KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii iliyoanza wiki iliyopita, nilijibu maswali mbalimbali niliyoulizwa na wasomaji wangu kuhusu suala la wagombea binafsi katika chaguzi za Tanzania.
Nilisema kwamba wananchi wa kawaida na hata wanasiasa wengine nchini wameshindwa kuelewa vya kutosha ni kwanini Serikali ya Chama cha Mapinduzi inakwepa na kuogopa kuruhusu wagombea binafsi na kwa nini hofu hiyo ina msingi (japo ni msingi wa kiwoga).
Katika sehemu hii ya mwisho ya makala yangu, naendelea kuyakabili maswali mbalimbali kuhusu wagombea binafsi ambayo watu mbalimbali wameniandikia, na ambayo badala ya kumjibu mtu mmoja mmoja nimeona ni vyema kuyaandaa majibu yangu ili hata wale ambao hawakupata nafasi ya kuniuliza waweze kupata majibu hayo kwa kina ili waweze kuelewa kuwa hakuna hoja yoyote ya kikatiba, kisiasa, na kiutawala ambayo inaweza kutolewa kupinga uwepo wa wagombea binafsi Tanzania.
Swali: Hata hivyo wagombea huru bado wanaweza kuwajibishwa na vyama vyao vya siasa?
Jibu: Ndiyo; kama mgombea huru anashinda na bado anataka kuwa na chama chake, basi, chama chake bado kinaweza kumtambua na kumpa nafasi na haki nyingine kama ilivyotokea kwa Bw. Lieberman kule Marekani ambaye licha ya kurudi bungeni kwa tiketi ya mgombea huru bado aliendelea na alishika nafasi zake za kichama Bungeni.
Hivyo, hata hapa Tanzania ikatokea (kwa mfano) mgombea wa CCM aliyeenguliwa kwenye kura ya maoni anashinda kama mgombea huru na akakubali kuondoa kinyongo na chama kikamkumbatia, basi, mwakilishi huyo anaweza kuchukua nafasi yake ndani ya chama - hakatazwi.
Swali: Itakuwaje sasa kwa wale ambao hawakuwa na vyama kabisa?
Jibu: Kwa mgombea ambaye hakuwa na chama kabla, huyo anapimwa na kusimamiwa na taratibu na sheria nyingine zinazosimamia nafasi yake. Lakini kubwa zaidi anasimamiwa na wananchi waliomchagua na atapimwa kwa miaka yake mitano na kama wananchi wanaona hawafai, basi, miaka mitano ikipita watamchagua mgombea mwingine (awe na chama au la).
Swali: Lakini hofu nyingine iko kwa urais, kweli tunaweza kuongozwa na Rais asiye na chama?
Jibu: Kinadharia jibu ni ndiyo! Rais wa Tanzania anaapa kulinda na kusimamia Katiba na haijalishi kama yuko kwenye chama au la. Kwa hiyo, hata Rais akitokea ambaye hana chama cha siasa bado atafungwa na sheria na taratibu zile zile za Kikatiba zinazomuongoza Rais aliye na chama.
Hata hivyo ni lazima tutambue ni vigumu sana kwa mgombea binafsi kuweza kushinda nafasi ya urais isipokuwa awe na uwezo mkubwa wa ushawishi, raslimali na kuungwa mkono. Tukumbuke kuwa hata mgombea binafsi akishinda nafasi ya urais bado atatakiwa kuchagua Waziri Mkuu kwa mtindo ule ule wa kuchagua mbunge wa jimbo la uchaguzi anayeungwa mkono zaidi bungeni na ataunda baraza la mawaziri kwa utaratibu ule ule.
Ni muhimu kuelewa kuwa mgombea huru siyo sawasawa na kutawala huru! Yaani, haina maana kwa vile rais, mbunge au diwani ameingia kwa tiketi huru, basi, atakuwa huru kufanya lolote analotaka bila kufuata sheria au taratibu zilizopo.
Hivyo, japo tunaweza kuruhusu kuwa na wagombea huru mpaka kwenye nafasi ya urais, ni vigumu sana kuwa na Rais ambaye atasimama bila ya kusimamishwa na chama.
Swali: Kama itakuwa vigumu hivyo kwa nini tusiruhusu tu wagombea binafsi kwenye nafasi nyingine isipokuwa kwenye nafasi ya Urais?
Jibu: Uzuri wa demokrasia ni kuwa endapo tunapata mgombea binafsi kwenye nafasi ya Urais naye anakubalika na anaungwa mkono anaweza kabisa kusababisha mabadiliko ya kampeni na hoja za uchaguzi.
Mgombea binafsi wa urais ambaye anaungwa mkono na anaonekana ana hoja nzito na anakubalika anaweza kabisa kusababisha wagombea wa urais kwa kupitia vyama kuangalia hoja zake, na hata kujaribu kuzichukua ili wapatwe kuungwa mkono naye.
Hilo lilitokea wakati Bill Clinton anagombea kwa mara ya kwanza kule Marekani dhidi ya George H Bush.
Swali: Serikali, hata hivyo, inasema kuwa muda uliobakia hautoshi kufanya mabadiliko ya Kikatiba kuingiza wagombea huru. Unasemaje?
Jibu: Kama uamuzi ungekuwa unatolewa mara ya kwanza baadaye mwaka huu, tungeweza kusema kuwa kweli muda haupo. Lakini uamuzi umetolewa zaidi ya miaka 15 iliyopita! Mtu yeyote mwenye akili timamu na kiongozi yeyote mwenye maono angeshaanza kujiandaa na ukweli ulioko mbele yake.
Baada ya kupoteza kesi ya kwanza na mara ya pili ningetarajia mtu mmoja (au kikundi chao) huko serikalini kujiuliza swali “kama tutashindwa tena na tena wagombea binafsi watafanya kazi vipi”. Kwa hiyo, mara moja wanaandaa mpango wa tahadhari.
Tukumbuke kuwa uamuzi wa mwisho wa suala hili mwaka 2006 ulisema wazi kuwa kuanzia wakati huo hadi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2010 wagombea binafsi wanaruhusiwa na serikali ilitakiwa iandae utaribu na mfumo wa kisheria kuhakikisha hilo linatokea.
Huo ulikuwa ni uamuzi wa Mahakama Kuu. Serikali ilitakiwa iwe imeanza kuutekeleza hata kama ilikuwa inapanga kukata rufaa.
Swali:Wangeweza vipi kuutekeleza wakati walikuwa wanataka kukata rufaa?
Jibu: Kukata rufaa hakusababisha uamuzi wa awali kusimamishwa mara moja. Ndio maana Jaji Mkuu Augustino Ramadhani alimkumbusha Naibu Mwanasheria Mkuu kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu wa 2006 bado unasimama (kwa maneno mengine ulitakiwa uwe umeanza kutekelezwa); kwani kwa serikali kukata rufaa hakukusababisha uamuzi ule kutokuwa halali.
Swali: Serikali, kupitia Waziri Marmo, wameshatamka haijalishi Mahakama itaamua nini msimamo wao ni kuwa “wagombea binafsi hawaruhusiwi”. Unasemaje kuhusu hilo?
Jibu: Kwanza Marmo alitakiwa atiwe pingu kwa kudharau mahakama na kama Rais Kikwete angekuwa ni kiongozi bora, angemtaka Marmo afute kauli yake hiyo. Wanachofanya ni kile kile kilichofanywa kwenye uamuzi wa kwanza wa Jaji Lugakingira, na walivyofanya kwenye kesi ya Valambhia kwamba Mahakama inafanya kazi kwa huruma ya Serikali. Safari hii nina uhakika wa asilimia 100 kuwa Mahakama yetu haitakubali kudharauliwa tena.
Swali: Sasa itakuwaje kama serikali itatekeleza uamuzi wake huo wa kutoitii Mahakama, na hivyo kutoruhusu wagombea binafsi?
Jibu: Kwanza nikuhakikishie Jaji Mkuu ataamua kujiuzulu kupinga hilo, na pamoja naye majaji wote wa Mahakama ya Rufani! Kama Serikali itashikilia msimamo wake wa kutoitii mahakama, kama ulivyoelezwa na Marmo na Chiligati na kutopingwa na Kikwete na Waziri Mkuu, basi, Mahakama ya Rufani haina sababu ya kufanya kazi yake na Kikwete atapata nafasi ya kuteua majaji wapya watakaocheza ‘ngoma’ ya serikali.
Swali: Unafikiri hilo linaweza kutokea Tanzania? Yaani majaji wachukue uamuzi kama huo?
Jibu: Tanzania ya zamani hilo lisingewezekana, Tanzania ya leo hilo linawezekana. Mlinzi wetu wa kwanza wa haki na raslimali zetu amekwisha anguka (yaani Bunge); mlinzi wetu wa haki na raslimali zetu wa mwisho ni Mahakama! Tukiacha na hii ianguke tutakuwa tumeingia rasmi katika utawala wa kidikteta ambapo Rais wa Tanzania anakuwa juu ya Mahakama na Bunge! Itakuwa ni siku ya huzuni.
Swali: Wewe mwenyewe ungependa kugombea kama mgombea binafsi au vipi?
Jibu: Siyo mimi tu, wapo Watanzania wengine wengi ambao wamechoshwa na siasa za vyama na wako tayari kuwatumikia wananchi wenzao bila kuogopa vikao vya chama. Wapo walio nje ya vyama hivyo sasa na wapo walio ndani na uamuzi wa kuruhusu wagombea binafsi ni haki ambayo haiwezi kufutwa tu kwa sababu CCM na serikali yake inaogopa. Waruhusu wagombea binafsi na utashangaa ni kina nani watajitokeza.

Barua-pepe: