Ngorongoro hatarini kukosa msaada wa Wajerumani

BENKI ya KFW ambayo serikali ya Ujerumani ni moja wa wabia imesitisha msaada wa Euro milioni 4.5 kwa wilaya ya Ngorongoro hadi hapo mgogoro wa ardhi katika pori tengefu la Loliondo utakapopatiwa ufumbuzi.

Fedha hizo ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 9 zilizotolewa na nchi hiyo ya Ulaya sawa na zaidi ya Bilioni 25 za Kitanzania kwa lengo la kutekeleza mradi wa maendeleo ya uhifadhi wa Ikolojia ya Serengeti (SEDCP).

Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti William Mwakilimwa mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika wilaya mbili za Ngorongoro mkoani Arusha na Serengeti mkoani Mara ambapo miradi kadhaa ya kijamii katika sekta ya maji na miundo mbinu itatekelezwa.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Wabunge wa Ardhi, Maliasili na Mazingira iliyotembelea eneo la pori tengefu la Loliondo Mhifadhi huyo alisema kuwa kwa upande wa Serengeti tayari mradi huo wa miaka mitano umeanza kutekelezwa.

“Kwa upande wa Ngorongoro wafadhili bado wanasita kutoa  fedha kutokana na mgogoro katika eneo hili la pori tengefu wakisubiri hatma na ufumbuzi wake,” alisema Mhifadhi huyo.

Pori tengefu la Loliondo lina kilomita za  mraba 4,000 na limekuwa katika mgogoro mkubwa wa matumizi yake baina ya wawekezaji hasa kampuni ya Falme za Kiarabu ya OBC na wafugaji wa jamii ya Kimaasai wanaishi ndani ya vijiji vinavyozunguka eneo hilo.

Aidha fedha hizo zinasubiri kutolewa pindi makubaliano ya kutenga eneo la Kilomita za Mraba 1,500 kwa ajili ya uhifadhi katika Pori Tengefu la Loliondo yatakapokamilika tayari kwa utekelezaji.

Mhifadhi aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo inayoongozwa  Mwenyekiti  Mhandisi Atashasta Nditie, kuwa ni muhimu maeneo hayo kuendelea kuhifadhiwa.

“Katika awamu ya kwanza zitatolewa  Milioni 7, wilaya ya Serengeti itapokea Euro Milioni 3.5 na Ngorogoro Euro Milioni 3.5….na kwa Ngorongoro fedha hizo zitatoka endapo tu eneo hilo litakuwa limekubalika kutengwa,” alisema Mwakilema.

Mhifadhi huyo aliongeza kuwa katika awamu ya pili zitatolewa  Euro Milioni 2 ambazo nazo wilaya ya Serengeti wametengewa Milioni 1 na Ngorogoro Milioni 1 fedha hizo ni kwa ajili ya miundombinu ya barabara.

Mhifadhi huyo alitahadharisha, “Machi 9 na 10  mwaka huu tutakuwa na mkutano na Wakurugenzi wa wilaya ya Serengeti na Ngorongoro kujadili namna gani mradi huu unatekelezwa na iwapo mgogoro huu utakuwa bado unaendelea kuna uwezekano fedha hizo zikarudi,” alisema Mwakilema. 

Naye mtaalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Wanyapori Tanzania (TAWIRI) Dr.Edward Kohi alieleza kuwa msaada huo utasadia sana kupunguza sana uharibifu wa mazingira katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti hasa uharibifu katika vyanzo vya maji.

“Kama shida ya wafugaji ni kufuata maji ndani ya hifadhi basi sasa fedha hizo zitatumika kuchimba mabwawa katika vijiji vyote vinavyozunguka maeneo ya uhifadhi ya wilaya zote mbili”alisema.

Dr.Kohi ambaye ni mtaalamu mbobezi katika utafiti wa wanyapori aliwaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa kulinda mazingira ya ikolojia ya Serengeti ni muhimu kutokana na msingi kuwa vyanzo vingi vya maji vya mto Grumeti unaotegemwa na wanyama na viumbe wengine katika hifadhi hiyo viko katika pori tengefu la Loliondo.

Katika ziara hiyo Kamati ya Bunge ilitembelea eneo la Loliondo na kujionea uharibufu mkubwa katika vyanzo vya maji  vyanzo vya mgogoro wa ardhi unaohusisha uhifadhi na kuchunga mifugo katika Pori Tengefu la Loliondo.

Akizungumzia kwenye ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati Nditie alisema, wamekuwa wakipata malalamiko na maelezo mengi kwamba kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa Loliondo na baadhi ya wawekezaji na hifadhi za taifa.

”Kamati imtembelea eneo la Pori Tengefu la Loliondo  kwa lengo la kujionea hali halisi na tumeshuhudia kwa kweli uharibifu mkubwa katika  vyanzo vya maji ndani na nje ya Pori hili vimeendelea kukauka kutokana na wingi wa mifugo”aliongeza Mwenyekiti huyo..

“Na kwa upande wa Mwekezaji OBC amekuwa akiona kama anahujumiwa kutokana na kuingizwa kwa mifugo mingi katika kitalu cha uwindani ambacho amelipia kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Baadhi ya vyanzo vya maji tulivyoonyeshwa vipo vinavyopeleka maji na chanzo cha maji ya Mto Gurmeti  unaolisha Hifadhi ya Serengeti.Tumelazimika kutembelea maeneo haya ili kujionea hali halisi kisha tutote tamko kama Wabunge litakalookoa hifadhi zetu,” alisema Nditie.

Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Professa Jumanne Maghembe aliwaambia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa Serikali imepanga kutenga eneo la kufuga peke lenye asilimia 62.5 ya eneo lote na eneo la uhifadhi asilimia 37.5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *