MMOJA wa waasisi wa dhana ya kutenganisha (kikatiba) shughuli za dini na serikali nchini Marekani, mwaka 1802, Thomas Jefferson, ambaye ni Rais wa tatu wa taifa hilo, enzi za uongozi wake aliwahi kutoa kauli elekezi kwa viongozi na raia wenzake. Ingawa miaka mingi imepita thamani ya kauli hiyo bado ipo.
Ni kauli inayowahusu viongozi au watu wenye hulka ya hasira inayoweza kuwaweka katika hatari ya kutamka maneno wanayoweza kuyajutia baada ya dakika, saa, siku, miezi au miaka kadhaa kupita.
Kwa mujibu wa kauli hiyo ya Jefferson, unapokuwa umezongwa na hasira si ajabu ukajikuta ukitamka matamshi tata utakayojutia. Na kwa kawaida, nguvu ya majuto hayo hudumu kwa kadri ya uzito wa kosa au kauli tata husika itakavyodumu.
Kwa kuzingatia mazingira hayo, Jefferson anasema: "When angry, count ten, before you speak; if very angry, an hundred." Kwamba; unapokabwa kwa hasira, hesabu hadi kumi kabla ya kuzungumza; na kama umekabwa kwa hasira kali zaidi, basi, hesabu hadi 100 kabla ya kuzungumza.
Mantiki anayojenga hapa ni kuwa mwangalifu, kujipa muda ili uweze kupima athari za kauli utakayotoa.
Na unaweza kujipa muda huo kwa kuhesabu namba. Wakati mwingine si lazima kuhesabu moja hadi 10 au 100, ukishajenga tu taswira ya kifikra kuhusu hesabu hizo, basi, hasira zinaweza kushuka na upeo wako wa busara na hekima ukarejea na hatimaye kujiokoa kutoka katika ukingo wa dimbwi la makosa ambalo ungeweza kutumbukia na kuzama au kuogolea bila tija yoyote.
Huu ndiyo ushauri wa safu hii kwa wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani nchini, na hususan wanamikakati katika vyama mbalimbali vya siasa. Lengo ni kuhakikisha kila mdau anatumia fursa yake kuwezesha mazingira bora zaidi ya kuchagua viongozi nchini. Izingatiwe kuwa, mazingira bora ya uchaguzi ndiyo huibua viongozi bora.
Leo kupitia safu hii pia naomba kuwa mstari wa mbele katika kuwasilisha ujumbe mahususi ambao ni hatua za mwanzo kwetu kuanza kutambua tulichoweza kuvuna kutokana na kura tulizopiga, hasa kura za kumchagua Rais wa Tanzania. Tunaweza kufanya hivyo kwa kuzingatia vigezo kadhaa.
Kati ya vigezo hivyo ni udhaifu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Udhaifu Katiba (au uimara kwa baadhi) ninaolenga kuutumia katika mjadala wa leo ni kutokumwekea masharti rais aunde serikali yenye ukubwa au udogo gani, kwa maana ya baraza la mawaziri. Lakini si Katiba tu, tatizo hili kwa mujibu wa uzoefu wa harakati za kisiasa nchini limegusa hata vyama vya siasa, na hususan ilani za uchaguzi.
Hata ilani za uchaguzi za vyama karibu vyote (zilizopita na baadhi za mwaka huu) hazionyeshi au kutamka ilani husika itatekelezwa kwa baraza la mawaziri lenye ukubwa au udogo gani. Mara kwa mara ilani zimekuwa zikijieleza jinsi serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi mkuu itakavyoweza kuongoza nchini lakini ikishindwa kubainisha idadi ya mawaziri au wizara kama moja ya vigezo muhimu kwa wananchi kufanya ulinganisho wa kisayansi kuhusu maudhui ya jumla ya ilani husika.
Kama timu za mikakati ya kampeni katika vyama vya siasa zingekuwa na mbinu za kuhakikisha kila fursa ya hoja inatumika kuwaomba wananchi kura, ikiwamo ya kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali na wakati huo huo kuhakikisha ilani husika inatakelezwa kwa ufanisi, basi, suala la ukubwa au udogo wa serikali kwa maana ya baraza la mawaziri ingekuwa sehemu ya hoja muhimu za kuomba kura.
Na wakati mwingine, kwa ilani zinazozungumzia kujenga bajeti inayojitegemea kwa kuzingatia raslimali za nchi zilizopo, ingekuwa changamoto zaidi ilani husika kutaja hata majina ya wizara sambamba na kuainisha majukumu ya kila wizara. Katika hali hiyo, bila shaka tungekuwa na ilani za kisayansi na zenye mantiki zaidi.
Lakini kwa kuwa huo si utamaduni wa ilani za vyama vyetu, na kwa maana hiyo ukubwa au udogo wa serikali si suala linalohusu chama cha siasa wala linalowekewa masharti katika Katiba, suala hili hubaki kuwa utashi wa mgombea au wagombea na baada ya uchaguzi mkuu kupita hutelekezwa mikononi mwa Rais pekee.
Hata hivyo, kwa kuwa msingi wa mjadala wa leo unahusu hatua za awali za kupima umakini wa rais tutakayekuwa tumekwishamchagua, kuna mambo mawili ya kuzingatiwa katika kuunda serikali ijayo kwa manufaa ya nchi. Masuala hayo yanahusu mazingira ya sasa ya kiutawala nchini.
Kwanza ni utanuzi wa serikali ngazi za mikoa na wilaya. Katika suala hili, mikoa mipya mitatu imeanzishwa, wilaya 18 mpya na halmashauri kadhaa. Suala la pili, ni uwezo wa kiuchumi kubeba serikali kuu kwa maana ya baraza la mawaziri. Mazingira haya ya kiutawala katika sura hizo mbili ni lazima yategemeane katika kuhakikisha nchi inanufaika zaidi.
Kama nilivyoeleza awali, ni lazima tumchague rais miongoni mwa wagombea watakaokuwapo naye ni lazima aunde serikali. Tatizo ni kuwa amepewa utashi mpana zaidi wa kuamua aunde serikali yenye ukubwa gani wakati mwingine bila kuzingatia uwezo wa kiuchumi. Hakuna masharti ya Katiba wala ya ilani ya uchaguzi, kama nilivyoeleza.
Kwa mantiki hiyo, suala la kuunda serikali ni utashi wa mtu mmoja anayeamua kuwashirikisha watu wengine wawili, makamu wa rais na waziri mkuu. Hawa ndiyo waamuzi wa nani aongoze nini, katika wizara, taasisi au bodi gani ili nchi ya watu milioni 40 isonge mbele.
Tumekwishaona Katiba haitamki ‘size’ ya baraza la mawaziri, na hata vyama vya siasa, CCM ikiwamo, havina maelekezo mahususi kwa mgombea wao wa urais. Yaani hata chama cha siasa anachotoka mgombea urais hakijui kitaunda serikali yenye ukubwa gani.
Basi kwa kuzingatia haya na mengine, tunapaswa kujiandaa kutumia udhaifu huo kumpima rais atakayechaguliwa ili kujua je, mwelekeo wake wa awali kama kiongozi mkuu unalenga kunufaisha wengi?
Ni wazi kuwa, kwa mgombea yeyote makini wa urais ni lazima anajua ukubwa au udogo wa serikali atakayounda. Anajua majina ya atakaowateua. Kikubwa kwa wananchi ni kujiridhisha kuwa uteuzi atakaofanya haugeuki kero kwao kwa kuzingatia vigezo mahususi, na hasa kigezo cha uchumi wa nchi.
Mazingira ya kiutawala ambayo ni kutanuliwa kwa utawala ulio ‘karibu’ na wananchi zaidi kwa kiasi fulani yanamlazimu rais makini kuunda baraza la mawaziri dogo. Anapaswa kuunda baraza dogo kwa kuwa utawala ngazi ya mkoa na wilaya umetanuliwa na kwa mantiki hiyo fursa za kiuchumi hazimpi nafasi kuunda baraza kubwa.
Najua ujumbe huu ni mchungu kwa wanaoota uwaziri na unaweza kuwaudhi, lakini kama alivyotueleza Jefferson; When angry, count ten, before you speak; if very angry, an hundred. Hatumchagui rais kwa ajili ya kuwapa nafasi za uongozi wenye kiu au njaa ya uongozi, tunamchagua ili tushirikiane kuijenga nchi.
Rais halazimishwi na Katiba wala ilani za vyama kama ilivyo utamaduni wa siasa nchini, lakini ni wakati sasa wa uchumi wa nchi kutangulizwa kama kigezo cha kumlazimisha kuunda serikali ndogo. Alazimike kuunda Serikali ndogo ikizingatiwa kuwa wigo wa utawala ‘uliokaribu’ na wananchi kwa maana ya mikoa, wilaya na halmashauri umetanuliwa zaidi.
Kinyume cha hapo, huyo hawezi kuwa rais makini katika hatua za awali za utendaji wake wa kiuamuzi. Hapo tutakuwa tumepata jibu la swali hili; je, tutakuwa tumemchagua rais anayejua aifanyie nini nchi na si awafanyie nini wanasiasa wenzake wenye njaa ya madaraka? Ili kuweza kupata jibu muafaka, ni lazima tupige kura kwa umakini mkubwa.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Simu:
0787-643151