Nyota Serengeti Boys amtoa machozi mamaye

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mama wa mshambuliaji wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), Yohana Nkomola, amemtoa machozi  mama yake mzazi, Neema Nkomola, baada ya kumuona kwenye luninga akiiwakilisha Tanzania kwenye mechi ya Tanzania dhidi ya Mali.

Neema aliutazama mchezo huo uliomalizika kwa sare tasa akiwa nyumbani kwake Temeke jijini Dar es Salaam. Alijikuta akibubujikwa na machozi hayo baada ya kumuona mtoto wake akiwa sehemu ya kikosi cha vijana wa Tanzania.

Mama huyo aliyetazama mchezo huo pamoja na mtoto wake mwingine, Stanley Nkomola, alishindwa kujizuia na kumwaga machozi hayo na Stanley naye akaanza kulia baada ya kumuona mama yake analia.

Baada ya kumalizika mchezo huo uliofanyika nchini Gabon, Stanley alisema alishangazwa na tukio la mama yake, lakini ghafla na yeye akajikuta katika hali hiyo na kusema wanachokifanya kama familia ni kumuombea nyota huyo azidi kufanikiwa.

Stanley alisema mama alikuja ukumbini hapo kutazama mchezo huo akiwa ameshika Biblia na alianza kutokwa machozi alipowasikia watangazaji wa mchezo huo wakimtaja mwanaye (Yohana) kama mchezaji wa kuchungwa na walinzi wa Mali.

“Ilimshangaza kila mmoja wetu kwa kweli. Mimi na mama tulijikuta katika hali tusiyoitarajia baada ya kutazama mpira tulijikuta tukibembelezana. Yohana amecheza mechi nyingi za kuonekana kwenye luninga akiwa na Serengeti Boys, lakini hakuna hata siku moja tuliyomtazama na kuwa katika hali ya leo (Jumatatu),” alisema kaka huyo wa Yohana.

Aliongeza: “Awali nilipomuona mama analia nilimshangaa, lakini kila mpira ulivyokuwa unaendelea nami nilijikuta nikianza kutokwa machozi, kitendo ambacho sijakitarajia kukiona kikitokea kwenye maisha yangu, lakini hii ni furaha iliyopitiliza iliyokuwa ndani ya miili yetu na ndiyo iliyosababisha tuwe katika hali hii ambayo sijawahi kuwaza kuna siku naweza kukaa na mama tukimtazama Yohana kisha tukaanza kulia kwa pamoja.

“Lakini tunahitaji kumuombea Yohana asipate majeraha ili aweze kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa, maana majeruhi ni kitu kibaya sana ambacho akikipata mchezaji anakuwa katika mazingira hatarishi ya kuacha mpira wa ushindani mapema.”

Stanley aliyewahi kukipiga JKT Ruvu na Serengeti Boys aliendelea kusema kuwa mdogo wake atakuja kufanikiwa kutokana na kujali mazoezi magumu kitu ambacho wachezaji wengi hawakiwezi.

Alisema kufanikiwa kunahitaji usugu wa kufanya mazoezi magumu bila kuchoka, kitu ambacho Yohana anakipenda. “Sio kama namsifia mdogo wangu (Yohana), mimi nimecheza mpira na najua jinsi wachezaji tulivyokuwa na uvivu wa kufanya mazoezi magumu yanayochosha, lakini Yohana huwa anakomaa kufanya mazoezi hayo magumu.

“Kufanikiwa katika soka ni mazoezi na nidhamu, lakini wachezaji wengi ni wavivu wa kufanya  mazoezi magumu na hapa ndiyo unaweza kuona tofauti ya wachezaji wanaojituma na wasiojituma.

”Binafsi naamini dogo atakuja kufika mbali kutokana na kujitambua mapema sana tofauti na sisi kaka zake ambao tuliupenda mpira, lakini hatukuwa tukifuatisha miiko yake ya kufanya mazoezi magumu yanayojenga. Sasa Yohana ana vitu vyote viwili, anapenda mazoezi magumu na ana nidhamu kwa kila mmoja,” alisema kaka wa mchezaji huyo.

Hata hivyo, katika mchezo huo wa ufunguzi wa Serengeti Boys dhidi ya Mali, vijana wa Tanzania walicheza vizuri, lakini walishindwa kwenye mipira mingi ya kugombania dhidi ya vijana wenzao.

Mara kadhaa wachezaji wa Serengeti Boys iliwawia ugumu kuishinda mipira waliyokuwa wakienda kupambana na kuwafanya vijana wa Mali wautawale mchezo muda mrefu, lakini umahiri wa mlinda mlango wa Serengeti Boys, Ramadhan Kabwili ulikibeba kikosi chake kupata sare hiyo.

Viungo wa Serengeti Boys, Zuderi Ada na Nashon Naftal walionekana kuwabana viungo wa Mali, lakini tatizo la upambanaji wa miili ilikuwa tatizo kwa viungo hao kuwa na uwezo wa kupiga pasi za mwisho kwa washambuliaji.

Wakati huu michuano inavyoendelea, kama Watanzania tunatakiwa kuliona tatizo la miili kwa wachezaji wetu kama moja ya tatizo kubwa kwa timu zetu zikikutana na timu za Ukanda wa Afrika Magharibi ambako wachezaji wao wana miili mikubwa.

Mlinzi wa kati wa Mali, Diaby, ambaye mara nyingi alikuwa akikwaruzana na Nkomola, alionekana kuwa mkubwa kwa wachezaji wa Serengeti Boys kutokana na kuishinda mipira mingi ya hewani na kila timu yao ilipopata mipira ya adhabu alipanda mbele kusaidia mashambulizi.

Tunahitaji kujua jinsi ya kulidhibiti tatizo hilo la vimo na miili ili kwenye michezo inayofuata dhidi ya timu za Niger na Angola na tujue Serengeti Boys inakwenda kupambana vipi na vijana wa timu hizo ambao nao wamejengeka misuli.

Kiufundi hatukuwa vibaya sana hasa ukitazama rekodi za Mali na rekodi zetu. Serengeti Boys inashiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza tofauti na Mali walioanza kushiriki michuano hiyo tangu mwaka 1997 na mwaka huu wakija kwenye michuano kama mabingwa watetezi.

Tulipongeze benchi letu la ufundi lililo chini ya Bakari Shime kwa kuwafahamu wapinzani wetu na kucheza soka la taratibu, huku tukiwashambulia wapinzani kwa mipira ya kushitukiza (Counter-attack).

Mbinu hiyo ilitusaidia kuwabana wapinzani ambao walionekana kuwa wasumbufu kwenye lango la Serengeti Boys, ambao kuna wakati wachezaji wake walicheza mpira ya kitoto kwa kupasiana mipira isiyofika kwa walengwa na Mali nao hawakuwa na umakini wa kutuadhibu kwenye makosa yetu.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Serengeti Boys.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *