SERIKALI kupitia kwa Katibu Mkuu wa Hazina, Ramadhan Kijjah ilisema wiki iliyopita ya kuwa imekuwa ikikusanya shilingi trilioni tano lakini ikitumia shilingi trilioni 10 kwa mwaka.
Kijjah alitoa taarifa hiyo katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam akieleza pia kwamba mapato ya Serikali yamepanda kutoka shilingi trilioni 2.167.6, mwaka 2005/06 hadi shilingi trilioni 5.096 mwaka 2009/10.
Alisema pia kwamba mfumuko wa bei umepanda kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 ulipokuwa ni asilimia tano hadi asilimia 12.2 Desemba mwaka jana, kabla ya kushuka kidogo kufikia asilimia 10.9 Januari, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kijjah, shilingi ya Tanzania imeendelea kuporomoka kutoka wastani wa shilingi 1,195.75 kwa dola ya Marekani mwaka 2008 hadi shilingi 1,318.71 ya dola moja ya Marekani, mwaka jana.
Tumeorodhesha takwimu alizotoa Katibu Mkuu Kijjah katika mkutano wake huo kuelezea jinsi hali ya kifedha nchini ilivyo ngumu, hali ambayo ndiyo wanayopambana nayo kila siku Watanzania wengi wanaoishi chini ya matumizi ya dola moja ya Marekani kwa siku.
Kuna vitu kadhaa vinajitokeza katika taarifa hizi za fedha. Kwanza, serikalini kuna matumizi makubwa mno na ambayo mengine hayana maelezo ya kueleweka, lakini pia kuna upungufu katika mfumo mzima wa makusanyo ya mapato.
Tuseme tu kuwa, maana pana ya taarifa hizi ni kwamba uchumi wa nchi unayumba, na kama uchumi katika ngazi ya nchi unayumba, basi uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja unayumba mara nyingi zaidi na ushahidi wa kuyumba huku ni hizi kauli ambazo sasa ni za kawaida, za kulalamikia ugumu wa maisha zinazotoka katika kila kona ya nchi kwenye tabaka za aina mbalimbali za umma.
Inawezekana kweli, kama alivyosema Kijjah mwenyewe, ya kuwa Serikali imejipanga kuikabili hali hii ya matumizi yasiyozingatia mapato kwa kuongeza idadi ya wahasibu na wakaguzi wa ndani katika wizara na serikali za mitaa, kuanzisha kitengo cha ufuatiliaji wa matumizi ya umma katika miradi iliyoidhinishwa, na kuongezewa meno kwa ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Tuongeze jingine: vitendo vivuke maneno. Ni suala moja kuzungumzia mipango mizuri ya udhibiti wa matumizi yanayovuka mipaka ya makusanyo, ni suala jingine kutekeleza kwa vitendo mipango hiyo mizuri kwa kuwa utekelezaji hakika hauhitaji maneno mazuri kila mara, bali utashi. Na si wengi wetu tunao utashi.
