KING Majuto alimpenda binti wa mtaa fulani lakini alishindwa kwenda na kumwambia juu ya hisia zake hizo. Alibakia akimwangalia kwa mbali tu na kuwaza na kumfikiria. Siku moja alimwambia rafiki yake jinsi anavyompenda binti huyo lakini hakuwa na ubavu wa kumwambia.
Rafiki, ambaye naye katika fani hiyo hakuwa mahiri sana, alimshakizia King Majuto kuwa akaze moyo na kwenda “kumtamkia” maneno ya mapenzi na litakalofuata, basi, ndilo litakalokuwa.
King Majuto siku moja aliamua kukata mzizi wa fitna na kujipeleka hadi mlangoni kwa binti yule. Alipokaribishwa na kumtia machoni binti yule, Majuto nguvu zikamuishia akayeyuka kama mshumaa kwenye makaa ya moto!
“Nikusaidie nini?”, binti akauliza kwa sauti ya upole akimuangalia usoni Majuto. Majuto akageuza macho kuangalia pembeni.
Majuto: “Samahani dada”.
Msichana: “Bila ya samahani, una shida gani”?
Majuto: “Dada mimi nina shida”.
Msichana: “Ndiyo nimekusikia, shida gani?”
Majuto: “Dada, hapa kwenu mwauza mbuzi”?
Dada wa watu akashangaa maswali ya mbuzi yametoka wapi tena wakati hakuna mbuzi kafungwa kamba nje, na wala hakuna uwezekano hata wa kuwa na banda la kuku!
“Mbuzi? Hapana, hatuuzi mbuzi”, dada akamjibu na Majuto akaitikia: “Asante dada.”
Kisha Majuto, huko vidole akijiumauma mdomoni kama mwali, akagangamala na hatimaye kupata nguvu: “Dada mimi nakupendaaaa!”, akasema kwa hamasa huku mguu ukiwa kisogoni. Akatimka bila ya hata kusikiliza majibu!
Alipoenda kwa rafiki yake akamtambia kuwa ‘amemwimbisha’ binti naye akaingia laini. Akatamba kuwa alimsemesha maneno matamu hadi binti ameamua kumualika aende pale jioni kwa chakula. Wanaokumbuka kisa hiki cha zamani (classic) cha Majuto wanajua kiliishaje.
CCM na tunu ya demokrasia ni sawa na Majuto na yule binti aliyempenda. CCM imekuwa ikitamba kuwa inapenda na kuheshimu demokrasia na viongozi wake hulitumia neno “demokrasia” kwa urahisi kabisa wakijionyesha kuwa bila ya wao demokrasia isingekuwepo nchini.
Ukiwasikiliza mara kwa mara unaweza kabisa kuamini kabisa kuwa demokrasia na CCM ni sawa na pacha wanaofanana.
Niruhusuni kurejea maneno ya Rais Kikwete katika hotuba yake wakati akilivunja Bunge ili kukaribisha mchakato wa kuelekea Uchaguzi Mkuu. Rais Kikwete akizungumzia Demokrasia alisema:
“Nchi yetu imeendelea kuwa kielelezo kizuri cha utulivu wa kisiasa na ukomavu wa demokrasia barani Afrika. Katika miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuhakikisha kwamba uhuru wa kisiasa, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kuabudu unaheshimiwa na kulindwa. Tumehakikisha kwamba wanasiasa pamoja na vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali na wananchi wote kwa ujumla wanafaidi haki zao za msingi.
“Tumefanya jitihada ya kuhakikisha kwamba uwanja wa ushindani wa kisiasa unakuwa sawia zaidi. Kwa ajili hiyo, tumefanya Marekebisho ya Sheria zetu za Uchaguzi na tumetoa ruzuku kwa vyama vya siasa vyenye madiwani kuanzia mwaka 2007. Hali hii imedhihirisha ukomavu wa kisiasa nchini.”
Maneno hayo ya kutia moyo yanafurahisha hisia, yanavutia usikilizaji na kwa upande mwingine yanatuma ujumbe kuwa “mimi dada nakupenda”. Ni maneno yenye kumfanya msikilizaji achanganyikiwe kidogo na hata kuweza kutoa ukaribisho wa chakula cha jioni au zaidi. Lakini kuna tatizo, tena tatizo kubwa tu.
Naomba mniruhusu nifyatuke kidogo tu.
Tatizo la CCM na serikali yake linapokuja suala la demokrasia, ni kuwa wanaiogopa kama gunia la misumari. Wanaisifia kuwa imestawi, wanatuonesha uwepo wa vyama “vingi” na chaguzi mbalimbali kuwa ni dalili ya ukomavu wa demokrasia. Lakini ukisogelea kwa ukaribu utaona ni jinsi gani wanaiogopa demokrasia ya kweli. Ndugu zangu, demokrasia ya kweli ni ile inayotoa uwezekano wa mtu kushindwa uchaguzi kwa haki.
Hii maana yake ni kuwa kwenye demokrasia ya kweli au mahali ambapo demokrasia ya kweli inajaribiwa kujengwa, mifumo na taasisi mbalimbali inakuwepo ili kuhakikisha kuwa mtu anaposhindwa katika uchaguzi, basi, hakuna sababu ya mtu kulia uchawi na pale panapotokea dhuluma katika uchaguzi, basi, inashughulikiwa kwa haraka na kwa uthabiti ili kuondoa hofu yoyote ya kupendelewa au kuonewa.
Lakini katika Tanzania yetu, mfumo uliotengenezwa ni ule wenye kufanya kushindwa kuwe ni kitu cha ajabu mno. Mara nyingi bado sijasikia mtu anashindwa akaridhika kuwa ameshindwa kihalali. Karibu mara zote wanaoshindwa hulalamikia rushwa, kubebwa, mfumo mbaya n.k .
Lakini naweza kwenda mbali zaidi na kudai kuwa mfumo umetengenezwa ili kufanya iwe vigumu sana kwa CCM kushindwa kwa haki.
Nichukulie mifano michache tu ya kuonesha hili. Kwanza, mfumo wa kumpata mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM ni mfumo ambao umeoneshwa tena kuwa si wa kidemokrasia na ni mfumo ambao unaonekana kufuatwa na vyama vya Upinzani vile vile.
Sielewi kuna maana gani kumlilia mtu mmoja awe mgombea pekee ndani ya chama badala ya kutengeneza mazingira ambapo wagombea mbalimbali wanajitokeza na yule atakayeshinda katika utaratibu huru na wa haki anakuwa ni mgombea. Matokeo yake wanaimba “demokrasia demokrasia” huku wanatumia vitisho, kejeli na dharau kumtisha mtu mwingine yeyote anayetaka kugombea dhidi ya Kikwete ndani ya CCM.
Si kwamba mtu huyo angeweza kumshinda Kikwete, la hasha; bali angeweza kusababisha Kikwete asishinde kwa kura “nyingi” zaidi. Matokeo yake wamejitengenezea mifumo miwili – ule wa kipindi cha mwisho cha miaka kumi ya Rais aliyepo madarakani na ule wa kipindi cha kwanza cha Rais mpya.
Hivyo, Mkapa alipogombea mara ya pili 2000 hawakuruhusu wagombea wengine wampe changamoto, na hivyo akapitishwa na kuwa mgombea pekee ndani ya CCM, lakini ilipofika mwaka 2005 wakakumbuka dhana ya demokrasia na kufungulia uwanja kwa watu wengine!
Na hivyo ndivyo watakavyofanya itakapofika 2015 ambapo kwa mara nyingine hata ambao wangeweza kuwa marais mwaka huu watajitokeza! Hii ni kejeli kwa demokrasia.
Pili, angalia utaratibu waliojiundia wa “kura za maoni” za kupata wagombea wa udiwani, uwakilishi na ubunge. Kama kuna kitu kinanikera kwamba kinatukanisha demokrasia ni huu utaratibu wa kura za maoni ambao kwa kweli ungefaa utumike huko Burma, Vietnam au China!
Yaani, kura za maoni zingekuwa zimenoga kama ushindani wa kweli wa kisiasa ungeruhusiwa kuanzia huko chini, huku kila mgombea anayetaka kugombea anatumia nafasi yake kwa uhuru huku serikali ikihakikisha tu kuwa rushwa haitumiki au hujuma hazifanyiki na kuwa amani na utulivu unadumishwa.
Leo hii, hata kushangilia wagombea wao wananchi wanazuiwa; huku hofu ya TAKUKURU imetanda kiasi kwamba mtu anaogopa kuonekana anashikana mikono kusalimiana na mtu mwingine. Hii nayo ni kejeli ya demokrasia. Wenyewe wanafikiri wanaimarisha demokrasia kumbe wanachofanya ni kituko cha demokrasia.
Nimesema hapo juu demokrasia ni lazima iweke nafasi ya watu kushindwa. Lakini kwa mtindo huu ambao wagombea wanaburuzwa kwenye gari moja kuwekwa kwenye mkutano mmoja, utamu wote wa shamrashamra za uchaguzi na kura ya maoni zinaondolewa.
Imefika mahali wagombea wa CCM wanafuatana utadhani kondoo wanaopelekwa machinjioni! Wanatoka kata hii wanaenda kata ile, hakuna mbiu, hakuna ngoma, hakuna shamra shamra wenyewe wanafikiria ni demokrasia! Wakiambiwa zungumzeni demokrasia ya kweli wanabakia “ooh hapa mnauza mbuzi?”!
Hata hizo kura za maoni zenyewe hazina umaana wowote kwa sababu siku ya mwisho watakaotangaza kwa uhakika nani kashinda ni kikao cha Kamati Kuu! Yaani, katika “demokrasia” ya CCM, kura za maoni za wana CCM hazikubaliki hadi ziweke mikono na kufukiziwa ubani na Kamati Kuu.
Kama kweli CCM ingekuwa inaheshimu kanuni za demokrasia, basi, maamuzi ya kura za maoni yangekuwa ya mwisho na atakayeshinda ameshinda, atakayeshindwa ameshindwa! Lakini demokrasia ya CCM ni sawa na King Majuto na kipenzi chake!
Aidha, fikiria jambo la tatu. Rais Kikwete na serikali yake wamejitapa kuwa wanathamini demokrasia kweli. Lakini ukiangalia kwa karibu utaona kuwa kama kweli wanathamini demokrasia, hii sheria yao ya “gharama za uchaguzi” waliipitisha vipi?
Nilipoikosoa sheria hii mwanzoni, watu wakaniona kama nina wazimu na nikasema mapema kuwa ni sheria mbaya. Lakini CCM ikaishangilia kuwa sheria nzuri hadi unapofika wakati huu wa kura za maoni na mtaona ya ajabu zaidi kwenye kampeni zenyewe!
Hadi hivi sasa kuna mambo ambayo yamefanywa na CCM na uongozi wake ambayo yanavunjavunja sheria hii kabisa, na nina uhakika zaidi ya kupewa maonyo hawawezi kupelekana mahakamani; vinginevyo watajikuta wanatakiwa kumpeleka mahakamani hadi Rais mwenyewe!
Naweza kuandika juu ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inatakiwa kusimamia demokrasia ya vyama vya siasa wakati yenyewe haina uhuru unaohitajika na matokeo yake kimekuwa chombo cha CCM. Wanaweza kukataa na kuapa kwa mizimu yao kwamba ofisi yao iko chini ya Waziri Mkuu na chini ya Waziri (mteuliwa wa Rais) ambaye ni mbunge wa kuchaguliwa, na hivyo haiwezi kusimamia demokrasia ya kweli. Naweza kusema hilo vile vile kwenye Tume ya Uchaguzi ya Taifa mambo ni yale yale, siyo chombo huru.
CCM haiwezi kuhimili demokrasia ya kweli. Haiwezi kuruhusu ushindani wa kweli ndani ya chama na nje yake. Haiwezi kujenga mfumo ambapo itaweza kushindwa yenyewe. Hivyo, kwa muda mrefu imetengeneza geresha ya demokrasia kwa kuchanganya kanuni za kidemokrasia na zile za utawala wa chama kimoja. Matokeo yake demokrasia huonekana ni demokrasia pale tu ambapo maslahi ya CCM yanalindwa.
Kwa CCM demokrasia ya kweli ni kama dawa ambayo inaweza kutibu lakini vile vile inaweza kusababisha matatizo kwa watumiao. Demokrasia ya kweli haiwezi kufuatwa na CCM kwani ikifuatwa kweli kweli itatengeneza uwezekana wa baadhi ya watu kuanguka katika chaguzi mbalimbali (pamoja na hara Rais wa wakati huo) na vile vile uwezekano wa chama chenyewe kushindwa uchaguzi.
Hivyo; tunaposubiri kuona watu wakipiga kura, kitu ambacho ni kidogo zaidi katika demokrasia, hatuna budi kutambua kuwa mfumo na muundo mzima wa utawala wa kidemokrasia umezimuliwa kama mtu anayezimua pombe kwa maji.
Hatuwezi kujitapa ati kuna demokrasia wakati kilichobakia ni mazingaombwe ya demokrasia. Hapa ndipo na mimi kama Majuto inabidi nitimke kabla sijasikia majibu!

Barua-pepe: