KAMPENI ndani ya vyama vya CCM na CHADEMA kwa wanachama wake kuomba ridhaa ya vyama vyao kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali mkoani Mbeya, zimeanza kwa kishindo; huku watu wakishuhudia vituko mbalimbali kuanzia baadhi ya wanachama wa CCM kukamatwa kwa tuhuma za rushwa hadi wagombea kususia vyakula.
Lakini kubwa katika yote ni hasira na jazba miongoni mwa wagombea wa CCM wilayani Kyela zilizosababisha mitafaruku hadi kuahirishwa kuanza kwa kampeni hizo na hatua ya mmoja wa wagombea kwenye kampeni za CCM wilayani Kyela kupingana hadharani na Katibu wake wa Mkoa, Verena Shumbusho kuhusu sababu za kuahirishwa kuanza kwa kampeni za chama hicho wilayani humo.
Wakati Katibu huyo wa Mkoa wa Mbeya akidai kuwa kilichosababisha kuahirishwa kwa siku moja kuanza kwa kampeni za uchaguzi wilayani Kyela ni dosari ndogo ndogo alizozitaja kuwa ni pamoja suala la magari na mafuta, mgombea, George Mwakalinga alipinga akisema sababu ya kuahirisha ni usambazaji kadi feki.
Mwakalinga anaitumia kasoro hiyo kujinadi akibainisha kwamba yeye ndiye aliyesababisha kuahirishwa kwa kampeni hizo na anaenda mbali zaidi akisema hata Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Lwidiko Nong’ona pamoja na msaidizi wake, Epmark Makuya, wameondolewa kwenye msafara wa kampeni baada ya yeye kuwakataa akiwatuhumu kuhusika na kashfa hiyo.
Kugoma kwa baadhi ya wagombea kuanza kampeni wilayani humo kulilazimisha sekretariati nzima ya CCM, ikiongozwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, kwenda wilayani humo.
Wajumbe wengine wa sekretarieti hiyo waliokuwepo Kyela ni Katibu wa Wazazi, Ernest Machunda, Mwenyekiti wa Vijana Reginald Msomba, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa, Mwashibamba na Athuman Sampa.
Hatua ya George Mwakalinga kutumia suala la kadi feki kwenye kampeni zake iliwachochea wananchi kumhoji kwamba iwapo anatoa tuhuma hizo, basi, awataje anaowatuhumu kusambaza hizo kadi.
Wanachama hao walienda mbali zaidi kwa kuhoji undumilakuwili wa Msimamizi wa Kampeni, Thabit Mzomozi kwamba amewakataza wasiulize maswali yao kumlenga mtu, lakini wakati huo huo maelezo ya mgombea George Mwakalinga yakiwa bayana kumlenga mtu; hoja iliyojibiwa na msimamizi kwa kusema:
“Wagombea walishaelezwa kipi cha kuongea na kipi si cha kuongea, hilo tumeliona na tunalifanyia kazi, lakini hapa hata yeye mwenyewe anajua anajiwekea tiki wapi.”
Mfanyabiashara na aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz pamoja na Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, hawakupona kwenye mashambulizi yake. George Mwakalinga aliwatuhumu wafanyabiashara hao akidai wanawapigia chapuo baadhi ya wagombea wenzake, hatua iliyotafsiriwa ni kujisafisha kutokana na yeye mwenyewe kwa muda mrefu sasa kutajwa kuwa miongoni mwa wagombea waliopelekwa jimboni humo na mtandao wa mmoja wa wafanyabiashara wakubwa nchini.
Wengine waliokabiliwa na maswali magumu katika siku ya kwanza ya kampeni hizo ni pamoja na Elius Mwakalinga aliyeulizwa alishirikiana vipi na mbunge aliyekuwepo ili awashawishi wamchague; naye akajibu alishirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya; ingawaje kabla ya kujibu Msimamizi alilizuia akidai halitokani na maelezo ya mgombea.
Yote hayo tisa, kumi ni pale wagombea wanne waliposusia chakula kilichoandaliwa na chama chao katika mgahawa wa New Karama uliopo Kasumulu wilayani humo kwa madai ya kuhofia usalama wao.
Tukio hilo lilianza baada ya wagombea wote watano kuingia kwenye mgahawa huo kwa ajili ya kupata chakula cha mchana; kisha mmiliki aliyefahamika kwa jina la Karama Mohamed kumkumbatia mbunge aliyemaliza muda wake, Dk. Harrison Mwakyembe na kumweleza kuwa asihofu kwani hana mpinzani.
Kauli hiyo ya Mohamed ilijibiwa na mmoja wa wagombea, Elius Mwakalinga kwamba atasemaje kuwa hana mpizani wakati wao wapo, na katika jibu ambalo hakulitarajia alijibiwa kwa kuambiwa: “Wewe si vuvuzela tu”, kauli iliyomchafua na kutoka nje akifuatiwa na wenzake watatu hivyo kumwacha Dk. Mwakyembe na baadhi ya viongozi na wanachama waliokuwemo kwenye msafara huo, kuendelea na chakula.
Minyukano ya wana CCM iliendelea katika majimbo mengine likiwemo la Mbeya Mjini ambako wagombea wakiwa katika Kata ya Sisimba, Jijini Mbeya, mwanachama mmoja aliingilia kati swali lililoulizwa na mwenzake akiwashutumu kuendesha kampeni chafu kwenye mkutano huo dhidi ya mbunge aliyemaliza muda wake, Benson Mpesya.
Mwanachama huyo (jina tunalo) alilazimika kuingilia kati swali lililoulizwa na mwanachama mwenzake ambaye ni diwani wa viti maalumu aliyemaliza muda wake na amepitishwa tena katika nafasi hiyo na akidaiwa vile vile kuwania ubunge viti maalumu kupitia chama hicho, ambapo alimtaka mbunge huyo kutoa sababu za kata yao kutokuwa na shule ya sekondari kama ilivyo kwa kata zingine, na ndipo mwanachma huyo aliposimama na kusema:
“Tusiwe wanafiki na kumbebesha lawama mtu asiyehusika. Shule tulikataa wenyewe tulipoletewa wazo la kuiboresha Shule ya Msingi Azimio ili iwe sekondari, tena tulikataa kwenye mkutano, leo tunataka kumtupia lawama mtu mwingine. Hapana, myonge mnyongeni haki yake mpeni.”
Msimamo wa mwanachama huyo uliungwa mkono na wenzake wengi tu waliohudhuria mkutano huo, ambao waliendelea kujadiliana wakimshutumu muuliza swali; huku wakifichua madhambi yake mengine yanayohusiana na harakati za uchaguzi zinazoendelea.
Pangine kwa kutoufahamu utamaduni wa wananchi wa Mkoa wa Mbeya, baadhi ya wagombea katika Jiji hilo walijikuta katika wakati mgumu pale wanachama waliposimama na kuwaeleza bayana kuwa wanaonekana kutoelewa wanachokiomba kutokana na kujikita kwenye kuelezea jinsi wanavyoendesha taasisi zao zisizo za kiserikali (NGOs) ambazo kwa wakazi wengi wa jijini humo huziona kuwa zipo kwa maslahi binafsi ya wamiliki kuliko jamii kama wanavyodai.
Hali sio shwari vile vile kwenye kinyang’anyiro cha ubunge viti maalumu mkoani Mbeya ambapo kampeni zake zinaelezwa kutawaliwa zaidi na madai ya rushwa na kashfa zinazoelekezwa zaidi kwa mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo ambaye anaonekana kuwa kikwazo kwa baadhi ya wanawake wanaowania nafasi hiyo.
Baadhi ya wanachama wanawake katika Wilaya za Mbeya na Kyela (majina tunayo) waliliambia Raia Mwema kuwa wagombea wawili wa nafasi hiyo (majina tunayo) kwa kusaidiwa na wapambe wao mkoani huo wanapita kwa wanachama wakiwapandikiza chuki dhidi ya mgombea huyo kwa kumzushia kashfa ambazo sio staha hata kuzieleza.
Katika hali ya kushangaza, baadhi ya wapambe wa wagombea hao wawili wanaotajwa kumchafua mgombea huyo wamo katika orodha ya wananchama wa CCM waliokamatwa na TAKUKURU kwa tuhuma za rushwa hivi karibuni katika Wilaya za Kyela na Mbeya Mjini.
Mbali ya matukio hayo mawili ya wanachama wa CCM kukamatwa na TAKUKURU wakidaiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, baadhi ya wanachama wa chama hicho wanayabainisha matukio mengine kadhaa ya vitendo vya rushwa yanayofanyika, yakiwemo madai ya mgombea mmoja kugawa Shilingi 50,000 kwa kila kata jijini Mbeya na shuka jeupe kwa kila mjumbe wa mkutano utakaochuja wagombea viti maalumu mkoani humo.
Madai hayo yanaenda mbali zaidi kwa kufichua mkakati kupitia vyuoni ambapo baadhi ya walimu walifuatwa kupewa fedha kwa lengo la kuwagawia wanachama wa chama hicho, lakini wakakataliwa baada ya walimu hao kuwashitukia na kuhofia wasije kamatwa na TAKUKURU.
Wakati CCM wakiendelea na minyukano yao, CHADEMA wao walianza Jumapili iliyopita ambapo miongoni mwa mambo yaliyowashangaza wanachama wake ni pamoja na hatua ya Daud Stembela Mponzi kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea ubunge katika Jimbo la Mbeya Mjini.
Mshangao wa wengi unajengwa na historia ya mgombea huyo ambaye katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbeya Vijijini, mwaka jana, aligombea kupitia Chama cha Wananchi (CUF) na kumwekea pingamizi mgombea wa CHADEMA, Sambwee Shitambala hivyo kusababisha kuenguliwa kwake hatua iliyoiwezesha CCM kushinda kwa urahisi.
CHADEMA na wananchi walio wengi mkoani Mbeya wanaamini hadi leo kuwa Shitambala ambaye ni mwanasheria wa kujitegemea alikuwa na nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo kutokana na kukubalika kwake jimboni na ukweli huo ulidhihirika kwa wananchi wengi kususia kupiga kura.
Haikushangaza, hata kwenye mkutano wake wa kwanza, kwa mgombea huyo kuulizwa maswali yaliyomhitaji kuelezea sababu za yeye kuhamahama vyama kila anaposhindwa ambapo baada ya kushindwa CCM mwaka 2000 na 2005 alikimbilia CUF mwaka jana wakati wa uchaguzi mdogo wa jimbo la Mbeya Mjini kabla ya kuhamia CHADEMA hivi karibuni ili ateuliwe kugombea Jimbo la Mbeya Mjini.
Katika kupangua kikwazo hicho, Mponzi alieleza kuwa CUF haikuwa nia yake bali aliombwa na Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba kugombea katika uchaguzi mdogo, jimbo la Mbeya Vijijini, kwa kuwa alikuwa Msafwa; lakini akibainisha kuwa yeye ni CHADEMA na pingamizi aliloweka wakati huo ilikuwa sawa na ndugu wawili wanaocheza timu mbili tofauti, mmoja akiwa mlinzi na mwingine mshambuliaji, mazingira aliyosema huwezi mwachia akufunge kwa sababu ni ndugu yako.
Mponzi alimwekea pingamizi mgombea ubunge wa CHADEMA kwa kujaza Fomu Na. 9B ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inamtaja kwa jina na kuweka saini yake Desemba 28, 2008 na pingamizi hilo kukubaliwa na Msimamizi wa Uchaguzi, Jimbo la Mbeya Vijijini, Juliana Malange.
Aidha, siku za mwanzo za kampeni za CCM mkoani Mbeya zimedhihirisha hofu kubwa miongoni mwa viongozi wa chama hicho kwa waandishi wa habari ambayo, hata hivyo, haieleweki kiini chake.
Uzoefu wa siku za mwanzo za kampeni za CCM umedhihirisha maumivu kwa waandishi wa habari ambapo hunyanyasika hata pale wanapotafuta usafiri wa kwao; kama ilivyotokea kwa mwandishi wa gazeti hili na gazeti la Uhuru huko Kyela ambako walitafutiwa sababu za kuzuia gari lao lisiwepo kwenye kampeni hadi walipoamua kutishia kumpigia Katibu Mkuu, Yusuf Makamba ndipo wakaruhusiwa.
