BAADA ya mgombea Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA ), Dk. Wilbrod Slaa, kubadili upepo wa kisiasa nchini kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, chama hicho sasa kimo katika mkakati mahususi wa kumpata mgombea mwenza mwenye ushawishi mkubwa kutoka Chama cha Wananchi (CUF), Raia Mwema limethibitishiwa.
Habari za uhakika kutoka CHADEMA na CUF zimethibitisha kwamba mazungumzo yasiyo rasmi yamekwisha kuanza pamoja na kuwa tayari majina mazito ya wanasiasa kutoka Zanzibar yameanza kutajwa kuombwa kuwa pamoja na Dk. Slaa katika uchaguzi huo wa Oktoba 31.
Wanaotajwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Juma Duni Haji na aliyekuwa Kiongozi wa Upinzani bungeni na mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, ambao wote ni watu wenye ushawishi mkubwa katika siasa za Visiwani na Bara.
Duni, ambaye tayari CUF imemteua kuwa Mgombea Mwenza wa Profesa Ibrahim Lipumba, anayebeba kwa mara ya nne bendera ya chama hicho katika kuwania Urais, anatajwa kutakiwa na CHADEMA kutokana na ushawishi wake ndani ya siasa za Zanzibar na hata Bara.
Kwa mujibu wa habari hizo, kukubali kwa Duni kutategemea zaidi msimamo wa chama chake katika kumuunga mkono Dk. Slaa, hatua ambayo imeelezwa kuanza kujadiliwa katika vikao visivyo rasmi kabla ya kuingia katika vikao rasmi vya vyama hivyo ili hatimaye kufikia maamuzi.
Mwaka 2000 CHADEMA walimuunga mkono mgombea urais wa CUF, Profesa Lipumba, ambako katika mikutano yake nchi nzima alisimama kuwapigia debe wagombea wa CHADEMA na CUF huku mitandao ya vyama hivyo ikitumika katika harakati za kampeni hizo, hali ambayo inaelezwa kupendekezwa kuwapo katika uchaguzi wa mwaka huu.
Kwa upande wa Hamad Rashid, anatajwa kama mtu aliye karibu na Dk. Slaa wakiwa wamefanya kazi kwa muda mrefu bungeni katika ofisi ya kambi ya Upinzani, na anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa waliomshawishi mwanasiasa huyo wa CHADEMA kuwania Urais.
Kabla ya CUF kumsimamisha Profesa Lipumba kuwa mgombea wake, Hamad Rashid, alitajwa kama mmoja wa watu ambao wangeweza kuwa mgombea mwenza wa Dk.Slaa na yeye mwenyewe kutajwa kuwa tayari.
Mapema mwaka juzi, Hamad Rashid alifanya mahojiano maalumu na Raia Mwema na kuchapwa katika toleo lake namba 30 ambapo alisema kwamba ameshauriwa kujiandaa kuwania urais mwaka 2015 lakini baadhi wametaka aanze mwaka 2010, akiwataja baadhi ya wabunge waliomshauri, wakiwamo wengine kutoka CCM.
“Ni kweli nina nia ya kuwania urais lakini si wa Zanzibar na kwamba nilijiandaa kwa mwaka 2015, lakini wabunge wenzangu baadhi kutoka CCM wamenishauri nianze kujitokeza mwaka 2010,” alisema Hamad, ambaye amewahi kuwa ndani ya Serikali ya Muungano katika wizara za Fedha na baadaye Mambo ya Ndani.
Tangu Dk. Slaa akubali kuwania Urais kupitia CHADEMA, kumeibuka maoni kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka vyama vingine vya siasa vimuunge mkono mgombea huyo kwani ndiye anayeonekana kukubalika zaidi lakini hadi sasa chama kinachoonekana kuwa makini zaidi cha CUF ndicho kinachosubiriwa kutoa msimamo wake rasmi.
Wakati mazungumzo ya kutafuta mgombea mwenza kutoka CUF yakiendelea, imeelezwa kwamba nguvu ya Dk. Slaa inaweza kubadili kabisa upepo wa kisiasa nchini ikiwa ataungwa mkono na wapinzani wengine hali itakayotoa changamoto kubwa kwa mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete.
Hadi tunakwenda mitamboni, jana Jumanne, hakuna yeyote ndani ya CUF na CHADEMA aliyekuwa tayari kuzungumzia kwa uwazi suala la mgombea mwenza wa Dk. Slaa kutoka CUF, ikielezwa kwamba hilo bado ni suala nyeti kusemwa hadharani.
Akiwaaga wapiga kura wake wa Karatu juzi na jana Jumanne, Dk. Slaa alitoa sababu nane ambazo zimemfanya akubali kubeba dhamana ya kuwania Urais, ikiwa ni pamoja na kuamua kuwakomboa wananchi aliosema wameporwa haki yao ya kikatiba ya kuwa ndio wenye mamlaka ya mwisho.
Katika mikutano yake iliyofurika umati mkubwa wa watu, Dk. Slaa amesema pamoja na kuwa hakuwa na mpango wa kuwania urais mwaka huu, hoja zilizowasilishwa na Kamati Kuu ya CHADEMA zimemfanya aone umuhimu wa kubeba dhamana ya kuutumika umma.
Amesema pamoja na Kamati Kuu, wasomi na watu wa kada mbalimbali walimuomba baadhi wakiwa wamemuandikia waraka maalumu ukiwa na orodha na saini zao.
Kuhusiana na wananchi kuporwa haki yao ya kikatiba amesema Katiba inasema kwamba wananchi ndio wenye mamlaka ya juu lakini kwa sasa ni asilimia tatu tu ndio wanaoshikilia uchumi na uongozi.
Ameahidi kufanya mabadiliko ya katiba ambayo yatatoa nguvu zaidi kwa umma.
Wakati hayo yakijiri, Kanisa Katoliki wiki hii liliibua mjadala mpya kwa kutoa kauli kukanusha kile kilichotajwa kuwa ni uzushi ulioibuliwa kwamba Dk. Slaa, anategemea udini wa Wakatoliki na ameingia makubaliano yasiyo rasmi na baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo katika harakati zake za kuwania Urais.
Katika taarifa yake kupitia Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (TEC), kanisa hilo limesema pamoja na kukanusha uzushi huo, litaendelea kutoa mchango wake na kushirikiana na raia wote wanaoitakia nchi mema, kuhakikisha Uchaguzi Mkuu ujao, unafanikisha kupata viongozi waadilifu, wanaojali maslahi ya wote na watakaosaidia nchi na watu wake kupata maendeleo.
Akizungumza na vyombo vya habari wiki hii, Rais wa Baraza hilo, Askofu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, alisema uzushi huo ulioibuliwa katika magazeti ya wiki iliyopita, licha ya kulichafua Kanisa, ni udhalilishaji mkubwa wa taaluma ya habari kauli ambayo imeanza kuelezwa kwamba imetolewa kuepuka kuwagawa Watanzania kwa misingi ya dini.
Katika mkutano huo Askofu Ruwa’ichi alisema kauli kwamba mgombea Urais wa CCM, Rais Kikwete ni chaguo la Mungu haikuwa kauli ya Kanisa; bali ulikuwa utashi binafsi wa aliyeitoa. Kauli hiyo ilitolewa na kurejewa tena hivi karibuni na Askofu Methodius Kilaini.
Hivi karibuni Kanisa Katoliki lilitoa waraka na baadaye mwongozo kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nyaraka ambazo zilionekana kuwataka wananchi kufanya maamuzi sahihi katika kuchagua viongozi wakianisha vigezo vya kiongozi bora na vipaumbele vya umma katika uchaguzi wa mwaka huu.
