KATIKA kuadhimisha miaka kumi ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na miaka 20 ya Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere alikubali kufanya mahojiano maalumu na mhariri wa gazeti la Uhuru. Huo ulikuwa ni mwaka 1987.
Katika mahojiano yale, Mwalimu Nyerere, akiwa mwenyekiti wa CCM, hakusita kutamka bayana kuwa Chama alichokuwa akikiongoza kilikuwa na kasoro na mapungufu mengi.
Mwalimu aliona kupungua kwa moyo wa kujitolea, aliona dalili za kupungua kwa maadili ya uongozi, aliona mioyo ya kimamluki ilivyoanza kuingia na kuenea ndani ya CCM na nchi yetu.
Mwalimu Nyerere alifikia hatua ya kumtamkia mhariri yule wa gazeti kuwa: “ Tumewapa uongozi watu wasiofaa. Nadhani wengi ndani ya Chama tumeanza kuutambua ubovu huu. Hatua ya kwanza kutibu maradhi ni kuyatambua.”
Ndio, Mwalimu aliona mbali. Hii leo, viongozi wanaofanya matendo maovu na ya kimamluki ndani ya vyama vya siasa na nchi kwa ujumla ndio wale aliowatabiri Mwalimu Nyerere miaka 23 iliyopita.
Makala yangu yaliyopita niliyaandika kwa dhumuni kuu la kuchokoza mjadala. Yalikuwa ni mawazo yangu huru kabisa. Ilihusu hoja ya wagombea binafsi.
Wengi wamejadiliana nami kwa njia ya simu na mtandao pia. Kuna waliopingana na hoja zangu, kuna walioniunga mkono pia, ndio maana ya demokrasia.
Kama nilivyobainisha juma la jana, demokrasia yetu bado ni changa mno.
Huu ni wakati wa kuwa makini katika kujenga misingi imara ya demokrasia yetu. Tusiangalie uchaguzi wa mwaka huu wa 2015 au 2020. Tuiangalie Tanzania yetu hata baada ya miaka 200 kutoka sasa. Na mawe hayo ya msingi wa demokrasia yanapaswa yakajengwe kwenye KATIBA yetu kwanza. Ndio, ‘ KWANZA KATIBA’.
Kule Marekani katiba yao ina zaidi ya miaka 200. Kubadili kipengele tu katika katiba ya Marekani inaweza kuwa ni mchakato wa miaka kumi. Hakuna hata Rais wa Marekani anayeweza kuichezea Katiba ya Marekani kwa maslahi yake. Anayejaribu kufanya hivyo anaweza kuishia gerezani. Wamarekani wale hata wakimweka ‘mwendawazimu’ Ikulu wanajua namna ya kumdhibiti kikatiba.
Ni tofauti na sisi. Mwanafalsafa Charles Montesque aliyeasisi nadharia ya mihimili mitatu ya dola alikuwa na maana pia ya kumpunguzia Rais nguvu nyingi ambazo angeweza kuwa nazo. Wakati huo huo alitaka kuongeza nguvu kwa Bunge na Mahakama.
Katika nchi zetu hizi, unapozungumzia kuliongezea nguvu Bunge na Mahakama, ina maana pia ya kutoa tafsiri ya kuipunguzia nguvu Serikali, na kwa maana hiyo kumpunguzia nguvu Rais.
Hilo la mwisho ndilo hufanya nchi zetu hizi siku zote zibaki zikipiga makitaimu, ziko pale pale. Hapo ndipo kilipo kiini cha matatizo mengi ya nchi zetu za Kiafrika.
Kimsingi, nchi zetu zina marais wenye mamlaka makubwa mno. Nchi ya Kiafrika inaweza kuwa na rais ambaye nguvu zake zaweza kufananishwa na za Mungu. Na ikitokea rais akazitumia vibaya nguvu hizo, basi, nchi hiyo inaweza ikajikuta inaelekea pabaya sana.
Kama kweli tuna dhamira za kweli za kuviandalia vizazi vijavyo mazingira mazuri ya kuishi, kuifurahia na kujivunia nchi yao, tuna lazima ya kuandaa mazingira ya kuwapo kwa Mkutano wa Kitaifa utakaojumuisha viongozi wa makundi yote ya jamii hii.
Hapo yaandaliwe mazingira ya kuandikwa kwa Katiba itakayokuwa na maslahi kwa Watanzania walio wengi, na kwa miaka mingi ijayo.
Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kuwa tiba ya maradhi yetu tuliyoyatambua ni kuwa na wagombea binafsi wasiotokana na vyama. Kwa wakati huu, hilo laweza lisitusaidie kabisa; badala yake tutakuwa ‘tumechanganya madawa’ yatakayoharakisha mauti yetu kama taifa.
Sisi tuna tofauti kubwa na Marekani na nchi zilizopiga hatua kubwa katika demokrasia. Bado naamini katika kuimarisha misingi ya demokrasia yetu kwa kuangalia zaidi mazingira yetu. Naikubali dhana ya kuwa na wagombea binafsi katika nafasi za uongozi, lakini watokane na vyama.
Na kusiwepo na wagombea binafsi katika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi, nafasi ya urais. Tuamini kuwa wagombea binafsi wanaotokana na vyama wangesaidia kuimarisha demokrasia ya ndani ya vyama .
Njia hii itavinusuru pia vyama vya siasa katika hatari ya kusambaratika zaidi. Kimsingi, kwa kuruhusu wagombea binafsi kuwania nafasi za uongozi nje ya vyama kutawafanya wagombea hao wasione umuhimu wa kushiriki katika siasa za vyama.
Ni muhimu kwa mgombea kuwa na utambulisho wa chama.
Mgombea anayewakilisha wananchi bungeni au kwenye baraza la madiwani anafanya shughuli ya siasa. Hivyo basi, ni vema mtu huyu nyuma yake akawa na chama ambacho itikadi, madhumuni, malengo na sera zake anakubaliana nazo.
Asipokiona chama chenye itikadi, sera na malengo yanayomridhisha yeye, basi mtu huyu apewe uhuru wa kushirikiana na wenzake wenye mawazo yenye kufanana ili aanzishe chama chake cha siasa.
Tusikubali kujenga utaratibu utakaoruhusu wagombea binafsi waharibu dhana nzima ya siasa na itikadi za vyama vya siasa. Kama taifa, tumeazimia kujenga na kuimarisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.
Hata tukiwa na wagombea wengi, basi, watokane na vyama vingi. Kuruhusu wagombea binafsi bila sharti la ushiriki wa siasa za vyama sio tu ni kukaribisha vurugu za kisiasa, bali pia tunawaweka wananchi; kwa maana ya wapiga kura wetu katika wakati mgumu.
Badala ya kuangalia mgombea na sera za chama chake, wengi wa wapiga kura watajikita zaidi katika kumwangalia mgombea, umaarufu wake, sura yake, namna anavyosaidia kutoa michango ya hapa na pale na kadhalika.
Umaarufu wa mtu na kwa kusaidiwa na fedha na labda vyombo vya habari unaweza kutangulizwa mbele badala ya kuangalia umahiri wake ikiwemo sera na misingi ya kiitikadi aliyosimamia mgombea husika.
Utaratibu wa mgombea binafsi ndani ya chama umwezeshe mgombea aliye mwanachama wa chama cha siasa kupewa haki ya kisheria. Isipokuwa katika nafasi ya urais, awe na haki ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uongozi wa kuchaguliwa na wananchi hata kama hakupitishwa na vikao halali vya chama husika.
Tutoe mfano: Mgombea X ni mwanachama wa chama Y. Amechukua fomu ya kugombea udiwani au ubunge kwa tiketi ya chama chake Y. Lakini chama chake hakikumpitisha kuwania nafasi anayoitaka ya kuwatumikia wananchi. Basi, mgombea X awe na haki ya kikatiba na kisheria ya kuchukua fomu ya kugombea kama mgombea binafsi kwa tiketi ya chama Y.
Mgombea huyu X akiwa majukwaani aonekane kuwa ni mgombea binafsi lakini ni mfuasi na mwanachama wa chama Y. Hata akiingia bungeni atatetea sera na itikadi za chama Y.
Endapo ikitokea katika kipindi chake cha ubunge mgombea X atadhani ameshindwa kubaki bungeni kutetea sera na itikadi za chama hicho, basi anaweza kufikia uamuzi wa kujivua unachama. Inawezekana pia mgombea X akavuliwa uanachama na chama chake.
Basi, mgombea X abaki kikatiba na kisheria, kuwa “mbunge pori” hadi kipindi cha uwakilishi wake wa wananchi bungeni kitakapofikia ukomo. Endapo mgombea X atapenda tena kutetea kiti chake cha ubunge katika uchaguzi utakaofuatia, basi, atalazimika kujiunga na chama kingine cha siasa au kujiundia chama chake cha siasa.
Maana, katika hili la wagombea binafsi tusije tukatoka kwenye dhana nzima ya Chama na umuhimu wake. Tukumbuke, mojawapo ya tafsiri ya chama cha siasa ni kama hii ifuatayo: Chama cha siasa ni mkusanyiko wa watu wenye itikadi, madhumuni, shabaha na malengo yenye kufanana. Ni chama kilichojiwekea kanuni za kufuatwa kwa viongozi na wanachama wake.
Katika hilo la hapo juu ni vigumu kukawa na chama cha siasa kitakachodumu muda mrefu kikiundwa na watu wenye itikadi tofauti na wasiokubaliana katika madhumuni na malengo ya msingi.
Kikishindwa kuwa na vitu hivyo muhimu, hakiwezi kuwa na kanuni zitakazofuatwa. Hicho ni chama kwa nadharia, lakini kimatendo, ni mkusanyiko wa vikundi vya watu wenye malengo, madhumuni na shabaha tofauti chini ya kivuli cha “chama nadharia”.
Nimeendeleza mjadala.
