WIKI iliyopita kulikuwa na habari nzito katika duru za siasa Tanzania: Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa alitangaza rasmi kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Mnamo Aprili 29, 2009 niliandika, katika safu hii, makala ya kumtia moyo Dk. Slaa kuendelea na mapambano yake bungeni iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka: “Songa mbele Dk. Slaa, usikate tamaa”.
Kwa kuzingatia tukio hilo la wiki iliyopita la Dk. Slaa kujitosa kwenye patashika ya kuwania urais, nimeshawishika kuirejea leo makala yangu hiyo ya mwaka jana; ikiwa ni njia ya kumtia moyo na kumtakia kila la heri. Katika sehemu ya makala hiyo ya mwaka jana niliandika hivi:
“Did you ever know that you are my hero?”, ni maneno yaliyomo kwenye wimbo maarufu wa mwanamuziki Bette Midler wa Marekani. Sina hakika ni mazingira gani yaliyomsukuma Midler kutunga wimbo wenye hisia kali kama huo; ila nina hakika ulilenga katika kumfariji na kumtia moyo ‘shujaa’ wake huyo.
Ingawa wimbo huo ni wa mapenzi, ninapenda kuazima maneno yake kutuma ujumbe kwa Mbunge wa Karatu (CHADEMA), Dk. Wilibroad Slaa); kwani ni shujaa wangu wa kisiasa wa sasa. Natuma ujumbe huo kumfariji na kumtia moyo kwa misukosuko anayoipata Bungeni.
Did you ever know that you are my hero? (Unafahamu kwamba wewe ni shujaa wangu?) Kama ulivyo mchapo kwenye video ya wimbo huo ambapo mlengwa anamjibu Midler kwa kusema: “No need for me to know, Iam everybody’s hero” (Si muhimu kujua, mimi ni shujaa wa watu wote), Dk. Slaa naye anaweza kunijibu hivyo hivyo; maana, kwa hakika, ni shujaa wetu sote!
Binafsi, sijapata kukutana na kuzungumza na mbunge huyo wa Karatu, lakini, kama Watanzania wengine, nimekuwa nikifuatilia kwa karibu kazi zake kama mbunge, na nikiri kwamba zimenisisimua.
Kwa hakika, kama ungeniuliza ni mwanasiasa yupi nchini anastahili kutunukiwa, mwaka huu, tuzo ya heshima ya Martin Luther King Jr, ningemtaja mbunge huyo wa Karatu. Kama mbunge Anne Kilango (CCM) alituzwa na Wamarekani kuwa mwanamke shujaa wa mwaka, basi, heshima kama hiyo kwa upande wa wanaume inamstahili Dk. Slaa.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Dk. Slaa amewaongoza wabunge kadhaa nchini kubadilisha kabisa mwelekeo wa uwajibikaji wa watawala wetu Tanzania. Aidha, amehangaika huku na kule nchini, ndani na nje ya bunge, kuwaamsha wapiga kura usingizini ili wawatathmini watawala wao (siwaiti viongozi) wakiwa na upeo mkubwa wa ufahamu.
Ninadiriki kusema kuwa hata kuwepo mahakamani, hivi sasa, kwa kesi za ufisadi za EPA na Twin Towers, ni matunda ya kazi ya kupambana na ufisadi ya Dk. Slaa na wenzake kadhaa pamoja na vyombo vya habari.
Kwa ufupi, kwa kazi nzuri iliyofanywa na Dk. Slaa na wabunge wenzake kadhaa (wakiwemo wa CCM), siasa za Tanzania kamwe hazitabakia vilevile zilivyokuwa miaka mitano iliyopita.
Lakini katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Dk. Slaa amejijengea maadui wengi ndani na nje ya bunge. Na hilo lilitarajiwa. Huwezi kupambana na ufisadi wa aina ya EPA, Deep Green, Meremeta, BOT Twin Towers, Richmond, Kiwira nk , na kisha usijizolee maadui kibao miongoni mwa wenzetu wasiojali umasikini wa wenzao wengi. Haiwezekani.
Ni maadui wake hao ambao sasa wanasaka usiku na mchana njia ya kummaliza kisiasa; huku wakiomba siku moja ateleze na kutumbukia katika skandali kubwa wapate kuitumia kummaliza; kwani hizo za nyuma walizomhusishanazo (ikiwemo ya ufuska), zimeshindwa kummaliza.
Ndugu zangu, hivyo ndivyo nilivyoandika kuhusu Dk. Slaa zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Na kwa kuwa wiki iliyopita alitangaza kuwania urais wa Tanzania, nashawishika kusisitiza tena kwamba siasa na kampeni za urais za Tanzania hazitakuwa kama zilivyokuwa miaka 15 iliyopita!
Nadiriki kusema kwamba, kwa mara ya kwanza tangu tuingie katika mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, CCM imepata ‘saizi yake’ katika kinyang’anyiro cha urais. Ni imani yangu kwamba Dk. Slaa atatoa changamoto kwa mgombea wa CCM ambayo hatujapata kuiona kwa miaka mingi.
Tofauti na wagombea urais wa upande wa Upinzani ambao tumepata kuwanao katika chaguzi zilizopita (Mrema, Lipumba, Mbowe, Dk. Sengondo Mvungi nk), Dk. Slaa yeye anaingia katika kinyang’anyiro hicho akiwa na rekodi safi ya utendaji jimboni na hata ndani ya Bunge.
Kama, kwa sasa, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu ndiyo mfano wa kuigwa nchini wa halmashauri zinazochacharika kuwaletea wananchi wake maendeleo makubwa, ni kwa sababu ya mchango mkubwa wa Dk. Wilibroad Slaa akiwa mbunge wa jimbo hilo na halmashauri ya Karatu ikiwa imejaa madiwani wa CHADEMA.
Kama leo bunge letu limechangamka na limesimama kidete kupambana na ufisadi nchini, ni kwa sababu ya kuwa na wabunge waliojitolea “kufa kidogo” kutetea wanyonge. Na katika orodha hiyo ya wabunge, Dk. Slaa yu namba moja.
Kwa ufupi, Dk. Slaa anagombea urais akiwa tayari amethibitisha kwa vitendo (na mifano ipo) uwezo wake, ujasiri wake na wito wake wa kuwatetea wanyonge wa nchi hii.
Wakati Rais Kikwete anajitosa kuwania urais mwaka 2005, hakuwa na rekodi yoyote ya kujivunia ya utendaji uliotukuka wa kuwakomboa wanyonge; licha kwamba alishika uwaziri katika wizara nyeti kama vile Fedha, Nishati na Madini (alikuwa waziri kipindi cha skandali ya mradi wa umeme wa IPTL).
Lakini Dk. Slaa anaingia katika kinyang’anyiro cha urais akiwa tayari na rekodi ya utendaji wa kutukuka jimboni kwake Karatu, na hata ndani ya Bunge; rekodi ambayo Kikwete hakuwanayo mwaka 2005; achilia mbali kina Mrema, Lipumba, Mbowe, Dk. Sengondo Mvungi nk walipokuwa wanawania urais.
Sasa, sisemi kwamba Dk. Slaa atashinda na kuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. La hasha. Chini ya mfumo wa sasa wa uchaguzi na chini ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo si huru, itakuwa ‘maajabu’ Dk. Slaa kumshinda Kikwete, Oktoba 2010!
Ninachosema hapa ni mambo mawili. Kwanza, kwamba Dk. Slaa ataleta changamoto kubwa kwa Kikwete na kwa wagombea ubunge wa CCM huko majimboni. Hilo ni muhimu; kwani linaweka mazingira ya kupata mshindi wa haki siku uchaguzi wetu utakapokuwa huru na wa haki chini ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (usiniulize lini!).
Pili, kwa sababu ya changamoto hiyo, Dk. Slaa anaweza kuusaidia Upinzani kushinda majimbo mengi, na hivyo kuongeza idadi ya wabunge wao bungeni. Hilo pia ni muhimu katika kuibana Serikali yetu ndani ya Bunge; Serikali ambayo inabweteshwa na wingi wa wabunge wa CCM.
Lakini la mwisho ni kwamba; kwa kujitosa kuwania urais, Dk. Slaa anaweka rekodi (kumbukumbu) kwa vizazi vijavyo kwamba hakutaka kuishia tu Karatu au bungeni tu; bali alitaka kukitumia kipaji chake cha uongozi kuwakomboa wanyonge wote Tanzania akiwa rais, lakini mfumo wetu wa uchaguzi haukumpa fursa hiyo.
Kwa maneno mengine, Dk. Slaa hatashinda uchaguzi wa Oktoba 2010, lakini historia itamtetea kwamba alijaribu, na alikuwa na kila sifa ya kuwa rais katika uchaguzi huo, lakini mfumo mbaya tulionao haukumruhusu kuwa hivyo.
Vyovyote vile; naamini Dk. Slaa anasafisha njia ya urais kwa ukombozi wa baadaye (narudia tena, usiniulize lini!), na ukombozi huo unaweza kupatikana wakati yeye pengine ameshastaafu siasa.
Nihitimishe kwa kusema kwamba, kwa mara nyingine, nadiriki kumwambia Dk. Slaa asonge mbele, na asikate tamaa.
Urais au bila urais, bado atabakia shujaa wangu katika duru za siasa nchini labda abadilike kiuadilifu. Did you ever know that you are my hero? Kwa hakika, wewe ni shujaa wa wanyonge Tanzania!
Ndugu zangu, nimeshawishika kuyaweka haya wazi mapema kuhusu Dk. Slaa kabla kampeni za urais hazijaanza rasmi; maana zitakapoanza Agosti sitakuwa na haki ya kitaaluma ya kuandika hayo; kwani yapo maadili yanayoiongoza taaluma yetu wakati wa kipindi cha kampeni; nami nayaheshimu.
Tafakari.

Barua-pepe: