KIPENGA cha kuomba kuwania ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM kimepulizwa lakini baada ya ‘mpira’ kuanza kumekuwa na kelele nyingi za wachezaji kuchezeana rafu.
Kwa mfano habari kutoka Sumve, mkoani Mwanza, zinadai kwamba mbunge anayemaliza muda wake, Richard Ndassa alizichapa kavukavu na mgombea mwenzake Dk. Paschal Mbelule wakiwa kwenye gari lao la kampeni.
Wakati huko Sumve inadaiwa wagombea walizipiga kavu kavu, mjini Arusha kuna madai kwamba Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Jubilate Kileo alizabwa vibao akituhumiwa kuwabeba baadhi ya wagombea.
Hilo la viongozi wa maeneo husika wa CCM na Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kudaiwa kuwabeba baadhi ya wagombea limelalamikiwa katika majimbo kadhaa.
Wapo wagombea waliosusa kuendelea na mchakato wa kujinadi baada ya kujiona ‘si wateule’ wa uongozi wa wilaya na UVCCM na wapo walioandika barua rasmi za kulalamikia jambo hilo.
Nayo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), imekuwa ikiripotiwa kuwanasa wagombea kadhaa kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wapiga kura za maoni.
Haya yanayotokea katika mchakato wa CCM wa kutafuta wanachama wake wa kugombea ubunge na udiwani yanasikitisha mno kwa kuzingatia ukubwa wa chama na heshima iliyonayo katika historia ya nchi yetu.
Ni uthibitisho wa kutosha kwamba hata huko nyuma mchakato huu ulijaa rafu ambazo nyingi zilipita bila ya kupigiwa filimbi kutokana na kutokuwapo kwa utaratibu huu wa sasa ambao ni wa wazi unaobaini vitu vingi vya ovyo vinapofanywa.
Pia hakuna shaka yoyote kwamba tunashuhudia vitimbwi vya ziada katika mchakato huu wa CCM kutokana na kuwapo kwa sheria ya Gharama za Uchaguzi ambayo imefanya TAKUKURU kuwa macho mno na kusanasa wagombea kadhaa kwa kukiuka sheria hiyo.
Ndiyo kusema kwamba ni mchakato mbovu wa CCM uliokuwapo wa kupata wagombea wa ubunge na udiwani ndio uliokuwa unafanya taifa letu lijikwae kiasi cha kupata baadhi ya viongozi ambao hawazingatii maslahi ya taifa?
Si rahisi kulijibu swali hilo kwa usahihi lakini ni imani yetu kwamba uwazi uliopo sasa katika mchakato wa CCM unasaidia kupembua pumba na mchele ili kupata viongozi bora wa kulisukuma mbele taifa letu.
Tunautakia kila la heri mchakato huu ili hatimaye viongozi watakaopitishwa ni wale ambao ni wasafi kweli kwa vitendo na kauli zao, watakaoifanya Tanzania iwe nchi salama na yenye neema kwa Watanzania wote.
