Ninapokubaliana na kutofautiana na Magufuli

AWALI  ya yote, namshukuru Mwenyezi  Mungu kwa kutulinda, kutupa uhai na afya njema hadi leo. Yote yamewezekana kwa kuwa amependa sisi wajoli wake tuwe hai na wenye afya.

Wako   wenzetu   wakati   huu   wako   hospitali   au   vitandani kutokana na maradhi mbalimbali. Tuwaombee wote walio wagonjwa.

Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujua kwanini wengine kawapa afya njema na wengine kawapa maradhi ya aina mbalimbali. Inawezekana kati ya mnaosoma makala hii sasa, wengine hamtaweza kuuona mwaka 2018.

Ndugu zangu  Watanzania,  ili tuweze kuwa na matumaini ya mwaka mpya wa  2017 tuliouanza, ni vema takatafakari mwaka tunaouaga wa 2016.

Huu ni mwaka wa kwanza tangu Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, ambapo tulimpata Rais mpya, John Magufuli na kuunda serikali yake. Ni  dhahiri kila tunapoingia kwenye uchaguzi, kila mmoja wetu huwa na matumaini ya matokeo ya uchaguzi kuleta unafuu katika maisha yetu ya kila siku.

Ndio maana wakati wa kampeni, tunasikiliza kwa umakini sera   mbalimbali   zinazoletwa kwetu. Hatimaye tunapiga kura kuichagua ile sera ambayo kila mmoja kwenye nafsi yake anaamini itamletea unafuu, itamtoa pale alipo kuelekea kwenye maisha bora.

Kwa wengine ni matumaini ya kutoka kwenye maumivu ya maisha kwenda kwenye unafuu. Kwa   uzoefu   wangu   wa   ubunge   wa   miaka   15   na   miaka   20   kwenye   siasa   ( active

politics), ninaelewa kabisa kuwa wako ambao siku ya pili baada ya uchaguzi wanataka kuona   kero   zao   zimeondoka. 

Kama   tatizo   lilikuwa   maji   safi   na   salama,   hawaelewi, baada ya kumpata kiongozi kwanini siku ya pili, ya tatu, mwezi na hata mwaka baadaye hakuna maji!

Hii ni hali ya kawaida kwa binadamu. Mimi nilichaguliwa  na   watu   wa  Karatu  kutokana   na  kero    kubwa  ya   maji  wilayani Karatu. Maji yalidhalilisha utu wa binadamu hasa akinamama.

Maji yalifanya watoto wadogo kubakwa kwenye vituo vichache   vya   maji   vilivyokuwepo.   Maji   yalifanya mahudhurio  ya   watoto   shule  za   msingi   yadorore   kwa  kuwa  watoto   walikesha   usiku kucha kusubiri maji  kwenye vituo vichache vya maji.

Nakumbuka kila nikipita mitaani, nilianza   kuitwa   tapeli   kwa   kuwa   miezi   sita   baadaye, na kisha mwaka   mmoja   baadaye,   maji yalikuwa   hayajaonekana   kwao.   Mwananchi   wa   kawaida   yeye   hajui   jitihada unazofanya kuleta maji.

Yeye kazi yake ilikuwa kupiga kura, mengine hayamhusu. Hajui kuwa maadui zako wanakuhujumu na kukuvuta chini ili usifanikiwe, kwani kufanikiwa kwako ni kuonyesha udhaifu wao.

Mwananchi haelewi kuwa mikakati ya utekelezaji wa mradi  wowote  haina  budi  kuandaliwa  kwa  umakini,  fedha   zitafutwe, kazi  ya  usanifu lazima   ifanyike.  

Kwa   Karatu,   maji   yalianza kutoka kwenye mabomba mwaka   2000,  wakati   uchaguzi   ulikuwa   1995.   Tone   la   kwanza   la   maji   lilipotoka, wananchi   hata waliokata tamaa, waliodhani wametapeliwa walilipuka kwa furaha ya ajabu.

Walisahau matusi yote waliyokuwa wamenishushia. Sasa wakaanza kubaini kwamba kumbe hawakuwa wakidanganywa. Waliokuwa wavumilivu   waliona   na   kushuhudia   hatua   zote   za   utekelezaji  wa   mradi.  

Waliokuwa wepesi kukata tamaa nusura watukatishe tamaa sisi watekelezaji kwa kejeli, kebehi, matusi tuliyokuwa tukimwagiwa mitaani.

Uvumilivu ulizaa matunda. Wananchi takribani 30,000 walipata maji ya uhakika ndani ya nyumba zao, wengine katikati ya kitongoji chao, vitongoji vingine vilikuwa na DP ( Distribution Points) zaidi ya mbili au tatu.

Hivyo mama anaenda na sufuria na akirudi anabandika jikoni. Hili ni tunda la uvumilivu. Ndugu   zangu   nimeeleza   kidogo   kwa   kirefu   hadithi   hii   ambayo   ilinipata   mimi   na wananchi   wangu   wa   Karatu.  

Ninafahamu pia kwamba mara baada ya ushindi wa Magufuli, makundi tofauti ya wananchi yatakuwa na matumaini tofauti kuhusu matarajio ya nini watakachokipata.

Wamachinga   walijua   mikopo   midogo midogo itapatikana   kwa   urahisi,   na   hawatakimbizwa tena mitaani kama   mbwa. Bodaboda waliozuiliwa kuingia katikati ya miji walijua sasa wamefunguliwa milango na hivyo biashara yao itakuwa rahisi.

Hali hii iko hivyo kwa takribani makundi yote ya kijamii. Kwa miaka mingi, wananchi wetu wameaminishwa kuwa nchi yetu ni tajiri na hivyo wana matarajio makubwa kwa viongozi wao.

Tuna rasilimali za kila aina kuanzia rasilimali chini ya bahari na maziwa yetu, magogo kwenye misitu yetu, rasilimali wanyamapori, ikiwa ni  pamoja na “twiga wetu” aliyekunjwa shingo na kuingizwa  kwenye ndege kutoroshwa.

Kuna kero nyingine pia kama vile maelfu ya  tembo  na  faru   waliokuwa   wakiuawa   bila   huruma    na   majangili   kwa   manufaa   yao binafsi, fedha zetu kwenye benki kuibiwa hovyo nakadhalika.

Wananchi haohao wamesahau kuwa mara baada ya uchaguzi, kazi kubwa ni mapambano dhidi ya “ wahujumu hao”. Kwa

bahati   mbaya   “mpira   usiocheza   hujui   si   rahisi   kujua   ugumu   wake.   Kumbe   hata ukiachiwa peke yako ufunge bao kwenye goli lililo wazi, unaweza kuupaisha juu kwa mshangao wa wengi!”

Hivi ndivyo ilivyo kwa serikali. Natambua  kabisa watumishi  wa  umma walitegemea  mishahara itapanda  na kukidhi mahitaji yao, wanafunzi wa vyuo  walijua mikopo sasa  itakuwa rahisi  na itatoka kwa wakati.

Wazazi walijua “ elimu itakuwa bure hadi kidato cha nne” na hawatasumbuliwa tena, hata kero ya madawati itatatuliwa bila mwananchi kuguswa kabisa! Natambua kuwa matamanio hayo si tu hayakutekelezwa bali maumivu yalikuwa makubwa zaidi kwa   mwaka   wote   wa   2016.

Mitaji   imepotea,   mabenki     hayakukopesha   kwa   hofu mbalimbali, mzunguko wa fedha ulikauka, hata wenye mitaji yao midogo ikaliwa. Hoteli nyingi   kufungwa   kwa   kushindwa   kulipa   mikopo   kutokana   na   kutokupata   wateja.

Watumishi wa umma hawakupewa mishahara iliyotangazwa kupanda. Hii ni hali ngumu na ninatoa pole sana kwa wale wote, kwa makundi yao, walioumia kwa namna moja au nyingine.

Kazi   ya   kwanza   ya   kiongozi   yeyote   makini   anaposhika   dola     ni   kuangalia   mianya mbalimbali ya wizi na  uozo wowote katika usimamizi wa rasilimali za umma. Nadhani wote tunakiri serikali hii ilipoingia tu madarakani, jambo la kwanza lilikuwa kubaini wafanyakazi  hewa.

Leo  tunazungumzia  wafanyakazi  hewa  takribani  20,000.  Fikiria  ni mabilioni   mangapi   kwa   mwezi   yalienda   kwa   wafanyakazi   hewa? Ni   dhahiri   fedha   hizi zingelitengeneza   mzunguko   wa   fedha   kama   zingelikuwa   kwenye   mkondo   sahihi. Hakuna   shaka   kwenye   hilo.  

Lakini   ni   wafanyikazi   hewa,   hivyo   taifa   halikuzalisha kutokana   na   wafanyakazi   hao   hewa.  Ghafla uhakiki unaonyesha kuwa kuna siyo tu waalimu hewa, lakini wanafunzi hewa zaidi   ya   60,000.   Mungu   atusamehe! 

Sijui   tumelogwa!   Taifa   la   ajabu.   Watu “wanatumbua” bila aibu.  Hawa walikuwa wakitumbua fedha zetu kwa manufaa ya “  matumbo yao” na familia zao.

Hatujakaa sawa tukaambiwa kuwa hata fedha za TASAF zilizolenga   kusaidia   kaya   maskini   sana   nazo zimeliwa.   Kaya   takribani   55,000 zilizokuwa   zinufaike   zimekosa huku baadhi   ya   viongozi   wa   serikali   wa   ngazi mbalimbali, wakiwemo maofisa wa TASAF wenyewe wakidaiwa kuhusika na wizi huo.

Hatujatulia mara maelfu ya wanafunzi ambao hawakuwa na sifa za kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu walipewa nafasi!   Ni dhahiri kuwa wazazi wa watoto waliofukuzwa wameumizwa na hatua hii.

Lakini ipi nafuu kuendelea kuwa nao na kuathiri ubora wa elimu hasa katika  dunia ya leo ya ushindani. Wenzetu kila siku wanapambana na ugunduzi wa mipango ya kwenda kwenye sayari mbalimbali kwa lengo la kutafuta sayari yenye kufaa kwa maisha ya binadamu.

Sisi tutaendelea kuwa na mijadala ya kutafuta fefha kwa matundu ya choo. Hadi lini!   Najua lilikuwa uamuzi Mgumu sana Mhe. Rais na Waziri wako wa Elimu. Lakini hapakuwa na njia.

Nashukuru kama wazazi mlifanya jitihada za kuwaelekezea vijana hao penginepo ili rasilimali watu za Taifa zisipotee na wao pia wanufaike na rasilimali za Taifa lao. Ni haki yao.

Haikuishia   tu   kwenye   fedha.  

Bandarini   Kontainer   zaidi   ya   11,000   zinaingizwa   bila kulipiwa kodi na ushuru mbalimbali. Hii ikasababisha milango na mirija   ya ukwepaji kodi kufungwa.

Na dhihiri waliokuwa wakinufaika na kupata “ super profit” kwa kukwepa kodi wataikimbia Bandari yetu. Kitendo cha kuikimbia Bandari, kwa muda athari yake ni kuwa bidhaa zitapungua, na makusanyo ya kodi za Serikali pia yatapotea.

Mzunguko wa fedha katika ujumla wako nao utapungua. Na hivyo hali ya maisha kuwa ngumu kwa kila kundi.

Ndugu zangu, kwa kiongozi yeyote jasiri, mwadilifu, mpenda Taifa lake anakutana na mtihani mkubwa sana. Aidha ni uchaguzi mgumu. Au  aache uozo huo wote kuanzia “ hewa”   hadi   “   ukwepaji   kodi   uendelee   au   audhibiti   kwa   njia   zote   zinazowezekana.

Akiuruhusu maana yake nimkuwa mzunguko bandia wa fedha utaendelea kuwepo na kundi dogo  linalofikiwa  na mzunguko   huo litaendelea  kunufaika lakini  umma  mpana utaendelea kuumia, kama tulivyokuwa tukiumia kabla ya uchaguzi.

Kwa bahati mbaya walio wengi ambao walikuwa hawanufaiki na uozo uliokuwa ukiendelea hawakuwa na pa   kusemea.   Leo   angalau   wamempata   Rais   anayewasemea   wao.     Rais   amekuwa akitumia   neno   “wapiga   dili”.  

Ni kweli waliokuwa wakinufaika ni hao wapiga dili waliotengeneza “ wafanyikazi hewa, hewa, hewa, kila sekta”.

Lakini kwa bahati mbaya wanaoathirika  ni  pamoja  na   mama  lishe,   na  wafanyibiashara     ndogo  ndogo  ambao kimsingi hawahusiki kwa lolote lile na kupiga dili.

Wao wanafanya biashara wakati hao wachache wakipiga dili.   Lakini hapa ndipo palipo na msemo, “mtego wa panya kuwakamata wahusika na wasiohusika”. Hii ndio inayoitwa “Dilemma”.

Unachagua kipi? Uache   uozo   na   ufisadi/   huu   mkubwa   uliofilisi   nchi   nzima   uendelee   kwa   ajili   ya kuwasaidia wenye biashara ndogondogo au funga njia, kwa muda tutaumia, rudisha nchi kwenye reli na   baada ya muda fungua milango kwa biashara halali.

Kweli kwa uamuzi huu liko kundi  litaumia sana. Lakini taifa likirudi kwenye reli, kundi hilo na wote tutanufaika. Taifa zima litanufaika. 

Nina   hakika   tukiisha     kurudi   kwenye   mstari  ajira zitatoka kwa utaratibu unaotakiwa,  fedha za  miradi  zitatoka na  mzunguko wa fedha utarudi kama kawaida. Maamuzi magumu yanahitaji kushirikiana lakini pia uvumilivu mkubwa. Hakuna jambo jema linapatikana kirahisi.

Najua kuwa kuna wengi wanalalamika. Wako wasomi kati yao. Lakini kama wasomi hao   wana   dhamira   njema,   miaka   yote nchi   ilipokuwa   inatopea     kwenye   dimbwi   la ufisadi,   uwizi   huu;   mbona walikaa kimya?

Mbona   hatujusikia   sauti   yao.   Wasomi   hao   wengine   wao   si   ndio walikuwa pia wakikusanya mamilioni wakati mwingine kwa “Dola Za Marekani” kwa kilichokuwa kikiitwa kazi za kiushauri  yaani Consultancies?

Wengine walikuwa wakiandika rasimu za sheria mbovu lakini wakiishia kujikusanyia mamilioni ya fedha. Kwa bahati nzuri sizungumzii nadharia. Ninayafahamu yote ninayosema kwa undani.

Mambo ya “ Watumishi hewa”, wanafunzi hewa Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Serikali za Mitaa tulianza  kuyazungumzia  mwaka 2007. Mbona   tangu wakati huo wakati  huo   hatukumwona  msomi   yeyote akifanyia utafiti ( hata baada ya kuwarahisishia   kwa taarifa za LAAC).

Tuache kudanganyana.   Hawa wasomi wetu hawakuona huo ufisadi , wizi   na   uozo   huu   wakati ulipoanza ?   Leo   ndiyo   wanaona   uchungu   au   kwa   sababu   kwa   namna   moja   au nyingine na wao pia wameguswa?  Japo si wasomi wote.

Watu   wanalalamikia     safari   za   nje   kuzuiwa.   Tena   wanaihusisha   na   mgawanyo   wa mamlaka   na   kuwa   Rais   anaingilia   mamlaka   zingine.   Hivi   mwaka 2014   nilipotaka   Bunge kufanyiwa   “Special   Audit”   kwa   ziara   za   kibunge   zilizokuwa   zikitumbua   fedha   bila manufaa kwa taifa walikuwa wapi?

Ni sekta ipi katika nchi yetu ambayo haikuguswa na Ufisadi? Hatimaye mwajibikaji mkuu wa fedha za Umma ni Rais kwa mujibu wa Katiba. Iweje basi akichukua hatua ionekane kuwa ameingilia mamlaka zao?

Ni kweli siyo kila kitu cha Serikali ya Awamu ya Tano mimi naunga mkono. Mimi siungi mkono kujenga  reli  kwa  fedha  nyingi kwa Standard  Gauge. Labda tuambiwe  kuwa wakati inajengwa kwa Standard Gauge wanazungumzia pia Electrification.

Nilikwishasema “ we do not have to re- invent the wheel”. Leo unatoka Hamburg kwenda Munich Ujerumani takribani umbali wa kilomita 1500 kwa muda wa saa 3 tu. Sisi tunakwenda Dar- Mwanza na treni inachukua siku tatu hadi nne.

Hii ni karne ya sayansi, hatuhitaji kuwekeza fedha kama hatutaenda   kisasa.   Inatakiwa   mtu   alalale   nyumbani   kwake   Mwanza   anaenda kufanya kazi Dar na kinyume chake.

Tunataka bidhaa za viwanda na za kilimo zizalishwe kwa wingi Mwanza, Mbeya na Kigoma na zifike katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda usiozidi saa tatu na si baada ya wiki.

Nchi hii haiwezi kuendelea kwa namna ya kufikiri ya mwaka 1947. Wasomi wetu wana jukumu la kujitafakari na kubadilisha namna yao ya kufikiri na kutoa mchango kwa taifa kama wanahitaji  tuwatambue kwa usomi wao.

Wanasiasa wetu nao ajenda isiwe kuingia Ikulu pekee. Ajenda iwe namna ya kuliondoa taifa kwenye “ mduara” ( Vicious Circle) tulioko na mkakati walio nao wa kulipeleka taifa tunakotaka.

Kwa   ujumla   nchi   ilikosa   mtu   wa   kusimamia   rasilimali.   Nchi   ilikosa   mtu   wa   kutoa maagizo   na   maamuzi. Nchi   ilikosa   usimamizi   na   mtu   wa   kukemea.   Rais   JPM

amejidhihirisha kuwa anayo nia, anayo dhamira na anao ujasiri na uwezo wa kufanya.


Mwandishi wa makala hii aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Jimbo la Karatu kupitia chama hicho. Anapatikana kupitia email ya wpakoslaa700@gmail.com

6 thoughts on “Ninapokubaliana na kutofautiana na Magufuli”

 1. Evodius Rwenyagira says:

  Nakubaliana na wewe Dk Slaa kwa mtazamo wako na maono ya mbali kwa lengo la kuendelea kupata mafanikio kwa taifa letu. Tofauti yangu ni juu ya ujenzi wa reli ya kati hapa napatazama kwa mfumo wetu wa umeme usio kuwa wa uhakika unaweza ukatuchelewesha kufanikiwa kwenda mbele. Tutakapo kuwa na uhakika wa umeme tunaweza fikiria kuwa electrification kwa upana wake .

 2. Msuha Odilo says:

  Hongera sana Dr. Slaa kwa makala nzuri,  ni kweli tulipofikia tunahitaji uvumilivu wa hali ya juu , ni kipindi cha mpito tutegemee mambo mazuri yanakuja lakn hayawez kuja kadiri dhamiri zetu zinavyotaka lazima tuweke misingi imara ili hata watakaokuja waikute nchi ikiwa  na Misingi imara ya kiutawala, ni kweli kero za wananchi huwezi kuzitatua kwa simu moja na zikaishi, tunamatatizo mengi kila sekta unayogusa inauozo, tulikuwa huru sana kiutendaji sasa tufanye kaz kwa kufuata misingi inayowekwa na mhe Rais.

   

 3. lawrence says:

  Electrification railway na electromagnetic trains ndio solution,umeme wa gesi unaandaliwa ,hilo lawezekana kwa awamu,na vision hii iwekwe ktk ilani za uchaguzi.

 4. Katema R M M says:

  Ni kweli na uko sahihi kabisa mzee, hii nchi ilihitaji mtu wa namna ya Magufuli. mi pia niko upinzani, lakini ukweli utabaki kuwa ukweli, mkuu wa nchi aliyemaliza muda wake alitufikisha hapo. meli zinaingia zaidi yasitini kisha zinayeyuka bila kulipa kodi kana kwamba hazikuwahi kuwapo. Flow meter bandalini ya kupimia kiwango cha mafuta yanayoingia nchini ili kodi itozwe sawasawa nayo ilikuwa imehujumiwa kwa miaka kadhaa, wafanyakazi hewa, mishahara hewa, wanafunzi hewa, tasaf, wanyama wetu mbuga na hifadhi za taifa kuuwawa na kutoroshwa nje ya nchi, mikataba mibovu ya wawekezaji inayopelekea wakati mwingine migogoro ya wakulima na wafugaji baada ya wawekezaji kumilikishwa maeneo makubwa, ufidadi na rushwa vya kupindukia ilikuwa kama ni sehemu ya maisha. Lakini pia nataka nikiri kwamba tulichelewa saana kupata rais kama MAGUFULI. RAIS sisi watanzania tulio wengi(bila kujali itikadi za vyama vyetu) tunakuunga mkono na tuko pamoja na wewe, ila tunaomba kitu kimoja tu, RUHUSU UHURU WA VYAMA VYA SIASA KUFANYA MIKUTANO ya kisiasa kama katiba na sheria za nchi zinavyotaka, maana jambo hili pekee ndilo linalokutia doa hata kwenye sura ya kimataifa, uliapa kuilinda na kuitetea basi ilinde. Asanteni

 5. Evaristo Sanga says:

  Ushauri wangu kwa watanzania,TUWE macho na makini na watu wanaoitwa WASOMI,wengi wao wanayajali matumbo yao na wako radhi kupindisha hata tafiti zao ili mradi kuwafurahisha wakubwa wao.Kwa uthibitisho embu wafanyieni tathimini jinsi miaka miwili iliyopita walikuwa wanasema nini juu ya utendaji wa serikali na sasa wanasema nini juu ya serikali hii? Na ninaamini wanaotuangusha siku zote ni hawa WASOMI WETU,Ni mkulima yupi anahusika na wafanyakazi hewa?TASAF hewa? wanafunzi hewa? na hadi wanatengeneza akaunti hewa za maafa! Natamani JPM angeongeza kukaza kamba

 6. Magdalena K.Ngaiza says:

  Yanayosemwa hayana ubishi lakini lazima tufahamu kuwa Wasomi wako katika makundi na taaluma mbalimbali. Kila taaluma ina mchango wake unaokubalika na usiokubalika. katika maisha yetu siasa iliyoitwa 'mchezo mchafu' ndiyo inayoruhusu sauti zitakazosikika na zitakazonyamazishwa. Hivyo ukifanya utafiti utakuta kuna michango ya wasomi iliyonyamazishwa kwa visingizio fulani ilimradi baadhi ya watu waendelee kufaidi. Mojawapo ya ugomvi kati ya msomi na serikali ni jinsi ya kubuni na kusaidia maendeleo ya mkulima bila watawala (structural dominance) kuingilia kati kivyao. Mfano, zimepatikana bilioni moja kwa maendeleo ya kijiji/vijiji fulani, hebu nipe picha ya sakata hilo! Au msomi aseme demokrasia haitoshi, anaitwa msomi kichaa,ingawa mimi pia nakubaliana na demokrasia kiasi (ushiriki) na udikteta zaidi (kwa muda) ili kujenga nidhamu na kasi ya maendeleo katika nchi kama yetu ambapo wenye uwezo wa kutenda kama nusu ya Rais Magufuli ni wachache. Kwa hiyo tukubali kwamba wasomi tuchukue sasa hatua katika kuonesha yale tunayoamini na kujua yatasaidia nchi kama vyama vya ushirika endelevu (vilitusomesha) na sayansi na tekinolojia. Wasomi lazima washuke chini katika kufanya tafiti na jamii (Action research) ili kuwezesha jamii kutembea kama 'jeshi' na si vinginevyo. Mfano wa maji wa Dr.Slaa ni moja ya mifano mizuri, na kuwaua watendaji/viongozi wazuri kama marehemu Mh.Phili Kunjombe ni hasara. Inabidi walindwe kwa nguvu zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *