- Dk. Salmin, Muungano na Kitengo cha Usalama wa Taifa Zanzibar
WIKI iliyopita katika sehemu ya nne ya mfululizo wa makala hizi nilieleza baadhi ya vituko alivyokumbana navyo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, katika mwelekeo unaodhihirisha ni mwendelezo wa mapigo kwa ukosoaji wake dhidi ya viongozi waandamizi nchini.
Nilieleza namna aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ali Mchumo, alivyomuepusha na balaa Mwalimu Nyerere, aliyefika Ikulu kukutana na aliyekuwa Rais wa Ireland, Bi. Mary Robinson.
Nilieleza namna aliyekuwa Waziri wa Habari na Utangazaji, Dk. William Shija, alivyozuia kipengele cha taarifa ya habari ya saa mbili usiku Redio Tanzania, kilichohusu mkutano kati ya wanahabari na Mwalimu Nyerere, kwake Msasani Dar es Salaam.
Hata wiki nalazimika kufanya masahihisho, kwanza Nyerere baadaye hakuwa msuluhishi wa mgogoro wa Rwanda bali Burundi, pili; gazeti la The Nationalist nililonukuu na kusema ndilo Daily News kwa sasa, si sahihi ukweli ni kuwa, Daily News imetokana na gazeti la The Standard.
Leo tujikite katika kauli ya Kolimba kuhusu hoja ya serikali tatu ndani ya Muungano, kwa sababu hoja hiyo ni kati ya mambo yaliyomfanya Mwalimu Julius Nyerere kukosoa uongozi wa nchi (akina Kolimba, Malecela na Mwinyi mwenyewe), kupitia kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania.
Tuendelee na mfululizo wa makala hizi kwa kugusa moja ya hoja iliyotumiwa na Kolimba, kujibu mapigo ya ukosoaji kutoka kwa Mwalimu.
Itakumbukwa katika moja ya makala zilizopita, tulieleza majibu ya Kolimba dhidi ya Nyerere na hasa alipojenga hoja kuwa, Mwalimu hataki kutambua, mantiki ya serikali tatu inatokana na misingi mibovu ambayo Muungano umesimikwa juu yake na kwamba tatizo si viongozi.
Nilieleza, kwa sababu Nyerere aliwaandama viongozi waandamizi waliokuwa wakishabikia serikali tatu ndani ya Muungano, Kolimba pia alihoji ni kwa nini Nyerere huyo huyo, hakumwandama aliyekuwa Jaji Mkuu, Francis Nyalali?
Nyalali ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa tume kuhusu mfumo wa vyama vya siasa na nje ya hadidu za rejea za tume hiyo, Nyalali na wenzake walipendekeza serikali tatu na hapo Kolimba akahoji; “Kwa nini damu ya Nyalali haikumwagika?” Yaani kwa nini Nyerere hakumwandama?
Leo, tuingie kwenye fikra za Kolimba kwa wakati huo kwa kurejea mahojiano kati yake na aliyekuwa mwandishi wa gazeti la Mzalendo, Joseph Kulangwa, yaliyochapishwa Juni 26, mwaka 1994.
Joseph Kulangwa (sasa ni Mhariri Mkuu-gazeti la Serikali la HabariLeo), alifanya mahojiano na Kolimba yaliyochapishwa katika safu ya “ana kwa ana” kwenye gazeti la Mzalendo.
Kulangwa alimuuliza Kolimba maswali tisa.
Lakini kabla ya kuanza kuuliza swali lake la kwanza, mwandishi alitoa maelezo akisema; “Wabunge hivi sasa wameanza kulipenyeza suala la Serikali ya Tanganyika katika majadiliano ya Bunge, wakati huo huo, utaratibu uliokubaliwa kutumika kuliamua suala hilo katika kikao cha pamoja, haieleweki umefikia wapi.”
Lakini kwa maelezo haya tu ya mwandishi, ukifanya tafakari fupi utabaini; mosi, kulikuwa na nguvu fulani nyuma ya wabunge, kusukuma suala la serikali tatu liingie bungeni.
Lakini je, nguvu (external force) hiyo inajumuisha viongozi gani ambao si miongoni mwa wabunge? Je, ni pamoja na wale ambao Mwalimu aliwakosoa na kueleza bayana, ushauri wao kwa Rais si mzuri, akiwamo Kolimba na hata Waziri Mkuu, John Malecela?
Pili, utabaini pia kuna nguvu nyingine tofauti inayoelekeza kupambana kuzima suala hilo kwa kutengeneza “utaratibu wa namna ya kuliamua suala hilo” kwa mujibu wa maelezo ya mwandishi aliyemuhoji Kolimba.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia maelezo hayo ya mwandishi ambaye bila shaka alikuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kadhia hiyo, ni dhahiri kulikuwa na ‘kambi’ ya Mwalimu Nyerere na kambi pinzani (inawezekana ni akina Kolimba na wenzake). Baada ya tafakari hiyo fupi kutokana na maelezo ya mwandishi, turejee katika swali.
Swali la mwandishi kwa Kolimba lilikuwa; “Chama kinatarajia kulikabili vipi shinikizo la wabunge kuhusu hoja hiyo?
Kabla ya kujua Kolimba alijibu nini, ndani ya swali hili utabaini kuwa; ni kama vile ‘kambi’ ya Mwalimu Nyerere (kama ilikuwapo) ilikuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuzima suala hilo lisizidi kugawa nchi na hata kuifanya isitawalike na hatimaye kuvunga Muungano kupitia ‘uchochoro’ wa serikali tatu.
Na mbinu mojawapo ni hiyo, kutumia chama (chenye hatamu na wabunge wake) kulikabili suala hilo mbinu ambayo hivi karibuni pia ilitumika kuzima wabunge wenye uchu wa posho nono, kwa chama kutoa kauli ya kupinga suala hilo.
Je, Kolimba alijibu nini? Baada ya maelezo na swali hilo, Kolimba akajibu: “Suala la serikali tatu ni hoja kubwa ambayo haitakiwi kuchukuliwa kwa pupa. Kwa hiyo, naamini bado tunao muda wa kutosha kulifanyia kazi.
Akaendelea; “Maoni ya wana-CCM tayari yamepokewa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM inayotarajiwa kukutana baadaye mwezi ujao (Julai, 1994) itayatafakari maoni hayo.
“Nina uhakika pia kwamba Serikali itajipa muda ili yapatikane maelewano kati ya wabunge, Serikali na CCM yenyewe. Siwezi kusema muda huo utakuwa upi, lakini ikumbukwe kwamba Azimio la Bunge lilisema suala hilo litakuwa limepatiwa ufumbuzi ifikapo Aprili, mwakani (1995).
Hayo ndiyo majibu ya Kolimba ambayo bila shaka, wakati wote wa chama kushughulikia suala hilo iwe kwa kusikiliza maoni ya wadau au vyovyote, ilikuwa ni wakati ambao misiguano ya mabishano ilikuwa ikiendelea chini kwa chini.
Inawezekana, kwa kadiri vuguvugu hili lilivyokuwa likishika kasi sambamba na jaribio la kutaka kulizima kwa kutumia chama likiendelea huku Kolimba akiwa Katibu Mkuu wa chama; je, Mwalimu Nyerere alikuwa na sababu za msingi kusaidia kulizima suala hili?
Ingekuwaje kama Nyerere angebaki kijijini Butiama akipalilia mahindi shambani kwake? Sauti ya ukosoaji kwa nguvu ya hoja na hata ikibidi hoja za nguvu kutoka kwa Mwalimu Nyerere ilikuwa na ulazima?
Pengine akikumbuka kilichowahi kutokea mwaka 1984, chini ya ‘mkono’ wa Aboud Jumbe, Nyerere aliamini hicho ndicho kilichokuwa kikielekea kutekelezwa na Rais wa wakati huo Zanzibar, Dk. Salmin Amour Juma na hivyo, na hivyo ilibidi kuingilia kati.
Ikumbukwe, kiini cha masuala haya ni pamoja na Dk. Salmin ambaye alionekana kuwa na ‘mabavu’ kiuongozi kuliko uongozi wa juu wa Jamhuri ya Muungano.
Salmin, pamoja na mambo mengine alitaka kuiburuza Zanzibar kujiunga na Umoja wa nchi za Kiislamu (OIC), bila kujali kufanya hivyo ni kuutia nyufa Muungano.
Swali la pili kwa Kolimba
Kabla ya kuendelea kuuliza swali la pili, mwandishi aliyemuhoji alitoa maelezo mafupi ya utangulizi kwa akisema; “kauli na vitendo vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar badala ya kutafuta muafaka vinaelekea kuchochea hisia za ‘wabara’ kudai Serikali yao.
Anatoa mifano akisema; “mifano ya hivi karibuni ni suala la ushuru wa makontena ambalo limeamuliwa nje ya sheria za Serikali ya Muungano na hivi juzi uamuzi wa kuanzisha kitengo cha Usalama wa Taifa maalumu kwa Zanzibar.” Kisha anamuuliza Kolimba; “unasemaje kuhusu hali hiyo?
Lakini kabla ya majibu kama tulivyofanya kwa swali la kwanza, tutafakari maelezo haya. Ni kwamba, mifano yote hiyo imejikita katika kudhihirisha uongozi wa Zanzibar ulilenga kuvunja sheria zilizokuwapo na si kupendekeza zifanyiwe marekebisho.
Kwa uongozi makini wenye malengo ya maridhiano na ustaraabu na hasa uongozi ambao uko madarakani, sheria hazivunjwi bali hupendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kadiri inavyofaa.
Uongozi kushabikia na kutekeleza uvunjaji wa sheria zinazokera kwao si ishara njema.
Ni kiashiria cha mpasuko, tena mpasuko wenye kuzongwa na maslahi yanayotarajiwa baada ya kutengana.
Baada ya tafakari hiyo fupi; je, Kolimba alijibu nini? Kwa swali hilo, alijibu: “Naamini kuwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais wa Zanzibar wanaupenda Muungano.
Wao ni viongozi ambao tunaweza kuwategemea kutatua matatizo ya mahusiano yaliyopo katika Muungano.
Hiyo ni sehemu ya majibu ya Kolimba na kabla ya kuendelea na sehemu nyingine ya majibu kuhusu swali aliloulizwa, tutafakari; Kolimba anasema anaamini viongozi Zanzibar wanaupenda Muungano.
Swali hapa ni je, kama waliupenda Muungano ni kwa nini walivunja baadhi ya sheria za Jamhuri (rejea uamuzi kuhusu makontena) badala ya kupendekeza zifanyiwe marekebisho?
Je, Kolimba alikuwa akiwalinda licha ya kutambua kasoro nyuma ya viongozi hao kuhusu Muungano?
Na je, kwa namna hiyo ya Kolimba ‘kufunika’ kombe badala ya kuwa muwazi, ilitosha kwa Mwalimu Nyerere kumtilia shaka na hasa ushauri anaoweza kumpa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati huo, Ali Hassan Mwinyi?
Kitengo cha usalama wa taifa Zanzibar
Tuendelee na sehemu ya majibu ya Kolimba kuhusu kitengo cha usalama; “...suala hilo nimeliona tu kwenye magazeti. Sina uhakika na madaraka ya kitengo hicho.
Siamini kuwa kimeondoa ama kuchukua au kuingilia kazi za idara za ulinzi na usalama katika Muungano. Kitengo hicho kinazuia uvujaji wa siri za Serikali toka ofisi mbalimbali za Serikali visiwani.
Anaendelea; “...chombo chochote kitapenda kuhakikisha kwamba taarifa za serikali zinazotoka ni sahihi na kuwa zinatolewa kwa utaratibu unaotakiwa.
Nadhani ndiyo nia kubwa ya kitengo hicho. Lakini nasisitiza kwamba sina taarifa kamili ya kitengo chenyewe.
Hayo ndiyo majibu yake, lakini cha kutafakari ni je, kwa nini atoe majibu hayo yenye mwelekeo wa kulinda ‘kasoro’ ya SMZ ilihali akikiri kutokuwa na taarifa kamili kwa mfano, kitengo cha usalama wa taifa alichoanzisha Dk. Salmin Amour?
Je, hii pia ni sababu iliyomfanya Nyerere kumhesabu Kolimba kuwa ni kati ya viongozi ambao Rais hapaswi kuamini moja kwa moja ushauri wao kama tulivyopata kuona katika makala zilizotangulia na hasa pale Kolimba alipolalamika kwamba Nyerere anamshawishi Mwinyi kutoamini ushauri kutoka kwake?
Wiki ijayo tutaendelea na uchambuzi wa maswali kwa Kolimba hali itakayotuweza kubaini kama Kolimba kwa majibu yake mwenyewe alikuwa na mawasiliano na kundi la wabunge waliokuwa wakitaka serikali tatu ndani ya Muungano, maarufu kama G55?
Inaendelea
Maoni ya Wasomaji
Huyu Salmin ni kweli alikuwa
Huyu Salmin ni kweli alikuwa mbabe sana, nadhani ndiye mwenye rekodi ya ubabe kati ya marais wa zanzibar waliotangulia. Alikuwa na kiburi hata kudharau mamlaka ya watawala kwa ngazi ya Jamhuri ya Muungano kama anavyosema mwandishi alikuwa anaelekea kuchafua hali ya hewa kama ilivyokuwa kwa Aboud Jumbe, mwaka 1984. Article ni nzuri, hongera mwandishi na gazeti la makini la Raia Mwema makala karibu zote ni nzuri na itatupa changamoto wasomaji kuamua kuanza kuisoma ipi kati ya makala hizo.
Naisoma kwa makini makala hii
Naisoma kwa makini makala hii, unajitahidi ila tu kwa kukushauri, si vyema kwa mwamndishi wa makala kila wiki kuleta masahihisho ya makala iliyopita, hii inasababisha uonekane SIO MWANDISHI MAKINI, MVIVU WA KUSOMA NA KUFANYA UTAFITI KUTOKA KWENYE RELIABLE SOURCES!! Jitahidi kuwa na uhakika na unachokiandika KABLA HAKIJACHAPISHWA! Makosa makosa hayapendezi kwenye maandishi ya kitafiti!
Hongera kwa uchambuzi mzuri
Hongera kwa uchambuzi mzuri sana wa habari hii. Huyo Okello yuko wapi kwa sasa?