Oxfam yajivunia kampeni yake ya Mama Shujaa

UNAWEZA ukajiuliza maswali mengi sana kwa nini wanawake wengi wameamua kujikita kwenye shughuli za kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za mikono?  Jibu la swali hilo ni kampeni ya Mama Shujaa wa Chakula iliyoanzishwa na Shirika lisilo la kiserikali la Oxfam Tanzania. 

Kampeni  ya Mama Shujaa wa Chakula ilianzishwa tangu mwaka 2011 ikiwa na lengo la kuwapatia fursa kina mama kuonesha uwezo wa kuchangia chakula kupitia shughuli za kilimo.

Mbali na kilimo lakini kina wanawakea hao pia walifundishwa namna bora ya  ufugaji ili pamoja na mambo mengine ufugaji huo uweze kuwainua kiuchumi.

Kampeni ya Mama Shujaa ilishirikisha wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania ambao walikutanishwa kwenye eneo moja na kufanyishwa shughuli za kilimo pamoja na uzalishaji wa chakula, mshindi aliyepatikana kupitia kura zilizopigwa na wadau mbalimbali kupitia baadhi  vyombo vya habari.

Kwa mujibu wa Oxfam, mshindi aliyepatikana kwenye kinyanyiro hicho alizawadiwa vifaa vya za kilimo kwa ajili ya kuendeshe shughuli za kilimo kwenye eneo lake analoishi.

Baada ya kampeni hiyo ya miaka mitano hivi sasa Oxfam inafanya tathimini ya Mama Shujaa tangu kuanzishwa kwake 2011 kuona ambavyo shindano limeweza kuwasaidia kina mama.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mawasiliano wa Oxfam Kisuma Mapunda, tathimini hii itafanywa na mtaalamu wa Oxfam kuona ni kwa namna gani shindano hili limeweza kuwasaidia wanawake kwenye shughuli za uzalishaji mali.

“Kwa kushirikiana na mtaalamu wetu tutawatembelea kina mama walioshiriki kwenye shindano kuona mafanikio yaliyopatikana na kuangalia fursa nyingine zilizopo lengo likiwa ni kuwainua wanawake wengi.

Mbali na kuwatembelea wanawake hao lakini pia tutatembelea sekta zote za kilimo  ambazo tumeweza kufanya nao shughuli kwa nia ya kubaini changamoto, fursa zilizopo na kuweza kuzifanyia kazi kwa ajili ya maandalizi mengine ya Mama Shujaa anayekuja.

Kwa mujibu wa Mapunda kwa mwaka huu 2017/19 Oxfam inafanya shughuli zake kwenye mikoa ya Limdi, Mtwara, Shinyanga, Kigoma kwenye kambi za wakimbizi pamoja Ngorongoro.

 “Makundi ambayo tunafanya nayo kazi ni wananchi wa kawaida kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara, Shinyanga pamoja na Kigoma kwenye kambi za wakimbizi, Ngorongoro kuwafahamisha namna ya kupata taarifa kwa kupitia simu ya mkononi.

“Tutatumia taarifa zao hizo kwa kuwekea mikakati ya kufanya kampeni za kupatia ufumbuzi wa changamoto zilizoibuliwa kupitia mawasiliano hayo”.

Katika hatua nyingine Oxfam kwa kushirikiana na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali inakusudia kuadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani Juni 20 kwa kuhakikisha wakimbizi wanapatiwa huduma ya maji pamoja huduma za afya ikiwemo kujengewa vyoo vya kisasa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mapunda kwa mwandishi wetu ni kwamba kwenye maadhimisho hayo kutakuwa na programu ya kuzuia ukatili wa kijinsia kwa kufanya kampeni kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Mbali na Oxfam lakini maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani yataadhimishwa na mdau mkubwa wa wakimbizi, UNHCR(Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi) pamoja WFP(Mpando wa Chakula Duniani).

Mapunda alisema: “Sisi kama Oxfam tunafanya kazi kwa pamoja na mashirika mengine akiwemo UNHCR ambaye ni mdau mkubwa wa wakimbizi.

“Wengine ni WFP(Mpango wa Chakula Duniani). Kama inavyofahamika WFP wao ni kuhakikisha chakula kinapatikana na sisi Oxfam jukumu letu ni kuhakikisha maji safi yanapatikana, vyoo vinajengwa pamoja na kuweka miundo mbinu ya kijamii ikiwemo kutengeneza  majiko  ambayo hayatumii kuni nyingi.

Kwa mujibu wa Mapunda maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi yanatarajia kufanyika Mkoa wa Kigoma Kasulu na Kibondo kwa kufanya shughuli mbalimbali kwa kushirikiana na halmashauri za mkoa husika.

“Katika siku hiyo wakimbizi watapata fursa ya kuelezea changamoto walizo nazo kule kambini, wataeleza jinsi wanavyopata misaada ya kuboresha maisha yao. Yote yatakayojadiliwa kwenye maadhimisho hayo itakuwa ni fursa kwetu kuweza kufanyia kazi”alisema Mapunda.

Siku ya Wakimbizi Duniani huadhimishwa Juni 20, siku hiyo iliundwa mwaka 2000 na azimio maalum la mkutano mkuu wa umoja wa mataifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka 2015 idadi ya wakimbizi kutoka nchini Burundi wanaokimbia nchi yao kuingia  Tanzania ilifikia 91,661 kwa takwimu za Septemba 8 mwaka 2015.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo wakimbizi hao walihifadhiwa katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu iliyoko  Wilaya ya Kasulu Mkoa wa Kigoma.

Taarifa iliongeza kudai kwamba, tangu kuanza kuingia kwa wakimbizi hao Aprili 2015, Wizara ya Mambo ya Ndani  ya Nchi kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na wadau wengine imekuwa ikiwapokea na kuwapa hifadhi na huduma nyingine muhimu. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *