UAMUZI wa hivi karibuni wa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete kumteua Mohamed Dk. Gharib Bilal kuwa mgombea mwenza ‘umemliza’ Rais anayemaliza muda wake Zanzibar, Amani Abeid Karume, ambaye hakuficha hisia zake kutaka nafasi hiyo wakati viongozi waandamizi walipokutana kujadili jina la mgombea mwenza,
Raia Mwema imeelezwa.
Gazeti hili limeelezwa kuwa uamuzi wa Kikwete kutaka kumteua Dk. Bilal ulipigiwa chapuo na rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye anatajwa kuwa alikuwa na kibarua kizito kumzuia Karume aliyekuwa akijipigia debe kupewa nafasi hiyo.
Hoja kubwa iliyokuwa ikitumiwa na Mkapa inatajwa kuwa ni kuhakikisha CCM inakabili changamoto za siasa za jukwaani Zanzibar .
Wanasiasa waandamizi waliokuwa karibu na viongozi wakuu walioshiriki kikao hicho nyeti, kilichofanyika mjini Dodoma wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM, kilichotajwa kumsaidia Rais Kikwete kuweza kutamka mgombea mwenza atakayekuwa na mshindo Unguja, baada ya mgombea urais wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein anayetoka Pemba kupitishwa, wamesema Rais Karume alikuwa amejiridhisha binafsi kabla ya kikao hicho kuwa nafasi ya makamu ingekwenda kwake.
Imeelezwa kuwa Mkapa alikuwa mkali kwenye kikao hicho akionyesha msimamo usio na unafiki katika kueleza hatari iliyokuwapo kwa CCM kama Karume angeweza kutangazwa mgombea mwenza wa Rais Kikwete na Dk. Bilal akiachwa.
Wiki mbili zilizopita gazeti hili lilichambua kuhusu kutokuwapo kwa uhusiano wa karibu kati ya Rais Karume na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour, Dk. Bilal, ikielezwa kuwa Karume alikandamizwa wakati wa harakati zake za kuwania urais wa Zanzibar na kuokolewa na Halmashauri Kuu iliyokutana mjini Dodoma, kwenye uchaguzi wa mwaka 2000.
Lakini safari hii hali ilibadilika kwani Karume alihakikisha Dk. Bilal hasimikwi ugombea urais wa Zanzibar (CCM) lakini wakati huo huo akashindwa kutimiza kilio chake cha kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano baada ya Dk. Shein, ambaye amekwishapongezwa hata na chama kikuu cha upinzani cha CUF, kuwezeshwa kuwa mgombea wa urais CCM Zanzibar .
Kutokana na Karume kutimiza upande mmoja wa ndoto yake na kushindwa kutimiza upande mwingine wa kuwa mgombea mwenza wa Kikwete, wana-CCM waandamizi wamelieleza Raia Mwema kuwa, kete pekee ya kuzidi kumjengea heshima kubwa mbele ya viongozi wenzake waandamizi katika CCM ni Karume kuhakikisha kura ya maoni itakayopigwa mwishoni mwa mwezi huu inaunga mkono maridhiano kati ya CCM na CUF ambayo ndiyo msingi wa kuundwa kwa Serikali ya Pamoja.
Hatua hiyo itamjengea Rais Karume historia ya kipekee katika CCM na Zanzibar akiwa kiongozi mkuu kufungua milango ya maridhiano yenye mafanikio makubwa Zanzibar , baada ya majaribio mbalimbali ya kuwapo kwa muafaka kati ya CUF na CCM kukwama na zaidi, ikizingatiwa kuwa aliyekuwa akitajwa kuwa hasimu wake wa kisiasa katika CCM Zanzibar, Dk. Salmin Amour alishindwa kusimamia muafaka kati ya CCM na CUF na kuibua matunda ya kihistoria.
Tayari hali hiyo ya Karume kupigania kura ya maoni kukubali maridhiano imeanza kujibainisha akianza kunadi kwenye mkutano wa hadhara uliotishwa hivi karibuni kwa ajili ya kile kilichotajwa kuwa kuwatambulisha mgombea urais wa Zanzibar , Dk. Ali Mohamed Shein na mgombea mwenza wa Rais Kikwete, Dk. Ali Mohamed Shein.
Lakini wakati mazingira hayo yakijitokeza na msingi wake ukiwa ni Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika mkoani Dodoma, hivi karibuni, yapo mengine yaliyojipambanua kwenye mkutano huo. Kati ya hayo ni changamoto ya kila wakati wa mkutano mkuu ya serikali kuwasilisha taarifa zake bila wajumbe kupewa muda wa kuzijadili.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na utendaji wa Serikali wanaeleza kuwa hiyo ni kasoro kubwa kwa chama tawala ambacho wakati wote kinatazamiwa kutoa mfano bora kwa vyama vingine vitavyojipanga kushika nafasi hiyo.
Viongozi wakuu watendaji wa Serikali katika mkutano mkuu wa Dodoma walitoa taarifa za serikali zote mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar.
Taarifa ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwasilisha katika mkutano huo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wakati ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwasilishwa na Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Wachambuzi wa masuala ya siasa na uongozi wanabainisha kwamba kwa kuwa mkutano huo unahusisha wajumbe kutoka kila kona ya nchi ilikuwa bora zaidi kwa wajumbe hao kuzijadili taarifa hizo ili Serikali itambue utendaji wake umeweza kugusa kwa kiasi gani maisha ya watu wa kawaida kwa kusikia sauti zao za ukosoaji, upongezaji au urekebishaji wa ripoti husika.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa CCM imeshindwa kutoa fursa kwa wajumbe hao kujadili ripoti za utendaji wa Serikali katika maisha ya miaka mitano ya ilani ya uchaguzi wa chama hicho kutokana na kikwazo cha fedha.
Hata hivyo, wengine walibainisha kuwa utaratibu angalau wa kujadili ripoti hiyo ungefanywa kwa ripoti kutumwa mapema kwa wajumbe kupitia uongozi wa mkoa au wilaya na kuzijadili huko na wanapofika kwenye mkutano mkuu Dodoma wawe na taarifa yao ya muhtasari na kila mkoa uisome.
