Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ni kati ya vyuo vikuu vichache katika ukanda huu chenye eneo kubwa na malengo makubwa ya kudahili wanafunzi wapatao 40,000. Mashirika kadhaa yanashiriki kujenga koleji mbalimbali za chuo hicho ukiwamo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi za Jamii (NSSF) ambao wiki iliyopita uliwaalika baadhi ya viongozi wa vyombo vya habari kushuhudia jinsi ujenzi huo unavyoendelea na hivi ndivyo Mwandishi Wetu alivyoshuhudia yaliyojitokeza.
KUNA uvumi Dodoma kwamba inawezekana alipotamka mwaka 2005 mjini humo kutajengwa chuo kikuu chenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 40,000, Rais Jakaya Kikwete, wakati huo akiwa mwishoni mwa kampeni zake, hakuwa na picha kamili ya dude linalojengwa sasa kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Uvumi huo unasema pia kwamba kwa sababu dude hilo linamshangaza kila mmoja kwa ukubwa wake, ndiyo maana karibu kila safari yake ya kuingia na kutoka Dodoma kwa ndege, Rais Kikwete huomba kwa rubani amwonyeshe uyoga wa majumba na mtapakao wa Udom.
Huu unaweza kuwa ni uvumi kweli. Lakini cha hakika ni kwamba hiki ni chuo kilichotapakaa katika umbali wa ekari takriban 12,000, kinajengwa na kusajili wanafunzi kwa kasi kubwa ambayo inakinzana dhahiri na umri wake wa miaka mitatu.

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)
Mifuko kadhaa ya hifadhi za jamii imegawana kujenga chuo hiki, wiki iliyopita moja ya mifuko hiyo, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) uliandaa safari ya baadhi ya wakuu wa vyombo vya habari kushuhudia ujenzi huo ambao unakwenda vizuri wa madarasa, mabweni na majengo mengine.
Anasema Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula kuhusu chuo chake: “Palikuwa na kejeli hapa. Mara chuo cha wanafunzi 40,000? Watatoka wapi? Wataajiriwa wapi? Mara ni chuo cha Waislam. Lakini sasa tuna wanafunzi 15,000. Hakuna hata senti ya kutoka nje iliyotumika kwa ujenzi, maana kulikuwa na uvumi hapa kwamba ni Bill Gates amemwaga pesa zake.”
Anaongeza: “Mimi ni Mwislam na najivunia hilo, babu na baba yangu na mama yangu ni Waislam, lakini hiki si chuo cha Waislam. Kwa saizi ya Dodoma kulikuwa na majungu kibao. Eti hawasomi Ijumaa (kwa sababu ya uislam). Mara tumekodisha mabasi, mara tunachukua fedha za mikopo ya wanafunzi tunaziweka kwenye akaunti maalumu zikiiva tunaweka riba mfukoni. Lakini hiki si chuo cha Mkapa (Benjamin, rais mstaafu) wala Kikwete, wala mimi, au Profesa Kinabo (msaidizi wake). Hiki ni chuo cha Watanzania wote,” anasema Profesa Kikula.
Kwake maneno yote haya ni changamoto lakini pengine changamoto kubwa anayoina yeye ni ya walimu. Anasema kwa idadi hiyo kubwa ya wanafunzi panatakiwa kuwa na walimu wa kutosha kwa idadi na ubora.
“Changamoto hapa ni walimu. Tunahitaji walimu wa juu ya wahadhari waandamizi. Hawa hawapo. Tumejiwekea mikakati ya kuwa na walimu wa muda, hawa wapo kama 50 na bado hawatoshi. Tumewapeleka vijana wapatao 115 tuliowaajiri nje, wakirejea hapa na shahada zao za pili watakuwa wahadhiri wasaidizi. Hawa watapanda polepole hadi kuwa wahadhiri waandamizi. Wengi tulianzia huko, mimi nina zaidi ya miaka 30, hawa ndio watakuwa nguzo yetu ya miaka ijayo.
“Lakini katika mkakati mwingine tunaajiri walimu kutoka nje. Tulipotangaza mara ya kwanza tulipata utitiri wa walimu, wengi kutoka Kenya. Tulipowasaili tulikutana na mambo mengi, wengine walikuwa na vyeti vya kughushi. Sasa tuna wengine kutoka India. Niwaambieni kwamba hatutaajiri Mhindi yeyote. Najua tunavyowafikiria Wahindi, lakini India wako makini sana katika masuala ya elimu ngazi hii. Tutapata walimu wengine kutoka Urusi, ambako pia utaratibu wa kupata mwalimu ni makini.
“Tutakuwa na koleji hapa ya sayansi ya afya. Tunataka tuwe na hosptali ya kujifunzia/kufundishia. Rais ametushauri tujaribu kuangalia madaktari kutoka Cuba. Mchakato huu uko mbioni,” anasema Profesa Kikula.
Kwa mujibu wa Profesa Kikula wakati NSSF inajenga koleji ya sayansi za jamii na sanaa kati ya koleji sita za chuo hicho, nyingine zinajengwa na mashirika mengine ya hifadhi za jamii nchini kama PSPF na PPF. Ukiacha koleji ya sayansi za jamii, koleji nyingine ambazo pia zina timu ya wakuu wake kama mkuu wa koleji, na wakuu wengine wa vitivo na wakurugenzi ni za elimu, mawasiliano (ict), sayansi za asili, sayansi za ardhi na afya.
Kuanza kwa Udom kumeuchangamsha mjini huo kwa kiasi kikubwa. Sasa Dodoma si ya miaka iliyopita. Idadi ya wanafunzi wapatao 15, 000 walipo sasa, kati yao wengi wakiwa wanasomea ualimu na walimu kunauchangamsha vilivyo uchumi wa Dodoma achilia mandhari ya mji.
“Maana ya chuo kama hiki ni kusomesha. Kwa hiyo tusiangalie hawa watakaohitimu hapa wataajiriwa wapi, bali kwamba machinga, au mkulima au mchuuzi aliyesoma ni bora kuliko asiyesoma. Sasa tuna miaka mitatu tangu tuanze. Mambo mengi hayajakaa sawa lakini tuna mawazo makubwa vichwani mwetu, ikiwa ni pamoja kukifanya chuo hiki kuwa sehemu ya utalii,” anasema Profesa Kikula.
Anaongeza: "Sisi wengine tunakaribia kustaafu. Kila siku tunaumiza vichwa juu ya jinsi gani tutakitunza na kukiwezesha chuo hiki. Tunawaza kuwa na kitu kama Mlimani City hapa; tumezungumza na Vodacom na Zain na tumekuwa tukitafuta mashirika ya kuweza kuendesha migahawa ya hapa. Tusingependa tukija hapa miaka kadhaa ijayo, tukute pameharibika. Jasho tulilowekeza hapa ni kubwa. Pakiharibika nitalia.”
NSSF inajenga majengo ya sayansi za jamii na sanaa ambayo yatakapokuwa yamekamilika yatachukua wanafunzi 20,000 kwa mara moja. Hayo ni mabweni, madarasa, majengo ya mihadhara, vyumba vya semina, maabara za lugha, maktaba, majengo ya utawala, ofisi za walimu, mabwalo ya chakula, zahanati yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 60 na viwanja vya kisasa vya michezo.
Msimamizi wa Mradi huu, Karim Mataka anasema gharama za usanifu wa majengo na usimamizi wa ujenzi ni shilingi 7, 585,751,601/60 na kwamba usanifu wa mejengo yote umekamilika.
Anasema kwamba kazi ya ujenzi iligawanywa katika awamu mbili, awamu ya kwanza nayo ikagawanywa katika sehemu mbili, ya kwanza ikihusisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi 5,000, kazi hiyo ikianza Oktoba 15, 2007 na kukamilika mwishoni mwa Septemba 2008 wanafunzi wakianza kutumia hosteli hiyo Septemba 27, 2008.
Anasema hadi Mei 2009 madarasa 24 yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 75 kila kimoja, kumbi kubwa mbili za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 365 kila mmoja, vyumba 24 vya semina vya kuchukua wanafunzi 52 kila kimoja, kumbi 18 ndogo, maabara za lugha za kubeba wanafunzi 252, mabwalo ya chakula kila moja lenye uwezo wa watu 1,200, zahanati yenye kulaza wagonjwa 60, maktaba yenye uwezo wa wanafunzi 3,000 na ofisi 186 za walimu vilikwisha kukamilika.
Kwa mujibu wa Mataka, ifikapo Desemba 2010, kazi ya ujenzi wa majengo yaliyobaki kama hosteli kwa ajili ya wanafunzi 15,000, majengo ya kufundishia, ofisi, maktaba, mabwalo ya chakula na viwanja vya michezo yatakuwa yamekamilika. Hadi mradi utakapokuwa umekamilika, kwa kazi ambazo zimo katika mkataba kati ya NSSF na Serikali, jumla ya shilingi 277, 269, 594, 577/28 zitakuwa zimetumika.
