MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP) Augustine Mrema ambaye wiki hii amemwandikia Spika Samuel Spika kusudio la kumshitaki, ameiambia Raia Mwema kwamba anatamani angelipwa mafao ya nafasi yake ya zamani ya naibu waziri mkuu.
Kiongozi huyo wa TLP ameteka vichwa vya habari vya magazeti mengi katika siku za karibuni baada ya kuonekana amekuwa mkereketwa zaidi wa chama tawala cha CCM kuliko waliomo ndani ya chama hicho.
Katika matukio kadhaa amejitokeza kukemea kwa nguvu zake zote wale wanaoibeza Serikali ya sasa ya awamu ya nne ya CCM inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kikubwa kinachowashangaza watu wanaoamini kwamba ameingia kwenye mkondo wa siasa usiokuwa wa kwake ni jinsi anavyoooneysha ukali kwa wale wanaombeza Kikwete ambaye pia ndiye mwenyekiti wa CCM.
Juhudi zake za kukemea anayoyaona kuwa ni maovu katika CCM zimemfanya sasa agombane waziwazi na Spika wa Bunge, Sitta.
Baada ya kulumbana naye kwa maneno, jana Jumanne Mrema alitangaza kwamba amemtumia barua ya kusudio lake la kumfungulia kesi ya madai kwenye Mahakama Kuu kama pamoja na mambo mengine hatamlipa Sh. bilioni moja kama fidia kwa ‘kumkasifu’ kwenye magazeti.
Wengi wanajiuliza kulikoni? Mrema ‘amekomunika’ lini kuwa mshauri mzuri wa CCM ili isisarambatike? Ana maslahi gani na Kikwete kiasi cha kuwa mkali anapoguswa?
Wapo wanaoamini kwamba kiongozi huyo wa TLP ambaye kwa mara ya kwanza tangu aingie katika Upinzani hatagombea Urais, ana ajenda ya siri na Kikwete.
Pamoja na mambo mengine wanaamini ya kuwa anajenga mazingira ya kuonewa huruma na Kikwete amlipe fidia ya unaibu waziri mkuu, cheo alichopata kuwa nacho chini ya Serikali ya awamu ya pili ya CCM iliyoongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi lakini ambacho kikatiba hakitambuliki.
Jana Jumanne Raia Mwema ilifanya mazungumzo na Mrema kuhusu mambo yanayosemwa juu yake na alipoulizwa juu ya suala hilo la fidia ya unaibu waziri mkuu, alisema bila kuficha kwamba anaamini anastahili kulipwa.

Augustine Mrema
Hata hivyo, alisema mambo anayoyafanya sasa ya kumkingia kifua Kikwete hayana uhusiano na azma yake ya kutaka kulipwa.
“Akinipa nitashukuru kwa sababu Maalim Seif (aliyekuwa waziri kiongozi wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad ), alipewa haki zake pamoja na kwamba aliwahi kushitakiwa kwa uhaini.
“Mimi nastahili kulipwa kwa sababu sijawahi kushitakiwa kwa uhaini. Nikiwa mtumishi wa umma sikuwahi kuhusishwa na rushwa wala ufisadi wa aina yoyote. Nilikosa tu msaada wa kupambana na maovu hayo ndiyo maana nikatoka (serikalini),” alisema.
Pilipili asiyoila inamuwashia nini? Kwa nini anaingilia masuala ya CCM na Serikali yake kiasi cha sasa kuwa karibuni kupelekana mahakamani na Spika Sitta?
Kujibu swali hilo, Mrema anasema kwamba anaingilia kati kuzungumzia masuala yale anayoyaona kwamba yanahatarisha usalama wa taifa.
“Kumbuka mimi ni trained officer wa usalama wa taifa, najua kulinda dola. Siwezi kunyamaza kwa vile tu ni Mwenyekiti wa TLP au niko upande wa Upinzani,” alisema Mrema jana Jumanne katika mahojiano na Raia Mwema .
Alisema huwa anaingilia kati kumkingia kifua Kikwete anapoona kwamba anashanbuliwa kama Rais wa nchi. Aliongeza Mrema: “Kikwete ni Rais wetu. Siwezi kumvumilia mtu anayeleta uchochezi dhidi yake.”
“Mtu anposema kwamba Kikwete amezungukwa na wezi ina maana gani? Si ina maana kwamba Kikwete mwenyewe ni mwizi? Huu ni uchochezi wa hali ya juu,” alisema.
Mrema anasema ya kuwa uchochezi wa aina hiyo na mambo kama hayo ndiyo uliofanya wananchi kuvamia Ikulu Madagascar na kumwondoa kiongozi wa nchi madarakani kwa fujo, kinyume cha sheria.
Alisema kwamba yeye hapingi mtu kuikosoa Serikali au kumkosoa Kikwete, bali afanye hivyo kwa utaratibu unaoeleweka na bila pia kutumia visingizio.
Alisema Mrema: “Watu kujificha katika kichaka fulani kusema, mambo ya uchochezi dhidi ya Rais ni vitu ambavyo siwezi kuvivumilia.”
Lakini pamoja na Mrema kujitetea hivyo, wapo wanaoamini ya kuwa anamzungumzia vizuri Kikwete kwa vile alimsaidia aende India kwa matibabu.
Tena inaelezwa kwamba alisaidiwa kupitia kwa ofisa mmoja wa Ikulu ambaye alimpatia Sh. milioni 40,000 zinazodaiwa zilitoka kwa mmoja wa wafanyabiashara wa Dar es Salaam marafiki wa chama tawala.
Mrema alikuwa mkali alipoulizwa hilo kwa kile alichosema kuwa ni uongo, uzandiki na unafiki wa hali ya juu.
Anasema ofisa huyo wa Ikulu ndiye anayepaswa kusema kama ni kweli alipewa pesa hizo na Kikwete au la.
‘Lakini mimi watu wananionaje? Wananiona lofaee…? Mbona nina pesa kwenye akaunti yangu milioni 37 ambazo zinapita zile za Waziri Mkuu Pinda (Mizengo) aliye na milioni 25?”, alihoji Mrema.
Kwa mujibu wa Mrema, amekuwa jasiri kueleza pesa alizonazo benki kwa sababu hakuzipata kwa njia ya kifisadi na anatumia pesa zake mwenyewe kufanya kila kitu ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto wake.
“Nimekuwa mbunge kwa miaka 10, nimekuwa ofisa usalama wa taifa, waziri, naibu waziri mkuu na kufanya kazi zangu kwa uadilifu mkubwa,” alisema.
Alisema kwa hali aliyonayo asingeshindwa kwenda India kwa matibabu hadi aombe nsaada wa Rais.
Katika barua yake kwa Sitta ya kukusudia kumshitaki, Mrema amesema amechukua uamuzi huo kutokana na spika huyo kumdhalilisha kupitia magazeti.
“Kwenye gazeti la Mwananchi la tarehe 5/3/2010 ulisema: ‘Mrema ni mhuni na amepitwa na wakati pia amefilisika kisiasa na kipesa anatafuta njia ya kujinasua katika hali hiyo,’
‘Pia kwenye gazeti hilo uliendelea kusema kwamba: Inawezekana huyu bwana anapata pesa ili kukipigia debe CCM.’
Mrema pia alimkumbusha Spika Sitta jinsi gazeti la Nipashe lilivyomnukuu kwamba: “Huyu Mrema ni mhuni katika siasa na ndio maana anapotosha ukweli wa umma, nadhani amechanganyikiwa.”
Mrema amedai katika barua hiyo kwamba kutokana na kauli zake hizo, amemmtukana, amemkashifu, amemvunjia heshima na amemdhalilisha mbele ya jamii akiwa mwenyekiti wa taifa wa TLP, chama cha nne kwa ukubwa nchini.
Amesema Spika Sitta amesababisha wanachama wa TLP wapatao laki tano nchini kote wakose imani naye.
“Pia kauli zako zimenivunjia heshima niliyoijenga na utumishi wangu uliotukuka, serikalini ambako nilifanya kazi kwa zaidi ya miaka 30 nikiwa kama Ofisa Usalama wa Taifa mbunge, waziri na baadaye Naibu Waziri Mkuu.
Mrema amsema pia kwamba kauli za Sitta zimemuathiri kwa sababu amekwisha kujitangaza kwamba atagombea ubunge wa Jimbo la Vunjo.
