Paul Makonda ni nani?

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari.

LEO, Februari 15, 2017, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, anatimiza umri wa miaka 35.

Katika Jumatatu hiyo ya kipekee (miaka 35 iliyopita), majira ya saa 1:30 asubuhi, familia ya mzee Makonda na mkewe, Suzan, walimkaribisha mtoto wao pekee wa kiume katika Zahanati ya Kolomije, wilayani Misungwi mkoani Mwanza.

Machi 13 mwaka jana, Rais John Magufuli, alibadili kabisa mwelekeo wa maisha ya kijana huyu kwa kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; akiwa mmoja wa wakuu wa mikoa wenye umri mdogo zaidi hapa nchini.

Na sasa, jina la Paul Makonda limekuwa maarufu kuliko la mkuu wa mkoa mwingine yeyote nchini. Katika maisha yake mafupi ya kisiasa, Makonda amebebwa na wanasiasa wa CCM na Upinzani, ameudhi na kukera wengine; amesifiwa na kubezwa katika uzito uleule.

Imekuaje Paul Makonda akawa Makonda huyu anayejulikana sasa? Na ingawa sasa amepata umaarufu zaidi kutokana na vita ya dawa za kulevya, Makonda alianza kupata umaarufu walau miaka minne hivi iliyopita.

Kwanza kama mwanaharakati mwanafunzi; halafu kijana aliyekuwa akiwindwa na vyama vya siasa; kisha kijana wa CCM aliyekuwa mstari wa mbele kwenye vita ya wanachama wa chama hicho kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015; mpinzani wa Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba na baadaye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Historia ya Makonda

Kwa ufupi, Makonda ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. Lakini safari yake ya kitaaluma ilikuwa ngumu kutokana na hali ya kipato cha wazazi wake.

Kabla ya kwenda Moshi, alipita katika Shule ya Msingi Kolomije na amesoma pia katika Chuo cha Uvuvi, Mbegani, Bagamoyo ambako alisoma hadi ngazi ya Diploma katika masuala ya uvuvi.

Watu wanaomfahamu Makonda tangu enzi akiwa mwanafunzi Kolomije wanamweleza kama mtu aliyekuwa akifuata dini na mwenye wazazi waungwana.

Yeye ni mtoto pekee kwao hivi sasa kwani alipata kuwa na ndugu wa kike lakini alifariki dunia mwaka mmoja na nusu tu baada ya kuwa amezaliwa.

Kufikia alipo sasa, Makonda amepitia kwenye maisha ambayo ni ndoto kulinganisha na maisha aliyonayo sasa. Kati ya mwaka 2001-2002, Makonda alikuwa anafanya kazi ya utingo kwenye vyombo vya usafiri na alipokuja Dar es Salaam, aliwahi kufanya kazi kama mchimba mchanga na mkata mkaa katika eneo la Mbezi Luis.

Hata hivyo, wanasiasa wa siasa za kitaifa walianza kumfahamu wakati alipoanza kuonyesha karama yake ya uongozi alipokuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Muccobs).

Mara baada ya misukosuko na minyukano ya siasa za ndani za CCM, hatimaye Rais Jakaya Kikwete alimteua Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni mnamo Februari 18, mwaka 2015.

Makonda na Chadema

Watu wanaomfahamu Makonda wakati akiwa mwanafunzi Moshi, wanamfahamu kama mwanaharakati ambaye mwelekeo wa siasa zake ulikuwa wa upinzani zaidi kuliko CCM.

Viongozi wa juu wa Chadema waliozungumza na gazeti hili wameonyesha kumfahamu Makonda na kuna maelezo kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alimshawishi Mkuu huyu wa Mkoa ajiunge na chama chake zamani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Kiumri, Makonda ni rika la wanasiasa vijana wa Chadema kama vile akina John Mnyika, John Mrema, Halima Mdee na Zitto Kabwe waliotafutwa katika taasisi za elimu ya juu katika siku za mwanzo za uenyekiti wa Mbowe.

Ziko taarifa kwamba Mbowe na aliyekuwa Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo, waliwahi kufadhili masomo na malazi ya Makonda wakati akiwa mwanafunzi na baadaye katika siku za mwanzo za maisha yake baada ya uanafunzi.

Raia Mwema lilimtafuta Mbowe kutaka kufahamu kama ni kweli aliwahi kumlipia au kumfadhili Makonda kwa namna yoyote katika maisha yake ya nyuma lakini Mbunge huyo wa Hai alikataa kuzungumzia suala hilo.

“Sikiliza mwandishi, mimi sina la kusema kuhusu hilo swali lako. Wakati mwingine naweza kusema kitu na halafu nikaonekana kama namsimanga mtu. Hapana, naomba nisiseme kitu,” alisema Mbowe.

Wakati wa mnyukano ndani ya CCM baina ya kundi lililokuwa likiongozwa na Edward Lowassa na jingine lililoitwa la wapinga ufisadi chini ya Samuel Sitta, Makonda akaibukia kwenye kundi la Spika huyo wa Bunge la Tisa.

Hadi sasa hakuna simulizi ya uhakika kuhusu ni kwa vipi hasa Makonda aliibukia kwa Sitta lakini baadaye, kijana huyo alifanikiwa kutengeneza uhusiano wa karibu na mbunge huyo wa zamani wa Urambo kiasi cha kumuita Baba.

Wakati mzee Sitta alipokaribia kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuanzisha chama kipya cha CCJ, Makonda anadaiwa kuwa katikati ya mpango huo; akiaminiwa na Sitta kupeleka taarifa muhimu kwa watu muhimu wakati wote.

Raia Mwema linajua kwamba siku ambayo Sitta hatimaye alikubali ushawishi wa kubaki CCM na kutohama, Makonda alikuwa mmoja wa watu watano waliokuwemo kwenye chumba kimoja nyumbani kwa mwanasiasa huyo aliyefariki mwaka jana.

Wengine waliokuwa pamoja na Sitta siku hiyo ni Waziri wa sasa wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, Mwenyekiti wa zamani wa Simba na Mbunge aliyepita wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage na Mbunge wa sasa wa Jimbo la Urambo, Margaret Sitta ambaye pia ni mjane wa Sitta.

Hata katika siku hiyo ngumu, Makonda alikuwa na msimamo mkali na gazeti hili limeambiwa alikuwa akitoa kauli za kutaka Sitta abaki na msimamo wake, kiasi kwamba mama Sitta kuna kipindi ilibidi aingilie kati na kumwambia kijana huyo; “ Waache wakubwa wazungumze”.

Katika Bunge la Katiba, ambalo Makonda alikuwa mmoja wa wajumbe walioteuliwa kujiunga nalo, alikuwa akifahamika kwa msimamo wake wa kuunga mkono Katiba Pendekezwa.

Yeye alikuwa mmoja wa vijana waliokuwa mstari wa mbele kutetea Katiba hiyo kiasi kwamba alikuwa mlengwa wa mashambulizi mengi kutoka kwa wafuasi wa vyama vilivyokuwa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kilele cha kufahamika kwa Makonda kilikuwa ni kutajwa kwake kushiriki katika vurugu zilizosababisha kuvunjika kwa mkutano wa kujadili masuala ya Katiba uliokuwa uhutubiwe na Jaji Warioba.

Wafuasi wa vyama vya Upinzani walivumisha kwamba katika tukio hilo la aibu lililotokea katika ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo, Dar es Salaam, Makonda alimfanyia fujo Warioba.

Hata hivyo, mahojiano ambayo yamewahi kufanywa na gazeti hili kwa mzee Warioba mwenyewe na Makonda pia, yalibaini kwamba Mkuu huyu matata wa Mkoa wa Dar es Salaam hakumfanyia fujo Waziri Mkuu mstaafu huyo na badala yake alikuwa akisaidia aondoke ukumbini kwa usalama.

Ndiyo sababu, wakati Kikwete alipomteua Makonda kuwa Mkuu wa Wilaya, mijadala mingi iliibuka katika mitandao ya kijamii na vyombo rasmi vya habari kuhusu kufaa kwa kijana huyu kwa nafasi hiyo.

Miezi sita baada ya uteuzi huo, Makonda alijibadili kutoka mmoja wa wanasiasa vijana wanaochukiwa hapa nchini na kuwa aina ya viongozi wapya waliokuwa wakihitajika kwa Jiji la Dar es Salaam.

Miezi michache kabla Rais Magufuli hajamchagua kushika wadhifa wake huo mpya, ilikuwa ikibashiriwa kwamba huenda Makonda akapandishwa cheo.

Makondanomics

Makonda, kama walivyo viongozi wengi vijana kwa sasa, hawajapitia mafunzo ya kiitikadi waliyokuwa wakipewa viongozi wa chama na serikali.

Hivyo ingawa ni mwana CCM, Makonda hafuzu kuitwa kada. Aina yake ya siasa anayofanya ni ile siasa inayoweza kuwavutia wananchi kwa wakati husika.

Utendaji wake unaendana na nguvu ya vyombo vya habari na mara zote umahiri wake kazini unategemea zaidi na namna anavyoandikwa au kuelezwa na vyombo vya habari.

Hadi sasa, ndiye Mkuu wa Mkoa pekee nchini, na pengine katika historia ya Tanzania, ambaye mikutano yake ya hadhara imekuwa ikionyeshwa mbashara na vituo vya luninga na redio.

Makonda amekuwa akifahamika kwa kuibuka na masuala ambayo yamepewa nafasi kubwa katika vyombo vya habari lakini hayaendi mpaka mwisho.

Kwa mfano, wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,  Makonda aliamuru walimu waweze kusafiri bure kwa vitambulisho maalumu ili kuwapunguzia mzigo wa kulipa nauli.

Wiki kama hii mwaka mmoja uliopita, Makonda alianzisha utaratibu wa kusaka vipaji kwa vijana kwa kuanzisha shindano la Kinondoni Talent Search ambalo mwaka huu halijaendelea.

Ni katika kipindi hichohicho, Makonda alitangaza mpango wa kuanzisha mtaa maalumu jijini Dar es Salaam utakaokuwa ukihusika na biashara ya vinywaji vikali na baridi na si baa kuzagaa kila sehemu.

Ni katika wakati huo ndipo alipotoa agizo kwa watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kwenda kuzisalimisha katika vituo vya Polisi vilivyo karibu nao.

Katika siasa ambazo hazina mwelekeo thabiti wa itikadi, namna pekee kwa wanasiasa wa aina ya Makonda kuweza kubaki madarakani ni uwezo wao kuibua vitu vipya kila kukicha.

Utajiri wa Makonda

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kabla ya kuibuka kwa vita aliyoianzisha dhidi ya biashara ya dawa za kulevya, machache yalikuwa yakifahamika kuhusu utajiri binafsi wa mwanasiasa huyu.

Kulikuwa na minong’ono ya hapa na pale lakini vita hii imeibua tuhuma kuhusu ukwasi wa mwanasiasa huyu ambao wanaomtuhumu wanadai zinahitaji kufuatiliwa na Tume ya Maadili ya Viongozi.

Kwa mfano, Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, ameibua madai kwamba Makonda anamiliki nyumba ya kifahari na amenunua zawadi kwa mkewe ambazo hazifanani na kipato chake.

“Makonda amenunua apartment pale Viva Towers kwa shilingi milioni 600 na amempa mke wake gari aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Dola 250,000 za Marekani (Sh. 550 milioni) kama zawadi ya ‘Birthday’,” alisema Selasini ndani ya Bunge wiki iliyopita.

Siku moja kabla ya Selasini kusema hivyo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Rushaku (Msukuma), naye aliibuka na tuhuma nzito dhidi ya Makonda na kutaka vyombo husika vimchunguze.

 “Mheshimiwa Spika, nasimama kwa kanuni ya 68(7) kuhusu jambo lililojitokeza jana (juzi) wakati wa mjadala wa Bunge…naomba mwongozo wako.

"Mimi binafsi naunga mkono jitihada za Rais kukamata wauza dawa za kulevya, lakini dalili ya kwanza ya kuanza kumhisi mtu kama anajishughulisha na biashara ambazo hazieleweki, kwanza ni mwenendo wa mtu yeyote…si mbunge wala si nani.

 “Anatumia Lexus ya petroli ya Sh. milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh. milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa serikali.

“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi? Na hawa mawaziri tulionao humu, kwa nini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwa nini mmepigwa ganzi?”

Siri ya Makonda

Makonda, ni kama vile ameimanya siri ya kuishi vizuri na wakubwa. Katika maisha yake ya kisiasa, siku zote amejinasibu na wanasiasa ambao wamemzidi umri kwa mbali.

Ni kama vile ameijua siri ya kukubalika kwa viongozi wa juu. Kwenye mikutano ya hadhara na mahojiano na vyombo vya habari, Makonda amekuwa akipenda kuonyesha kuwa anachofanya yeye ni kutimiza tu maagizo ya mabosi yake.

Mmoja wa wanasiasa maarufu vijana hapa nchini ametumia lugha ya Kiingereza kueleza siri ya kupanda haraka kisiasa kwa Makonda.

“ Makonda knows how to massage the ego of his superiors. Wakati wenzake watasema Rais Kikwete, yeye atasema Rais Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete.

“ Wengine wakiishia kusema Rais John Magufuli, Makonda atasema Dk. John Pombe Joseph Magufuli. Wewe ukimwita Kiongozi Spika, yeye atamwita Baba. Anajua kucheza na akili za viongozi wa juu,” alisema mwanasiasa huyu.

Muda utaeleza ni wapi safari ya kisiasa ya Makonda itaishia.

6 thoughts on “Paul Makonda ni nani?”

 1. Amour says:

  Tatizo letu Watanzania hatutaki kukubali ukweli kwamba hatuwezi kamwe kupata maendeleo ya kweli bila kwanza kukubali kila mmoja wetu kuamua kutimiza wajibu wake pasina kutanguliza mbele maslahi binafsi. Sasa inapotokea kiongozi kama Mhe. Makonda kusimamia kwa dhati majukumu yake kwa mujibu wa wadhifa wake, hapo ndipo Watanzania hao hao tunapoanza kumlaumu. Mimi binafsi nimeshuhudia watu wengi huku Pemba vijijini wakilia machozi baada ya kufika mashambani mwao na kukuta mazao yameibiwa na wala unga, huku wezi wa mazao hayo wakitetewa na kulindwa na Polisi. Imefikia hadi baadhi wanavijiji hawamiliki tena kuku, ndizi, matikiti n.k baada ya walaunga kuendeleza wizi kila siku ili wapate pesa za kununulia unga. Mimi binafsi namuombe dua Mhe. Makonda, Allah amlinde na maadui zake na ampe nguvu zaidi za kupambana na Wahusika na Madawa ya kulevya, Amin.

  Mpenda maemdeleo wa kweli.

   

 2. nsas says:

  Tatizo letu Watanzania hatutaki kukubali ukweli kwamba hatuwezi kamwe kupata maendeleo ya kweli bila kwanza kukubali kila mmoja wetu kuamua kutimiza wajibu wake pasina kutanguliza mbele maslahi binafsi. Sasa inapotokea kiongozi kama Mhe. Makonda kusimamia kwa dhati majukumu yake kwa mujibu wa wadhifa wake, hapo ndipo Watanzania hao hao tunapoanza kumlaumu. Mimi binafsi nimeshuhudia watu wengi huku Pemba vijijini wakilia machozi baada ya kufika mashambani mwao na kukuta mazao yameibiwa na wala unga, huku wezi wa mazao hayo wakitetewa na kulindwa na Polisi. Imefikia hadi baadhi wanavijiji hawamiliki tena kuku, ndizi, matikiti n.k baada ya walaunga kuendeleza wizi kila siku ili wapate pesa za kununulia unga. Mimi binafsi namuombe dua Mhe. Makonda, Allah amlinde na maadui zake na ampe nguvu zaidi za kupambana na Wahusika na Madawa ya kulevya, Amin.

  Mpenda maemdeleo wa kweli.

   

 3. Mark Mambo says:

  Kero ya waliotapeliwa viwanja iliishia wapi?

 4. Pingback: Tanzania – Is parliament waking up? | Democracy in Africa
 5. Trackback: Tanzania – Is parliament waking up? | Democracy in Africa
 6. Skeeter says:

  Jamani watanzania wenzangu. Kwanini tuu wepesi kusahau? Si tulisema tunataka mabadiliko?? Mnafikiri maana ya mabadiliko ni nini? Wengine watalia na wengine watacheka. Hakuna asiye na Mapungufu, hilo linajulikana wazi kabisa. Tumeona nia njema ya kiongozi wetu Makonda ya kupambana na madawa ya kulevya ambalo ni tatizo kubwa linalotesa wengi. Kwanini tusimpe ushirikiano wakati tunaelewa fika anachokifanya ni kwa faida ya watanzania? Kwanini tunakuwa wepesi kuhukumu? Kwanini hatupendi kutambua jitihada zake katika kugusa eneo ambalo wengi walilifumbia macho na ambalo limeleta vilio kwa watanzania wengi? Jamani tuwe macho. Safari ya maendeleo sio rahisi hata kidogo. Maendeleo hayawezi kuja kama hakutakuwa na mabadiliko. Na mabadiliko hayaji bila kuumiza wengine.

  Mtanzania mwenye kiu ya maendeleo

 7. Massanda O'Mtima Massanda says:

  Katika dunia hii ya leo ambayo haina huruma, yenye "mimi kwanza", yenye roho za 'Utajiju', yenye upofu wa kuona mema, Makonda hawezi kuwa msafi!

  Ninachoweza kusema, Mwenyezi Mungu pamoja na Watanzania wenye uzalendo na matamanio ya mstakabali mwema wa nchi hii, watakuwa pamoja naye na kwa hakika, atavuka salama!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *