Nyerere na fitna za Upemba na Uunguja

ALIPOFARIKI  dunia Mwalimu Julius Nyerere Oktoba 14 mwaka 1999, gazeti la Guardian la Uingereza liliniomba niandike makala maalumu ya kuyatathmini maisha yake.

Nilipokuwa naanza kuiandika tathmini hiyo iliyochapishwa siku ya pili yake, niliyakumbuka aliyowahi kuyasema Mwenyekiti Mao wa China kumhusu Josef Stalin, mtawala wa pili wa Muungano wa Sovieti baada ya Vladimir Lenin.

Nami nikayatumia maneno hayohayo kuanzia makala yangu  kwa kuandika: Julius Nyerere was "a great leader who made great mistakes," as one ruler once famously said of another.(“Julius Nyerere alikuwa “kiongozi mkubwa (adhimu) aliyefanya makosa makubwa,” chambilecho mtawala mmoja aliyewahi kumuelezea hivyo mtawala mwenzake.)

Nyerere alifanya makosa ya kinadharia, ya kifikra na ya kiutendaji katika utekelezaji wa sera zake. Sikulidhukuru jina la Stalin kwa sababu sikutaka wasomaji wangu wafanye kosa la kudhania namfananisha Nyerere na Stalin.  Siamini kama Nyerere alikuwa na uovu wa Stalin.  Na kama ilivyokuwa kwa Stalin si yote ya Nyerere yaliyokuwa maovu.  Alitenda mema yanayostahiki sifa.

Watu wa kale wasema: “Kheri ya mja ni ulimi wake na shari ya mja ni huohuo.”  Kwa ulimi wake Nyerere aliwahi kutamka maneno ya maana na mengine ya kibahaluli. Baadhi ya maneno yake yalikuwa kama lulu na baadhi yalikuwa kama utumbo kama pale, kwa mfano, aliposema kuwa hakuna watu waitwao Waswahili.  Nilimsikia akiyasema hayo alipotoa hotuba katika ukumbi wa London School of Economics alipokuwa ziarani London kabla ya kuuacha urais.

Yote hayo yaonyesha kwamba Nyerere alikuwa mja, mtu kama watu wengine.  Hakuwa Mungu, hakuwa malaika. Wala hakuwa mtume na hata hakuwa mpigaji ramli.  Na si kila alichokitamka kilikuwa sahihi.  Lakini binadamu yule alikuwa na ulimi uliowalaza wengi na kuwafanya waache kufikiri kwani alikuwa na kipaji cha kuwafanya waamini kwamba kila alilolisema lilikuwa la kweli kabisa na hivyo hapakuwa na haja ya kumfanya mtu mwengine alifikirie.  Ilikuwa nadra kumpata mtu aliyethubutu kumpinga au kumkosoa, hasa kadamnasi.   Walikuwapo waliochelea kukiona cha mtema kuni na wengine waliridhia kuwa vibarakalla vya kuitika tu ‘hewala bwana.’

Moja ya makosa makubwa aliyoyafanya Nyerere kwa kusudi au kwa sadfa, ni hilo la kuwafanya wananchi wenzake waache kufikiri na wawe wanayafuata tu aliyokuwa akiyasema bila ya kuyazingatia au kuyapima.

Miongoni mwa aliyowahi kuyasema Nyerere ni kuwa ati iwapo Zanzibar itaachana na Tanganyika basi Tanganyika kutakuwa shuwari lakini Wazanzibari wataanza kubaguana baina ya Wapemba na Waunguja na halafu wataendelea kutafutana asili zao. 

Tangu wiki iliyopita waandishi kadhaa wa Bara wamekuwa wakiyanukuu haya kana kwamba ni maneno yenye ukweli usiopingika.  Hii ni fitna tu; na inatumiwa kuwatisha na kuwagawa Wazanzibari.

Wakoloni walipowaona wanaowatawala wanaungana kuwapinga, basi walitumia mbinu ya kuwagawa wazidhoofishe nguvu zao ili waendelee kuwatawala. 

Mbinu kama hiyo inatumiwa siku hizi na baadhi ya viongozi wa CCM wa Bara pamoja na baadhi ya waandishi wa huko huko Bara ‘walioshtushwa’ na mwamko wa kisiasa uliowafanya Wazanzibari wawe na ujasiri wa kuujadili kwa mapana na marefu Muungano wa Tanzania. 

Ujasiri huo umewafanya wengi wao waseme kwamba ama wanaupinga muundo wa sasa wa Muungano au hawautaki kabisa na wanataka Zanzibar iwe dola huru yenye mamlaka yake kamili.

Huo si mwamko wa leo au wa jana; tumekuwa tukiugusia miaka nenda miaka rudi lakini tukionekana kuwa ni wazushi na wazandiki.  Sasa mambo yanajidhihiri yenyewe.  Matokeo yake ni kwamba waliokuwa wakijidanganya sasa wamegutuka na hawajui jinsi ya kulizuia hilo wimbi la uzalendo Wakizanzibari minghairi ya kutumia hoja finyu za kikabila na udini.

Mmoja amefika hadi ya kuandika kuhusu ‘Waarabu’ na ‘watu Weusi’ kana kwamba hao wanaonasibishwa na uarabu ni wa rangi aina ya pekee iliyo tofauti kabisa na ya Wazanzibari wasio na asili ya Kiarabu.  Mwandishi huyohuyo alitishwa na sura rahimu ya Sheikh Farid Hadi Ahmed, mmoja wa viongozi wakuu wa Uamsho. 

Aliandika kwamba baada ya kuiona picha ya Sheikh Farid yalimjia mawazo kwamba Uamsho si jumuiya ya kidini na wala si ya Wazanzibari na kwamba Sheikh Farid ametumwa (hakusema na nani) kuwafitinisha Wazanzibari.  Alichotaka kusema mwandishi huyo ni kwamba kwa vile Sheikh Farid ana asili ya Kiarabu basi Uamsho inataka kuurejesha usultani.

Ni uchambuzi uchwara, tena wenye kutumia lugha ya kibri. Unashtua kwa vile ni ‘uchambuzi’ wa hatari unaofanana na simulizi za  Wahutu wa Rwanda kabla ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini humo. 

Hizi fitna za ‘Upemba’ na ‘Uunguja’, za ‘ubwana’ na ‘utwana’ na za ‘ugaidi’ wa Uamsho ni fitna zinazotiwa na watu walio maluuni.  Lengo lao kubwa ni kuwapotosha Wazanzibari wauzime mjadala wa Muungano.  Hawajali iwapo watalitimiza lengo hilo kwa kuyakiuka maadili ya uongozi au ya uandishi. 

Hila wanazotumia ni kwanza, kuwafitinisha Wazanzibari kwa kutia fitna za kikabila na za kidini.  Kwa mfano, wanawatisha wahafidhina wa CCM/Zanzibar, wale wenye kusherehekea kaulimbiu ya ‘Mapinduzi Daima’, kwa kuwaonya ya kuwa Uamsho ina “msukumo wa kiarabu”  na kwamba kusudio lake ni hatimaye kuyapinga Mapinduzi na kuirejesha Zanzibar katika ‘utumwa’. Maneno ya kijinga kabisa.

Hila yao ya pili ni kuwagonganisha vichwa Waunguja na Wapemba kwa kutumia hoja zisizo na mshiko wowote wa kimantiki.  Wanasema wamewapata Wapemba wengi wenye kutaka Muungano uendelee kama ulivyo. Wamewahoji na matamshi yao kusambazwa na magazeti fulani nchini.  Huu ni mfano mzuri wa propaganda ya kitoto.

Hila yao ya tatu ni kutumia lugha kuparaganya mambo.  Ingawa Uamsho ni jumuiya kamili wao badala yake wanasema kuwa hiki ni kikundi. Sio kundi bali ‘kikundi.’  Na wanaishtumu jumuiya hiyo kuwa ‘inawatumia’ baadhi ya vijana kufanya vitendo vya kihuni vya kuchoma moto makanisa. Hakuna ushahidi wa hili.

Nne, wanajaribu kuwatisha Watanzania na hasa wakuu wa dunia hii kwa kuifananisha Jumuiya ya Uamsho na mitandao ya kigaidi ya Al-Qa’eda, Boko Haram na Al-Shabab.  Bila ya shaka wenye kueneza fitna hii hawajui walisemalo na wanajikashifu si mbele ya Watanzania wenzao tu bali hata machoni mwa balozi za nchi za Magharibi. 

Sijui kama wanaelewa ya kuwa maofisa wa baadhi ya balozi za Magharibi wameshakutana na viongozi wa Uamsho katika juhudi zao za kuitathmini Jumuiya hiyo na wanayaelewa makusudio halisi ya Uamsho.

Kwa hakika, kinyume na wanavyoandika baadhi ya waandishi wa Bara, Jumuiya ya Uamsho haikuzuka juzi. Imekuwako kwa muda wa takriban miaka 10 sasa.  Jumuiya hii ni kama mwavuli ambao chini yake kuna jumuiya mbalimbali za Kiislamu, pamoja na ile ya maimamu. 

Uamsho imekuwa ikiendesha harakati zake kwa msaada wa taasisi za nchi za Magharibi.  Ilikuwa miongoni mwa  waangalizi rasmi wa Uchaguzi Mkuu uliopita na ripoti yake kuhusu uchaguzi huo ni ya kupigiwa mfano kwa maelezo yake ya kina. 

Kati ya wafadhili wa Jumuiya hiyo katika harakati hizo za kuangalia uchaguzi lilikuwa shirika la USAID la Marekani.  Hata vizibao wanavovaa baadhi ya viongozi wa Uamsho na vikuza sauti vyao walipewa na Wamarekani wakati huo wa uchaguzi uliopita.

Wenye kujuwa mambo watakwambia kwamba kuna tofauti kubwa kama ya mbingu na ardhi kati ya jumuiya ya Uamsho na mtandao wa Al-Qa’eda au kundi la al-Shabab.  Huwezi kabisa kuzifananisha falsafa zao au makusidio yao.  Hata Boko Haram nayo licha ya mbinu inazozitumia inatofautiana sana na al-Qa’eda.

Huko Zanzibar mafatani hawa wana washirika wanaojulikana.  Nao ni wale wanaochomwa na kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).  Ndiyo maana wakaruka harakaharaka kuwatupia lawama za machafuko ya hivi karibuni viongozi wa CUF waliomo kwenye SUK na kutaka watimuliwe kutoka serikalini.  Na ni wao waliohusika na vipeperushi vilivyotolewa wiki iliyopita kuwafitinisha Wapemba na Waunguja.

Na ni haohao wenye kujaribu kuwachimba waasisi wakuu wa Maridhiano yaani Rais mstaafu Amani Abeid Karume na Maalim Seif Sharif Hamad.

Inasikitisha kuwaona baadhi ya Wabara wenye kujigamba kuwa ni wasomi wakitaka mijadala ya kisiasa ipigwe marufuku katika majukwaa ya kidini. Hawaelewi kwamba ni dhima ya dini za Ukristo na Uislamu kuzungumzia na kuyatafutia ufumbuzi mambo yanayoyagusa maisha ya kila siku ya waumini wa dini hizo. Na mambo hayo yawe yepi kama si ya kisiasa?

La kutisha ni kuwa  ‘wasomi’ hao wanamtaka Rais Jakaya Kikwete awachukulie hatua za kimabavu wakuu wenzake walio serikalini kwa kisingizio kuwa ati wanaunga mkono harakati za Uamsho. 

Ulimwengu haukufunga macho wala haukuziba masikio.  Unawaona na kuwasikia.  La ajabu ni kwamba wanasiasa na waandishi wenye kuchochea hisia kama hizo wamesahau ni nyakati gani tulizo nazo na ni ulimwengu gani tulio nao.  Katika ulimwengu wao wa leo Wazanzibari wanasema hawakubali tena kugawanywa kwa propaganda za kikabila au za kidini. 

Inatisha kwamba kuna wanasiasa na waandishi waliosahau kwamba siku hizi kuna Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) na mahakama nyingine mahsusi za kimataifa, mithili ya ile Mahakama Maalumu ya Sierra Leone. Mahakama kama ile ya Sierra Leone inaweza kuundwa mara moja na Umoja wa Mataifa kuwatia adabu wenye kupalilia fitna zinazoweza kuzusha mauaji ya kimbari. 

Ni hiyo Mahakama Maalumu ya Sierra Leone iliyomhukumu Charles Taylor, rais wa zamani wa Liberia, kifungo cha miaka 80 baada ya kupatikana na hatia ya  kuishushia nakama Sierra Leone.

Dhana waliyonayo baadhi ya wasomi na waandishi wa Bara ni kwamba viongozi wa Uamsho ni mijitu isiyosoma.  Kuna mmoja aliyepandwa na jeuri na kuandika kwamba mbali na kujua kusoma Qur’an viongozi hao ni watu wasiojuwa kuandika wala kusoma.

Ukweli ni kwamba viongozi wa Uamsho ni wasomi waliohitimu masomo ya chuo kikuu na wana shahada za juu za uzamili katika fani mbalimbali kama vile za uhandisi, sayansi na jiografia.  Ni wasomi wa nyanja zote — za dini na dunia.

Mfano mzuri ni Sheikh Msellem ambaye mbali na kuwa gwiji wa tafsiri ya Qur’an pia alisomea taaluma ya hali ya hewa. 

Baadhi yao walisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako walivutiwa na hotuba za kidini za Professor Malik, mtaalamu wa fani ya hesabati, ambazo ziliwashajiisha na kuwafanya wawe na mwamko wa Kiislamu.  Wengine walisoma kwenye vyuo vikuu vya nje vikiwemo vile vya Sudan, Saudi Arabia na Qatar.

Ni wazi kutokana na ripoti na taarifa zao kwamba baadhi ya wasomi na waandishi wetu wa Bara wanawadharau Wazanzibari. Nadhani hizo dharau zao ndizo zinazowafumba macho wasiweze kuona nani hasa aliyechochea fukuto hili la upinzani dhidi ya makandamizo ya walioshika hatamu za utawala wa Muungano.

Maandishi yao yamebainisha wazi kwamba hawaamini ya kuwa Unguja na Pemba si majimbo wala koloni za Bara.  Inakirihisha kuona namna wengi wao wanavyozitapika hadharani chuki zao (na udini uliowapamba) bila ya hata staha na uvumilivu wa kimaadili.

38 thoughts on “Nyerere na fitna za Upemba na Uunguja”

 1. anonima says:

  Ahmed Rajab umejaa chuki moyoni mwako! Upemba na uarabu umekuvaa vibaya! Hizo unazoziiita fitna ndio ukweli wenyewe, Mpemba na Muunguja ni CHUI na PAKA tangu asubuhi, hata ufanyeje Muunguja hawezi kumthamini Mpemba. NI ukweli usopingika na ukweli unauma.

 2. kp says:

  Unataka uthibitisho gani kuwa Uamsho ndiyo waliochoma makanisa? Udhaifu wa maoni yako ni kutokana na wewe kujijua hujui unachotetea bali ni ubinafsi, udini na ubaguzi!

 3. john says:

  Ahmedj Rajab leo umenena vyema sana.

  Tena makala yako ya leo imehitimisha kabisa mfulilizo wa makala zako za mambo ya Muungano ambazo umeziandika kwa muda sasa kwenye gazeti hili.

  Umetuonesha jinsi ambavyo wewe ni mmoja ya watu wenye chuki na upande wa pili wa Muungano. Japo katika makala zako za awali hili lilionekana, lakini sasa umweka wazi kabisa.

  Umeonesha kwamba unaunga mkono vitendo vya kidhalimu vilivyofanya na kundi hilo….. pale uliposema "ushahidi upo wapi kwamba wao ndo waliochoma makanisa"

  Pia kwako lolote linalosemwa na wasomi au wandishi kuhusu tukio hilo" limetoka kwa waandishi uchwara au wasomi uchwara" Lililopo sahihi kwako wewe ni kufanya vurugu, kuwapiga watanganyika, na kuonesha kwa kila hali kwamba Zanzibar inaonewa.

  Tumeshakuelewa na kheri umejiweka bayana mapema

 4. gabriel says:

  Sijui hawa jamaa zetu wa visiwani wanapata wapi jeuri ya kuamini wana haki miliki ya matusi. Weledi unamtaka mtu aheshimu mawazo ya mwenzake hata kama hakubaliani nayo. Sasa huyu jamaa kuyaita mawazo ya wengine ni ya 'upuuzi', 'kitoto', nk inaonyesha hajakomaa, au amepofushwa na hasira za chuki, udini, uzanzibari na jazba zisizo na mshiko. Nimekua nasoma makala zake lakini tangu leo nachania mbali. Mtu mzima hovyo sana huyu ahmed. 

 5. kibwetere says:

  Leo napata sura halisi ya Watanganyika, Mr Ahmed umeongea maneno ya dhati mpaka wengine wanasusa kama wanawake eti hawatosoma makala zako, huu ni utoto na lack of professionalsm, huu ndio msimamo wa wazanzibari na alioueleza hapo ndio msimamo wa Tanganyika kumuona Nyerer kama muungu wakati ndio source ya umaskini unaowaandama Watanzania. Huyu ni muandishi makini sio waandishi wa Kitanganyika waliodiriki kuchapisha picture za matukio ya morogoro na kuyaita eti wamefanya uamsho.

  Naomba Watanganyika muwe proffesional. Kwa nini munaogopa kivuli chenu sijui kwa nini munakataa kuitaja Tanganyika yenu, mumekosa uzalendo. Anaekataa kwao Mtumwa.

 6. Amani Lulu says:

  Chuki na unyama ni asili ya waarabu waliodiriki kuwakamata waafrika na kuwafanya watumwa. Asili hii ipo mpaka sasa kwa wafuasi wa kizazi hicho. Cha kushangaza hata wabantu kama huyu mwandishi wameshindwa kuujua ukweli huo. Aliyoyasema Mwl. Nyerere kuhusu Upemba na Uunguja ni ya kweli kwani matendo machafu yasasa hapa zanzibar yanadhihirisha. Dalili ya mvua ni mawingu tusipoziba ufa mengi yaliyosemwa yatajidhirisha. Tusingoje yatokee, tulinde amani ili tuweze kujenga uchumi na jamii yenye kuheshimiana na kupendana.

 7. Mchwaka says:

  Ahmed Bin Rajab, Leo umewambia ukweli WATANGANYIKA JUU YA MTUME WAO NYERERE….!!

  Nyerere Alikua Fitna tena ni Jitu lenye Chuki za dhahir juu ya WAZANZIBAR NA WAISLAM KWA UJUMLA…. 

  Nyerere Alisahau kama Alipotoka msituni Alikuja na Boxer (Bukta) Mjini.

  Nyerere kwa Kujionesha kama yeye ni MNAFIKI. Alifika kusema juu ya SIFA ZA WAZANAKI.. Akiwa yeye ni Mmoja wao

  WAONGO, WATU WASIOTIMIZA AHADI, NA WAUWAJI….!!

  Nyerere Hakufaa hata kua TARISHI,Alikua ni jitu lililojaa CHUKI, UBINAFSI, UDINI NA ROHO MBAYA…..!!

  kWA FITNA HIZO ALIZOTOA JUU WA WAZANZIBAR ZITAWARUDIA WATANGANYIKA WENZIWE……!!!

 8. novatus says:

  ahmed makala zako ni nzuri sana lakini na wewe usipinde ukweli nyerere hakusema wazanzibari watabaguana na bara watabaki shwari endapo muugano utavunjika alichosema ni kuwa wale watakaoanza chochoko za kuuvunja muungano na wakafanikiwa kwa ubinafsi wao hawatukuwa salama iwe ni zanzibar au bara.   Mimi nafikiri ni vizuri waandishi wenye majina kama wewe kuwa makini na makala zenye reference za viongozi hasa wale wanaoheshimika kama nyerere sema madhaifu yake lakini usipinde ukweli wake kujenga hoja yako

   

 9. Msomaji wetu says:

  ndugu zangu watangayika nadhani tumeona wazi ni jinsi gani wazanzibar wasivyo tuhitaji kwa lolote. ni lipi linalotusukuma kuwang'ang'ania hawa jirani zetu?

  ndugu yangu Ahmed msingi wa muungano ni udugu na mshikamano baina ya Tanganyika na zanzibar, kweli umenena kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa malaika wala si mtume wala si nabii wala sio chochote zaidi ya kuwa Bin Adam aliejaliwa kipaji.

  La msingi sisi Wa Tanganyika ni kutafakari jinsi ya kuishi na majirani zetu kwa amani mbona kwa upande wa kushoto wapo wa congo, warundi,wanyarwanda na wa zambia na juu wapo waganda na wakenya wote hawa tunaishi nao kwa amani na kila mtu ana nchi yake nasi Tujivunie Utanganyika wetu sio kila siku tunanyanyasika kama vile tunaona haya kujitambulisha na Utanganyika wetu wakati wenzetu wanapata faraja na sifa kutangaza utaifa wao. nasi tujitangaze kwa Utanganyika wetu na tuipende na kuiendeleza Tanganyika yetu. kauli mbiu iwe Tanganyika iliyo bora na iliyoendelea inawezekana. TUNAZEWA NA TANGANYIKA YETU.

 10. Muhsin, Muhsin says:

  Sheikh Ahmed shukurani za dhati kwa kueka sawa dhana hii mbovu ya kuwatifinisha wazanzibari.Ni ukweli usiopingika kuwa hakuna ushahidi wa aina yoyote ile unaohusisha makanisa yaliochomwa na uamsho.Kama upo na upelekwe mahakamani, ili yawe bayana kila mmoja wetu awafahamu hao waliohusika na kitendo hicho kiovu. Watanganyika wengi, hata kama mtu ni msomi linapokuja suala la Zanzibar basi huvaa gwanda ya ujinga.Nadhani naweza pata exception kwa watu wachache sana akiwamo Generali Ulimwengu na watu kama hao.Lakini hakuna cha Prof.Baregu wala askofu wa Mbagala wote ni wabinafsi. Kuna video moja youtube, gari inachomwa moto.Mwandishi anasema vijana wa uamsho, wakati shahidi anasema gari iliongua imetokana na bomu la machozi.Hii ni kudhihirisha ajenda iliobebwa na media za kibara.

 11. Mzanzibari says:

  Watanganyika munashidwa hata kuargue kwa piont badala yake munakuwa so bias, hebu munatakiwa mujibu hizi hoja za Mr Rajab sio kuongea mambo ambayo hayana mashiko, munaonekana waziwazi jinsi gani munapozungumza munaweka chuki na jazba mbele sisi tunapojadili muungano tunakuwa na point ndio maana munashindwa kujibu, mimi hapa u-Tanzania siutaki hata kuuona hata nnaposafiri utaifa wangu kwanza najitambulisha kama mzanzibari, nawashangaa sana watanganyika munakuwa wavivu wa kufikiri, leo munakuja na hoja eti waarabu waliwatuma waafrika huu ni ujauzito wa kufikiri hebu angalieni kuna nchi gani ya kiarabu kuna watu ambao nyinyi munaosema walikuwa watumwa, waliowatoma waafrika ni wazungu ila hamutaki kuueleza huu ukweli " munaturn blind" angalieni carebian, US, Europe. Waarabu wao ni wafanya biashara kwa hiyo wakati huo biashara ilikuwa ni watumwa kwa hiyo wao walikuwa wako kwenye biashara na wazungu ndio waliowanunuwa waafarika kutoka kwa waarabu na waafrika wenyewe ndio waliokuwa wakiwakamata wenzao kuwauzia waarabu.

  Tukirudi kwenye suala la Muungano sisi Wazanzibari tutapigana mpaka kieleweke ila zanzibar Watawala Tanganyika mutaitoa, na hizo arguement zenu za kitoto za kutokufikiri eti tukitoka kwenye muungano tutauwana ni za choyo na fitina, Zanzibar ilikuwepo kabla ya Tanganyika, na muungano ulikuja 1964 jee huko nyuma tuliuwana?

  Vitisho kama hivi waliambiwa Wasingapore na wamalaysia kuwa mukijitenga mutakufa kwa sababu hata maji ya kunywa munaitegemea malaysia, jee leo Singapore wako wapi? 1 Singapore dolar= 3MR, ni the reachest country in Asia.

  Twachiwee tupumuweeeeeeeeeeeeeeeee

 12. Mussa says:

  Nafikiri usomi au taaluma sio tu Kuwa na vyeti bali heshima itiokanayo na upeo na uelewa. Vile vile kuheshimu mawazo ya wengine hata Kama ukubaliani nayo. You agree to disagree! Nilichoelewa ni Kuwa wengine wanafikiri wakiitwa wasomi au wataalamu basi mawazo yao pekee ndio sahibi na si ya mtu mwingine. Naweza kusema labda sijui inawezekana hata Nyerere na bwana Ahmed pia wanaamini hivyo. Huo ni mtizomo wao na mawazo yao na mwingine pia ana mawazo yake na kila mtu anastahili heshima, kuheshimiwa kwa mawazo yake bila kujali elimu, rangi, dini Kabila wala utaifa wake. Nadhani tukijenga tabia ya kuheshimu mawazo ya kila mtu hata Kama hatukubaliani nayo tutakuwa wasomi na wataalamu wa kweli.
  Mussa.

 13. Mwalala says:

  Ha ha ha

  Ahmed bwana. Unaposema Nyerere hakuwa mtume una maana gani? Kwani kuwa mtume ndio kutofanya makosa? Mbona kuna mitume historia zinaonyesha wameoa mpaka mabinti wa miaka tisa na wamlikuwa waporaji wakubwa wa mali nyakati za vita?

 14. Maji marefu says:

  Tuwaache Wazanzibar waende zao. Kwa nini tutukanane? kwani tutakosa nini Watanganyika?

   

  Mbona vikaratasi vilivyosambazwa vya kuwataka Watanganyika waondoke Zanziba hawavisemi?

   

  Rajab, Waambie Wapemba waliopo bara warudi Pemba ili mjenge Pemba yenu mnayoona mmeingiliwa na Watanganyika!

  Toka lini bomu la machozi likatoa Moto? Mtu mzima anazungumza mambo ya ajabu.

  Tuwaache jamani Wazanziabri waende zao. Hivi mnadhani Watanganyika tunawang'ang'ania  – kwa lipi?

 15. Nyamburi says:

  Ahmed Hongera!

  Binadamu tumezaliwa kuwa wachoyo. Siku zote binadamu ukimpa kati ya vitu viwili lazima kuna kimoja atakichagua. Yeye Bw. Ahmed kuwepo Muungano au kutokuwepo Muungano atachagua kutokuwepo Muungano. 

  Bw. Ahmed siku zote yeye anaonesha kuwa uarabu ni bora kuliko uafrika wa wafrika weusi. dhambi hii imemkaa na hakuna njia ya kuiondoa. Lakini, nadhani, anakosea kwani kwa dunia inavyosonga mbele na kuwa kama kijiji kwa kuwa na teknolojia ya mawasiliano ya haraka duniani kote weusi (waafrika), waarabu, wazungu, na waasia na wahindi wekundu wote wameanza kujiona ni binadamu tu na si wanyama. Wote wanahitajiana. 

  Bw. Ahmedi anajaribu kusema kwama tunaomuona Nyerere kama Mungu mtu. Si kweli. Nyerere alichofanya tofauti na anavyozani Bw. Ahmedi ni kusikiliza mawazo ya wengi. Mzee Msuya aliyewahi kuwa kwenye baraza la mawaziri wa Nyerere na Baraza la Mawaziri wa Mwinyi amewahi kukiri kuwa Nyerere aliruhusu mijadala na kufuata wengi wanasemaje. 

  Leo chuki zako binafsi za Uarabo kuwa bora zaidi ya wengine haziwezi kuzima historia. Wajapani wameendelea sana kwa kuheshimu watu wenye kipaji kuliko wengine. Wewe unashindwaje kuona Nyerere alikuwa na kipaji kuliko tulivyo wengi ikiwa ni pamoja na wewe. 

  Bw. Ahmedi acha ubaguzi wa rangi. Wazungu waliyokuwa wabaguzi wa rangi, leo hii hawabagui Wachina ila wanataka wafanyenao biashara. Uarabu wako hauwezi kuuwa ukweli kuwa binadamu wote ni sawa ila rangi ndiyo sio sawa.

 16. George says:

   Lakini dhambi ya kubaguana, na kuchochea chuki  itawatafuna!!!!!! w

 17. Mussa says:

  Tukumbuke Kuwa uwanja huu wa mawazo ni mpana sana kila mtu ana haki ya kutao maoni yake kwa uhuru kabisa ilimradi havunji sheria za nchi. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa Watu wengine wameamua kusema kwa niaba ya wenzao bila idhini ya Watu husika anaotaka kuwawakilisha kwa njia ya maoni yake. Hakuna popote duniani ambako mtu moja au kikundi au jumuia Iyoyote ile Ina haki ya kusema kwa niaba ya mwingine bila ya Kupata idhini au kibali cha kufanya hivyo. (Legal representation)
  Na hapa namaanisha viongozi wa nchi, dini, vikundi au asasi za kijamii, waandishi wa habari na kadhalika na kadhalika. Kwa wasomi au wataalamu wataelewa wazi kuwa kuna sheria inayoweza kukushtaki aidha kwa kutumia mawazo ya mtu mwingine bila kuonyesha idhini au kibali cha mtu husika Kuwa unamnukuu mtu huyo au unamwakilisha mtu huyo.
  Kwa hili nilitaka tu kumfahamisha mwandishi huyu ambae anajiita msomi au mwana taaluma Kuwa anachokieleza katika makala yake, na kusema kweli Mimi napenda sana makala zake lakini sina maana Kuwa nakubaliana nae na kwa maana hiyo aelewe wazi Kuwa mawazo yake si ya wazanzibari , watanzania au wasomaji wapenzi wa makala zake kama mimi,maana hana idhini ya kuwakilisha mawazo au maoni yetu vyovyote vile kwa njjia ya mawazo yake Hali kadhalika hata kikundi cha uamsho ambacho hata wazanzibari na watu wote kwa ujumla wengi tunapenda kuhudhuria mihadhara yake nakipenda sana ila sina maana Kuwa nakubaliana nao, nacho vile vile hakina idhini ya kuwakilisha mawazo au maoni ya wazanzibari maana kila mzanzibari Ana haki ya kutao maoni yake. Ieleweke wazi Kuwa waandishi wa makala mbalimbali hawawakilishi mawazo na misimamo ya wasomaji wao, uamsho haiwakilishi wazanzibari , viongozi wa dini hawawakilishi waumini wao, maoni au mawazo ya mkristo au mwislamu sio msimamo wa wakrito au waislamu wenzake na Kama atafanya hivyo basi sharti atoe uthibitisho wa kibali au idhini ya kuwawakilisha Watu au kikundi husika. Narudia tena kila mtanzania, au mzanzibari mkristo au mwislamu ana haki ya kutao maoni yake na hakuna mtu yoyote alietoa kibali cha Kuwa represented na kila mtu, taasisi, dhehebu, jumuia au kikundi kielewe wazi Kuwa hayo ni maoni na misimamo yao binafsi sio vinginevyo.

 18. John says:

  Ahmed, umejadili kwa chuki sana…ila mawazo yako wala siyakatai kwani yapo mengi yana point.

  Ila lazima uzingatie kwamba kuna uwezekano asilimia kubwa ya wakazi wa Zanzibar watakuwa wametoka afrika ya mashariki hii ni kutoka na mazingira yaliopo kati ya sehem hizo mbili. Sasa habari ya waarabu na wazungu kuishi zanzibar ni muingiliano wa kibiashara.

  Ahmed, si vizuri kumsema Nyerere vibaya kiasi hicho, na nikifikiri vyema sioni kama waanzilishi wa muungano walikuwa na lengo baya. Na hata huyo nyerere amekuwa objectively maisha yake mengi hasa pale anapokuwa anaamua maisha ya watu walio wengi. Siwezi kumfananisha na sultan au viongozi wetu walio wengi kutoka Afrika. Hapa naona ni vyema muungano ukafa kwa amani kuliko kuja kuvunjika ndivo sivyo.

  Bara wanahitaji kuwasikiliza hawa jamaa, nafikiri umefika wakati waachwe wajitawale, nitafurahi wakaachiwa mapema kabla hata na hayo mafuta hayajachimbwa. Hii itatuweka huru….nao watakuwa huru…..Hii itasaidia labda kufungua fursa nyingi zaidi kati yetu sote…

  Heshim baba na mama yako uishi miaka mingi na heri duniani.

  Mungu Ibariki Tanzania.

 19. mtanganyika says:

  Bw Ahmedi, unajipunguzia heshima sana kwa kuandika maneno ya kutunga na kudai yalisemwa na Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere. Si kweli kwamba Nyerere alisema Wazanzibari wataanza kubaguana baada ya kuvunja muungano na kwamba Watanganyika tutaendelea vizuri. Mwalimu alisema kwamba dhambi ya ubaguzi na sawa na ile ya kula nyama ya binadamu, kwamba ukianza kwa ubaguzi, utaendelea na ubaguzi huo mpaka kuangamiza jamii yako.  Kwamba Wazanzibari wanaotaka kuvunja muungano kwa sababu za kibaguzi, ambazo na wewe unazipigia chepuo, wataendelea na ubaguzi huo huo, kwanza kwa kubagua Wazanzibari dhidi ya Wazanzibara, then itakuja Waunguja dhidi ya Wapemba n.k

  Na nikiwa kama mTanganyika, nasema ZANZIBAR CAN GO TO HELL!! LET'S DO AWAY WITH THIS STUPID NMUUNGANO. MUENDE ZENU MKATAWALIWE NA MABWANA ZENU WA OMAN. HADITH LAANA KUU NYIE!

 20. Seiff Suleiman Kibwana says:

  Nashangazwa na Muandishi Muhamed Rajabu namna alivyofanikiwa kuyageuza maneno

  ya Baba wa Taifa Nyerere na kuyatumia atakavyo kwa kuondosha maneno mengine

  yenye umuhimu mkubwa katika kuweka wazi lengo la Mwalimu lililokusudiwa

  kwenye hotuba yake. Ukiisikiliza vyema hotuba ya Mwalimu ni kwamba yeye

  alitoa mifano ya utengano, aliziweka Zanzibar na Unguja, lakini pia aliwaweka

  watanganyika katika mazungumzo hayo hayo na hata akathubutu kutoa mifano

  zaidi kwa kutumia makabila ya Tanganyika. Sina haja ya kuirejea hotuba,

  lakini ipo na inaeleweka. Tatizo ni kwa wale ambao hawajaisikia. Lakini

  muandishi kwa makusudi ameyaondosha hayo na kujenga hoja ya Makosa ya

  Nyerere! Jambo la pili ni kuhusu makanisa yaliyochomwa moto. Muandishi asema

  kuwa hakuna uthibitisho wa kuwa eti waliotajwa kuhusika na matukio hayo kuwa

  ndio. Sasa iweje matukio hayo yaende sambamba na maandamano ya watuhumiwa?

  Huwezi kujenga hoja kwa kukanusha tu bila ya kuleta ushahidi wa kutosha na

  pia ukayafanya maelezo yako kuwa eti ndio hoja tosha ya kutokuwepo tukio

  husika. Jambo la tatu, simuelewi muandishi kwa kukanusha kwake udini wakati

  ambapo jambo hilo lilionekana wazi wakati wa maandamano hayo, na wahusika

  wakuu wanajlikana katika tukio la maandamano.

 21. Mimi Haswa says:

  Ahmed kajichanganya kweli kweli, kwanza kasema Nyerere alisema " 

  "Zanzibar itaachana na Tanganyika basi Tanganyika kutakuwa shuwari lakini Wazanzibari wataanza kubaguana baina ya Wapemba na Waunguja na halafu wataendelea kutafutana asili zao".Ingawa amekosea ukweli kunukuu hotuba nzima ambayo haikugusa Zanzibar pekee, kwamba ilikuwa mbinu yake mwalimu kuwagawa na kuwatawala Wazanzibar. Halafu anasema, Uamsho sio kikundi cha ugaidi na kinatambuliwa na balozi za nchi za Magharibi, "Sijui kama wanaelewa ya kuwa maofisa wa baadhi ya balozi za Magharibi wameshakutana na viongozi wa Uamsho katika juhudi zao za kuitathmini Jumuiya hiyo na wanayaelewa makusudio halisi ya Uamsho". Huyu mwandishi anaonesha, kwa nadharia yake, Magharibi wako nyuma yao kutugawa, hataki ionekane bara inawagawa Wazanzibar ila anabariki mbinu za viongozi wa Magharibi kutugawa. Vikundi vingi vinavyochochea machafuko duniani vinafadhiliwa na Magharibi. Kwa ushahidi wa maneno ya mwandishi, UAMSHO ni kikundi cha kigaidi. Maana hata Al Qaida chanzo chake ni Marekani (CIA);

 22. mpenda watu says:

  sasa mmeambiwa mlete hoja za kuvunja muungano. kwa nini msifanye hivyo haraka? 

  ninyi wazanzibari ipo siku matusi yenu kwetu sisi wabara mtayajutia. ntamani muungano uvunjike haraka na halafu tuone ni kina nani wenye shida ya kuwa na wacheza bao. 

  mtaishia kushikana uchawi hadi mjute kuzaliwa. muungano na nyie ni sawa na kufanya urafiki na MAITI. mnaudhi sana kila wakati mnapotukana. tunawashukuru kwa matusi yenu ila nawaombea mpewe sawa na mnachokitoa. kuna keo na kesho. 

  libya walimtukana na kumdjhalilisha Gaddafi leo hii ni waislamu wenzio waliokuwa wanaishi kama peponi ila leo hii hawajui kesho itakuwaje. 

  hakuna aliyefikiri kwa ufupi kama bwana rajab na wenzako

 23. LUCAS MGAYA says:

  MIMI NADHANI TANZANIA IENDELEE KUWA NA UMOJA ULIOPO NA WANAOUKATAA UMOJA KWA SASA WANAFAHAMIKA YATAKAYOWATOKEA BAADAE WATAANZA KUTUOMBA MSAADA TUKAWASAIDIE KUTULIZA USALAMA PALE AMBAPO AMANI ITATOWEKA KWAO SIJUI WANAWAZA NINI? ILA NINACHOJUA ENDAPO ITATOKEA BASI WAJUE HAWATAKAA SALAMA SISI YETU MACHO NA MASIKIO

   

   

 24. Msomaji wetu says:

  Makala nzuri na safi kabisa na waandishi uchwara akiwemo Mwanakijiji mnapaswa kusoma kutoka kwa waandishi wa aina ya AHMED RAJAB. Aidha wabara tunapaswa kuona kwamba Nyerere alikua si Mungu ni binadamu kama wengine hivyo anaweza kukosea, kutokana na hali hio tujaribu kupunguza kumuabudu.

  Waandishi wa Bara na wasomi wapumbavu punguzeni fitna kidogo, mnatia uchungu manake usomi wenu mneweza kuutumia kupunguza umasikini wa angalau ngazi ya familia zenu.

 25. king kibichwa says:

  LAZIMA JAZBA ZIPUNGUE ,wakati tunajadili lazima tujaribu kupunguza jazba , kwa pande zote iwe znz au bara sisi ni walewale, na muandishi ni mmoja wetu, tukichukulia chuki hatutoki kwenye tatizo lilopo tutabaki kulaumia na kung´oana meno tu. jazba tuzipunguze ili tuachie ukweli uchukue nafasi yake huu ndio wakati wake na wakati tutaupoteza ikiwa tu tunajadili kwa jazba, kwa upande wangu maumivu ni yaleyale tu na kama hatutokuwa makini basi tutayazidisha haya maumivu na kama kawaida ni wazee na watoto na wanawake ndio wataoathirika, kwani mwanzo wa moto mkubwa ni cheche ndogo tu. mungu ibariki Afrika, tanzania, zanzibar, tanganyika pamoja na dunia kwa ujumla

 26. kichimbo says:

  Ahmed umesema ukweli mtupu,siku zote ukweli unauma jamaa imewagusa si mukae tanganyika yenu na sisi Dubai na zenji yetu then tubaki na ujirani mwema?

 27. Msemakweli says:

  Watanzania na wengine wote nakusalimieni,

  Tupunguze jazba, tuongeze hikma halafu tuheshimiane. Kila mtu ana haki ya maoni yake. Pongezi muandishi, umeupiga nyundo msumari kichwani! Wenye kumpinga wajenge hoja. Pia ni haki yao.

  Nyerere: kwa wengine ni baba wa taifa na kwa wengine ni baa (balaa) wa taifa. Inategemea mtizamo wako. Kwa wakristo wengi ni baba wa taifa kwa sababu kawanufaisha na kawaneemesha. Kwa waislamu wengi na kwa wanzanzibari wengi ni baa wa taifa kwa sababu kawadhoofisha na kawakwamisha kimaendeleo — kwa makusudi. Na uthibitisho wa yote haya mwenye macho atauona.

  Muungano: zimeungana nchi 2, Tanganyika na Zanzibar. Hakuna kulazimishana, anayetaka kujadili/kurekebisha/kuvunja muungano ni haki yake. Mwenye maslahi na muungano anautaka, asiye na maslahi na muungano hautaki. Ni jambo jepesi kama hivi. Hamna haja ya vitisho wala matusi. Tuseme kweli tu, hata watu walio oana wakichoka huachana – no bid deal, au vipi?

  Utumwa: kweli waarabu walifanya biashara ya utumwa na ni jambo la kusikitisha, la kupingwa na la kulaaniwa. Kweli waarabu walikuwa wafanya biashara na waliona watumwa ni kama bidhaa. Lakini bado ilikuwa ni makosa kufanya hivyo. Kweli watumwa wengi walinunuliwa na wazungu wakapelekwa marekani [north & south]. Kweli wazungu pia walihusika na biashara hii kiasi kikubwa. Biashara inahitaji vitu vitatu: 1. soko [mnunuzi], 2. bidhaa, 3. muuzaji. Muuzaji tunamjua, bidhaa tunaijua, soko [mnunuzi] kajificha [kafichwa]. Hivi hatujui wale watu weusi wote kule USA, South America na Carribean wametoka wapi? Biashara hii wazungu waliipiga marufuku baada ya soko lao kuwa halihitajii tena watumwa. Kwa sababu walitaka ku-modernize na kuanza kutumia machines badala ya binadamu. Ndio pia sababu ya civil war ya marekani baina ya north na south, south ilitaka kuendelea kutumia watumwa. North ilitaka kutumia machines. Nenda arabuni kawatafute watu weusi. Wachache waliopo wame-assimilate na wamechanganyika na waarabu kwa sababu walionekana ni binadamu. Nenda USA, South America. Mpaka leo africa americans wanabaguliwa/wanadharauliwa. Ni kweli na tukubali.

  Mustakbal: tujadiliane kwa heshima. Kuna haja ya kurekebisha tofauti zilizopo baina ya jamii ya watanzania. Kuna haja ya kuwapa raia wote haki sawa. Bila ya kujali dini/kabila au sehemu. Kuna haja ya kutafakari bila ya jazba na kutizama ukweli kidhati. Bila ya hivyo tunapoelekea kubaya.

  Idumu Tanzania.

  Idumu Tanganyika

  Idumu Zanzibar.

  Asanteni.

   

 28. Jonas says:

  Ahmed Rajabu, nimekuwa nafuatilia maandishi yako tangu ukiandika na gazeti lile la 'Africa Now'. kuna kitu nakiona kutoka kwenye maandishi yako

 29. pye Chang shen says:

  Tuwe waadilifu hata kwa jamaa zetu mungu ndio anapenda ukweli usemwe kila mmoja apewe haki yake basi tuishi

 30. Joseph lugemba says:

  Mimi nadhani sisi waTangsnyiks tumekuwa sio waadilifu kwa miaka yote tangu Huo Muungano uanxishwe….kwanini tusijiulize tu huo Muungano ulibuniwa kwa sababu zipi na kwa maslahi ya nani ?

  mbona kuna waTanganyika kwa asilimia fulani hawautaki huo Muungano…wakati huo huo kuna waZanzibar waluowengi mno wasioutaka Muungano…Nadhani jambo la busara ni kuwepo na Referrendum.ili.ijulikane kwa ushahidi wa maoni ya wapiga kura..kwa maana huko awali waliamua watu wawili tu bila ya kushirikishwa au kuhusishwwa raia wa pande xote mbili .na bila ya kuwepo vikao vya bunge…hivyo uhalali wa huo Muungano wenyewe una utata mkubwa.

  Namalizia kwa kumpongeza Mwanfishi kwa kutoa maoni yake na fikra zake …nasisi tutumie kalamu zetu kwa kujibu hoja au 

 31. Gombara says:

  MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR ULIOUNDA HII INAYOITWA TANZANIA,HAUNA UHALALI WOWOTE KISHERIA,UPO KISIASA NA KIMABAVU,SASA KWA NINI WASOMI MNASHINDWA KULIONGELEA HILI BADALA YAKE MNAJIKITA KWENYE MAHOJIANO YA AJABU.

  WATANGANYIKA WALIO WENGI HAWAUTAKI,WAZANZIBARI WALIO WENGI HAWAUTAKI, HII NDIO MISIMAMO YA WALIO UNGANISHWA KWA NGUVU HIVI SASA,HII KULUMBANA NANI HAMTAKI MWENZIWE NI UBISHI WA KITOTO, KILA MMOJA KESHA MCHOKA JIRANI YAKE, TATIZO NI HIKI CHAMA TAWALA CHA CCM KULAZIMISHA,VYAMA VYOTE VYA UPINZANI BARA NA VISIWANI WANAELEWA UKWELI HUU.

  KUWALAUMU WALIO UANZIASHA KARUME NA NYERERE NI KUPOTEZEANA MUDA, KWA KUWA WAO WAMESHA FARIKI, HAYA HAYAWAHUSU TENA,WALA KWA KUWA WAMEYA ASISI WAO HAINA MAANA HATUWEZI KUREKEBISHA PALE WALIPO KOSEA,URUSI WAMEFIKA KUYANG'OA MASANAMU YA LENIN MUASISI WA TAIFA LAO KWA KUWA WAKATI ULIFIKA NA WALIAMUA KUFUATA SIASA MBADALA NA KUSONGA MBELE.

  LEO TANZANIA INAONGOZWA KAMA ZIZI LENYE MIFUGO TOFAUTI, HAKUNA ANAE JUA KESHO MALISHO  WAPI AU MNYAMA GANI  ATATOLEWA KAFARA, KWA VISINGIZIO VYA SHEREHE AU MSIBA. {MAJIPU} YALE MUHIMU NA YA MAANA KWA TAIFA HILI KAMA KATIBA MPYA YA WARIOBA, NA MUUNGANO UPI UTATUFAA KAMA LAZIMA UWEPO HAWAYATUMBUI, HUU NI UONGOZI MBOVU HAUNA BARAKA ZA MUNGU WALA SHETANI NI AIBU YA UDHAIFU WETU TUNAO TAWALIWA NA WATAWALA WOTE TUNA NIDHAMU YA WOGA.

  LAZIMA KUWAKOSOA WATAWALA HATA KAMA WANAJIDAI KUWA NA NGUVU ZA AJABU WAO NI WAAJIRIWA TU KWETU SIO KINYUME CHAKE,WANALINDANA OVYO BAADA YA KULIFILISI TAIFA KWA KUJISIFU BADO TUMEKAA KIMYA SISI NI VIUMBE WA AINA GANI HAPA TANZANIA. 

   

   

 32. Harunams says:

  Ahmed Rajab nimesoma makala zako nyingi ila hii ndio umeamua "kuonyesha rangi zako" wazi. Naheshimu mawazo ya kila mtu hata wewe pia hivyo kutofautiana kimtazamo ni jambo la kawaida. Pia, tunashukuru kutuhabarisha (kama kweli) kuwa kuwa UAMSHO wanafadhiliwa na Balozi za Magharibi pamoja na mashirika yao kama vile USAID. Hilo halishangazi kwani hata Al-Qaeda ilianzishwa na kufadhiliwa na U.S.A ikijumuisha na makundi mengine hatarishi duniani. Kinachonishangaza ni kuwa, wewe umekuwa wa kwanza kutuhabarisha hilo, bila shaka Serikali yetu inalitambua hilo pia.

 33. Esteemed Reader says:

  Hivi ni yule jamaa ambaye alikuwa Mhariri wa gazeti la African Event mjini London. Hivi hili gazeti lilikuwa na udhamini wa Sultan wa zaamani wa Zanzibar? Marehemu Prof Ali A'lamin Mazrui alikuwa pia mchangiaji mkubwa wa makala na kuuambia ulimwengu kwamba Ukristo umefelisha maendeleo au ustaarabu wa dunia; mkombozi ni Uislamu!

 34. Saidi R Fundikira says:

  Nawaunga mkono wote waliopendekeza kwamba, endapo huu ndio utashi wa Wazanzibri wengi, ni heri Tanganyka ijitoe kwenye Muungano. Nasema hivi kwani tangu nianze kufuatilia siasa hizi za muungano, jambo ambalo nakiri nimeanza hivi juzi juzi tu, sijamsikia Mzanzibari akijitokeza mbele kuutetea Muungano, pengine kwa sababu tunaowasikia ni wasomi wa Kizanzibarii tu. Ila tutatake tusitake watu kama huyu ndugu yetu hapa ndio viongozi wa Zanzibar, hivyo kauli zao zina uzito sana.  Tutjitoe kwa kuanza na hizo serkali 3, au hata kutamka tu kwamba tunajitoa.

 35. Alex says:

  Baba katka jina la LA mwanao Yesu kristu nawakabidhi wote hawa uwaone kwa jicho lako na mkono wako wa kuume ukawaelekeze palipo sahihi na vinywa vyao ukavishike kwa lijamu ya maelekezo ya bongo zao kwani mioyo yao ukaitembeze palipo mahala sahihi ili wafike wapahitajipo kwani dini zetu ni njia za kuukimbia moto na kuona ufalme wako na sio kuwa na dini ni tiketi ya wema rangi zetu ni mapambo tu kwani hata mfano wa njiwa wanarangi tofauti tofauti ili kuipendezesha dunia na sio kuwa na rangi flani eti unabusara au akiri nyingi bara wajua wewe uwezo kwa kila mmoja, makabila yetu pia ulileta wewe Mungu wakati wa ujenzi wa mnara ili tu kupunguza au kuondoa kabisa umoja wa ujenzi wa mnara ule, Baba utaifa wetu sisi wanadamu ndiyo tuliweka mipaka kwa akiri zetu hivyolazima hili litokee maana pengine hawakufunga na kukuomba wewe uwape hekima na ufahamu wa kufanya vile. Yesu wangu hizi ni nyakati za mwisho watu hawafikiri tena juu ya utu bali uchochezi, chuki, uzushi, utumiaji wa nguvu zao ili kupata jambo flani, ubabe, kutaka heshma, kuabudiwa, kuuana, ubakaji, usengenyaji, kuingiliana kinyume na maumbile na hakika ulisema hutasamehe tazama hizi ni dhambi chache zinazo tutafuna YESU DAMU YAKO IKANENE MEMA, maana akili zetu na mawazo yetu twategemeza zaidi kuliko maneno yako matakatifu Bwana Yesu nasema asante maana u mwaminifu na hushindwi na kitu hivyo utawapa busara na hekima na si kufikiri kila jambo na kutaka liwe kwa akili za uanadamu na sio tena kwa msaada wako.

  Wote tusema Amen 

 36. Simon says:

  Ama kweli waswahili husema "Kikulacho——. Kwani hawa wazazibaraa hawa tuna haja gani nao waondoke maana dar na kwingineko kwenye ardhi yetu wamejaa wao waondoke waone kama sisi watangawanyika tutaenda kuwaomba msaada kwao, mijitu ilizoea kitawaliwa na imetuletea hats mila za ajabu bado mnaibembeleza MIPUNDA iacheni ishazoea kutumikishwa kwa ujira was BOFOLO. Tena waende umbea tu wanaandika kuomba nini si waondoke na mabwana zao hao magharibi? Ningekuwa Nina kamadaraka japo kidogo ningevunja Leo hii.

   

 37. Kaite Kataitika says:

  Hivi huyu ndiye alikuwa mhariri wa gazeti la Afrika Event huko London? Gazeti la Sultan aliyekimbilia Uingereza likiwa na waandishi wengine wa makala kama akina hayati Prof. Dk. Ali A'Alamin Mazrui, mwenye kuamini kuwa Uzungu na Ukristo vimeangusha dunia na mkombozi ni Uislamu?

   

  kama si yeye, naomba radhi!

 38. Bob Ritchie says:

  Ahmed Rajab ndiye mhariri wa gazeti hilo na ikisoma mada nyingi huwa hazina ukweli zimejaa kejeli na maneno au misemo maalum kwa wakristo au watu wa bara 

  Ni mwandishi mahiri ktk kupotosha umma kwa habari zinazoficha ukweli lakini ni muhimu sana ndicho kielelezo sahihi cha mawazo ya wanzanzibari wengi hivyo ni vizuri akiendelea kuandika ili kufahamu dira ya mwenendo wa zanzibar 

  kila kitu alichosema kuhusu fitina za Mwl Nyerere ndicho kinachotokea leo zanzibar sasa na nani mkweli kila mtu anafahamu kuwa Nyerere alikuwa binadamu na si Mungu sasa vipi yeye aseme kuwa alidhani ni Mwenyezi Mungu au ndiyo njia ya kuwaamsha waislamu wa siasa kali kutafuta njia ya kumuuwa yeye au wafuasi wake kwa sababu alidai yeye ni Mungu maana dini ya kiislamu kuondoa uhai wa mtu si jambo gumu kama unapigania imani yako hata kama si madai ya kweli

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *