Ofisi ya madini Mwanza taabani

OFISI ya Madini Mkoa wa Mwanza inakabiliwa na ukata hivyo kujikuta inadaiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) deni la pango la nyumba linalofikia Sh milioni 70 kwa sasa.

Taarifa ya ofisi hiyo iliyowasilishwa kwenye kikao cha wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza mbele ya Makamu Mwenyekiti, Richard Ndassa wiki iliyopita, ilifafanua kwamba gharama ya pango hilo ni Dola za Marekani 2,600 (swa na Sh milioni 5.72) kwa mwezi.

“Tumewasilisha maombi kwa Katibu Mkuu (wa Wizara ya Madini) ili atusaidie kulipa (deni la Sh milioni 70) kwa kuwa fedha ya matumizi ya kawaida haitoshi kutenga fedha za kulipa deni hilo.

“Aidha, upungufu wa fedha za OC (Matumizi Mengine) umesababisha tushindwe kusimamia shughuli za ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ipasavyo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, makusanyo yake ya maduhuli ya serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 kufikia Februari 28, mwaka huu ni Sh bilioni 1.11 na Dola za Marekani 945,744. 76 (sawa na Sh bilioni 2.08).

Wachimbaji wadogo

Taarifa zaidi kutoka ofisi hiyo inayoongozwa na Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi Yahya Samamba, zinasema kumekuwapo na wachimbaji wadogo wengi wanaochimba kwa kubahatisha kutokana na kukosa mitaji ya kugharimia utafiti wa madini kwanza.

Aidha, wachimbaji wengi wa madini mkoani hawamudu majukumu ya kulipa ada za mwaka za leseni zao kwa wakati hali inayosababisha kufutiwa leseni hizo.

Lakini pia maeneo ya utafiti mkubwa wa dhahabu yamekuwa yakivamiwa na wachimbaji haramu, hivyo kukwamisha uanzishaji wa migodi mipya ya kati na mikubwa.

Kikwazo kingine kimetajwa kuwa ni kuongezeka kwa gharama za uchimbaji kadiri kina cha mgodi kinavyoongezeka hali inayodhoofisha juhudi za wachimbaji wadogo ambao mara nyingi hawakopesheki kwenye taasisi za fedha.

“Kushuka kwa bei ya dhahabu na nikeli katika soko la dunia kumechangia kuchelewesha uanzishaji wa migodi maeneo ya Nyanzaga wilayani Sengerema,” inadokeza taarifa hiyo.

Leseni za madini

Ofisi inabainisha kuwa Mkoa wa Mwanza una leseni hai za uchimbaji madini zipatazo 69. Kati ya hizo, Wilaya ya Misungwi inamiliki 32, Kwimba (19) na Sengerema (18), huku Nyamagana, Ilemela, Ukerewe na Magu zikiwa hazina leseni hizo.

Mkoa hauna leseni za uchimbaji mkubwa wa madini, lakini una leseni hai 10 za uchimbaji wa kati wa madini. Kati ya hizo, saba ni za uchimbaji wa madini ujenzi (mawe, kokoto na mchanga), mbili ni za dhahabu na moja ya almasi.

Madini ujenzi huingiza serikalini wastani wa Sh milioni 30 na dhahabu wastani wa Sh milioni 26 kwa mwezi mkoani Mwanza.

Mkoa pia una leseni hai 295 za uchimbaji mdogo wa madini zikiwamo 185 zilizopewa hati ya makosa kutokana na kushindwa kutekeleza matakwa ya sheria. Wahusika huenda wakafutiwa leseni hizo ikiwa hawatazirekebisha.

Kwa upande mwingine, kuna wafanyabiashara 18 wenye leseni za uchomaji madini na tisa wanaopewa vibali vya muda mfupi kujihusisha na shughuli hizo mkoani.

Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa dhahabu ni Mihama na Iluja Mate wilayani Misungwi. Pia Mwagiligili lililopo mpakani na Wilaya jirani ya Kwimba.

Inaelezwa kwamba uzalishaji wa almasi ni wa kiwango kidogo na wanunuzi wake wakubwa wapo Mkoa jirani wa Shinyanga.

Majukumu ya ofisi

Mjukumu ya ofisi ya madini Mwanza ni kusimamia shughuli zote za sekta hiyo mkoani kwa mujibu wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009, Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Marekebisho yake ya Mwaka 2017 na Kanuni zake, Sheria ya Baruti ya Mwaka 1963 na Kanuni zake za Mwaka 1964.

Huduma zinazotolewa na ofisi hiyo ni pamoja na kupokea, kufanya mchakato na kutoa leseni za uchimbaji mdogo, za biashara ya madini na mawakala.

Na pia kutoa vibali mbalimbali vinavyohusu masuala ya madini na matumizi ya baruti, ukaguzi wa migodi mikubwa, ya kati na midogo kuhusu uzalishaji, uchimbaji salama, afya na utunzaji wa mazingira.

Huduma nyingine ni ukaguzi wa leseni za utafiti na uchenjuaji wa madini, huduma za ugani kwa wadau wa madini, elimu ya uelewa wa Sheria ya Madini na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatokanayo na shughuli za madini.

Mafanikio patikana

Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ofisi hiyo imeweza kuelimisha jamii inayoishi maeneo ya madini kuhusu mambo ambayo mmiliki wa leseni ya madini anapaswa kufanya kwa wamiliki wa ardhi kabla ya kuanza uchimbaji.

“Lakini pia elimu imetolewa kuhusu masuala ya afya, usalama na mazingira kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu eneo la Mwamazengo,” inaongeza taarifa ya ofisi hiyo.

Imeweza pia kufanya uhakiki wa uzalishaji wa dhahabu na kukusanya maduhuli ya serikali kwenye maeneo husika, udhibiti wa kukusanya maduhuli ya madini ujenzi na kuanzisha vituo sita vya ukaguzi wa madini hayo.

Mikakati iliyopo

Ili kuongeza ufanisi katika sekta ya madini, ofisi hiyo imejiwekea mikakati ya kuwapatia wachimbaji elimu ya ujasiriamali waweze kufahamu mahitaji muhimu ya shughuli zao.

Mikakati mingine ni kubaini na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kutoa leseni za utafiti mkubwa.

Sambamba na hilo, panatakiwa Wakala wa Jiolojia Tanzania kusaidia kufanya utafiti wa awali kwenye maeneo yanayotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadodo wa madini.

Na pia kuanzisha soko la pamoja la dhahabu jijini Mwanza ili kudhibiti utoroshaji wa madini hayo kwenda nje ya nchi na kutafuta njia bora ya kufanya biashara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *