Ninavyousoma mchezo wa Shinzo Abe

DESEMBA 26 mwaka jana, nilimuona kwenye televisheni Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, akiweka shada la maua katika bandari ya Pearl, kule Hawaii, Marekani, ambako marubani wa jeshi la Japan walijilipua kwa staili ya Kamikaze, mwishoni mwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Ziara ya Abe kwenye eneo hilo ni ya kwanza kufanywa na Waziri Mkuu wa Japan tangu kutokea kwa tukio hilo lililosababisha Marekani kuamua kutumia silaha za nyuklia kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki nchini Japan.

Lakini kuna jambo moja ambalo halisemwi kuhusu ziara hiyo ya Abe. Kwamba Waziri wake wa Ulinzi aliyefuatana naye Marekani, Tomomi Inada, alitembelea hekalu la Yashikuni mara tu baada ya kurejea Japan.

Hekalu la Yashikuni ni sehemu ambako Wajapani huenda kuwaombea na kuwatukuza mashujaa wa taifa lao. Miongoni mwa wanaoombewa na kutukuzwa ni watu ambao walifanya unyama kwenye nchi mbalimbali huko nyuma.

Miongoni mwao ni Hideki Tajo, Waziri Mkuu wa Japan wakati wa vita hiyo ambaye alihukumiwa kifo baadaye kutokana na na matendo yake ya wakati wa vita.

Majirani wa Japan, nchi kama China, Korea Kusini na Ufilipino, hukasirika mno wakati viongozi wa Japan wanapotembelea hekalu hilo. Kwao, hekalu hilo ni alama ya unyama waliofanyiwa na Wajapani huko nyuma.

Inada anafahamika kama mmoja wa mawaziri walio vipenzi vya Abe. Kitaaluma, mwanamama huyu ni mwanasheria na hana uzoefu wowote wa masuala ya kijeshi.

Nadhani Abe amempa nafasi hiyo kwa sababu kuu mbili; mosi kwamba mama huyu ana mrengo mkali wa kisiasa na pili ni taaluma yake.

Inafahamika kwamba Abe anatamani kufanyiwa mabadiliko kwa Ibara ya Tisa ya Katiba ya Japan iliyotungwa baada ya kumalizika kwa Vita ya Pili ya Dunia.

Marekani iliyoshinda vita hiyo haikutaka Japan iwe na jeshi lenye nguvu baadaye, na hivyo kwenye ibara hiyo iliwalazimisha Wajapani kwamba wasitumie zaidi ya asilimia moja ya Pato lake la Taifa kwa ajili ya matumizi ya kijeshi.

Hii ni ibara ambayo Abe anataka kuinyofoa kutoka katika Katiba yao. Kwenye mizungu hii ya kisheria, atahitaji sana mchango wa Inada ambaye ni mwanasheria.

Atahitaji pia suala hilo lipitishwe na Bunge la Japan na wananchi wa Japan pia katika Kura ya Maoni. Lakini, na muhimu sana, ni lazima kwanza Marekani ikubali.

Nadhani Abe ameangalia fursa na kuona hakuna wakati mzuri kama huu akitaka kufanya hivyo. Kwanza Marekani imepata Rais ambaye ametangaza rasmi kwamba hataki kuingia gharama kuzilinda nchi nyingine kama Japan.

Ndiyo sababu Abe alikuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kukutana na Donald Trump hata kabla hajaapishwa.

Ni wazi atakuwa amemwambia kwamba kama Marekani itakubali Japan iondoe ibara hiyo, yeye hatahitaji msaada wa Marekani kama ilivyo sasa.

Pili, Wajapani hawana amani sana na ukuaji wa China kiuchumi na kijeshi. Wanafahamu kwamba historia yao ya nyuma inamaanisha mambo yanaweza kuharibika wakati wowote baina yao.

Trump pia yaonekana haipendi China. Ni wazi kwamba Shinzo Abe atakuwa amemwambia kuwa Japan inahitaji kujilinda dhidi ya China. Ili iweze kufanya hivyo, inahitaji ibara ya tisa ilegezwe au kufutwa kabisa.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan, hayati Lee Kuan Yew, amewahi kuandika mara nyingi kuhusu Wajapani. Kwamba kwanza viongozi wake, hasa wale wa kutoka chama cha LDP, hawajawahi kuomba radhi kwa matukio ya nyuma ya askari wake.

Yew alieleza kwamba wakati Wajerumani wamewahi kuomba radhi kwa makosa yaliyofanywa wakati wa utawala wa Adolf Hitler na wanawafundisha hadi watoto kuwa wasije wakarejea huko, Wajapani hawafanyi hivyo.

Kwa mfano, ni jambo la kawaida kuona wasifu wa Mjerumani ukieleza namna alivyoshiriki kwenye Vita ya Pili ya Dunia.

Kama alikuwa askari, mateka, mfungwa nakadhalika lakini Wajapani wengi utaona hawajazi kitu kuhusu walichofanya kati ya mwaka 1936-1945. Ni kama vile hawataki kuzungumzia wakati huo.

Kama Wajapani hawako tayari kuomba radhi kwa yaliyotokea huko nyuma, maana yake ni kuwa wanaweza kufanya hivyo tena itakapotokea fursa hiyo.

Katika wasia wake wa mwisho kabla ya kunyongwa, Tajo aliandika kwamba Japan walipigwa kwa sababu walizidiwa na Jeshi lililokuwa na nguvu kuliko wao. Ni kosa ambalo vizazi vijavyo havitakiwi kulirejea.

Shinzo Abe anajaribu kurekebisha kile ambacho Tajo alikisema wakati huo. Kwa kuweka mazingira ya Japan kuwa na jeshi kabambe.

Lee Kuan Yew ameasa katika mojawapo ya maandishi yake kwamba dunia inatakiwa iwe makini sana na nyendo zozote za Japan kutaka kurejesha nguvu yake ya kijeshi.

Wakorea, Wachina na Wafilipino wanajua nini maana ya kuwa chini ya mkono wa kijeshi wa Japan. Ni habari mbaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *