WAKATI makala hii inasomwa, huenda tukawa tayari na baraza jipya la mawaziri. Laweza kuwa jipya, au lenye viraka, lililosukwa upya au vyovyote vile, lakini cha msingi ni kuwa tutakuwa na kitu kinachoashiria kuwa ni kipya.
Hatua hii inafuatia mjadala ulioibuka bungeni kuwa mawaziri wanane wameshindwa kufanya kazi zao vizuri na kusababisha ubadhilifu wa fedha za umma katika wizara zao.
Kamati Kuu ya chama tawala cha mapinduzi (CCM), ama ikaunga mkono au ikashinikiza yafanyike mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri.
Makala hii haina lengo la kuwatetea walioshinikizwa kujiuzulu au kuwahukumu, inalenga kuwatahadharisha baadhi ya watu ninaowaheshimu.
Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa “inahitaji mtu uwe na moyo wa mwenda wazimu kutetea Azimio la Arusha”. Wakati ule aliona mwendokasi wa kupuuza maadili ya uongozi wa kisiasa na katika utumishi wa umma kuwa ulikuwa unatisha.
Kwa mantiki ile ile, mtu anahitaji kuwa jasiri sana kutetea yanayoelezwa kufanywa na viongozi wetu wa kisiasa kama tulivyoshuhidia bungeni majuzi.
Kwa kuwa sasa tuhuma hizi zinasemwa na wenye chama wenyewe na kwamba wameridhia kuwa Serikali isukwe upya kwa sababu ya ufisadi wa mawaziri hiyo ni hatua moja kubwa imefikiwa.
Hapa nina maana kuwa mawaziri wanaoitwa wezi na mafisadi hawakuanza tabia hiyo walipoteuliwa kuwa mawaziri.
Tabia hii waliianza mapema kabla hawajajitupa uwanjani kugombea ubunge. Kama walihonga ili kununua kura, au kama waliiba kura ili kushinda, hawakufanya hivyo kwa ajili yao wenyewe.
Walifuata sera ya mafiga matatu (diwani, mbunge na rais). Jinai hiyo ya kuhonga na kuiba haitakwisha katika fikra za watu hivi karibuni.
Kimsingi, anayeteua mawaziri ni yule yule aliyeteua hawa walioshindwa na kuachwa katika baraza jipya. Ukiwauliza walioachwa katika baraza hili na waliowahi kuachwa katika mabaraza yaliyopita ya Rais huyu huyu, wanakueleza kuwa tatizo ni la aliyewateua na si tatizo lao.
Kwamba, Rais akishawateua anaacha kuwaamini na kuwasikiliza au akiwasikiliza hafuati ushauri wanaompa.
Kwamba, wakati wote wa kutekeleza majukumu yao ya uwaziri, hawakuwa na uhakika kuwa watalindwa na kuheshimiwa na yule aliyewateua.
Ni hali hii hii ambayo watu wengi wamekuwa wakiichambua kuwa pale wanapopata matatizo, wateule wengi hutoswa pale wanapoingia katika matatizo ya kiutendaji.
Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda amepata misukosuko mingi ya kisiasa tangu ateuliwe kuwa Waziri Mkuu. Yawezekana sana hakujua nini kitamtokea alipokubali kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu. Alishindwa kujiuliza ni kwa nini Rais alishindwa kumlinda swahiba wake wa siku nyingi. Kosa la kushindwa kujiuliza swali hilo, hivi sasa linamgharimu sana. Mara nyingi ama amelazimika kushughulikia madhara ya maamuzi mabovu au maamuzi yaliyochelewa sana. Na wakati wote huo, Pinda huwa hana uhakika kama bosi wake atasimama naye hadi mwisho wa safari.
Tumeyaona ya sakata la David Jairo, misamaha ya kodi kwa mashirika ya dini, Mahakama ya Kadhi, mgogoro wa madaktari na sasa mgogoro wa shinikizo la kujiuzulu kwa mawaziri.
Wakati wa misukosuko hiyo, tumeona kwa hakika kuwa Rais anawasikiliza na kuwaamini baadhi ya mawaziri kuliko anavyomuamini Waziri Mkuu Pinda.
Hata katika sakata nyinginezo, Pinda amejikuta anasikilizwa akiwa mtu wa pili. Hii ingetosha kumfanya Pinda aombe kupumzika kuliko kusubiri siku moja kupumzishwa bila kujiandaa.
Kosa la kukubali kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu linasameheka, lakini la kukubali kuendelea hata baada ya Serikali hii kupata likizo ya wiki moja na zaidi, nina mashaka kama litasameheka.
Kuna uvumi umeenezwa kuwa Waziri Mkuu ameomba kupumzika asiwemo katika baraza jipya (lililosukwa upya). Inadaiwa ya kuwa Mzee Pinda amesisitiza kuwa asifikiriwe kuendelea kuwa Waziri Mkuu kwa sababu anadai amechoka na kuwa yupo tayari kusaidia kwa njia nyingine.
Inasemekana wametumwa watu kadhaa kumwomba Mzee abadili uamuzi wake huo na kwamba atapewa timu bora zaidi ambayo haitampa kazi kuiongoza. Natamani hizi ziwe ni tetesi za kweli kama zilivyo nyingine ambazo hukanushwa lakini zikabakia kuwa za kweli.
Kama Mzee Pinda ameamua hivyo amefanya vema. Pinda ni mtu muungwana na uungwana wake ndio kitanzi chake cha hatari.
Kupitia uungwana wake, amedhalilika mbele ya umma na kuishia kuuguza vidonda vya tumbo.
Kazi ya punda anayoifanya ili kufunika aibu ya Serikali hii, haijampatia heshima mbele ya waliomteua. Kwa kuwa sasa imetokea fursa kuwa baraza linaundwa upya, ni ruksa na busara kwake yeye kumwomba Rais apumzike hata kama kwa kufanya hivyo atatafsiriwa kuwa ameogopa na ni mdhaifu.
Uamuzi wa Mzee Pinda kuomba kupumzika kama ni wa kweli, unapaswa kuigwa na wabunge wote waliobakiza chembechembe za maadili katika maisha yao ya uongozi wa umma.
Kukosekana kwa uadilifu miongoni mwa baadhi ya mawaziri kunawatesa wale wachache walio waadilifu. Imefikia hatua sasa kuaminika kuwa hakuna mtu mwadilifu ndani ya Serikali ya CCM na hakuna hatua zinazochukuliwa.
Kutowachukulia hatua viongozi wasio waadilifu kunawaumiza na kuwakatisha tamaa wale walio waadilifu katika utumishi wa umma.
Pinda huyu akatangaza kuwa ni mwiko kuagiza magari ya kifahari, bado yakaagizwa. Pinda akapiga marufuku misafara mirefu ya magari katika ziara za viongozi, badala ya kupungua ikaongezeka. Pinda akapiga marufuku semina maofisini; zikaachwa au kupunguzwa lakini malipo yakabaki pale pale. Pinda akaagiza watendaji watoke maofisini waende kutembelea miradi na kusikiliza kero za wananchi; matokeo yake hata waliokuwa field wakarudi maofisini na kuacha kabisa kwenda.
Pinda akatoa waraka wa kuhakiki watumishi hewa, badala ya kupungua wakaongezeka. Pinda anatoa amri kwa watendaji, kabla hawajatekeleza, wanamuuliza Rais au Waziri Mkuu aliyepita ikiwa watekeleze au waache.
Pinda anapokea maagizo kutoka kwa wasaidizi wa Rais hata yale yaliyo kinyume cha yale aliyoagizwa yeye mwenyewe binafsi na Rais. Jambo moja Mzee Pinda amebakiza, nalo ni heshima na huruma ya Watanzania wanaomwona akilialia kila anapokumbana na dhoruba za kisiasa.
Kama atafanya kosa la kukubali wajibu wa uwaziri mkuu, ajue kuwa huruma hiyo hataipata tena maana muda uliobaki kabla ya siasa za uchaguzi ni mfupi. Si ajabu katika baraza hili jipya ndimo alimo Rais ajaye na huyo hawezi kukubali kumtii Pinda wakati anataka kuweka mikakati ya ushindi. Kwa kuwa Pinda hapendi urais wala ubunge mwaka 2015, apishe kwa wema ili wenye meno waendelee kula nchi.
Maoni ya Wasomaji
AQhh makala hii nzuri lakini
AQhh makala hii nzuri lakini kidogo inanishangaza. pinda huyo anaesifiwa na kuonewa huruma mwazoni na katikati ya nakala, ni huyo huyo tena amabae anatoa maagizo amabayo walio chini yake hawayatekelizi (anagalia sehemu ya mwisho ya makala hii). Sasa tuamini lipi, ni udhaifu wake mwenyewe katika kufuatilia maagizo anayoyatoa au anadhauauliwa na watendaji wake kwa sababu ya udhaifu wake mwenyewe? nauliza tu!
Makala hii inachanganya kama
Makala hii inachanganya kama zilivyo nyingine zilizokwisha andikwa. Mwandishi anachanganya mawazo mengi katika makala moja hivyo inamuweka njia panda msomaji.
Katika kuchangia hoja ya viongozi kujiuzulu nafikiri watanzania tuna kasumba ya kufikiri kuwa kujiuzulu kwa viongozi ni suluhishi la matatizo yetu. Viongozi wa Tanzania ni mimi na wewe je ni wapi tumetayarishwa kuwa viongozi. Baadhi ya nchi zina utaratibu wa kutayarisha viongozi kutoka serikalini, vyama vya siasa na watu binafi ili pindi wanapopewa madaraka waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuweka maslahi ya nchi kuliko binafsi; kwamba wadhifa wanaopewa ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi yao na kadhalika. Katika utaratibu huu anayekosea anajiuzulu bila kuambiwa kwa vile anajua ameteleza wapi na ndiyo maana unakuta wanashtaiwa hata kufungwa pindi wanapokiuka mipaka ya uongozi.
Sina lengo langu kutoa mhadhara lakini watanzania tujiulize viongozi wetu wanatayarishwaje kuongoza nchi bila ili waweze kutoungoza kujali tofauti ya wananchi wanawaowangoza na muelekeo wa kisiasa wa kila kundi? Naomba kutoa hoja.
hivi wewe mwandishi unadai
hivi wewe mwandishi unadai huenda rais ajae akatoka kwenye baraza la mawaziri jipya, je huoni jinsi ccm ilivyopoteza mwelekeo na huoni jinsi Chadema kinavyokubalika na watanzania?
mimi si mtabiri lakini ccm kushinda uchaguzi ujao labda ndovu/tembo apite katika tundu la sindano.
nashangaa hata wewe mwandishi huoni hali inavyoendelea tanzania. kwa kweli unachanganya.
Kwa wanaodai kuchanganywa na
Kwa wanaodai kuchanganywa na makala hii, poleni sana.
Pinda ameishafanya kosa, atalijutia baadaye. Tuliomuonya tulifanya kazi yetu, lakini wajibu wa kutekeleza ulikuwa wake. Atachukiwa na walioondolewa, waliorudishwa, na anayeteua. Waziri Mkuu asiye na uwezo wa kutekeleza hana nafasi ya kuwawajibisha mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na hata maafisa wa kata na vijiji. Hawa, wana uwezo wa kumstaki Pinda kwa Rais wakasikilizwa kuliko yeye, na ndivyo ilivyofanyika kwa hawa mawaziri.
Kuhusu CCM kushinda mwaka 2015 si juu yangu. Nilichosema ni kuwa katika baraza hili la mawaziri, wamo wagombea urais wa mwaka 2015 na Pinda si mmoja wao. Kama watashinda au la, hilo si langu. Natamani washindwe kama walivyoshindwa wengine lakini wakatangazwa washindi na hakuna rufaa!