KATIKA sehemu ya kwanza ya makala hii, wiki mbili zilizopita, nilieleza jinsi Mahakama ya Rufaa ilivyojilemaza [kwa makusudi au udhaifu?] kutafsiri vyema Katiba ya nchi, Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu (The Basic Rights and Duties Enforcement Act) ya mwaka 1994, na Sheria ya Uchaguzi ya 1985 [kama ilivyorekebishwa], na kushindwa kufikia uamuzi sahihi juu ya kuwapo au kutokuwapo kwa mgombea huru (mgombea binafsi).
Lakini kabla ya kuendelea kuwasilisha sehemu ya pili ya makala hii ili kuonyesha hatari inayoweza kuikumba jamii ya Kitanzania kutokana na uamuzi wa mahakama hiyo ya juu, yenye kauli ya mwisho katika utoaji haki, naomba nitoe shukrani kwa msomaji wangu mmoja, Dakta Emmanuel Kandusi [0754-402033] ambaye, licha ya kukubaliana kwa kiwango kikubwa na uchambuzi wangu uliotangulia, alikwenda mbali zaidi kwa kukosoa matumizi ya neno “mgombea binafsi”, kwamba haliwasilishi wala kutoa maana sahihi ya mtu anayegombea nafasi ya uongozi bila kupitia vyama vya siasa, na linadhalilisha.
Dakta Kandusi alisema (nami nakubaliana naye na kujisahihisha hima) kwamba neno sahihi linalopaswa kutumika ni mgombea huru; kwa maana ya mtu asiyefungwa na minyororo wala mifinyango ya vyama vya siasa.
Hata hukumu ya Mahakama ya Rufaa imetaja independent candidate kwa tafsiri ya “mgombea huru”, na sio private candidate kwa maana ya mgombea binafsi ambayo ni kweli.
Kwa kauli thabiti amesema; neno mgombea binafsi lina mtizamo wa mtu na mke wake bila kuhusisha wala kugusa shughuli za kiumma; lakini mgombea huru; kwa maana ya uhuru wa kushiriki katika shughuli za umma, ni tofauti na mgombea binafsi ambaye, hata hivyo, hayumo katika msamiati wa Katiba na Sheria za nchi hii.
Mgombea huru hajipeleki Ikulu au Bungeni kutenda mambo yake na mkewe; bali anakwenda kutekeleza kazi za umma. Pili, mtu huyo ataapa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba ya nchi, na si kwa Katiba yake na mkewe, atasimamia, kutetea na kuwajibika kwa umma wa Kitanzania na si kwa familia yake.
Pengine ni matumizi haya potofu ya maneno mgombea binafsi yanayofanya mgombea huru aonekane miongoni mwa wanasiasa vipofu na wasiojali demokrasia, kama binadamu wa ajabu kutoka dunia ya pili na asiye na nafasi katika jamii.
Nilimalizia sehemu ya kwanza ya makala haya kwa kueleza kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa walijijeruhi wenyewe kwa kufikia uamuzi usio sahihi kwamba hakuna msingi wa kisheria wa kuruhusu mgombea huru, na pili kwamba suala hilo ni la kisiasa, si la kisheria; na tatu, kwamba Mahakama Kuu haina madaraka ya kutamka kuwa kifungu chochote cha Katiba ni batili, au kinakwenda kinyume na matakwa ya Katiba.
Nilieleza kwa kunukuu Katiba ya nchi yetu na Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu ya 1964, kuonyesha kwamba Mahakama ndiyo pekee yenye madaraka ya kutafsiri sheria zote; na pia kwamba Katiba, pamoja na kuwa sheria mama, nayo inaingia katika kundi la sheria ambazo mahakama ina madaraka ya kuzitafsiri bila kujali utaratibu unaotumika Bungeni.
Kwa kifupi, kazi ya Mahakama ni kufafanua [to declare] sheria mahali ambapo Bunge lilipungukiwa upeo wa kufanya hivyo na kuzuia ubabe wa Serikali, na pia kutekeleza wajibu wake kwa uadilifu, haki, bila upendeleo na bila ya shinikizo kutoka nje.
Kwa hiyo, kwa kuwa kazi ya Mahakama ni kutafsiri Katiba na Sheria, basi, kama kuna mgongano ni lazima Mahakama ionyeshe njia ya kuondoa mgongano huo, kwa mujibu wa ibara ya 30 (3) na 108 (1) ya Katiba; na kifungu cha 8 (1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu ya 1964, ambapo haki hizo zimeainishwa vyema kwenye ibara ya 12 – 29 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977.
Uamuzi huu uliofanywa na Mahakama ya Rufaa umekuja wakati mbaya ambapo jamii yetu inapiga miayo kwa uchovu wa kulilia demokrasia na mwelekeo wa nchi iliyokosa itikadi, sera na dira ya maendeleo katikati ya mtafaruku unaotishia demokrasia na kushamiri kwa mikataba katika jamii na kunukia kwa ukoloni mamboleo.
Ni wakati na ni mfano mbaya pia nchi inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu ambapo Mahakama zitakabiliwa na kazi kubwa ya kuamua mashauri ya kisiasa wakati na baada ya uchaguzi, ambapo uadilifu utahitajika kuhakikisha kwamba maamuzi hayo yanazingatia haki ya msingi ya mwananchi kushiriki katika utawala wa nchi, mikutano na maandamano, uhuru wa kujieleza pamoja na umuhimu wa kuendeleza hali ya amani na utulivu nchini.
Je, mahakama za chini zijifunze nini kutoka Mahakama ya Rufaa kama Mahakama hiyo inajilemaza yenyewe kwa shinikizo la kisiasa kutoka nje, na hivyo kuzitizama haki za msingi za Watanzania kwa jicho moja?
Ni jambo lililowakanganya Watanzania kwa Mahakama hiyo kunukuu katika ukurasa wa 48 wa hukumu yake, matakwa ya Mikataba ya Kimataifa juu ya Haki za Msingi za kiraia na kisiasa, na ibara ya 21 ya Katiba yetu; kwamba “Haki ya mtu ya kugombea [nafasi za uongozi] isibanwe [au kuporwa] bila kutumia busara, kwa kumtaka kuwa mwanachama wa chama au aina fulani ya vyama”; na bado Mahakama hiyo ikaendelea kutoa uamuzi unaokinzana na dhamira hiyo!
Hapa tuna kila sababu ya kuhoji: Je, Mahakama yetu ya Rufaa imeamua kesi hii kwa uhuru kiasi gani, au imeamua kwa shinikizo, woga au ushabiki wa kisiasa? Hebu angalia kasoro moja katika hukumu hiyo:
Katika rufaa yake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliitaka Mahakama hiyo ijibu swali lifuatalo: “Je, Mahakama Kuu ina madaraka ya kufuta kifungu cha Katiba?”
Lakini katika uamuzi wake, tofauti na swali lililokuwa mbele yake, Mahakama hiyo imejibu swali tofauti la “Je, Mahakama Kuu ina madaraka ya kutamka kwamba kifungu cha Katiba ni batili?”
Hata katika hukumu ya misingi ya Mahakama Kuu, hakuna mahali popote majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo, waliposema kwamba Mahakama hiyo ina madaraka ya kufuta kifungu cha Katiba, walichosema ni kuwa “Sheria iliyoleta mabadiliko kwenye baadhi ya vifungu ilikuwa batili” tangu kutungwa kwake; na kwa sababu hiyo haiwezi kuhesabiwa kuwa iliwahi kuwapo.
Kwa kifupi, Mahakama ya Rufaa imejiundia hoja ambayo haikuwa sehemu ya rufaa mbele yake, na kuitolea uamuzi tofauti na uliotarajiwa kwa kuzingatia hoja ya rufaa yenyewe. Kama hiyo si kasoro kubwa ya Mahakama ya Rufaa katika hukumu hiyo, ni nini? Na kwa nini umma wa Kitanzania usiguswe na uamuzi huo tata unaoangamiza demokrasia nchini?
Hata kama uamuzi wake ungekuwa sahihi, haikuwa sababu kwa Mahakama hiyo ya Rufaa kusukumia Bunge suala la mgombea huru bila kutoa AMRI na kuweka muda maalumu kwa Bunge hilo kuifanyia marekebisho Katiba, kama ilivyofanya Mahakama Kuu.
Lakini ifahamike kwamba Bunge letu ambalo limegeuka kuwa Bunge la kitabaka, ndilo linalopinga nafasi ya mgombea huru kwa sababu wabunge wake wengi hawana ushawishi kwa umma, wanashinda chaguzi kwa nguvu, ujanja na ulaghai kwa nguvu na hila za vyama; bila hivyo wangebwagwa na wagombea huru makini na waadilifu walio nje ya vyama.
Na ndiyo maana mfumo wa uchaguzi umebakia usio wa kidemokrasia kwa sababu ni mpango wenye hila wa kibwenyenye [Chama] madarakani, katika kuendeleza utawala wao wa kitabaka.
Ni hapa ambapo ile tafsiri ya Karl Marx ya “Chama cha Siasa”, kwamba “ni taasisi ya Kitabaka yenye malengo dhahiri ya kiuchumi na ulaji”, inajidhihirisha.
Kuhusu Mamlaka ya Kisiasa, Karl Marx anasema: “Nguvu ya kisiasa, kama inavyoweza kuitwa, ni mkusanyiko wa nguvu ya tabaka moja [dogo] kwa ajili ya kukandamiza wengine” [Marx and Engels, Selected Works, pg. 127].
Ni ukweli usiopingika, hivi leo, kwamba vyama vyetu vya siasa si vya wanachama; bali ni vya tabaka la viongozi na wafanyabiashara wanaotaka kutumikiwa badala ya kutumikia.
Je, umepata kujiuliza: Kwa nini siasa [udiwani, ubunge] umevamiwa na tabaka la wafanyabiashara na wasomi? Ni kwa sababu siasa sasa, kupitia vyama vya siasa, ni taasisi ya kitabaka iliyohodhi maamuzi na utawala wa nchi, na hao sasa ndio wanaokula matunda ya uhuru kwa kuwapora wananchi haki zao za msingi na demokrasia bila hofu ya kuulizwa wala kuwajibishwa!
Na kwa sababu tabaka hili la watawala linazidi kujiweka mbali na wananchi wa kawaida, na kubakia madarakani kwa nguvu ya fedha, linajua wazi kuwa haliwezi kudumu kisiasa kwa njia ya Serikali yenye haki madarakani. Kwa sababu hii limekamata hatamu za Serikali, kiasi kwamba leo huwezi kutofautisha mamlaka ya Chama cha Siasa na Serikali na taasisi.
Kwa sababu hiyo, wananchi wana kila sababu ya kuingiwa na wasiwasi na kuhoji wanapoona muhimili wa kulinda haki; yaani Mahakama unaanza kutikisika, kuyumba na kucheza kwa mdundiko wa tabaka la wanasiasa na watawala.
Ni kwa sababu hii kwamba tabaka hili, badala ya kutulia na kupanga uchumi na maendeleo ya nchi kwa wote, limo katika harakati za kujihami daima kwa vitimbwi na ujanja wa kisiasa [political gimmics] kutoka uchaguzi mmoja unapomalizika hadi unaofuata ili kuendelea kubakia madarakani kwa hila.
Ni kwa sababu hii pia kwamba nchi yetu inaendelea kuzama katika lindi la migogoro ya kiuchumi na umasikini, kwa sababu mawakala/wadau wa maendeleo, kwa maana ya umma wa Kitanzania, wameporwa mamlaka yote ya kuamua, kiasi cha kujiona daima kama wageni tu katika mchakato wa kisiasa na utawala nchini mwao.
Moja ya wajibu wa Mahakama za kutoa haki [Courts of justice] ni kuzingatia na kulinda maadili ya kidemokrasia [democratic values] kwa hamasa ya haki za binadamu na demokrasia kuliko kujihusisha zaidi na harakati za kukwepa migogoro na mihimili mingine ya Serikali.
Je, katika uamuzi huu Mahakama ya Rufaa imetekelezaje wajibu wake, na kwa manufaa au faida ya nani?
…Itaendelea wiki ijayo.

Simu:
0713-526972
Barua-pepe: