GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndullu, amesema wameshaanza mchakato wa kutekeleza maagizo ya Bunge kutaka kuziondoa mahakamani kesi hewa zilizofungiliwa na benki hiyo mahakamani.
Akizungumza na Raia Mwema kwa simu jana Jumanne, Profesa Ndullu, amekiri kuwapo kwa ucheleweshaji wa utekelezaji wa maagizo hayo, lakini alisema ni kutokana na kuhusisha mfumo wa Mahakama ambao unaongozwa na mhimili mwingine wa dola.
“Kila jambo lina utaratibu wake, si kwamba sisi BoT tumechelewesha bali suala hili kama unavyojua linahusisha Mahakama na hivyo lazima mchakato wake ufuate mkondo wa kimahakama na sasa wanasheria wetu wanalifanyia kazi,” alisema.
Profesa Ndullu amekanusha kuwapo kwa uzembe katika kitengo cha sheria cha BoT kwa maelezo kwamba taarifa hizo hazina ukweli kutokana na usimamizi unaofanywa na menejimenti yake.
“Hili suala liliibuka kwenye kamati za Bunge baada ya hesabu kuonyesha kwamba kuna matumizi makubwa katika hizi kesi na kutokana na mazingira kubadilika ikaonekana sasa tubadili mwelekeo. Tulikubaliana na maagizo ya Bunge na sasa tunayafanyia kazi,” alisema.
Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kutoka ndani ya BoT kwamba baadhi ya kesi zimekuwa zikifunguliwa kwa malengo na maslahi binafsi ya baadhi ya maofisa wa benki hiyo, hali iliyowashitua baadhi ya wabunge ambao walitaka maelezo kutoka kwa uongozi kabla ya kufikia uamuzi wa kupendekeza kesi zisizo na tija kufutwa.
Katika tuhuma hizo, inadaiwa kuwa baadhi ya maofisa hao wa BoT wakiwamo baadhi ya wanasheria wamekuwa wakibuni kesi na kuhakikisha zinasimamiwa na kampuni za uwakili binafsi ambazo baadaye huandaliwa malipo makubwa na BoT.
Sehemu ya malipo hayo makubwa yanayofanywa kwa kampuni hizo za uwakili ambazo baadhi zinahusisha wanasiasa wanasheria, yamekuwa yakigawanywa na sehemu ya mgawo kurejeshwa kwa maofisa wa BoT waliofanikisha ‘mchezo’ huo wa kifisadi.
