Makala
Oscar Kambona: Upande wa pili wa shilingi III
Maggid Mjengwa
Toleo la 195
20 Jul 2011

OSCAR Kambona aliondoka nchini na kuacha nyuma yake vumbi zito. Kulikuwa na   kamata kamata  iliyoendelea.  Hakukuwa na habari kamili, bali uvumi ulioshamiri.

Na katikati ya vumbi  na uvumi huo ulioshamiri kulikuwa na kimya kikuu. Kulijengeka hofu miongoni mwa wananchi,  hususan wale wenye fikra za upinzani.

Wengi walikuwa wapinzani kwa  kunong’ona. Na utaratibu wa kila nyumba kumi kuwa na balozi wake kimsingi haukuwa na maana nyingine  zaidi ya Chama tawala kuwa na udhibiti wa mambo ikiwamo fikra za wananchi.

Balozi  wa nyumba kumi aliogopewa. Nje ya nyumba ya Balozi kulipepea bendera ya TANU.

Utaratibu wa kuwa  na balozi wa nyumba kumi ungekuwa wa maana zaidi kama ungekuwa ni wa  mawasiliano ya dhati ya njia mbili. Balozi wa nyumba kumi ilikuwa na maana ya balozi wa TANU katika  kila nyumba kumi  badala ya kuwa balozi wa wananchi kwa TANU.

Balozi alitumika kupenyeza kwa watu wake yale yanayotoka juu. Na kutoka chini, kazi ya balozi mara nyingi ilikuwa ni kuwaripoti kwa viongozi  wa juu wa TANU; ’ wakorofi’ walio katika nyumba zake kumi. Ndio chanzo cha wananchi kumwogopa hata balozi wao wa nyumba kumi. 

Balozi wa nyumba kumi naye alikuwa kama  ’shushushu’, Jina walilopewa wale waliokuwa wakifuatilia nyendo za wananchi wenye kupinga mambo ya Chama na Serikali. Hii nayo ni historia yetu, imechangia katika kutufikisha hapa tulipo. Kujaribu kuikana historia hii ni kujaribu kujikana wenyewe.

Turudi kwa Oscar Kambona.  Hatimaye baada ya kuikimbia nchi, Kambona akaishia London, Uingereza. Alikimbilia ’ Kwa mama’.  Huko akapewa hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa.  Vumbi aliloliacha nyuma likachukua muda mrefu kutuama. Maana,  huko alikokuwa, Kambona bado aliendelea kumtimulia vumbi rafiki yake Julius Nyerere. Oscar akawa  mmoja wa ’ maadui wa nje’.

Mengi hayajulikani juu ya maisha ya Kambona akiwa Uingereza na hasa harakati zake za chini chini dhidi ya rafiki yake wa zamani Julius Nyerere. Na mara kadhaa, ulipotokea uvumi  wa  jambo baya au hujuma dhidi ya Serikali ya Tanzania, jina la Kambona lilisikika likitajwa.

Ni Kambona yule aliyeimbwa kwenye nyimbo za mchakamchaka mashuleni ; kuwa  ’ aliolewa Ulaya’ kwa vile wivu ulimkereketa! Mathalan, katika kesi ya uhaini ya mwaka 1970, Oscar Kambona  alituhumiwa kuwa nyuma ya mpango wa  kumpindua Julius Nyerere. Miongoni mwa waliotuhumiwa kuhusika na mpango huo ni Bibi Titi Mohammed.

Jina la Oscar Kambona liliibuka tena na  kuzungumzwa mitaani  mara ile, mwaka 1982, vijana akina Memba na wenzake wanne  walipoiteka ndege ya  Shirika la Ndege la Tanzania, ATC, Boeing 737. iliyokuwa ikitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam. Waliilazimisha ndege hiyo chini ya kapteni George Mazola itue Nairobi. Hapo ikajaza mafuta, kisha ikaruka na kutua Jeddah, Athens na hatimaye uwanja wa Stansted, Uingereza.

Watekaji wa ndege, akina Memba na wenzake walitaka  Oscar Kambona afike uwanjani hapo ili aongee nao. Kambona, alifika na kuongea na wale watekaji ndege. Hawakuwa na madai mengine bali kutaka wasaidiwe wabaki Uingereza. Na kuna abiria wengine pia waliotaka wabaki Uingereza.

Machoni mwa dunia ilionekana, kuwa Watanzania mfano wa akina Memba na wenzake walikuwa tayari kutumia mbinu zote alimradi waondoke kwenye nchi ambayo inadai imefanikiwa sana kwenye sera zake za Ujamaa. Hivyo basi, tukio lile lililotangazwa sana kimataifa  kwa namna fulani liliudhalilisha utawala wa Julius Nyerere.

Juu ya yote, Oscar Kambona alikuwa nje ya mipaka ya Tanzania. Alipoteza mengi ikiwamo mmoja wa watoto wake aliyeuawa London na watu ambao mpaka leo hawajulikani.  Na jina la Oscar Kambona likazidi kusahaulika kwa Watanzania wa vizazi vilivyofuata.

Na kuna Mtanzania aliyekuja na kuanza taratibu kufungua milango ya uhuru wa Watanzania kuongea ikiwamo kumshutumu   mkuu wa nchi, Chama na Serikali,  hadharani na kwa sauti. Si kwa kunong’ona. Mtanzania huyu anaitwa Ali Hassan Mwinyi. 

Kama Urusi ya zamani ilikuwa na Mikhael Gorbachev aliyefungua milango ya uhuru wa kuongea na kushutumu hadharani, basi, kwa Watanzania, Ali Hassan Mwinyi ndiye Gorbachev wetu.

Nilikuwa na Othman Nyamlani pale viwanja vya Ukumbi wa Diamond siku ile Nyerere anang’atuka rasmi na kumwachia mikoba ya Chama na Urais  Ali Hassan Mwinyi.  Mimi na Nyamlani tulikuwa wanafunzi wa Kidato cha Pili pale Tambaza Sekondari.  Othman Nyamlani sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF).

Hotuba ile ya kwanza ya Ali Hassan  Mwinyi pale Ukumbi wa Diamond ilifungua ukurasa mpya kwa nchi yetu.  Mwinyi alionekana kuwa mnyenyekevu na mtu asiyejikweza. ” Ndugu zangu, kama mtanilinganisha mie na Mwalimu, basi, Mwalimu ni sawa  na Mlima Kilimanjaro na  mie ni kichuguu!” Alitamka Ali Hassan Mwinyi huku akiwaacha wajumbe wa mkutano wakimshangilia .

Haukupita muda nikakiona ’ Kichuguu’ kile; Ali Hassan Mwinyi, katika nafasi ya Urais. Alasiri moja nilimwona Rais wa nchi, Ali Hassan Mwinyi akiwa amechuchumaa pale Mtaa Kongo, Kariakoo na kuongea na akina mama wauza mayai.  Mwinyi  alitembea kwa miguu akiongea na wananchi huku magari yasiyozidi manne ya msafara   wake yakiwa yameegeshwa kando ya Ukumbi wa DDC Kariakoo.

Ndio, Mwinyi yule niliyemwona, alishuka chini na kuanza kuwasikiliza wananchi badala ya kusimama tu majukwaani na kuhutubia.

Na ni Mwinyi huyo huyo katika uongozi wake, akasikia, kuwa Oscar Kambona yuko njiani kurudi nyumbani.  Kuna nguvu zilizokuwa zikitaka kuhakikisha Kambona hatui Dar es Salaam, lakini, yaonekana Ali Hassan Mwinyi hakuona ubaya wa Kambona kurejea nchini. Maana, mwaka ule wa 1992, zilipokuja habari za kuaminika kuwa Kambona yuko njiani kuja, tulimsikia redioni  Augustino Mrema akitamka kwa  Kama Kambona angetua  Dar es Salaam angekamatwa  kwa vile alikuwa ana  kesi ya uhaini.

Ikafika siku, Kambona akatua, hakukamatwa na wala  hakuitwa mahakamani. Kama Rais Mwinyi angekuwa Rais mwenye chuki na kisirani, basi,  angemwacha Mrema atume FFU Uwanja wa ndege. Waende wakamkamate Kambona na kuwapiga virungu wafuasi wake.

Inaendelea

Soma zaidi kuhusu:

Tufuatilie mtandaoni:

Wasiliana na mwandishi
Maggid Mjengwa
mjengwamaggid@gmail.com
+255-754678252, +255-712956131
http://mjengwa.blogspot.com

Maggid Mjengwa pia ni Mwandishi wa Kitabu; "Maisha Ya Barack Obama, alikotoka, aliko na anakokwenda". Kinapatikana mitaani.

Toa maoni yako