wala haikushangaza alipotangazwa kuwa hivyo.
Watu walikuwa wakimtaja Lionel Messi wa Barca (tamka Basa) kuwa mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2009 kabla hajatangazwa na kweli ikawa hivyo. Watanzania pia tulijua wazi kuwa Desemba 2009, Ngassa alikuwa mfungaji bora wa mashindano ya Chalenji ya Afrika Mashariki na ya Kati.
Tuliziona pia pasi nyingi za mabao alizotoa kwenye mashindano hayo. Kwa ujumla tuliuona mchango wake mkubwa kwa timu yake hata kama ilikosa hata ushindi wa tatu.
Tukauona tena mchango wake wa kufunga mabao na kutoa pasi za mabao ulioiwezesha Yanga ya Tanzania kuleta taji pekee nchini mwetu kwa mwaka 2009 ambalo ni la Tusker.
Pamoja na yote hayo, TASWA imeona kuwa mtunisha misuli, David Nyombo amefanya makubwa Desemba kwa kuwa mtunisha misuli bora katika mashindano ya kutunisha misuli yaliyofanyika Mauritius.
Hapana, huu ni usanii wa hali ya juu uliokusudiwa kumnyima Ngassa haki yake. Inakuwaje kwa mwezi mzima mtu awe bora kwa tukio bora moja tu zaidi ya yule aliyefanya matukio mengi bora ndani ya mwezi huo mzima?
Wakati wanachama wa TASWA wakitueleza kuhusu mambo makubwa ya Ngassa kupitia habari zao ndani ya mwezi mzima wa Desemba 2009, mbona hawakutueleza lolote kuhusu mtunisha misuli wetu Nyombo ndani ya mwezi huo, kuonyesha kwamba alichofanya si habari kubwa ikilinganishwa na habari kubwa ya aliyoyafanya Ngassa?
Kama utaratibu ni huu wa kutafuta michezo ambayo ni ya kisanii na kuishindanisha na michezo halisi, kwa nini mwezi wa kushinda uchezaji bora Salum Kanoni wa Simba, mashabiki wa Yanga waliomo ndani ya TASWA wasimpe Mtanzania mcheza drafti au bao atakayeshinda mchezo huo Kenya au Rwanda?
Kwa mtazamo wangu, kutunisha misuli, zaidi ni sanaa na si mchezo ambapo mchezo wake unaostahili kushindanishwa kama mchezo ni kunyanyua vitu vizito.
Kutunisha misuli kwa wanaume hakuna tofauti na mashindano ya urembo kwa wanawake na ndiyo maana Miss Tanzania ni mrembo kama Miriam Gerald wakati Mr Tanzania ni mtunisha misuli kama anavyoweza kuwa David Nyombo.
Kwa mantiki hiyo, kuna siku tutakuwa na mwanamichezo bora wa mwezi Miss Tanzania akifanya mambo makubwa huko nje kama aliyoyafanya Nancy Sumari mwaka 2005!
Naomba niishauri TASWA kuwa kwa sababu vipindi vya uchezaji bora, kama huu alioupata Nyombo mwezi Desemba 2009, ni vya mwezi mwezi, itakuwa sahihi akiangaliwa mwanamichezo wa mchezo wowote ule (siyo msanii) aliyefanya vizuri mchezoni ndani ya mwezi huo badala ya kuimarisha utaratibu unaojengeka sasa wa kuangalia tu mwanamichezo huyo ameleta sifa gani kwa taifa kwa mwezi huo.
Mtazamo huu wa mchango wa mafanikio ya taifa au timu, kwa wale wenye michezo ya kitimu na kwa taifa, kwa wale wenye michezo isiyo ya kitimu, unapaswa uwe tu kwenye uchaguzi wa mwanamichezo bora wa mwaka ambapo mafanikio ya timu yake na/au ya taifa zima, yataonekana kwa mwaka mzima unaofaa kwa kufanyia tathmini hiyo kamili.
Pamoja na baadhi ya watu kukerwa na niliyoyaeleza hapa, ukweli unabaki palepale kwamba Mrisho Ngassa amedhulumiwa haki yake ya kuwa mwanamichezo bora wa mwezi Desemba 2009.
Baada ya dosari hiyo, nashauri TASWA ipitie upya utaratibu wake wa kupata wanamichezo bora wa mwezi. Vinginevyo, Uyanga na Usimba ndani yake utavuruga utaratibu huu mzuri sana unaohamasisha wanamichezo kujituma.

Simu:
0713 297085
Barua-pepe: