NJE ya uwanja, viongozi wa Yanga walicheza ‘kamari’ na ikalipa lakini ndani ya uwanja wachezaji wa Simba wakachezea shilingi chooni na ikatumbukia shimoni na kuwasababishia wao na wapenzi wao maumivu.
Pengine hivi ndivyo unavyoweza kuielezea kwa kifupi mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga Jumamosi iliyopita na Yanga kuibuka mshindi kwa kuwanyuka mahasimu wao hao bao 1-0.
Kwa ushindi huo, nafasi mbili za mwanzo kwenye msimamo wa Ligi Kuu hazikubadilika zaidi ya Yanga kujiongezea pointi tatu muhimu na kufikisha pointi 24 lakini wakiendelea kuwa nyuma ya Simba wanaoongoza Ligi hiyo kwa pointi zao 27.
Sitazungumzia sana yaliyotokea ndani ya dakika 90 za mchezo huo kutokana na ukweli kwamba hakukuwa na jipya na kwamba yale yote yanayotokeaga kwenye mechi zinazopambanisha mahasimu hawa huwa hayana tofauti sana kati ya mechi moja ama nyingine, iwe mwaka jana ama mwaka kesho.
Sitazungumzia pia tuhuma za mchezaji mmoja kumpiga mchezaji mwenzake wa timu moja akimtuhumu kukosa mabaoi kwa makusudi. Kama ni kweli ilitokea mpigaji vichwa huyo aulizwe kwa nini yeye hakufunga bao. Aulizwe pia kama na yeye apigwe vichwa na kisha ashauriwe kuacha mchezo wetu mzuri wa soka na kujiunga na kick-boxing!
Tuseme tu hapa kuwa msisimko pekee wa mechi hiyo ulikuwa ni pale tu mshambuliaji mzambia Davis Mwape alipofunga goli pekee la mchezo huo kwenye dakika ya 72 ya mchezo kutokana na mabeki wa Simba ‘kuchezea shilingi chooni’ na hivyo kupeleka kilio mtaa wa Msimbazi.
Kinadharia na kimahesabu Simba walikuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda mchezo huo. Si tu kwamba timu hiyo ilikuwa inafanya vizuri kwenye Ligi bali pia ilikuwa ndio kwanza imepata nguvu za ziada kwa kuongezwa kwenye kamati zake mbali mbali majina ya watu wenye ushawishi mkubwa miongoni mwa jamii ya Watanzania akiwemo Zitto Kabwe, mbunge wa jimbo la Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA.
Pengine hili ndio lililosababisha baadhi ya mashabiki kuanza kushangilia kwa maneno ya ‘CCM! CCM!’ hasa baada ya Yanga kufunga bao lao la ushindi.
Ni bahati mbaya kwa Simba kwamba mpira hauchezwi kwa nadharia na mahesabu pekee bali ni jumla ya mambo mengi ndani na nje ya dakika tisini za mchezo.
Nadharia mojawapo kubwa iliyotumika kuipa Simba nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo ilikuwa ni ile iliyotokana na viongozi wa timu ya Yanga kubadilisha kocha wa timu hiyo siku nne tu kabla ya mchezo huo kufanyika, hatua iliyowashangaza na kuwatia tumbo joto wengi wa wanachama na wapenzi wa timu hiyo.
Yanga waliamua kukatisha ghafla mkataba wao na kocha wake Mganda, Sam Timbe na kuingia mkataba mpya na kocha asiyekuwa mpya kilabuni hapo, Kostadic Papic ambaye walimfungisha virago miezi minane kabla.
Tukumbuke kuwa Sam Timbe aliingizwa Yanga kwa vishindo akitanguliwa na sifa kubwa ya kuwa kocha pekee aliyeweza kutwaa ubingwa wa michuano mikubwa kwa vilabu kwenye kanda hii ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati akiwa na vilabu vinne tofauti.
Alifanikiwa kuongeza uzito kwenye CV yake hiyo pale alipoiwezesha Yanga nayo kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati na hivyo kuwa kocha wa kwanza kutwaa kombe hilo akiwa na vilabu vitano tofauti, sifa ambayo huenda ikawachukua makocha wengine muda mrefu kuifikia.
Kwa hakika ilishangaza na kuwashitua si vidogo wapenzi wengi wa Yanga kuona timu yao ikiamua kumtema kocha wake huyo wakati ikiwa kwenye maandalizi ya kupambana na mpinzani wake wa jadi pamoja na kuwa kocha huyo alikuwa ameiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kuanza kwa kusuasua.
Badala ya Timbe, Yanga iliamua kulamba matapishi yake na kumchukua tena kocha waliyemtema Februari mwaka huu, Kostadic Papic ambaye baada ya kuondoka nchini alipata kibarua cha kufundisha timu ya El-Hilal ya Sudan na baadaye kuiwezesha kufika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Mabingwa la Afrika.
Naam, yale yale ya ukiona wa nini wenzako wanajiuliza watampata lini! Napenda kuamini kuwa viongozi wa Yanga walifadhaika kwa kiasi fulani kuona kocha waliyemfungisha virago akiiwezesha timu ya nchi ya jirani ikifika hatua ya nusu fainali kwenye michuano mikubwa ya vilabu barani Afrika ambayo timu zetu bado zinaishia kuiota tu ama kukumbushia rekodi ya mwaka 1974 ya Simba ya kufika robo fainali!
Upo uwezekano mkubwa kwamba mfadhaiko huu ndio uliowafanya viongozi wa Yanga kuamua kumrejesha kwenye benchi lake la ufundi kocha huyo. Lakini basi ndio iwe siku nne kabla ya timu hiyo haijapambana na mahasimu wake wa jadi?
Nionavyo viongozi wa Yanga walikuwa wamepiga mahesabu ya ‘ki kamari kamari’ hivi, ya kutarajia timu yao kuifunga Simba na hivyo sifa za ushindi huo kurundikwa kwa kocha Kostadic Papic hivyo kuhalalisha kurejeshwa kwake klabuni hapo na hivyo kuzima shauku za wanachama na wapenzi wa timu hiyo kutaka kufahamu sababu za kweli za kuondoshwa Sam Timbe.
Kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao, hilo limewezekana na hali sasa inatarajiwa kuwa shwari Yanga na hakuna atakayekuwa na haja ya kutaka kujua kilichomuondosha Timbe.
Ni dhahiri kwa ushindi huo pia hakuna Mwanayanga atakayejiuliza swali muhimu la kwamba ni hatua gani zilizochukuliwa na viongozi wa timu hiyo kuhakikisha kuwa kilichomuaondoa Papic Februari hakitajirudia na kumuondoa tena Desemba mwaka huu!
Sam Timbe ameondoka lakini ni kweli kwamba tunatakiwa tuamini kirahisi tu kuwa ni uwezo wa kocha mpya asiye mpya klabuni hapo Kostadic Papic ndio umeiwezesha timu ya Yanga kumfunga mpinzani wake na hivyo sifa zote za ushindi huo zimuendee yeye aliyechukua timu siku nne tu kabla mechi?
Jasho la mtu halipaswi kuliwa kirahisi hivyo jamani! Tusimuone baniani mbaya lakini daluga lake tukaliona zuri. Sam Timbe apewe sifa zake anazostahili kwa kuiandaa timu vyema na kuitoa huko mkiani ilikokuwa inashangaa shanga mwanzoni mwa Ligi hadi nafasi ya pili wakati ikijiandaa na mchezo wake na mahasimu wake.
Tusisitize hapa kocha huyo kupewa haki zake zote na kuondoka kwa amani bila manung’uniko yoyote ili isionekane kuwa Watanzania ni wazuri sana katika kuajiri makocha na wachezaji kutoka nje lakini linapokuja suala la kuvunja mikataba na kuwalalia haki zao, pia tu wazuri sana! Hii sio sifa njema.
Pengine Sam Timbe hana haja ya kukosa sana amani kwa kufungishwa kwake virago ghafla kutokana na ukweli kwamba kwa jinsi timu zetu kubwa hizi zilivyo na ‘aleji’ ya kudumu na makocha, upo uwezekano mkubwa kwamba kwenye mchezo ujao unaozikutanisha timu hizo yeye ndio atakuwa anarejeshwa kikosini huku Kostadic Papic akitakiwa kuchapa lapa!
Pengine jambo la kwanza muhimu wanalopaswa kufanya Yanga baada ya ushindi wao dhidi ya ‘Mnyama’ ni kumuweka Papic kitimoto na kumtaka awaeleze siri ya kuifikisha El-Hilal nusu fainali ya Kombe la Mabingwa Afrika wakati hapa walimuona hafai kitu na kumtaka aishie. Kwamba wao Wasudan wameweza wana nini hadi sisi tushindwe tuna nini?
Tatizo ninaloona ni iwapo viongozi hao wataambiwa kuwa siri pekee ni kuacha kuendesha klabu kwa uswahili swahili na blah blah kibao na badala yake kuziendesha kisayansi na kibiashara zaidi! Hapatatosha. Nimalizie kwa kuwapongeza Yanga kwa ushindi wao na timu zote mbili kwa mchezo wa amani.
Toa maoni yako