MWENYE akili timamu halazimiki kuchagua ni upande gani aushabikie katika malumbano baina ya Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party, Augustine Mrema na Spika wa Bunge, Samwel Sitta. Hapa hatupambani na suala la ushabiki, bali kinachojitokeza ni suala la mantiki inayompa taabu Bwana Mrema.
Mrema hakuanza na Sitta katika jukumu jipya alilojivisha la kutetea “usalama wa taifa.” Amesema kwa sauti kubwa, nasi tumemsikia, kwamba wale wanaomkosoa Rais Jakaya Kikwete katika utendaji kazi wake wanahatarisha “usalama wa taifa,” na kwamba yeye yuko tayari “kumtetea” Rais Kikwete kwa nguvu zake zote.
Hili la pili la yeye kuwa tayari “kumtetea” Kikwete ni haki yake bila shaka, kwani hiyo ni haki ya kila mtu. Lakini lile la kujaribu kuwafananisha wanaomkosoa Rais Kikwete na wahaini ni jambo la kuzua, jambo la ki-Mremamrema ambalo halina budi kutazamwa kama kumtuma nyau kumtishia mtu mzima.
Nyau huyu anatumwa kuwasuta wanasiasa wakongwe wanaotumikia Taasisi ya Mwalimu Nyerere, MNF, ambao siku chache kabla Mrema hajazua yake walikuwa wamenukuliwa wakibainisha kutoridhishwa kwao na utendaji kazi wa Rais Kikwete.
Hili si jambo jipya, kwani tumeshuhudia watu wengi wakisema maneno kama hayo hayo katika mijadala magazetini, redioni, kwenye luninga na makongamano, kama vile ambavyo tumewasikia wanaomsifia Kikwete katika magazeti, makongamano na matokeo ya tafiti.
Wanaomkosoa Kikwete na wanaomuunga mkono wote wanayo haki ya kufanya hivyo alimradi hawavunji sheria. Kwa Mrema kudai kwamba kumkosoa Rais ni kuhatarisha “usalama wa taifa” anakwenda mbali mno, na hilo ndilo linamfanya aonekane kama yule “nyau” wetu wa kumtishia mtu mzima.
Wakuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere anaowasema Mrema ni wakubwa sana kisiasa kwake Mrema, ni watu wenye historia iliyotukuka katika utumishi wa umma kuliko yeye, tukiacha ile ajali iliyomkumba Mzee Ali Hassan Mwinyi ya kumfanya Mrema kuukwaa uwaziri na unaibu waziri mkuu, kiasi kwamba neno “kukwaa” likapata maana yake halisi. Mrema kusema wazee hawa wanayumbisha “usalama wa taifa” kwa kumkosoa Rais ni kusahau historia yake yeye mwenyewe.
Akiwa kiongozi wa NCCR-Mageuzi, chama chake kiliwahi kumtuhumu rais aliyekuwa madarkanai wakati huo kwamba alipokea rushwa ya shilingi 900,000,000 (milioni mia tisa) zilizoingizwa kwenye akaunti maalumu mjini Geneva. Kwa Mrema hilo halikuwa tamko la kuhatarisha “usalama wa taifa” ila hili la akina Butiku, Salim, Mangula na Sitta.
Wale wenye kumbukumbu ndefu kidogo kuliko ya “nyau’ watakumbuka matamko mengine mengi ya Mrema yaliyowakashifu wakuu wa dola wakati akisaka ama urais, mwaka 1995 au ubunge wa Temeke, mwaka 1996, ikiwa ni pamoja na kuvishutumu vyombo vya usalama wa taifa kwa kutomtendea haki.
Inaelekea anaijutia kazi yake ya zamani kama ‘shu shu shu’, na kama ni hivyo angeomba arudishwe kazini, labda kama ‘consultant’ kwani umri nao umekwenda.
Lakini asiruhusiwe kuendelea na mchezo huu wa nyau kwa sababu tunazo kumbukumbu za mtu huyu. Anapowaambia akina Sitta waondoke CCM wajiunge na Upinzani, eti kwa sababu wanapinga chama chao papo hapo anashindwa kuona mantiki ya yeye kujiunga na CCM kwa sababu anaipigia debe?
Mrema anasema “Sijanunuliwa.” Inawezekana ikawa kweli, lakini ni dhahiri kuna kitu anauza.
