Kwa Waziri wa Mikiki na Makeke,
Uzitoni Street,
Bongo.
Mpenzi Frank,
Wasemaje dia? Unaendeleaje huko? Umeshakula pilao ya wagombea wangapi teh teh? Lakini shida yako huna kadi ya kada hivyo naona msimu huu wa kula utaendelea kukonda tu. Pole mpenzi wangu.
Ninachoshangaa ni kwamba watu hawaoni shida kula hivyo ingawa wanajua ni kosa lakini wanaona shida sana kula kwa huyu na kutoa kura kwa yule, eti si uaminifu.
Kula kwa huyu na kumpa kura ni ukosefu wa uaminifu tayari tena ukosefu wa uaminifu kwetu sisi sote tutakaoathirika na ufuska wake wa kisiasa, iweje wajidai waaminifu kwa kumpa kura mhongaji eti kwa kuwa amewapa pesa haramu wao wampe kura halali?
Ni kama wehu wasioona shida kufanya mapenzi nje ya ndoa lakini wanaona ni dhambi kubwa kutumia kondomu. Dhambi ni mapenzi nje ya ndoa, basi!! Ndiyo maana napenda ule msemo wa fyatu wako Makengeza, eti kula kwa huyu, kura kwa yule.
Aliyenipa pilao ya bure ni mhongaji na atatafuta namna ya kurudisha hongo zake zote hivyo nitakula leo na kuliwa vibaya sana kesho. Au vipi mpenzi wangu. Leta stori ulifanikiwa kubugia pilao ngapi huko?
Mimi sijambo sana ingawa nahisi pilao kwetu imepungua maana pesa zote za bosi zinaenda kununua pilao za wengine. Mpaka binti bosi alilalamika juzi.
‘Jamani mama, mbona hatuendi auti siku hizi?’
‘Wewe si unajua mwanangu. Huu ni msimu wa kupanda. Ngoja mambo yawe mazuri na tutavuna zaidi.’
‘Lakini nimechoka mama.’
‘We shukuru kwamba angalau unakula vizuri, na unaenda shule bila taabu. Na kwamba baba yako atashinda. Wako wengi wanazika pesa zao hivihivi. Honga kushoto, honga kulia na mwisho wa siku hawaambulii kitu. Hata wale wapinzani wa baba yako wanapanda mbegu zote walizo nazo lakini kumbe wanapanda kwenye mawe. Hawawezi kumshinda baba hata kidogo.’
BB akanyamaza lakini niliona alikubali shingo upande sana. Lakini hata mimi nashangaa watu wanavyojitosa ulingoni. Hawafahamiki kabisa, lakini wanapopata wapambe wawiliwatatu wanaanza kujimwaga utadhani wanao uhakika wa kushinda.
Mwisho wa siku wanaambulia kura mbili za wapambe wao tu, na wameshaharibu bajeti yao ya miaka mitatu. Yaani kwa wengine naona huu uchaguzi ni kama ugonjwa wa kucheka wa sisi wasichana mashuleni. Mmoja akianza na wengine wanafuata mmojammoja. Wanaambukizana.
Na uchaguzi vilevile. Nikiona fulani amejimwaga, basi na mimi nawashwa na upupu hadi nijimwage na mimi. Kumbe twajibwaga.
Haya, hii ndiyo shida ya wenye ndoto za mchana. Lakini kuna wengine nawashangaa zaidi. Siku hizi, nalazimika kwenda kufanya manunuzi mwenyewe maana magari yote ya bosi yako kwenye kupanda tu. Hivyo napanda midaladala kweli ingawa huko Uzitoni, daladala ziko chache kwa sababu wanajua wanene wa nchi wana magari yao manene pia.
Lakini potelea mbali, ni raha pia kuweza kutoka kupumua hewa huru badala ya kufungiwa ndani siku nzima. Na nikichelewa, Mama Bosi hawezi kulalamika sana maana namwambia daladala hakuna.
Lakini juzi kidogo nipatikane maana nilichelewa sana, kisa mabishano makali. Nadhani Hidaya wako naye ana ugonjwa wa kuambukiza pia. Mlevi wa mijadala maana najua nitaambulia mbilitatu. Basi, siku hizi, kila nikitoka, kwenda sokoni, au dukani, nawasikia watu ndani ya daladala, na sokoni kwenyewe, na barabarani, kila mahali nawasikia wengine wakilalamika, wakishtumu, wakipiga kelele za aina zote kuhusu ufisadi hapa, uzembe kule, ulaji kwingine, kiburi huko, shule mbovu, huduma mbovu, nini sijui utadhani wamepewa mdomo kwa ajili ya kulalamika tu.
Lakini akitokea mtu na kuwaambia kwamba wao ndio wenye uwezo wa kubadilisha hii hali weeeee! Mara moja wanageuka tena mara oooooh haiwezekani! Oooh! Watazuia, wataiba kura, watafanya hili au lile, heri kutafunwa na zimwi likujualo. Kisha watarudia kulalamika. Ama kweli wanazimwa na zimwi hadi wanaliwa.
Na hali hii imeongezeka sana tangu kile chama kingine kimteue mgombea, eti anapoteza muda kabisa, bora abaki bungeni, huu ni mtego wa kummaliza kisiasa na nini sijui. Basi nilipoenda sokoni juzi, mambo yalikuwa vilevile lakini wakati wazee wanalalamika kama kawaida yao, akajitokeza vijana wawili.
‘Lakini nyinyi wazee, tunashindwa kuwaelewa kabisa. Mkilalamika utadhani ni mwisho wa dunia lakini hamtaki kufanya lolote kubadili hali hii.’
‘Nyie watoto msitusumbue. Kinda wa juzi mnajua nini?’
‘Kwani wakati wa kuondoa ukoloni, mngebaki na kulalamika hivyo, si tungetawaliwa hadi leo?’
Mzee mmoja akakasirika.
‘We mtoto, usifananishe hali ya sasa na ukoloni. Eboo! Bila kuwaondoa wale washenzi, tusingekuwa tumepiga hatua vile. Hata huu uhuru wa kulalamika tusingekuwa nao.’
Mwingine alidaka.
‘Hata kama tunaliwa siku hizi, angalau tunaliwa na wenzetu hivyo ni chungutamu.’
Vijana walizidi kucheka.
‘Unaona. Sisi hatujasema afadhali ukoloni hata kidogo. Hayo ni yenu. Tumesema kwamba mliwaondoa wakoloni kwa sababu mlikataa kukata tamaa. Wakoloni walikuwa na nguvu nyingi lakini kwa kuwa mliamka na sauti moja, mkoloni ilibidi afyate mkia. Sasa kama mambo ni mazuri leo, basi!
Acheni kulalamika hivyo maana tunavyowasikia tunashangaa sisi sote hatujafa hadi sasa. Na kama hayo malalamiko ni kweli na hatufanyi lolote kubadili hali, basi yabidi tujilaumu wenyewe.’
Wazee wale walizidi kuwaponda vijana lakini mimi nilivutiwa kweli nao.
‘Ndiyo! Ndiyo maana sisi vijana tumeamua kwamba hatukubali kubaki na hali hii. Hadi lini?’
Mzee mmoja alicheka sana.
‘Kweli ninyi vijana mnachekesha. Wewe unajua nguvu ya hawa jamaa? Unafikiri watalala chini na kuwaruhusu kuwakanyaga huku wakiwa na hamu ya kuendelea kula? Hata kidogo. Ndiyo maana wanasema ushindi ni lazima … watazuia kwa njia yoyote, kwa hela au hila na mtaona mmepoteza muda wenu.’
Kijana mmoja alimwangalia.
‘Hapana baba. Nyinyi ndio mnaopoteza muda. Kulalama kunasaidia nini? Kila siku kulalama tu, kisha waenda kumchagua yuleyule unayemlalamikia. Bora kujaribu na tukishindwa basi angalau tunajua kwamba tumejaribu kwa nguvu zote. Na tutaleta mabadiliko. Malalamiko hayaleti mabadiliko hata siku moja.’
‘Haya potezeni nguvu zenu hivihivi. Mtabaki mnajuta kama huyu naniihii wenu aliyejitosa taifa badala ya kuendelea na posho zake bungeni.’
‘Kwani huyu anafanya kwa ajili ya posho tu? Unafikiri watu wote wanafikiria matumbo yao basi? Na tukiwa wengi wa kutosha tunaokataa hii hali, hawawezi kufanya hila maana macho ya wengi yatawazuia.’
‘Hizi ni porojo ya mchana. Hiki ni chama chetu na kitaendelea tu.’
Vijana walikasirika.
‘Haya wazee wetu, nyinyi mnataka kudhoofisha lakini sisi haturudi nyuma. Tunataka mabadiliko. Tunashukuru wako walio tayari kujitosa kuleta mabadiliko lakini mtu mmoja hawezi kufanya hivyo. Akishindwa si kosa lake, ni kosa letu. Kwa herini.’
Vijana waliondoka huku wazee wale wakiendelea kuwadhihaki kwa nguvu na mimi nikashtuka nimekaa pale saa nzima nikisikiliza mjadala. Ilibidi nikimbilie daladala haraka sana na kurudi nyumbani nikapata maneno kibao ya MB eti nimeanza kuwa mhuni siku hizi, mbona nimechelewa hivyo, si ajabu nina mimba hadi basi.
Lakini sikumsikiliza sana maana nilikuwa nawaza maneno ya wale vijana. Kweli tukibaki kulalamika kuna mwiba mguuni, bila kuchukua hatua ya kuondoa mwiba si tutaota tende na mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Akupendaye daima kijana mwenzangu maana najua hata na wewe huwezi kukaa kwenye genge la kulalama tu. Mwaka huu tunataka mabadiliko si pilao za kutulewesha kama bangi.
Hidaya.

Barua-pepe: