Makala
Nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere? IV
Godfrey Dilunga
Toleo la 226
15 Feb 2012
  • Siku RTD ilipoamrishwa kufuta taarifa ya habari za Nyerere

WIKI iliyopita katika mfululizo wa makala hizi, nilirejea baadhi ya hoja za aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Horace Kolimba, katika kujibu mapigo dhidi ya ukosoaji wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwake na wenzake ambao ni Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, kupitia kitabu chake maarufu, Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.

Niliahidi pia wiki hii kurejea baadhi ya vituko alivyokutana navyo Mwalimu Nyerere, ikiwa ni pamoja na siku alipofika Ikulu, Dar es Salaam, kuzungumza na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson.

Itakumbukwa kuwa katika makala zilizopita na hasa makala ya kwanza, nilieleza namna ambavyo haikuwa ikijulikana wazi kama Rais Mwinyi kwa wakati huo na Waziri Mkuu Malecela, walikuwa wakiunga mkono mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere, na hasa ikizingatiwa Kolimba alijibu akitumia magazeti ya chama (Uhuru na Mzalendo), akiwa Katibu Mkuu na mwenyekiti wake, Rais Mwinyi akibaki kimya.

Katika ukimya huo, kuna mambo tunaweza kuyatafakari. Kwanza, inawezekana Mwinyi na Malecela na baadhi ya viongozi wakubwa walikuwa nyuma ya Kolimba lakini hawakutaka kumkabili Mwalimu moja kwa moja na kwa hiyo, wakatumia matukio mengine kuzidi kumkosesha ‘raha’ Mwalimu Nyerere ambaye hakuwa na madaraka zaidi ya kuwa mstaafu, ingawa aliendelea kuwa na ushawishi katika mifumo ya dola.

Hebu turejee baadhi ya mikasa inayoweza kuhusishwa na ‘hasira’ dhidi ya Mwalimu ambaye aliamini uongozi umefeli katika masuala muhimu ya kuongoza nchini kwa wakati huo hadi kutunga kitabu cha kuukosoa uongozi huo.

Jumanne ya Oktoba, 11 mwaka 1994, moja ya magazeti ya binafsi nchini lilichapisha habari ikiwa na kichwa cha habari; “Nyerere akosa mapokezi Ikulu.”

Lilikuwa ni gazeti la kila wiki (WAKATI ni Huu), wakati huo likitamba katika kuibua habari zenye mitafaruku (controversies), Mhariri wake akiwa Katibu Mkuu wa sasa wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mukajanga.

Ikumbukwe kuwa kwa wakati huo, tayari Mwalimu alikwishaanza kuwakosoa viongozi waandamizi wa Serikali, akiwamo Rais kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa kiuongozi na nchi ilikuwa ikielekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.

Mwandishi wa gazeti hilo ambaye hakutajwa jina aliripoti kwamba; “katika hali isiyokuwa ya kawaida, maofisa wa Ikulu mwishoni mwa wiki walishindwa kumpokea rais mstaafu, Mwalimu Nyerere wakati alipowasili katika ofisi za Ikulu kwa mazungumzo na Rais wa Ireland , Bi. Mary Robinson.

“Ingawa ratiba ya ziara ya Rais wa Ireland iliyotolewa siku moja kabla ya kuwasili kwake ilikuwa inaonyesha wazi wazi kuwa Mwalimu angekuwa na mazungumzo na Rais huyo, hakuna kiongozi wa Ikulu aliyeonyesha kujishughulisha kumpokea”.

Mwandishi anaendelea kuandika; “Mwalimu ambaye alifika Ikulu saa kumi na moja na robo, jioni Ijumaa, alijikuta hana mtu wa kumlaki na kumwelekeza.”

Lakini swali jingine ni je, hali ilikuwaje katika kumnusuru Mwalimu? Hapo, mwandishi huyo anaandika kwamba, ili kumuepusha Mwalimu Nyerere na balaa la kuendelea kuduwaa, mpambe (msaidizi) wake alimpeleka kwenye makochi inapofanyika mikutano ya kila wiki ya waandishi wa habari na mwandishi wa Rais (Patrick Chokala).

Katika hali inayothibitisha mwandishi alikuwa akishuhudia kile ambacho yeye na waandishi wenzake walikiita ni udhalilishaji dhidi ya Mwalimu Nyerere, mwandishi huyo anaandika; “….kabla ya kuketi, Mwalimu alichukua muda kuangalia huku na kule kulitazama jumba lililokuwa ofisi yake miaka tisa iliyopita.”

Na baadhi ya waandishi wa habari waliokuwapo wakati Nyerere anawasili Ikulu, walisema kuwa kitendo hicho cha kutokuwapo mtu wa kumlaki Nyerere kilikuwa cha kumdhalilisha.

Waandishi hao wananukuliwa wakisema; "Huu ni udhalilishaji. Haiwezekani viongozi wa itifaki wa hapa washindwe kuwa na mawasiliano kwamba Mwalimu anawasili."

Pengine tuzidi kukumbushana, hatupo nje ya mada kuu kwamba nini kilichotokea kati ya Kolimba na Nyerere, kwa sababu, tunalo swali la msingi, je, mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere yalikuwa yakiungwa au kutoungwa mkono na viongozi wengine waandamizi ambao Nyerere aliwashambulia kwa pamoja?

Na kabla ya kuachana na kisa hiki kinachotusogeza katika nafasi ya kutafakari kama ukosoaji wa Mwalimu dhidi ya viongozi waandamizi, ikiwamo Ikulu, uliwakasirisha kiasi cha kumfanyia vituko, tutazame nani aliokoa jahazi la udhalilishaji.

Inaelezwa kuwa, siku hiyo kama asingekuwapo aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ali Mchumo, Mwalimu angezidi kuzubaa hapo Ikulu.

Alikuwa msaidizi wa Mwalimu ndiye aliyemuona Balozi Mchumo, akamwita kutoka katika chumba (ofisi) alimukuwamo Rais Mwinyi na mgeni wake, Bi. Robinson na kwa mujibu wa ofisa mmoja wa Ikulu aliyezungumza na mwandishi huyu, basi Nyerere angeendelea kusubiri kwa muda mrefu na iliaminika kuwa uvumilivu ulianza kumwishia Mwalimu na alikuwa akijiandaa kuondoka Ikulu, bila kuonana na mgeni, kama ilivyopangwa kwenye ratiba.

Taarifa ya habari RTD ‘yazimwa’

Iliripotiwa na moja ya magazeti na tena bila kukanushwa siku zilizofuata, kwamba aliyekuwa Waziri wa Habari na Utangazaji, Dk. William Shija, alizuia taarifa ya habari ya saa mbili usiku, kutosomwa kwa habari iliyotokana na mkutano kati ya Nyerere na waandishi wa habari, waliokutana nyumbani kwake, Msasani, jijini Dar es Salaam.

Kwa wafuatiliaji wa mambo, itakumbukwa kuwa kulikuwa na mvutano mkubwa kati ya msimamo wa Mwalimu Nyerere na Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, kuhusu mauaji yaliyokuwa ya raia yaliyokuwa yakiendelea nchini Rwanda, na mvutano huu ni kati ya mambo ambayo, Nyerere aliamini uongozi wa nchi ulikuwa ukiyumba si tu kutokana na udhaifu wa Rais, bali hata washauri wake wakuu.

Ilikuwa Julai 4, mwaka 1994, Mwalimu alikutana na waandishi wa habari na akishinikiza Serikali ya Tanzania , nchi aliyokuwa akiifahamu kuwa madhubuti katika kutetea haki za watu popote duniani, iweke wazi msimamo wake kuhusu Rwanda .

Hadi Mwalimu anazungumza, tayari takriban watu 700,000 walikwishauawa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe Rwanda, tangu Aprili 6, 1994 alipouawa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana.

Mwandishi wa habari wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) aliyehudhuria mkutano huo wa Nyerere alirudi ofisini, akaandika kilichojiri huko kwa ajili ya kurushwa hewani katika habari ya saa 2:00 usiku kama kawaida.

Lakini licha ya habari hiyo kupitiwa na mhariri wa zamu na mhariri mkuu na kuridhiwa, inadaiwa kiongozi mmoja wa zamu (studio) alimpigia Waziri Shija, kumuuliza habari hiyo itangazwe au la. Ikabidi Waziri Shija akasomewe kwanza habari hiyo kabla ya kuamua na baada ya kusomewa, akakataa itangazwe.

Swali muhimu ni je, kwa nini habari ya Mwalimu ilizuiwa? Je, ni kwa sababu inaishinikiza Serikali? Je, ni kwa sababu imetamkwa na Nyerere bingwa wa kuwakosoa viongozi waliokuwapo madarakani? Au je, ni kwa sababu kuna viongozi walijenga mtandao wa kumuasi Mwalimu? Na kama kulikuwa na mtandao huo, je, ulikuwa nyuma ya mapigo ya Kolimba dhidi ya Nyerere?

Kimsingi, katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mwalimu ambaye baadaye alikuwa msuluhishi wa mgogoro huo wa Rwanda , aliilaumu Serikali kwa kushindwa kueleza msimamo wake wa wazi katika vita hiyo ya Rwanda .

Waandishi waliokuwapo kwenye mkutano huo wa Mwalimu waeleza alichosema Nyerere kuwa; “…anashindwa kuelewa ni vipi nchi iliyokuwa huko nyuma inao msimamo unaoeleweka ilikuwa inayumba kiasi hicho katikati ya wimbi lenye kasi kubwa ya mauaji ya raia wa nchi jirani.

Ikulu yasema ni hisia za Nyerere

Kama tulivyojiuliza maswali machache hapo awali, je, kwa nini Mwalimu aliandamwa? Sasa baada ya mkasa huo wa Nyerere na RTD, mkasa ambao ni wenye mwelekeo wa kuzidi kukosoa uongozi mkuu wa nchi, aliyekuwa mwandishi wa habari wa Rais, Patrick Chokala, alikutana naye na waandishi wa habari, Ikulu siku chache baadaye.

Lakini katika mkutano huo, Chokala hakutoa nafasi kwa waandishi kumuuliza maswali zaidi, ingawa mada ya mkutano wake huo ilikuwa kuhusu suala la Rwanda , ambalo kwa mujibu wa ukosoaji wa Mwalimu, uongozi wa nchi ulikuwa unayumba kimsimamo.

Chokala pengine akitambua kuwa waandishi walikuwa wanazo taarifa nyingi zaidi ambazo ni mbaya kwa Serikali, alimpinga tu Mwalimu kwa kusema alichopata kueleza ni “hisia zake” tu na kukwepa maswali.

Nyerere ‘alimkumbuka’ Karume?

Bila shaka, ukosaji wa Nyerere dhidi ya akina Kolimba na wenzake kupitia kitabu cha uongozi wetu na hatima ya Tanzania , umezingatia mambo mengi.

Bila shaka, ukosoaji wake haukuzingatia tu mwenendo alioamini wa ovyo kuhusu namna uongozi unavyoamua, kudhibiti au kutolea msimamo mambo mazito ya nchini na kimataifa, bali pia ulizingatia namna walivyoihangaikia nchi, yeye na waasisi wenzake, akiwamo Abeid Amani Karume na hasa zinapojitokeza dalili za kuhujumu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar .

Utaona kwamba, licha ya Mwalimu kuchukizwa na namna uongozi ulivyoyumba kusimamia Muungano, lakini pia alichukizwa na namna uongozi unavyoshughulikia mambo mengine ya msingi yenye kujenga taswira ya nchi kimataifa. Yote haya yalimfanya kuwakosoa washauri wakuu wa Rais na Rais mwenyewe, kupitia kitabu chake.

Ni kweli, yapo mengi yanayoelezwa kuonyesha pengine Karume alichoshwa na Muungano ambao Nyerere aliutetea na hata kuwakosoa baadhi ya viongozi.

Lakini hata hivyo, ni Karume huyo huyo, ambaye aliwahi kunukuliwa na gazeti la The Nationalist (sasa Daily News), akisema Muungano unanufaisha wananchi, asiyeutaka ahame nchi.”

Gazeti la Julai 30, mwaka 1964, The Nationalist, liliandika habari hiyo kutokea Zanzibar nami ninukuu katika lugha iliyotumika; “The  first vice president of the United Republic, Abeid A. Karume told a mammoth rally here yesterday (July 29) that anyone who did not like the union between Tanganyika and Zanzibar "should quit the soil of the United Republic immediately."

Na katika hali ya msisitizo kwenye mkutano huo uliotajwa kuhudhuriwa na watu zaidi ya 50,000, gazeti linaandika katika lugha ya Kiingereza likimnukuu Karume; "The Union has been created for the benefit of the people of the two countries. It embraces their aspirations…..The doors of the United Republic are open to any of our brothers who want to unite with us.

Kwa kiongozi aliyetambua malengo halisi ya Muungano kama hivi ambavyo Karume alivyonukuliwa akisema; bila shaka, si ajabu kumwona Nyerere akipingana na waliokuwa wakitishia uhai wa Muungano lakini kubwa zaidi, kuona Serikali na uongozi wa nchi ukiyumba katika masuala ya msingi ya kiuongozi, kama tulivyoona kupitia makala ya leo kuhusu vituko dhidi ya Mwalimu.

Inaendelea

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Godfrey Dilunga
gdilunga@raiamwema.co.tz
+255-787643151

Maoni ya Wasomaji

Kumbe hata Nyerere alinyanyasika sana na hawa watawala wakati Katiba ya nchi inatamka kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake na kukosoa ni kutoa maoni hawakuwa waungwama jamani hata taarifa ya habari inazuiwa?

Aisee ni kweli viongozi waliokuwa madarakani walistahili kukosolewa na sijui kwa nini walikuwa wanakerwa pale Nyerere alipokuwa anawakosoa, hawakuwa waungwana.

Wewe Hassan achana na mawazo hayo huoni kwamba Mwalimu Nyerere naye alikuwa anavuka mipaka ni kama alitaka kujifanya Rais kivuli. urais sio kama uwaziri bungeni ambako kuna mawaziri vivuli alaa!

Namsifu Nyerere kwa kujitahidi wakati wote kuwa mkweli na kuwakosoa wanaokosea bila kujali wanaweza kumfanyia matukio ya kipuuzi.

Toa maoni yako

Filtered HTML

  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Allowed HTML tags: <a> <em> <strong> <cite> <blockquote> <code> <ul> <ol> <li> <dl> <dt> <dd>
  • Lines and paragraphs break automatically.

Plain text

  • No HTML tags allowed.
  • Web page addresses and e-mail addresses turn into links automatically.
  • Lines and paragraphs break automatically.
To prevent automated spam submissions leave this field empty.
Image CAPTCHA
Enter the characters shown in the image.