WIKI iliyopita nilitembelea Ghana. Nikaeleza jinsi matarajio yangu ya nchi iliyokuwa ya kwanza katika Afrika ya ukweli kupata uhuru yalivyonyimwa visa. Matarajio yangu ya kuona nchi tajiri iliyopata uhuru mapema imepiga hatua kubwa zaidi kudhihirisha kwamba Waafrika wanaweza, hayakukaribishwa kwa furaha.
Lakini nitakuwa mtovu wa udadisi kama nikishindwa kutambua pia historia ya Ghana iliyokuwa imejaa mapinduzi ya kijeshi tokea miaka ya kwanza kabisa ya uhuru.
Na nitajishangaa mwenyewe endapo sitatambua ukweli kwamba katika Afrika kuwa na raslimali nyingi si kigezo cha kupata maendeleo. Wakati mwingine raslimali huwa chambo cha kuvuta wavurugaji wa amani na walafi wa kimataifa ambao hutaka kukomba kila kitu.
Pamoja na kuelezea masikitiko yangu kuhusu nchi ile, bado yapo mambo niliyoyaona kule ambayo ni muhimu kwetu kujifunza. Nilivyofuatilia yaliyomo katika vyombo vya habari nilibaini kuwa kulikuwa na mwamko zaidi miongoni mwa wananchi wa nchi ile kuhusu Uafrika wao huenda kuliko ilivyo hapa kwetu.
Nilifuatilia majina yao, mavazi yao, masuala wanayoyajadili na vitu wanavyojivunia, nikabaini kwamba kumbe pamoja na kwamba wako nyuma kimiundombinu na haya mashkolo mageni ya kuremba miji, Waghana wako katika njia bora zaidi ya kuwapeleka katika maendeleo kuliko tunavyoweza kuhitimisha.
Na kwa kuthibitisha hilo, Waghana wameweza kujipambanua katika utengenezaji wa nguo za Kiafrika kama bazee na wanashona mashati na nguo zingine kwa ubora wa kimataifa.
Kumekuwa na Watanzania wengi tu ambao husafiri kwenda Ghana ambako hununua mashati na kuyauza katika maduka ya Tanzania.
Japokuwa kuna wakati Wachina walijaribu kuyaiga, wakayatengeneza na kuyamwaga kwa wingi sokoni, bado ubora na upekee wa mashati ya Ghana umezidi kumiliki soko.
Kwa muhtasari tu ni kwamba madhali Waghana wanajitambua na wanafikiria kuzalisha vitu vyao – hata vya asili – kwa ubora na viwango vya kimataifa, upo uwezekano mkubwa sana wa wao kupiga hatua muhimu kimaendeleo.
Kuanzia wiki hii nitajaribu kuelekeza udadisi wangu katika umuhimu wa uchaguzi tunaotarajia kuwa nao mwaka huu. Nitafanya hivyo kutokana na ukweli kwamba bado, kama taifa, tunalo tatizo la kufanya mambo kwa mazoea.
Kwamba kwa bahati mbaya, upo ushahidi wa kutosha kwamba tumekuwa tukifanya mambo kwa mazoea na baada ya hapo sisi wale wale tunakaa chini na kuanza kulalamika kuhusu ugumu wa maisha.
Na kama ambavyo amekuwa akisema Jenerali Ulimwengu, ni dhahiri kwamba kufanya jambo lile lile, kwa njia ile ile, na kutarajia matokeo tofauti, ni ujuha.
Kwamba ni kwa vipi tunapata fursa ya kupiga kura kuchagua viongozi tunaowaona wanatufaa lakini wakatokea wagombea hadaa wakatuhonga fulana, kofia, kanga, pombe na pilau tukalewa na kuwachagua; halafu kesho yake wasipofika kutusikiliza matatizo yetu tunalalama? Au pale wanapoanza kuwakilisha familia zao bungeni tunalalama! Au pale wanapoanza kuwawakilisha waliowapa hela walizotuhonga kushinda uchaguzi tunalalamika!
Niliwahi kusoma na mwanafunzi kutoka nchi moja ya Afrika Magharibi ambako hata sasa hawajui huyo kiongozi wao atatoka lini madarakani. Yeye anajiita vyeo vyote muhimu duniani. Ana vyeo vya kisomi, vya kidini, vya unajimu, vya kijeshi, vya kitamaduni na kadhalika.
Na nchi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili haijui uchaguzi huru una maana gani. Kiongozi wao aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi akiwa mvulana na sasa ni mtu mzima. Na madhali yeye mwenyewe ni mnajimu, anajua siku atakayokufa na huenda akatoka madarakani akiwa babu.
Lakini lipo jambo moja aliloniuliza yule bwana tuliyekuwa tukisoma wote kuhusu Tanzania. Akauliza: Huwa mnafanya uchaguzi kila mara. Nikamjibu; ndiyo. Akauliza: Huwa mnakuwa huru kuchagua viongozi mnaowataka? Nikajibu; ndiyo.
Akauliza tena: “What difference does it make in Africa?” Alimaanisha kwani kuwa na uhuru wa kuchagua viongozi mnaowataka Afrika inaleta tofauti gani na sisi tunaotawaliwa kijeshi na kibabe na bila uchaguzi kabisa?
Nilijibu tu haraka haraka kwamba sisi Tanzania tulikuwa na marais wastaafu wawili na aliyeko madarakani alikuwa amesema akimaliza tu anatoka kumwachia mwingine. Akaniuliza swali jingine: “Niliposema difference sikumaanisha kuwa na mlundikano wa marais wastaafu, nilimaanisha tofauti kati ya maisha ya mamilioni ya wananchi wenu na wale wa nchini kwetu.”
Na hilo ndilo suala ninalotaka kulidadisi katika safu hii katika siku za usoni nikiamini kwamba kwa miongo miwili sasa tumekuwa tukizungumzia demokrasia ya vyama vingi na tumekuwa tukifanya chaguzi kila baada ya miaka mitano.
Katika hilo la uchaguzi kila baada ya miaka mitano, hakuna shaka kwamba tumepiga hatua kubwa. Kwamba chaguzi zinafanyika kila baada ya miaka mitano katika namna inayoonekana kama huru vile!
Katika hilo, tumewazidi wananchi wa ile nchi aliyotoka rafiki yangu (japokuwa siku hizi nao wanaigiza kufanya uchaguzi ambao wanajua tayari mshindi) ambao huko nyuma walikuwa hawapati fursa ya kuchagua viongozi.
Lakini ni kiasi gani sisi wenyewe tumebadilika na kuwa waumini wa kweli wa misingi ya demokrasia, ni suala linalotetemeka kwa baridi ya masikitiko. Na kwamba ni kiasi gani chaguzi za kidemokrasia zimeongeza fursa za kuwaletea maendeleo wananchi wetu ni suala lililokwama katika foleni ya mashaka.
Je ni masuala gani muhimu na ya msingi ambayo tunapaswa kuanza kuyatazama na kuyajadili kutokana na umuhimu wake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu?
Je vyama vya siasa tulivyo navyo hadi sasa vimetuambia nini kuhusu yale vinayoyaamini? Je tukipima matendo ya wenye vyama hivi tunaridhika kwamba vimetekeleza kwa vitendo yale vinayoyaamini? Je mwaka 2005 vyama hivi vilituahidi nini na hadi sasa vimefanya nini?
Je wagombea wanatuambia nini kuhusu kinachowatuma kutafuta madaraka? Je rekodi zao zinatufundisha nini kuhusu ahadi zao? Je wagombea wanatumia hila (au mbinu) gani kutushawishi ili tuwaamini?
Je tunajua kwamba tukichagua leo itachukua miaka mitano mingine (endapo hakukutokea jambo katikati) kuwa na uchaguzi mkuu mwingine?
Inatupasa kuyajadili haya na masuala mengine yanayohusu demokrasia yetu. Wakati wa kufanya hivyo ni sasa.

Barua-pepe: