LEO, mimi na wenzangu tuliopo kuzimu ambao tunawaonea huruma kwa jinsi mlivyokwama kimaendeleo, tunapenda kuendelea kuwakumbusha matatizo yenu makuu yanayomikabili ili muwe na uhakika kwamba mtakaowachagua katika uchaguzi wenu mkuu ujao wana uwezo wa kuyashughulikia.
Tuendelee kwa kuanzia na tatizo kuu la NJAA linalochochewa zaidi na kutelekezwa kwa wakulima wadogo. Watu wengi Afrika wanaishi vijijini na maisha yao yanategemea kilimo na uzalishaji wa chakula. Kwa Tanzania ni 87. Kwa miaka mingi wakulima wadogo wametumia kilimo cha mseto kwa mazao kwa sababu wanajua mazao mchanganyiko yanaongeza rutuba katika ardhi. Na ilikuwa ni mwiko kufanya shughuli za ukulima au ufugaji kwenye vyanzo vya maji.
Hizi juhudi za kuendeleza kilimo kikubwa kinachotegemea mbolea na dawa za kemikali zina nia ya kuwakuza wakulima wakubwa wa kimataifa wakishirikiana na wa ndani, ambao kwao kilimo ni njia ya kupata faida na wala hawakitegemei kwa maisha yao ya kawaida, tofauti kabisa na nyinyi.
Kwa wastani, sera fukarishi, dhuluma, uwezo mdogo wa kuzalisha, usambazaji mbaya na uporwaji wa ardhi, ndio visababishi vikubwa vya njaa. Kwa hiyo, mbinu yoyote ya kuongeza uzalishaji wa chakula ambayo itaendeleza sera hizo haitafanikiwa katika kuondoa njaa na maafa yanayotokana na njaa Afrika.
Viongozi wana ushahidi tele wa kuwaonyesha wafadhili watambue uzito wa tatizo, na waheshimu kwamba Watanzania, na hasa vijijini wanataka mbinu mbadala ambazo zinaongozwa na jamii yenyewe na wasomi waliojikomboa kifkra ambao wanatumia elimu waliyoipata katika kuitafsiri kwa vitendo kwa kuzingatia mazingira yenu kwa mtazamo wenu.
Mahitaji yenu ya kimkakati: Vijiji vyote vipimwe, viwe na hati miliki, mwananchi mmoja mmoja apate hati miliki wanazostahili. Aidha, wajue sheria ya ardhi vijijini na mijini ya mwaka 1999, wawe na mpango wa matumizi ya ardhi na maendeleo ( wizara ya ardhi, tamisemi, chuo cha ardhi, wataalamu wa upimaji, NGOs , serikali za vijiji nk) washiriki katika zoezi hili wakiongozwa na madiwani/ wabunge. Kila Halmashauri itenge fedha .
Kila wilaya ifanye mahesabu ya raslimali zake, vyanzo mbalimbali vya mapato kwa ajili ya wananchi ili wawe na uwezo wa kulipa kodi. Ziainishwe motisha kwa ajili ya watalamu kwenda kufanya kazi vijijini (barabara, nishati, maji, nyumba, usafiri, zawadi kama ngo’mbe au trekta). Mipango yenu ijikite katika kujitegemea, msaada uwe nyongeza tu na si wao kuja kuwafanyia nyie kazi za upimaji, wawe walimu wa watoto wenu mashuleni, wawe na uwezo wa kuwasha au kuzima stima na maji.
Hizo ni baadhi ya huduma nyeti ambazo hakuna nchi duniani inastahili kuwaachiwa wageni wazitekeleze; tena kwa masharti yao na fedha zao! Mnatutia soni wazee wenu huku kuzimuni kwa kufanya hivyo.
Madai elekezi kwa chama cha siasa na serikali
Kwa kuzingatia hali nyeti ya sera fukarishi za ‘utanda-wizi’ unaoongozwa na ubepari, mnatakiwa kudai yafuatayo kwa chama kitakachopata ridhaa yenu kutumikia serikali yenu katika miaka mitano ijayo :
- Kwa vile ni vita vya ukombozi wa uchumi, bila upendeleo wa aina ye yote, muwe na majemadari jasiri na wenye uzalendo, wa kike na wa kiume, ambao hawajachoka kifkra na wenye ubunifu wa hali ya juu ili mbadili mbinu za kupambana na ubeberu na ubepari katika karne ya 21.
Katika miaka hamsini iliyopita bei ya bidhaa za viwandani emeendelea kupanda na bei za malighafi mnazozalisha zinazidi kushuka, halafu mnashangaa ufukara unaongezeka mwaka hadi mwaka!
- Nchi yenu iongoze vita vya ukombozi wa kiuchumi Afrika na kuwa na kamati ya ukombozi Tanzania itakayoratibu nguvu za pamoja za kupambana na kujikinga na ubeberu na ubepari. Na si vinginevyo. Mkiungana wote mtapona, mkitengana wote mtaangamia!
- Inabidi muwe na sera zenu wenyewe kuhusu kujitosheleza na kujitegemea katika masuala ya chakula na kilimo. Mikakati itakayo hakikisha malighafi mnazozalisha zinakuwa chachu ya kuendeleza viwanda vitakavyozalisha bidhaa bora kwa ajili ya soko la ndani na kisha kuuza nje. Serikali irudishe tume ya kudhibiti bei na hasa kwenye chakula ili watu wawe na uwezo wa kununua.
Uchumi wenu hauko salama dhidi ya midororo ya kimataifa, kwa hiyo sera zenu ziwahakikishie kwamba maendeleo na kukua kwa uchumi ni kwa faida ya walio wengi na sio watu watumikie ukuwaji wa uchumi bila maendeleo!
- Sera zitungwe ili kuendeleza kilimo kinachozingatia ikolojia na ziwe sera ambazo zimefanikiwa sehemu zingine duniani zenye mazingira na asili kama yetu.
Msidharau elimu ya jadi ambayo iko vijijini iliyosaidia kulinda vyanzo vya maji, mioto ya asili na mazingira kwa jumla. Anaedharau asili yake ama kweli ni mtumwa!
- Raslimali ya kutosha itengwe kwa ajili ya kuboresha mifumo ya barabara mijini na vijijini, nishati isambae nchi nzima na hasa ya jua, upepo na taka kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwanda vidogo vidogo.
*Ni lazima suala la kupunguza matabaka ambalo linaendelea kukua kati ya watu fukara na matajiri lishughulikiwe haraka ili muweze kufikia azma ya kuwa na haki za msingi kwa kila Mtanzania kwa kuzingatia kuwa watu wote mmeumbwa sawa.
Kuna asasi fulani iinasema katika miaka ya 1970 tofauti ya kipato kati wafanyakazi wanaopata mshahara ilikuwa ni 1:7 leo hii ni 1:29. Tathmini ya asasi moja kuhusu ajira ya wanawake inaonyesha wengi wameajirwa katika kazi za chini zenye mshahara wa kima cha chini; na wale ambao hawajaajiriwa wanafanya kazi ambazo hazina malipo. Wanalea watoto, wanatunza wagonjwa na wazee, wanachota maji, wanazalisha chakula nk. Hawana Bima ya aina ye yote na hawamo katika bajeti ya serikali lakini wanachangia 63% ya pato la taifa! Kama unabisha waulize wanawake.
- Wazalishaji wa chakula na hasa wadogo, na wale wasio na ardhi, wanawake wakulima, wavuvi, wafugaji na wengine wanastahili wapewe ruzuku ili waweze kupata pembejeo wanazohitaji (na elimu ya matumizi) ambazo zitaendeleza mbinu za uzalishaji wa kujitegemea na serikali inunue bidhaa kutoka kwa wazalishaji kwa kuzingatia bei ya soko ili walanguzi wasiwadhulumu wazalishaji! Nani kasema hawahitaji kima cha juu cha mshahara?
- Mapinduzi ya matumizi ya ardhi kwa lengo la kugawa ardhi, kuwa na ushirika wa uzalishaji wa chakula na kuhakikisha kuwa wale walio pembezoni katika jamii wawe wa kwanza kufaidika. Kuongeza rasilimali katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi na kuwawezesha wapate teknolojia zinazofaa, mikopo nafuu, masoko na mazingira ya kuwawezesha wazalishaji watoe bidhaa bora hasa wanawake hayana mjadala .
- Rasilimali ardhi inayotengwa na kupewa wawekezaji wa mashamba makubwa ya nishati mbadala na anasa zingine isitishwe mara moja na badala yake itumike kwa chakula. Magari ya Ulaya yanataka hiyo nishati, lakini ninyi mnahitaji ardhi hai na maji yasiyo na sumu kwa ajili ya chakula.
Kama wataleta kesi basi ipeleteni kwa wana wa nchi wenye mali yao na tulioko kuzimuni tutafungua kesi zetu dhidi yao! Kudadadek!
- Azma iwe kuendeleza uzalishaji wenye uwiano wa ki- ikolojia ili kuiponya maji na ardhi iliyo haribiwa na kemikali zenye sumu. Lengo ni kujitosheleza na kujitegemea katika uzalishaji wa chakula bora na maji safi yaliyo salama.
Ardhi na watu mnao kinachotakiwa ni sera safi na uongozi bora.
- Mjenge ari na uwezo zaidi wa kuendeleza uzalishaji wa mbegu za asili badala ya kutegemea hizo zinazo itwa mbegu bora. Mnao wanasayansi kwa nini wasiachiwe wakatumia ujuzi wao kwa kushirikiana na wanasayansi wa asili vijijini ili muwe na akiba ya mbegu zenu kama zamani?
*Watanzania kataeni kuwa dampo la bidhaa za nje kwenye soko la ndani wakati nchi yenu inawekewa vikwazo tele na haiwezi kuuza bidhaa katika masoko ya Ulaya na kwa binamu zao Marekani hasa yale yanayotokana na kilimo na kuongezwa thamani. Mdai kuwa na viwanda vyenu ili vijana wenu wawekeza katika uzalishaji na kufanya kazi kwenye viwanda vyenu.
Tanzania mmelegeza masharti ya biashara kuliko hata ilivyostahili kufuatana na sheria za Shirika la Biashara la Dunia. Hii imesababisha muwekewe vikwazo vya kibiashara kama vile viwango vya usafi, hali ya mazingira ya sehemu iliyotoka bidhaa hiyo; je udongo na maji ya kumwagilia yana kemikali kali, je watoto wametumiwa katika uzalishaji? Ni lazima mkulima aeleze kwa maandishi ama sivyo bidhaa haitaingia kwa Wazungu!
- Wakati umefika muwe na sheria ya uwekezaji inayoeleweka ya wafanyibiashara wadogo. Kuwe na kanuni inayokataza wageni kufanya biashara za rejereja au kuchukua nafasi ya viwanda vidogo vinavyomilkiwa na wanawake na vijana. Motisha na vivutio ambavyo serikali ilikuwa inawapa wawekezaji wapewe wazawa ili waweze kuwa walipa kodi wazuri.
Kwa muda mrefu wafanyi biashara wadogo na warejareja walikuwa wametawala soko la ndani. Lakini baada ya Biashara ya reja reja kuwa huria na makampuni ya biashara ya nje nayo kuingia kwenye ushindani hali imekuwa ngumu. Dhamana ya maisha ya wafanyibiashara hao wadogo wengi wakiwa ni wanawake na vijana iko mikononi mwa Chama mtakacho kipa ridhaa kwa kura zenu
- Inabidi mdai Sheria za Utalii zitakazo hakikisha makampuni yanazingatia sheria ya kufanya biashara ya utalii na wenyeji ili muendelee kujijengea uwezo, na sheria za ajira ziwaguse wafanyakazi wa nje ambao sio Watanzania, na yasipewe motisha ya kuwekeza nchini kwa masharti mazuri ya kodi. Serikali inatakiwa iweze kuyawajibisha makampuni ambayo yatawanyanyasa wafanyakazi, wanakijiji au kuharibu mazingira. Sheria hii inaweza kupunguza shughuli za makampuni ya nje yanayokuja kuwekeza nchini kwa faida yao.
Itaendelea.
