MALI mbalimbali za Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU), mkoani Mwanza, vikiwamo viwanda, mitambo, magari na viwanja, zimeuzwa kinyemela kwa bei ya kutupwa na fedha za mauzo kupotea katika mazingira tata, Raia Mwema, imethibitisha.
Gazeti hili limebaini kuwa baadhi ya mali hizo zimeuzwa kwa kampuni za vigogo, ambao ni wanasiasa wanaomiliki kampuni za ununuzi wa pamba na wafanyabiashara.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa, sehemu ya mali hizo zilizouzwa kwa wanasiasa na wafanyabiashara hao hazina stakabadhi za malipo ya ununuzi.
Imebainika pia kuwa ufujaji wa mali hizo zenye thamani ya mabilioni ya fedha ndiyo chanzo cha NCU kuwa katika hali mbaya kifedha, kikielemewa kwa mzigo wa madeni na vyanzo vyake vya mapato vikizidi kupungua.
Wakati Raia Mwema ikibaini hayo na wahusika wakuu wakiwa ni uongozi uliopita wa NCU, mmoja wa viongozi hao, alikuwa Jacob Shibiliti ambaye alipoulizwa na gazeti hili kuhusu madai hayo hakuwa tayari kuyazungumzia akidai kuwa yupo kwenye mchakato wa kura za maoni katika CCM, akiwani kuteuliwa kugombea ubunge.
Jacob Dalali Shibiliti sasa ni mwanasiasa, ni kati ya wabunge wa Bunge lililovunjwa mwezi huu na Rais Jakaya Kikwete, anayewania tena kiti cha Jimbo la Misungwi.
Alikuwa Mwenyekiti wa Nyanza kuanzia mwaka 1999 hadi mwaka 2005, akitokea katika kamati iliyokuwa imeundwa na Rais, wakati huo, Benjamin Mkapa, ya kuchunguza pamoja na mambo mengine, matatizo ya Nyanza. Kumbukumbu zinaonyesha kwamba mali nyingi za Nyanza zimeuzwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 na 2005.
Watu waliozungumza na Raia Mwema katika uchunguzi wa matatizo haya ya Nyanza, wanasema kama ushirika huyo unaweza kurejea katika hali yake ya zamani, basi hilo linaweza kufanywa tu na Rais Kikwete kwa kuwa jitihada nyingi zimeshindwa au zinakwamishwa.
Hiyo ni kutokana kwamba hata baada ya kutaarifiwa, Serikali mkoani Mwanza imeshindwa kuingilia kati kukinusuru chama hicho licha ya kujua kwa kinagaubaga kinachoendelea ndani ya ushirika huo.
Hata ahadi kadhaa zilizowahi kutolewa na mawaziri wanaohusika na kilimo na ushirika kwa nyakati tofauti, ikiwamo ya mwaka jana iliyotolewa na Stephen Wasira wakati akifungua mkutano wa NCU na kuahidi kuwashughulikia wote walioifikisha Nyanza hapo ilipo ahadi hiyo imebaki kuwa ahadi.
Habari za uhakika kutoka ndani ya NCU zinasema kuwa mali hizo ama ziliuzwa na uongozi wa NCU au kupigwa mnada kwa maagizo ya Mahakama ili kulipia madeni yake lakini vyote hivyo vilifanyika katika mazingira ya kutatanisha hivyo kusababisha chama hicho kupata hasara kubwa.
Halmashauri Kuu ya NCU (1984) LTD iliyokuwa madarakani kati ya mwaka 1999 hadi 2005, chini ya uenyekiti wa Shibiliti inahususishwa na ubadhirifu mkubwa wa mali za NCU na kukiachia chama hicho katika hali mbaya kifedha na madeni makubwa.
Vyanzo vya uhakika na nyaraka ambazo Raia Mwema inafanikiwa kuziona zinaonyesha kuwa ubadhirifu huo wa kutisha ulibainika pale uongozi mpya ulipoingia madarakani mwaka 2006 baada ya Serikali kuuvunja uongozi wa Shibiliti Oktoba 24, mwaka 2005 kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana japokuwa ni wazi kuwa ilikuwa ni hatua ya kukinusuru chama kwani kilikuwa kinaelekea kufa kabisa.
“Unajua baada ya bodi mpya ya NCU kuingia madarakani na kukabidhiwa mali zake ilikuta union inakabiliwa na madeni makubwa na hata mali nyingine za union hazikuwa katika mpangilio unaofaa hivyo bodi ikaona kuna haja ya kuunda kamati ya kufuatilia mali za union ili kujua zilizopo na zilizouzwa. Na zile zilizouzwa tulitaka kujua kama ziliuzwa kihalali na kwa ridhaa ya bodi au wanachama,” anasema ofisa mmoja wa Nyanza.
Kwa mujibu wa ofisa huyo,
kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wanne ambao ni Mwenyekiti William Bunuma na Katibu Kabindo Bomani; wajumbe wakiwa N’habi Mojo na Emmanuel Malugu.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi ya kamati hiyo ambayo Raia Mwema imefanikiwa kuiona, mali kadhaa za NCU ziliuzwa katika mazingira ya kutatanisha huku nyingine zikiuzwa kwa bei ya kutupa.
Uuzaji wa mitambo
Ripoti hiyo inasema kuwa mwaka 2001, uongozi wa NCU uliuza mtambo wa kukamua mafuta (Expeller Rosedown Mark III na Kettle yake) kwa bei chee ya shilingi milioni nane wakati thamani yake ilikuwa shilingi milioni 80 hivyo kuisababishia NCU hasara ya shilingi milioni 72.
Mtambo huo ulikuwa katika kinu cha kuchambulia pamba cha Nassa (Nassa Ginnery) na ulinunuliwa na kampuni ya Jambo Oil Mill ya Shinyanga inayoaminika kuwa inamilikiwa na aliyekuwa Mbunge wa Meatu katika Bunge lililopita, Salum Khamis Salum.
Aidha, NCU iliuza mtambo kama huo uliokuwa Buchosa Ginnery kwa bei ya Sh. milioni 8.5 wakati bei yake ni shilingi milioni 80. Mnunuzi safari hii alikuwa ni Matondo Oil Mill.
“Wanunuzi wote wawili walipendekeza bei wao wenyewe. Maombi walituma Mei 2, mwaka 2001 na kujibiwa (kwa kukubaliwa) Mei 3, mwaka huo wa 2001. Uongozi uliafiki bei ya mnunuzi ya shilingi milioni nane na shilingi milioni 8.5 kama ilivyo kwenye maombi. Hii inaleta utata mkubwa,” inasema ripoti hiyo.
Uuzwaji wa kiwanda cha kukamua mafuta cha New Era
Utata mwingine unahusu uuzwaji wa kiwanda cha kukamua mafuta ya kula cha New Era Oil Mills kilichopo eneo la viwanda la Igogo, Kitalu Na. 80-84. Kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha madebe 500 ya mafuta ya kula kwa siku kiliuzwa Februari 20, mwaka 2001 kwa kampuni ya Nyanza Gas Oil kwa shilingi milioni 354 wakati thamani yake baada ya kufanyiwa tathmini (valuation) ilikuwa shilingi 629,178,000. Mkutano Mkuu wa NCU ambao ulitoa idhini ya kuuzwa kwa kiwanda hicho ulitaka kiuzwe kwa shilingi bilioni 1.2.
Aidha, inaelezwa kuwa siku kiwanda hicho kinauzwa kwa njia ya mnada kulikuwa na mnunuzi mwingine aitwae M/S Mwenge Enterprises ambaye aliomba akinunue kwa shilingi milioni 580 lakini katika mazingira ya kutatanisha hakuuziwa.
Mbali ya kuuzwa kwa bei hiyo ya kutupwa na kinyume cha taratibu za manunuzi, kamati ilibaini upungufu zaidi ikiwamo kutokuwapo kwa stakabadhi ya fedha kutoka NCU kwenda kwa mnunuzi kuonyesha mauzo ya kiwanda hicho.
Imefahamika pia kwamba hakuna nyaraka zozote kwenye kumbukumbu za makabidhiano ya mali za NCU yanayohusiana na kiwanda cha New Era Oil Mill hivyo kumaanisha kuwa kiwanda hicho hakijakabidhiwa kwa mnunuzi.
Kadhalika, kamati hiyo ilibaini kuwa pamoja na mkataba wa ununuzi kuonyesha kuwa fedha hizo milioni 354 zitalipwa kwa mkupuo, mnunuzi Nyanza Gas Oil hakufanya hivyo na hadi kamati hiyo inakamilisha ripoti yake Julai, 2006, miaka mitano tangu kiuzwe, mnunuzi alikuwa hajalipa fedha hizo.
“Baada ya Kamati kutembelea ili kubaini uhalali wa kuuzwa kwa New Era, mnunuzi alishindwa kuthibitisha ununuzi wa kiwanda hicho na hana hata stakabadhi ya kulipia fedha anayodai amelipa NCU (1984) LTD kupitia benki.
Malipo ya sh milioni 354 anayodai amelipa, kamati imeshindwa kukubaliana nayo kwa vile yanaonyesha ni malipo tangulizi ya ukodishaji wa kiwanda. Kamati imebaini kwamba kiwanda cha New Era bado hakijauzwa na uhamishaji wa milki kutoka ushirika wa NCU kwenda kwa aliyekuwa mkodishaji M/S Nyanza Gas Oil ni batili,” inasema ripoti hiyo.
Kamati hiyo pia ilibaini kuwa zabuni za kukiuza kiwanda hicho haikuvihusu viwanja Na. 80, 81 na 82 kama sehemu ya kiwanda kwani hata mkataba unasomeka kuwa ni viwanja Na. 83 na 84 tu ndivyo sehemu ya kiwanda. Kwa mantiki hiyo, kamati imesema haikuwa halali mnunuzi kupewa viwanja Na. 80, 81 na 82 kama mali yake.
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Raia Mwema umebaini kuwa baada ya kuibuliwa kwa utata huo wa uuzwaji wa New Era, kampuni ya Nyanza Gas Oil ambayo inamilikiwa na mmoja wa wafanyabiashara wakubwa jijini Mwanza, Samson Ng’walida, kiwanda hicho kiliuzwa tena kwa kampuni ya Simon Group Limited ambayo ndiyo inakiendesha hivi sasa. Simon Group ni kundi la wanasiasa na wafanyabiashara linalomiliki viwanda kadhaa vya pamba katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na ya Kati.
Simon Group ni kati ya kampuni zilizopewa na Serikali mgawo mamilioni ya shilingi ili kuhimili mdororo wa uchumi katika kile ambacho huwa kinatajwa na wanasiasa kuwa ni stimulus package. Kati ya wamiliki wanaotajwa wa Simon Group ni pamoja na waziri mmoja kutoka Mkoa wa Tabora.
Kilichokuwa kiwanda cha ASHOCK
Orodha ya mali za NCU ambazo zimeuzwa katika mazingira tata inajumuisha pia mali za kilichokuwa kiwanda cha ASHOCK katika viwanja Na. 11, 11a na 12.
Kamati inasema kuwa thamani ya mali hiyo (viwanja vitatu na majengo ilikuwa milioni 157 wakati mnunuzi M/S Vickfish alitoa shilingi milioni 140 kupitia benki.
Hata hivyo, mnunuzi huyo alitoa tena shilingi milioni 20 ambazo alidai aliombwa na menejimenti ili kufikia thamani halisi ya 157,000,000 kama ilivyothaminiwa na wataalamu lakini hakuna maelezo wala kumbukumbu yoyote juu ya nyongeza hiyo.
Aidha, wakati zabuni hiyo ilihusu viwanja Na 11, 11a na 12 tu mnunuzi alikabidhiwa umiliki wa mali yote ya ASHOCK vikiwamo viwanja vingine sita ambavyo ni 12a, 13, 13a, 14, 14a na 16.
Kiwanda cha mkonge, dengu na kinu cha kusaga nafaka
Kampuni ya Nyanza Gas Oil imeendelea kuhusishwa na kashfa katika ununuzi wenye utata wa mali za NCU, wakati iliponunua viwanda vya mkonge, dengu na kinu cha kusaga nafaka, vilivyopo viwanja Na. 41 na 79 eneo la viwanda Igogo jijini Mwanza.
Thamani halisi ya viwanda hivyo baada ya kuhakikiwa na mthamini mali hadi kufikia mwaka 2003 ilikuwa ni shilingi 266,353,000. Baada ya zabuni yake kutangazwa hakuna mzabuni aliyefikia kiwango hicho cha thamani lakini kamati ya zabuni ya NCU iliamua kuuza kwa mzabuni, kampuni ya Nyanza Gas Oil, kwa shilingi milioni 123.
Hata hivyo, kamati inasema kuwa mnunuzi alishindwa kuonyesha kumbukumbu za malipo hayo aliyodai kafanya kupitia benki. Na kwa upande wa NCU hakuna kumbukumbu za kupokelewa kwa fedha za kununuliwa kwa kiwanda na mali zake kutoka Nyanza Gas Oil.
“Vile vile hakuna kumbukumbu za makabidhiano baina ya NCU na Nyanza Gas Oil. Kamati haikupata mkataba wa kuuzwa kwa kiwanda cha mkonge,” inasema kamati.
Viwanja vya Bwiru
Mali nyingine zilizogubikwa na utata ni viwanja vyake vilivyopo Bwiru kitalu A Na. 75, 77 na 79 na Kitalu B viwanja Na. 80 na 81 kutokuwepo kwenye orodha ya mali za NCU na vimevamiwa na watu binafsi lakini katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza mmiliki wa viwanja hivyo anaonekana NCU.
Kuvunja mkataba wa pamba
Uongozi wa NCU chini ya Shibiliti unadaiwa pia kuwa katika msimu wa mwaka 2003/2004 ulivunja mkataba na wanunuzi wa pamba yao kutoka nje ya nchi na kuisababisha NCU hasara ya dola za Marekani 173,414.35 kama fidia ya kuvunja mkataba kwa kampuni hizo za nje ya nchi.
Mkataba huo ulivunjwa kwa kile menejimenti ya NCU ilichodai kuwa haikuwa na ubora wa kuuzwa nje na badala yake pamba hiyo ikauzwa kwa kampuni ya Nyanza Cotton Oil Ltd.
Malipo ya madeni
Kamati ilibaini kuna wadaiwa wa NCU ambao mali zao zilikamatwa na kupigwa mnada kwa amri ya Mahakama lakini mali hizo ziliuzwa kwa bei ya chini kuliko thamani halisi.
Mali hizo ni pamoja na lori la mdaiwa M/S Milembe Oil Mill Ltd lenye namba za usajili TZC 2565 na tela (trailer) lake lenye namba za usajili TZC 820 ambalo thamani yake ilikuwa milioni 80 lakini liliuzwa kwa shilingi milioni 28 na kwamba siku ya mnada liliuzwa mapema asubuhi kabla ya muda uliopangwa kwa mnada kuanza.
Mali za NCU zilizouzwa kwa utata kufuatia amri ya mahakama
. Transport House
Jengo Transport House lipo Barabara ya Kenyatta Kitalu T, kiwanja Na. 242. Liliuzwa Agosti 4, mwaka 2002 kwa amri ya Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara kutokana na kesi iliyofunguliwa na kampuni ya BP (T) dhidi ya NCU.
BP ilifungua kesi hiyo ya kibiashara Na 49 ya mwaka 2001 baada ya NCU kushindwa kuilipa shilingi milioni 49 ikiwa ni deni la mafuta iliyotumia. Mbali na deni hilo, BP ilitaka Mahakama iamuru NCU kuilipa riba ya asilimia 30 tangu muda wa deni hilo pamoja na gharama za kesi.
Hata hivyo, katika hukumu yake ya Agosti 17, mwaka 2001 Jaji J. Nsekela aliamuru deni hilo kulipwa pamoja na riba ya asilimia 7 kuanzia Novemba 1999 pamoja na gharama za kesi. Kutokana na hukumu hiyo ndipo jengo la Transport House lilipopigwa mnada na dalali, Jibreas Auction Mart and Court Broker.
Utata wa mnada
Wakati ripoti ya Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam (UCLAS) inasema thamani ya jengo hilo ni shilingi milioni 750 kwenye mnada liliuzwa kwa shilingi milioni 72.5 tu mnunuzi akiwa ni mfanyabiashara Antonia Zakaria.
Aidha, mkanganyiko mwingine ni kama mnada wa jengo hilo ulihusu mali zote zilizokuwapo eneo hilo ikiwa ni pamoja na kituo cha mafuta na mitambo, magari na vipuri vilivyokuwa kwenye uwanja (yard) ya eneo hilo.
Uongozi wa NCU unadai kuwa Zakaria ameendelea kuvishikilia vitu hivyo pamoja na kuendesha kituo cha mafuta wakati havihusiki kwenye mnada huo na kwamba hata thamani yake ni kubwa kuliko hata hiyo bei aliyonunuliwa jengo.
Utata zaidi
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na ambayo hata uongozi wa sasa wa NCU unashindwa kuielewa ni hatua ya uongozi uliokwapo kipindi hicho kuilipa BP (T) deni lake shilingi 49,025,514.25 (milioni 49) kupitia akaunti ya BP (T) Na. 01060005419900 iliyopo Standard Chartered na kupewa risiti Na. 92959 ya Januari 12, 2004.
Malipo haya tata yamefanyika ikiwa ni takribani miaka miwili tangu jengo lipigwe mnada kulipia deni hilohilo. Hakuna maelezo yoyote ya kwanini malipo yalifanyika wakati tayari jengo limepigwa mnada na BP imekwishakuchukua fedha zake.
Aidha, haieleweki kwanini BP ilikubali kupokea fedha hizo kwa malipo ya deni ambalo halipo na kama ni malipo ya deni halali kwa nini mali za NCU ziendelee kushikiliwa na mshindi wa mnada wakati NCU haidaiwi tena na BP.
Juhudi za Bodi mpya ya NCU iliyoingia madarakani mwaka 2006 kudai haki yao kisheria sasa ni dhahiri kwamba zimegonga mwamba kwani tayari Mahakama ya Rufaa imetupilia mbali maombi yao mbalimbali likiwamo la kuomba kukata rufaa nje ya muda.
Mahakama hiyo iliridhika kuwa hapakuwa na sababu za msingi za uongozi wa NCU wakati huo (chini ya Shibiliti na Meneja Mkuu Moses Kaseko) kushindwa kukata rufaa au kuonyesha nia ya kukata rufaa kwa wakati muafaka baada ya hukumu kutolewa. Kwa ujumla Mahakama iliona kulikuwa na uzembe wa hali ya juu hivyo kutupilia maombi hayo ya kukata rufaa nje ya muda.
Ghala la Igogo
Ghala hili lipo eneo la viwanda Igogo kitalu A, kiwanja Na.104, lilipigwa mnada Julai mosi, 2007 kutokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza kwa ajili ya kulipa deni la kampuni ya uwakili ya W.K Butambala and Company Advocates ambayo ilikuwa inaidai NCU shilingi milioni 53 zikiwa ni gharama za huduma ya kisheria.
Kwa mujibu wa uthamini uliofanywa na wathamini wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, thamani ya ghala hiyo ilikadiriwa kuwa shilingi bilioni 1.78, lakini ghala hilo liliuzwa kwa shilingi 62,000,000.
Pamoja na NCU kujaribu kufungua kesi kupinga namna ghala hilo lilivyouzwa, juhudi zao zimegonga ukuta.
Mapendekezo ya Kamati
Baada ya Kamati ya Bunuma kukamilisha zoezi la kufuatilia mali za NCU (1984) LTD na kubaini uozo uliokuwapo ilitoa mapendekezo kadhaa kwa uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mwanza.
Kwanza ni kuwachukulia hatua za kisheria viongozi wote waliohusika katika kuhujumu mali za NCU ambao wanatajwa wazi kuwa ni wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Halmashauri Kuu ya NCU ambao ni Shibiliti (Mwenyekiti); John Magulu (Makamu Mwenyekiti); Zena Jacon (mjumbe); Andrew Shikimayi (mjumbe); Sospeter Kaponoke (mjumbe); Bernard Pollycarp (mjumbe na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi) na Mathias Mahumanga (mjumbe).
Kamati ilipendekeza pia kwamba watendaji wanaotuhumiwa nao wachukuliwe hatua za kisheria, hao ni pamoja na: Kaseko, Meneja Mkuu (sasa marehemu); Daniel Lugwisha (Mhasibu Mkuu); Thomas Mugwe (kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani) na George Joseph (Afisa Biashara Mwandamizi).
Ingawa taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mwenyekiti wa NCU Modesta Bulugu iliwasilishwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. James Msekela tangu Julai, 2006 hadi hivi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa kwa wahusika mbali ya kuondolewa kwa watendaji wote waliotajwa.
Juhudi za kumpata Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro kuelezea ripoti hiyo hazikufanikiwa kutokana na kuwa yuko jimboni Kalenga ambako anawania kupitishwa kuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hata hivyo, ofisa mmoja mwandamizi mkoani Mwanza ameliambia Raia Mwema ya kuwa hana hakika kama ripoti hiyo ilimfikia Kandoro.
Meneja Mkuu wa NCU Donat Gabagamba naye amesema kuwa hajawahi kuiona ripoti hiyo tangu aanze kutekeleza majukumu yake NCU mwaka jana hivyo hawezi kuitolea maelezo.
“Nami nasikia tu kwamba kuna kitu kama hicho lakini binafsi sijawahi kuiona labda uende mkoani wanaweza kukupa ‘details’ zaidi na kama kuna hatua zozote zilichukuliwa wao ndio wanajua lakini sisi hapa hatujui lolote,” alisema meneja huyo na kuongeza:
“Hili la Transport House na Ghala la Igogo nalijua kwani tulikuwa tunalishughulikia kisheria, lakini kusema kweli hatuna matumaini sana kwani Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali maombi yetu kwa hatua ya jaji mmoja, tukaomba kwa majaji watatu nao wakatupa maombi yetu sasa tunaangalia kama tunaweza kuomba majaji watano. Lakini wataalamu wa sheria wanatuambia hakuna matumaini.”
Ni kutokana na hali hiyo sasa inaonekana kwamba hatima ya mali hizo za NCU zilizouzwa na kupigwa mnada katika mazingira yenye utata mkubwa pamoja na viongozi waliohujumu mali hizo iko mikononi mwa Rais Kikwete mwenyewe baada ya kuonekana dhahiri kuna kila dalili ya kulindana katika ngazi ya Mkoa na wizarani.
Mjumbe mmoja wa Halmashauri ya sasa ya NCU ameiambia Raia Mwema kuwa uongozi wa chama hicho uliandaa ripoti na kuomba ijumuishwe kwenye Taarifa ya Mkoa iliyotolewa kwa Rais Kikwete alipombelea Mkoa wa Mwanza, Juni mwaka huu, lakini dakika za mwisho uongozi wa Mkoa ‘uliichomoa’ taarifa hiyo kwa sababu ambazo hazikuwekwa bayana.
Wanaushirika wa NCU wanaamini kabisa Rais Kikwete anaweza kukinusuru chama chao kutokana na ufisadi huo ili kwenda na hotuba yake aliyoitoa hivi karibuni wakati anahitimisha Bunge la 9 alipozungumzia hali ya ushirika nchini.
Rais Kiwete alisisitiza kuwa waliohusika na ubadhirifu wa mali za ushirika wanatakiwa washughulikiwe na wasipewe nafasi ya uongozi.
“Sasa sisi tunataka kauli hiyo ya Rais itekelezwe kivitendo hasa kwa upande wa NCU. Isiishie tu pale bungeni na kuonekana ni porojo. Kauli ya Rais ni agizo hivyo tunasubiri hatua zichukuliwe maana hapa mkoani wameshindwa. Na hata Wasira alituahidi kuwa wahusika watachukuliwa hatua lakini mpaka leo ‘wanapeta’ mitaani huku wakitumia fedha za ushirika kujipatia vyeo.
“Hii ripoti ni ya tangu mwaka 2006 na leo tunaelekea 2011, karibu miaka mitano. Iko wazi na vielelezo vipo, ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi? Hivi hata hawa nao ni ‘vigogo’ ambao Serikali inaogopa kuwachukulia hatua? Leo hii Nyanza isingekuwa hapa ilipo.
“Ukiona mali zilivyouzwa kwa bei ya kutupwa utajua ni kwani nini (NCU) inachungulia kaburi. Kwa mali ilizokuwa nazo Nyanza haikupaswa kwenda kuipigia magoti benki ili ipewe bilioni moja au mbili kununulia pamba. Hebu tazama haya mabilioni yaliyopotea kwa kuuza mali ovyo, yangenunua kilo ngapi za pamba?” alihoji mmoja wa viongozi wa sasa wa halmashauri ya NCU.
Mwenyekiti wa NCU Leonard Bugomola anakiri kuwa tangu wawasilishe ripoti yao kwa Mkuu wa Mkoa mwaka 2006 hakuna hatua ambazo zimechukuliwa mpaka sasa na wala fedha kwa ajili ya mauzo ya New Era hazijatolewa.
Anasema Bugomola: “Ni kweli mpaka sasa hakuna hatua zilizochukuliwa na hizo fedha kwa ajili ya kiwanda cha Newa Era bado hatujaziona na nasikia kimeuzwa kwa mtu nwingine. Haya mambo ya ushirika ni magumu sana.
“ Jengo la Transport House linaendelea kukarabatiwa na mali za ushirika zilizokuwa pale zinashikiliwa na mnunuzi pasipo na sababu. Hali hii inawasikitisha sana wana ushirika wetu.
“Mwaka jana wajumbe wa Mkutano Mkuu walitaka kuandamana kwenda kulibomoa jengo hilo lakini tukawaomba wawe na subira kwani mwaka 2005 Rais wetu Kikwete aliahidi kulishughulikia suala hili. Na mara kadhaa amelisemea.
“ Kwa hiyo sisi bado tuna imani kubwa kwamba Rais Kikwete atamaliza suala hili kwani tunajua ni msikivu na anajua kilio chetu cha muda mrefu.
“ Kama Rais wa watu tunajua hili litaisha tu hivyo tunaendelea kuvuta subira kwani haya mambo yako wazi kabisa, si majungu wala kumwonea mtu.”
Akitoa ufafanuzi wa malipo mara mbili yaliyofanyika kwa kampuni ya BP, Mwenyekiti huyo anasema kuwa baada ya kupigwa mnada, mnunuzi alishindwa kutimiza masharti ndipo uongozi wa NCU ukaamua kukubaliana na BP kumlipa ili jengo lisiuzwe.
“Mnunuzi alishindwa kutimiza masharti ya mnada na tukakubaliana na BP tuwalipe deni lao ili mambo yaishe. Tukawalipa kupitia benki lakini tukaja kushangaa jengo limechukuliwa tena na mnunuzi wakati mwanzoni tuliambiwa ameshindwa kutimiza masharti. Hii ndiyo maana unaona ‘double payment’ na hizo fedha zitakuwa bado benki baada ya sisi kwenda mahakamani,” alisema.
Bugomola anasema kwa kuwa Rais Kikwete analijua vyema tatizo hilo, wanasubiri kwa hamu uamuzi wake ili kujua hatima ya mali za NCU kwani mbali na yeye hakuna mwingine wa kuwasaidia.
