WAKATI kila Mtanzania anajiuliza ni nani atamrithi Rais Jakaya Kikwete, 2015, (maana 2010 kuna dalili za kupita bila kupingwa), kuna mapendekezo yanayojitokeza kwamba sasa ni zamu ya akinamama kuliongoza taifa letu la Tanzania.
Wengine wanakwenda mbali hadi kutaja majina ya akinamama hawa. Bahati mbaya wengi wa akina mama hawa wanaotajwa umri umewatupa mkono. Mawazo haya ni mazuri na ya msingi. Wanawake wana uwezo mkubwa; si kweli kwamba kuna mambo wanayoyaweza wanaume tu na wanawake hawayawezi.
Hakuna haja ya kutaja kwamba wanawake madaktari wanaongezeka kila kukicha, wasichana wanajiunga kwenye fani ya uinjinia na kwamba tunao wanawake mainjinia, uhasibu na fani nyingine ambazo zilifikiriwa kuwa fani za wanaume tu huko siku za nyuma.
Uamuzi wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Magharibi (Bukoba) na Dayosisi ya Karagwe, kuwabariki wachungaji wanawake limekuwa pigo kwa “Wahaya” na “Wanyambo” walioamini kwamba huduma za ki-chungaji ni kazi ya wanaume tu!
Tanzania ina historia ndefu ya akina mama kushiriki katika mapambano ya kuleta uhuru na kuchangia maendeleo ya taifa. Majina ni mengi; yanaanzia kwa akina Bibi Titi, Lucy Lameck hadi kwa kina Sofia Kawawa nk. Hata leo hii akina mama walio kwenye uongozi kama mawaziri wanatoa mchango mkubwa katika kulijenga taifa letu na kuchochea kasi ya maendeleo.
Mkoani Kagera kuna mchango mkubwa uliotolewa na akinamama ambao sasa hivi wengi wao ni wazee sana na wengine wamekufa. Akinamama hawa ni wale waliojiingiza katika biashara ya kuuza miili yao. Biashara inayojulikana kwa jina la “ukahaba”.
Walisafiri hadi Mombasa, Nairobi Kisumu, Mwanza, Dar es Salaam na miji mingine ya Afrika mashariki iliyokuwa ikifikika kwa usafiri wa meli na treni. Pesa walizokuwa wakizipata huko walinunua vitu kama vinanda, vyerehani, baiskeli nk., na kuvileta mkoani Kagera. Pia walitumia pesa hizo kununua mashamba, kujenga nyumba na kusomesha watoto.
Mji wa Bukoba una mtaa unaoitwa Uswahilini. Hii ni kati ya mitaa iliyokuwa imeendelea na kuwa na nyumba bora kwenye miaka ya 1950-1960. Nyumba hizi ambazo zimedumu hadi leo hii, zilijengwa na akina mama walioitumia miili yao si kwa manufaa yao tu bali kwa manufaa ya kuiendeleza jamii.
Wasomi wa kwanza wa mkoa wa Kagera, walisaidiwa na Kanisa na Chama cha Ushirika cha Kahawa, lakini ipo idadi kubwa iliyosomeshwa kwa msaada wa pesa za akina mama hawa walioiuza miili yao.
Ni wazi “ukahaba” ni kitu cha aibu. Si rahisi mtu kuungama wazi kwamba alisomeshwa na pesa kutokana na biashara hiyo. Lakini ukweli unabaki palepale kwamba biashara hii ilichangia kiasi fulani maendeleo ya mkoa wa Kagera katika nyanja mbalimbali.
Tusi kwamba Wahaya wana jadi ya “umalaya” si la haki. Mnamo mwaka wa 1910, Mjerumani Hermann Rehse aliandika kitabu akielezea kwamba “umalaya” lilikuwa ni jambo jipya mkoani Kagera.
Mwandishi mwingine anayejulikana kwa jina moja la Bwana Swantz anakubaliana na Hermann Rehse kwamba “umalaya” ulianza kushika kasi mkoani Kagera mnamo mwaka wa 1920.
Zipo sababu nyingi zilizosababisha biashara ya ukahaba kushika kasi mkoani Kagera. Baada ya Wajerumani na Waganda kuingiza biashara hii mkoani Kagera, ilishika kasi. Magonjwa ya zinaa yalisababisha ugumba, na kama ilivyo kawaida, wanawake ndio walinyoshewa kidole.
Wale ambao hawakufanikiwa kupata watoto walifukuzwa kwenye ndoa na kulazimika kuishi kwa kujitegemea. Kwa vile wanawake walikuwa hawaruhusiwi kumiliki kitu kwa wakati huo, njia pekee ya kujitegemea ilikuwa ni kuuza miili yao.
Wakati huo ndio Ukristu ulikuwa unaiingia na ilisisitiza ndoa ya mume mmoja mke mmoja. Wanaume waliokubali kubatizwa waliwafukuza wake zao wengine na kubaki na mke mmoja wa ndoa. Hawa wengine hawakuwa na njia ya kujitegemea zaidi ya kusafiri na kufanya biashara ya kuuza miili yao.
Mpaka leo hii, sote tunaamini kwamba ukimwi uliingia Tanzania kutokea Uganda. Wanaolaumiwa kwa kuuleta ugonjwa huu na kuueneza Tanzania, ni wafanyabiashara na wanajeshi waliopigana vita ya kumwondoa nduli Idi Amin. Pia magonjwa ya zinaa yaliingia Tanzania kutokea Uganda.
Mfalme Kabaka Mwanga (1880) wa Buganda, mwenye vituko vingi, aliamini kwamba magonjwa ya zinaa yalikuwa na heshima na utukufu wa aina yake! Kwa mtazamo huo, magonjwa hayo yalienea kwa kasi. Wahaya waliokwenda kufanya kazi kwenye mashamba ya pamba kule Uganda ndiyo waliyoyabeba na kuyaleta Bukoba.
Mpaka leo hii kuna msemo kwamba wale waliokwenda kutafuta pesa Uganda, walileta pesa, maendeleo, magonjwa ya zinaa na dini za kigeni: Ukristu na Uislamu!
Ingawa akina mama waliouza miili yao, walionekana kuwa adui wa jamii kwa kusambaza magonjwa ya zinaa na kusambaza jina baya la wanawake wa Bukoba – jina la umalaya, hatuwezi kukwepa mchango wao mkubwa na mzuri katika jamii.
Hata chama cha TANU kilipata michango ya pesa kutokana na kipato cha akinamama hawa. Watoto au jamaa wa mama hawa, walisoma kwa pesa zilitokana na biashara ya umalaya.
Nakumbuka niliwahi kuandika makala yenye kichwa cha habari: “Ukombozi wa mwanamke, adui ni mwanamke mwenyewe”. Pamoja na ukweli kwamba wanawake wana uwezo mkubwa na wanaweza kutoa mchango mkubwa katika kuliendeleza taifa letu, bado kuna mawazo potofu kwamba mwanamke hawezi kitu. Bahati mbaya mawazo haya kwa kiasi kikubwa yamo kwenye vichwa vya wanawake wenyewe!
Ikitokea mwanamke akafungua biashara ya hoteli au mgahawa, atapenda kuajri mpishi mwanaume na wahudumu wanaume. Ukiuliza; jibu linakuwa kwamba wanaume wanapika vizuri na kuhudumia vizuri na kwamba ukiwaajiri wasichana watakuharibia kazi yako!
Kwa kawaida kuna mafundi wa nguo za kike, wanaume na wanawake. Idadi kubwa ya akinamama na wasichana wanapenda nguo zao kushonwa na mafundi wa kiume. Ukiuliza; jibu linakuwa kwamba wanaume wanajua kushona na kubuni mitindo mizuri zaidi ya wanawake!
Utakuta mmiliki wa saluni ya nywele ni mwanamke lakini walioajiriwa kutengeneza nywele, kupaka rangi kwenye kucha, kurembesha uso ni wanaume. Ukiuuliza; jibu ni kwamba wanaume wanasuka vizuri, wanapaka rangi vizuri na ujuzi wao wa kurembesha uso wa mwanamke ni wa hali ya juu kuliko wanawake.
Siku hizi saluni ambazo hazina wanaume hazina wateja! Ni kweli wanaume wana ujuzi wa kutengeneza nywele kuliko akinamama? Ni kweli wanaume wana ujuzi wa kupaka rangi na kurembesha uso kuliko akina mama? Na je, haya ni mambo ambayo akinamama hawawezi kuyamudu?
Mvulana akiendesha gari linaonekana ni jambo la kawaida na hakuna anayekuwa na wasiwasi kwamba huenda gari hilo si la kwake. Akiendesha msichana, utawasikia wasichana wenziwe wakiteta; “huyu naye na kuringa. Kwanza gari si lake, ni la mshikaji ni mali ya “buzi”!
Nimeshuhudia akinamama wakimkimbilia daktari bingwa wa magonjwa ya akinamama mwanamme kuliko mwanamke mwenzao mwenye ujuzi uleule. Wanadai kwamba daktari wa kiume ana uwezo mkubwa, ana “mkono mzuri” na ana huruma kuliko daktari wa kike.
Haya yanasemwa na akinamama bila kulazimishwa, bila vitisho na bila unyanyaswaji wa aina yoyote ile. Ni wazi ni matokeo ya kupumbazwa. Ni ugonjwa unaohitaji tiba. Ni ugonjwa mkubwa kuliko tunavyoweza kufikiri na kujidanganya.
Sasa hivi, kwa sababu zinazotofautiana, watumishi wengi wa ndani ni wavulana kuliko wasichana! Kuna malalamiko kwamba hata wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, wanawatesa, wanawanyanyasa na kuwadhalilisha wasichana wanaofanya kazi majumbani.
Umekuwepo pia ukweli wa wasichana wa ndani kupindua na kuingilia ndoa za waajiri wao. Yote haya yamejikita katika hali nzima ya mwanamke kutojiamini na kutojithamini.
Hata zile ajira ambazo kwa kiasi fulani zingekuwa za akinamama na akina dada, bado zinachukuliwa na wanaume na kuwalazimisha wasichana kuishia kwenye “uchangudoa”. Sitaki kuliongea hili kwa sasa, lakini kuna ukweli kwamba hata “Changudoa” wanatumia pesa zao kutunza watoto, kujenga nyumba, kusaidia ndugu na jamaa, sifa ile ile ya akinamama kuitumia miili yao si kwa manufaa yao tu; bali kwa kuchangia kuliendeleza taifa letu.
Tuna akinamama wengi wenye uwezo wa kutawala nchi hii. Anayewakataa ni nani? Ni wanawake wenyewe. Jinsi wanavyowakatalia kufanya kazi kwenye mahoteli, saluni na kususia ufundi wao wa kutengeneza nguo za kike ndivyo pia wanavyowasusa wanapoomba kura kwenye uchaguzi. Watasema: Mwanamke ataongoza nini? Wanaume ndio wanafaa kuongoza.
Ukiwauliza; mbona wanaume hawa wametuletea matatizo makubwa? - Wanagombania madaraka, wanaleta vita, damu inamwagika, angalia yaliyotokea Zanzibar, angalia yanayotokea kila siku, rushwa, uporaji, nchi inauuzwa. Jibu litakuwa: Mwanamume ni mwanamume, hata kama ni lofa!
Si kwa kuambiwa. Nilimsikia mwenyewe mwanamke mmoja mwenye cheo kikubwa serikalini akisema kwamba: “Ukubwa ni ofisini, nikiingia nyumbani kwangu mimi ni mama wa ndani. Ninapika na kumtunza mume wangu, na mume wangu ndiye kiongozi na mtawala wa nyumba yetu. Machachari yote haya mnayoyaona yanabaki nje ya mlango wa nyumba yetu.”
Huyu ni mama mwenye cheo cha juu katika serikali yetu. Ni kati ya wale wanaotajwa kufaa kuliongoza taifa letu! Je, nywele zake zinatengenezwa na mvulana au msichana? Siri yake!
Mwingine ni rafiki yangu ambaye yuko mstari wa mbele kutetea haki za akinamama. Tunawaita wanaharakati. Sikuamini macho yangu aliponiandikia akilalamika: “Ninatamani ningezaliwa mwanamume ili niwe padri. Ninaipenda sana kazi hii, na ninawaonea wivu mapadri. Ni bahati mbaya nilizaliwa mwanamke!”
Kama mwanaharakati wa kutetea haki za wanawake anaona ni bahati mbaya kuzaliwa mwanamke, je akinamama wa kawaida ambao hawakufanikiwa kusoma, wanawake wa kule vijijini watasema nini? Watawezaje kuwa na mawazo ya kumchagua mwanamke diwani, mwanamke mbunge na mwanamke rais?
Kazi kubwa ni ile ya kumfanya mwanamke kujiamini na kujithamini, kuwaamini na kuwathamini wanawake wenzake. Jinsi jamii nzima ilivyoshiriki kuwapumbaza wanawake, ndio ilivyo kazi ya jamii nzima kushiriki katika kuwapatia akinamama mwanga mpya wa kujiamini na kujithamini.

Simu:
0754 633122